​Usiwaguse masihi wangu wala usiwadharau manabii zangu!!

Kuna jambo lingine nyeti naomba nilisemee hapa ili litusaidie kwenye mwili wa Kristo.

Mungu tunayemwabudu ni Mungu anayeheshimu sana kanuni za kiroho ambazo Yeye mwenyewe ameziweka, ili kwenye Ufalme Wake kuwe na nidhamu na mambo yasijiendee tu hovyo hovyo.

Maneno ya kichwa cha mazungumzo haya nimeyatoa kwenye bibilia.

Akisema, Msiwaguse masihi wangu, Wala msiwadhuru nabii zangu. (ZAB. 105:15 SUV).

Mungu ameweka huu utaratibu wazi na ameagiza wapakwa mafuta Wake wasiguswe wala manabii Zake wasidhuriwe kwa namna yoyote.

Asiwaguse kwa neno, tendo au wazo. Usiwadhuru kwa neno, tendo wala wazo.

Kizazi cha watu wa Mungu leo wamejichukulia mikononi mwao kuwasema wapakwa mafuta wa Mungu na manabii Zake au watumishi Wake kana kwamba ni kitu cha kawaida tu na wala hawaoni shida kabisa kufanya hivyo.

Umetoa wapi ujasiri huo wa kuwazungumzia vibaya wapakwa mafuta au watumishi wa Mungu.

Je, Mungu amekuweka wewe kuwa mamlaka Yake ya udhibiti wa viwango vya kutumika kwao?

Kuna mambo nayaona na kuyasikia yakifanya na mwili wa Kristo mpaka nahisi damu yangu kupata baridi na hili ni kwa sababu najua neno la Mungu lina nini ya kusema kuhusu hili.

Kwanza kabisa, neno la Mungu linasema:

Mtu akinitumikia, na anifuate; nami nilipo, ndipo na mtumishi wangu atakapokuwapo. Tena mtu akinitumikia, Baba atamheshimu. (YN. 12:26 SUV).

Mungu anasema wazi mtu akimtumikia Yeye atamheshimu. Sasa kama Mungu anamheshimu mtu huyu na Mungu anaujua undani na unje wa mtu huyu, mimi ni nani nimdharau huyu mtu? sio kwamba najitafutia matatizo mie kweli? Namdharau mtu ambaye Mungu anamheshimu, mwisho wa siku itakuwaje katika maisha yangu?

Ninapata huo ujasiri wa kumhukumu mtu ambaye sio mimi nimemweka katika huo utumishi? Hivi Mungu hana utaratibu sahihi wa kunialalisha  kudhibiti watumishi Wake mwenyewe? Ninatoa wapi huo ujasiri? Hivi ninafikiri mimi ni nani hasa kujichukulia mwenyewe mkononi mwangu kuanza kuwahukumu na kuwasema vibaya watumishi Wake!

Wewe u nani unayemhukumu mtumishi wa mwingine? Kwa Bwana wake mwenyewe yeye husimama au huanguka. Naam, atasimamishwa, kwa kuwa Bwana aweza kumsimamisha. (RUM. 14:4 SUV).

Sijui kama tunaona uzito wa hayo maneno hapo juu?

Kunakosa baya alilifanya Musa. Alioa mwanamke wa kiafrika ambaye ilikuwa ni kinyume kabisa na utaratibu wa Mungu. Kaka yake Haruni na dada yake Miriamu wakaamua kusimama kinyume naye kwa ajili ya huo udhaifu aliyokuwa nao bila kufikiri mara mbili kuwa Mungu alikuwa analijua hilo na bado kachagua kumtumia Musa na sio wao.

Kisha Miriamu na Haruni wakamnenea Musa kwa sababu ya mwanamke Mkushi aliyekuwa amemwoa; maana, alikuwa amemwoa mwanamke Mkushi. Wakasema, Je! Ni kweli BWANA amenena na Musa tu? Hakunena na sisi pia? BWANA akasikia maneno yao. Basi huyo mtu, huyo Musa, alikuwa mpole sana zaidi ya wanadamu wote waliokuwa juu ya uso wa nchi. BWANA akanena ghafula na Musa, na Haruni na Miriamu, na kuwaambia, Tokeni nje ninyi watatu, mwende hemani mwa kukutania. Basi hao watatu wakatoka nje. BWANA akashuka katika nguzo ya wingu akasimama pale mlangoni pa Hema, akawaita Haruni na Miriamu, nao wakatoka nje wote wawili. Kisha akawaambia, Sikizeni basi maneno yangu; Akiwapo nabii kati yenu, Mimi, BWANA, nitajifunua kwake katika maono, Nitasema naye katika ndoto. Sivyo ilivyo kwa mtumishi wangu, Musa; Yeye ni mwaminifu katika nyumba yangu yote; Kwake nitanena mdomo kwa mdomo, Maana, waziwazi wala si kwa mafumbo; Na umbo la BWANA yeye ataliona. Mbona basi ninyi hamkuogopa Kumnenea mtumishi wangu, huyo Musa? Hasira za BWANA zikawaka juu yao; naye akaenda zake. Kisha hilo wingu likaondoka kutoka pale juu ya hema; na tazama, Miriamu akawa mwenye ukoma, mweupe kama theluji; Haruni akamwangalia Miriamu, na tazama, yu mwenye ukoma. (HES. 12:1-10 SUV).

Ni kweli kabisa kuwa Musa alifanya jambo lisilostahili. Lakini je Haruni na Miriamu walikuwa na haki kweli ya kumdhalilisha mdogo wao kiasi hicho huku wakijua wazi kuwa Mungu amemtuma pamoja na kwamba alijua ana shida hiyo? Musa hakuwa sahihi hata kidogo kuoa Mkushi na  ilimletea shida maana kuna wakati mvutano kati yake yeye na mkewe ulimfanya Mungu akaribie kumwua Musa maana huyu mwanamke hakuwa anaheshimu taratibu za kiagano ambazo Mungu aliwawekea Wana Wa Israeli.

Pamoja na yote hayo hawa ndugu hawakufikiria kwa kina wakakurupuka tu.

Mungu alipochefuka kwa tendo lao hilo akaja na wala hakuzungumzia masuala hayo ya Musa, akawakumbusha tu utumishi aliyonao na Musa na akawauliza pamoja na kujua yote haya namna ninavyomtumia Musa imekuwaje hamkuogopa kumnenea mtumishi wangu?

Hivi wewe, unautoa wapi huo ujasiri wa kumnenea hivyo mtumishi wa Mungu? Hivi wewe ndo ulimwandika katika huo utumishi. Na je Huyo aliyemwandika hayajui hayo unayofikiri wewe unayajua? Imekuwaje sasa pamoja na Mungu kuyajua hayo kuhusu mtumishi Wake bado akamwandika katika utumishi! Ahaaaaaaaaaa! Wewe umekuwa na busara sasa kuliko Mungu sio? Unamrekebisha Mungu sio? Unamwambia Mungu, mtumishi gani huyu umetupa? Mimi nafikiri unajiwashia moto ambao hutaweza kuuzima.

Mungu alipoondoka kwenye yale mazungumzo na wale ndugu watatu, Miriamu akapigwa na ukoma. Kwanini unajitafutia madhara kutoka kwa Mungu bila sababu?

sikatai yamkini hao watumishi au wapakwa mafuta wana issues!

Wanazo. Mwachie Mungu Yeye anajua jinsi ya kuwaadabisha maafisa Wake mwenyewe. Usimsaidie. Kamwulize Uzzah atakusimulia alipojaribu kumsaidia Mungu nini kilitokea. Alijaribu kuzuia sanduku lisianguke, hapo hapo akapigwa na Mungu na kuuawa. Hata maji hakuomba. Mungu alikuwa anatuma ujumbe wazi kwa Daudi na vizazi vijavyo, “MSIJARIBU KUNISAIDIA.”

Mfalme Sauli alimkorofisha Mungu mpaka Mungu akauondoa upako Wake juu ya Sauli badala yake akampaka mafuta Daudi kuwa mfalme. Sauli alipoteza upako lakini hakupoteza nafasi ya Upakwa Mafuta. Tofautisha sana hivyo vitu viwili. Upako, na Mpakwa Mafuta.

Basi, roho ya BWANA ilikuwa imemwacha Sauli, na roho mbaya kutoka kwa BWANA ikamsumbua. (1 SAM. 16:14 SUV).

Sauli alipoteza mafuta hakupoteza nafasi yaupakwa mafuta. Daudi alikuwa na mafuta lakini hakuwa na nafasi ya mpakwa mafuta.

Zingatia sana hilo itakusaidia.

Angalia Daudi mwenye upako alisema nini kuhusu Sauli asiye na mafuta lakini ana nafasi ya mpakwa mafuta.

Akafika penye mazizi ya kondoo kando ya njia, na huko kulikuwa na pango; Sauli akaingia ndani ili kuifunika miguu. Na Daudi na watu wake walikuwa wakikaa mle pangoni ndani sana. Nao watu wa Daudi wakamwambia, Tazama, hii ndiyo siku ile aliyokuambia BWANA, Angalia, nitamtia adui yako mikononi mwako, nawe utamtenda yo yote utakayoona kuwa mema. Basi Daudi akainuka, akaukata upindo wa vazi lake Sauli kwa siri. Lakini halafu, moyo wake Daudi ukamchoma, kwa sababu amekata upindo wa vazi lake Sauli. Akawaambia watu wake, Hasha! Nisimtendee bwana wangu, masihi wa BWANA, neno hili, kuunyosha mkono wangu juu yake, kwa maana yeye ni masihi wa BWANA. (1 SAM. 24:3-6 SUV).

Sauli alikuwa anamwinda Daudi ili amwue. Kimsingi Daudi ndiyo alikuwa na upako wa mfalme ila nafasi hakuwa nayo maana Mungu alikuwa hajaamua kumwondoa Sauli na kama Mungu hajamwondoa Daudi asingeweza kumsaidia Mungu hiyo kazi ya kumwondoa Sauli.

Katika kimbia ya Daudi alipata fursa ya kumshughulikia Sauli na watu wa Daudi wakamwambia Mungu amemtia adui yako mikononi mwako. Mshughulikie. Daudi hakumdhuru, daudi limgusa kwa kukata pindo la vazi lake. Alipofanya hivyo tu moyo ukamchoma akajua amekosea. Akasema siwezi kumgusa masihi wa Bwana bila kuwa na hatia.

Wewe ndugu yangu sio unawagusa mpaka unawadhuru alafu unafikiri huna hatia. UNAYO  NA MUNGU AKUREHEMU.

Daudi akasema, nisitende neno hili kuunyosha mkono wangu juu ya bwana wangu maana yeye ni masihi wa Bwana. Angalia nidhamu ya Daudi kwa mambo matukufu. Alijua sio yeye amemweka Sauli kwa hiyo sio yeye atakaye mwondoa. Ninajua kwa makusudi kabisa Mungu alimwacha Sauli kama kipimo kwa Daudi. Je Daudi ataheshimu itifaki na kujiepusha na kuchukua mikononi mwake mambo yasiyomhusu?

Hii fursa ilijitokeza tena kwa Daudi akasema maneno kama yale yale.

Lakini Daudi akamwambia Abishai, Usimwangamize; kwani ni nani awezaye kuunyosha mkono wake juu ya masihi wa BWANA, naye akawa hana hatia? (1 SAM. 26:9 SUV).

Ndugu yangu kumgusa kwako masihi wa Mungu, kuwasema kwako watumishi wa Mungu kwa sababu halali au siyo halali unakosea na una hatia.

Mwachie Mungu hilo kama Daudi alivyosema:

Daudi akasema, Aishivyo BWANA, BWANA atampiga; au siku yake ya kufa itampata; atashuka kwenda vitani na kupotea. Hasha! Nisiunyoshe mkono wangu juu ya masihi wa BWANA; lakini sasa tafadhali twaa hili fumo lililo kichwani pake, na hili gudulia la maji, nasi twende zetu. (1 SAM. 26:10, 11 SUV).

Mungu mwenyewe anajua jinsi ya kuwashughulikia watumishi Wake waliyo na utovu na kukiuka kanuni na taratibu za utumishi wao.

Mwisho niseme hili:

Lakini, ndugu, tunataka mwatambue wale wanaojitaabisha kwa ajili yenu, na kuwasimamia ninyi katika Bwana, na kuwaonyeni; mkawastahi sana katika upendo, kwa ajili ya kazi zao. Iweni na amani ninyi kwa ninyi. (1 THE. 5:12, 13 SUV).

 Inapokuja kwenye suala la watumishi jifunze kuwastahi. Zuia mdomo wako, mawazo yako na maamuzi yako. Mungu Yeye atashughulika nao

 –Mwalimu Conrad Conwell Matimba
Advertisements

7 thoughts on “​Usiwaguse masihi wangu wala usiwadharau manabii zangu!!

 1. Barikiwa mtumishi.

  Mimi ni mmoja wa watu wanaoamini WATUMISHI WA MUNGU wanastahili heshima, kustahiwa na kurekebishwa kwa taratibu maalum inapobidi.

  Hii tabia imeibuka sana Facebook na wala siogopi wala kuona haya kuikemea. Nilishawahi kushambuliwa Facebook lkn sitabadili.

  -Wengi huwa ni wale tunaojiita tumeokoka na hufanya hivyo kwa nia ya kuwaaibisha tu (HILA) na wala SIYO kwa nia ya kuwasaidia watumishi au wafuasi au kadamnasi. TENA huwa hawatoi maneno mjadala kurekebisha. Hupost na kuondoka

  -Wengi wao ni vijana ambao hawanaga uzoefu wala historia ya kuongoza kanisa au hata waumini 10

  – Wengi hupost clips au maandishi toka vyanzo mbali mbali (mitandao ya kijamii) pasipo kufanya uchunguzi wa kina….kufuatilia mafundisho au mwenendo mzima wa mtumishi husika.

  -Wengi huexpose watumishi wa makanisa mungine tu hata kama za watumishi wao zipo.

  Siamini kuwa MTU yeyote/kila MTU ana uwezo/ruhusa ya kuhukumu/kuwaadabisha au kudhalilisha watumishi.

  MUNGU ATUSAIDIE

 2. Mwl Conrad,

  Kwanza kabisa nikupongeze kwa makala nzuri inayoturejesha kulitazama Neno la Mungu, ambalo ndio kioo chetu cha kujitazama mwenendo wetu, je, tunamfanania?

  Ni kweli, kuna lawama nyingi sana siku hizi kuhusu watumishi wa Mungu! Tena ktk hili, hao wenye kulaumu hukosa hata staha inayomstahili yeyote mwenye akili timamu! Na jambo linalotia aibu zaidi ni pale watumishi wenyewe wanapokuwa vinara wa kuziongoza lawama hizo, na hivyo kuwaambukiza na waumini wao!

  Mtumishi wa Mungu, ninaamini, ni yule aliyetumwa na Mungu kuifanya kazi ya Mungu. Kwahiyo, huku tuliko ktk Agano Jipya, kimsingi tunapoyarejea Maandiko ili kulitazama suala hili la utumishi, huku tunawaona mitume wakiwa ndio kundi la kwanza la hao waliosajiliwa ktk utumishi. Na kutokana na utumishi wao, ndio wamezaliwa watumishi wengine, makundi kwa makundi. Na ktk makundi hayo wamo pia waliojiingiza kwa hila na kujipachika utumishi Yud 1:4 “Kwa maana kuna watu waliojiingiza kwa siri, watu walioandikiwa tangu zamani hukumu hii….”!

  Basi mtumishi wa Mungu hupaswa kuifanya kazi ya Mungu. Je, kazi ya Mungu ni nini? YN.‬ ‭6‬:‭29‬ “Yesu akajibu, akawaambia, Hii ndiyo kazi ya Mungu, mmwamini yeye aliyetumwa na yeye.” ‬‬Kwahiyo, kazi ya Mungu kwa hawa watumishi unaowazungumzia ni kuwaamini mitume kwanza, ndipo wathibitike ktk utumishi wao kulingana na Neno la Mungu.

  Sasa labda nikuulize mwl Conrad, “Baba Mtakatifu” wa kanisa Katoliki, anapojichukulia nafasi hiyo ki sifa, nafasi ambayo hakuna hata mtume mmoja aliyeifundisha, je, kwa mawazo yako huyo anastahili kuitwa mtumishi wa Mungu? Au mtumishi anayeikataa sehemu ya mafundisho ya mitume, je, huyo hajawakataa mitume? Na je, huyo pia astahili kuitwa mtumishi wa Mungu?

  Kwa mifano michache niliyoitoa unaweza kuona kwa uwazi kabisa kwamba kwa sehemu kubwa, hao wanaojiita watumishi wa Mungu, ukweli ni kwamba Mungu HAJAWATUMA, ni ‘vishoka’ wa Injili tu, kwahiyo lawama na kuneneana vibaya ni sehemu ya maisha yao kulingana na kazi wanayoifanya wasiyotumwa!!

  Mtumishi wa kweli, aliyepakwa mafuta hawezi kumnenea vibaya mpakwa mafuta mwenzake, vivyo mwaminio aliyepakwa mafuta! Mfano wa Daudi ulioutoa unalionesha wazi jambo hilo, ingawa Mungu alimtia Sauli mkononi mwake bali hakuthubutu kumuua; tofauti na yule askari asiyepakwa mafuta, yeye aliishia kumuua Sauli kwa kukosa ufahamu wa mambo hayo. Hukumu ya kifo ilimfuata kwa kosa hilo; na ninaamini watumishi wanaoyakataa mafundisho ya mitume, hawana tofauti na huyo askari aliyemuua mpakwa mafuta, pia hatma yao; maana kwa kuwakataa wapakwa mafuta ni ishara kwamba hao hawana mafuta!

  Mwisho, labda nikuombe uyakague tena Maandiko kuhusu machache kati ya hayo uliyoyaandika, uyaweke sawa ili tuiepuke kesi ya kuwanenea vibaya watumishi wa Mungu!
  1. Unasema, “”Kunakosa baya alilifanya Musa. Alioa mwanamke wa kiafrika ambaye ilikuwa ni kinyume kabisa na utaratibu wa Mungu.””
  Kulingana na Maandiko, nimejaribu kulitafuta humo “kosa” hilo lakini sijaliona! Ninachokijua ni kwamba Musa alikimbilia huko Midiani, na akapokewa huko na akaoa mke ktk nyumba aliyopokewa. Na pia nafahamu hayo yalikuwa ktk Mapenzi ya Mungu. Iwapo hilo lilikuwa ni kosa kubwa kama unavyolisema, basi kwa Rahabu huyo aliyekuwa kahaba itakuwaje? Maana twafahamu kwamba mfalme Daudi atokana na huyo, Rahabu hakuwa Muisraeli alikuwa ni Mmataifa. Na Ruth je?

  Kwahiyo sidhani kwamba ni sahihi kusema kwamba Musa alikuwa na udhaifu kwa kumuoa huyo binti wa kiMidiani. Mazingira ya Samson na Musa ni tofauti kabisa; Samson alikuwa aki flirt, bali Musa alioa na akatulia kuilea familia yake maana huko Misri waliko nduguze asingaliweza kurudi, naye Mungu analitambua hilo, Kut 4:19 ” Bwana akamwambia Musa huko Midiani, Haya, nenda, karudi Misri; kwa kuwa wale watu wote waliokutaka uhai wako wamekwisha kufa.” Miriam alikuwa ni prophetess, ndiko ulikoanzia wivu, kwenye vipawa! Mke wa Musa alikuwa ni kisingizio tu ktk hila hiyo, ndio maana alipigwa ukoma, Haruni hakuwa spiritual, ndio maana aliachwa awe shahidi wa upuuzi waliouendekeza!

  2. Unasema, “”Musa hakuwa sahihi hata kidogo kuoa Mkushi na ilimletea shida maana kuna wakati mvutano kati yake yeye na mkewe ulimfanya Mungu akaribie kumwua Musa maana huyu mwanamke hakuwa anaheshimu taratibu za kiagano ambazo Mungu aliwawekea Wana Wa Israeli.”
  Katika hili pia utakuwa umeliangalia vibaya, huo mvutano unaousema haukuwepo na wala Mungu hakutaka kumuua Musa kwa ajili hiyo unayoisema ya kwamba huyo mwanamke hakuziheshimu hizo taratibu za kiagano; Mungu alitaka kumuua Musa kwa sababu hakuzitimiza taratibu hizo, hakumtahiri mwanaye kama ilivyoagizwa ktk taratibu hizo ndipo yule mwanamke akamuokoa mumewe kwa kumtahiri mwanae fasta!!!
  Kut 4:24-25 “Ilikuwa walipokuwa njiani mahali pa kulala, BWANA akakutana naye akataka kumwua. Ndipo Sipora akashika jiwe gumu na kuikata govi ya zunga la mwanawe, na kuibwaga miguuni pake akasema hakika wewe u bwana arusi wa damu kwangu mimi”

  Gbu!!

 3. Conrad na wapendwa wenzangu…

  Hivi kila mtu anayejiita ni Mtumishi wa Mungu kweli ni Mtumishi wa Mungu…? Nani ni Mtumishi wa Mungu….? Hata Daudi alipozini alifuatwa na kuonywa…..Hata Petro aliposhindwa kusimama katika Kweli ya Mungu alikemewa na Paulo…!!!!

  Maandiko yako wazi mno tena wengi wanaojiita watumishi wa Bwana si watumishi wa Bwana……ni mfano wa Nuru…..wanafanya kwa ajili ya matumbo yao….! Paulo anasema alipiokua Mileto kuwa “kati yenu ninyi (yaani waumini” watatokea watumishi na mafundishi ya kulirarua kundi” Kama ilivyokuwa huko nyuma, ndio hata leo……Wengi wa wa watumishi wa leo hata wakisema Bwana amewaambi lisha kundi langu” unaona wazi wanalisha kondoo matango mwitu….!

  Unapokuta anayejiita mtumishi anapokuja na mafunuo ambayo hayako katika kuujengwa mwili wa Kristo bali ni utata mtupu….au uchu wa fedha….hadhi…..power…umaarufu ndio unaiendesha ministry utasema ni mtumishi wa Bwana huyo….?

 4. unadhani kwa nini haruni hakuadhibiwa kama mwenzake miliam????
  tukubari tukatae haikwepeki watumishi kulaumiwa ikiwa wao ni viongozi huku hawatandi wanayoyaubiri.
  tena kwa mfumo uliopo sasa tunawezaje kutofautisha mtumishi msaka tonge namtumishi halali alieitwa na Bwana kwani wote kwa mfumo uliopo unaitwa mpakwa mafuta ikiwa umehitimu chuo cha biblia tu….
  mwisho wote waliookoka ni watumishi wa Bwana na wapakwa mafuta, kwa hiyo hata wakiongea na wao si kosa ndo maana hata mungu siku hizi apigi mapigo ya hapo kwa papo kama zamani.

  nahisi sjaelewa plz naomba ufafanuzi zaidi.

 5. mwl Conrad huu ni ujumbe ambao mtu asipousoma akaurudia kwa makini na asipomruhusu roho mtakatifu amfundishe na kumfunulia maana yake basi tutashangaa madudu yakiandikwa humu. angalizo linapoletwa somo au hoja tunapaswa tujiulize hili somo mimi kama mimi linanifundisha au kunionya vipi? kabla hatujaanza kuangalia vibanzi vya wengine, maana Paulo anasema haya yaliandikwa ili kutuonya sisi tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kristo na awafunze wale waliozoea kuwabwatukia watumishi maana kweli hali mi mbaya na hawajui kwamba wanajiharibia. em tutafakari Nuhu amelewa mtoto anamuona hamchungulii bali anamuona tu, tukumbuke macho hayana pazia, hamu kumuona baba yake uchi haikuwa kosa bali kosa lilikuwa kwenda kumtangaza baba yake. wengi wanaona makosa ya watumishi badala ya kuwaombea wanaanza kutangaza madhaifu yao na wengine kufikia kusema kwamba eti si watumishi wa Mungu, mara ooh manabii wa uongo. labda niulize swali daudi baada ya kuzini na kuua alibadilisha uamuzi wa Mungu kwamba alimpaka mafuta? sauli alipoenda kwa waganga biblia imetubadilishia maandishi kwamba kwakuwa sauli amekosa basi hapo mwanzo hakupakwa mafuta? Tunapaswa kuelewa kwamba at last it’s between me and God sio between us and God. kama alipewa upako akaona hautoshi akaenda kuongeza kwa kalumanzira mwisho atatoa hesabu yake kwa aliyemtuma. daudi, sauli, hamu, Samsoni, Miriam na wengine wote waliomkosea Mungu aliwaadhibu mwenyewe hakutaka kusaidiwa. wapo wengine wanaona sifa kusema mtumishi fulani yupo hivi wakisingizia wanawaonya watu ili wasidanganywe na mtumishi yule hawajui kwamba yaliyomkuta Miriam, kora, hamu, herode, wanaweza kuwakuta na wao pia. alamsiki

 6. 1 Yohana 2:20
  Nanyi mmepakwa mafuta na yeye aliye Mtakatifu, nanyi mnajua yote.

  1 Yohana 2:27
  Nanyi mafuta yale mliyopata kwake yanakaa ndani yenu, wala hamna haja ya mtu kuwafundisha, lakini kama mafuta yake yanavyowafundisha habari za mambo yote, tena ni kweli wala si uongo, na kama yalivyowafundisha, kaeni ndani yake.

  Ndugu mwandishi; wapakwa mafuta ni wote ambao wamezaliwa na Mungu, si manabii na mitume, au wale tunaowaita watumishi wa Mungu pekee, ambao umeelezea kwamba watu wanawahukumu.

  Lengo langu ni kuweka sawa mtazamo kabla ya kuendelea na mjadala

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s