Kudharau vitu vidogo kutatuletea maangamizo makubwa!!

  • kitaso picha

    Katika mfululizo wa makala zilizopita tuliangalia maadui wa mafanikio ya mwanadamu kwa kuanza na kukosa maono, na kukata tamaa. Wiki hii tunaendelea na adui wa tatu ambaye ni dharau. Karibu katika mwendelezo wa maadui wa mafanikio kwa kuangalia dharau.

 “Hakuna atakayekuona dhaifu pasipo ruhusa yako.” Eleanor Roosevelt

 Dharau ni kikwazo kikubwa pia cha mafanikio kwa mtu yeyote anayetaka kufanikiwa; na dharau hapa haina maana moja ya kuwadharau wengine ila inaenda juu zaidi ya hapo kwa kutazama kujidharau mtu kama mtu, kudharau vitu vinavyomzunguka na pia kujidharau yeye mwenyewe kuwa hawezi kufikia mafanikio na kuona kuwa hawezi kabisa.

 Kujidharau 

Ni wewe tu unayeweza kuwafanya watu au jamii ikuzungukayo ikudharau au ikuheshimu.

Mtu anayejidharau ni vigumu sana kukubalika na watu wengine na pia ni vigumu sana kwa yeye mwenyewe kufanya mambo makubwa kwa kuwa ujidharau na kuona kuwa hawezi kufanya mambo hayo. Ni kweli kuwa zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kumsababisha mtu akajidharau ila ya kutojitambua kuwa yeye ni nani inakamata maeneo yote kwa kuwa mtu anayejitambua na uthamani wake hata kama hana vitu ila kamwe hatokaa kujidharau kwa vile alivyo na hata kama watu wengine wanamdharau lakini yeye hawezi kukubaliana nao na kuanza kujidharau kama wengine wajionavyo.

Watu wengi sana wameuza utu wao kwa tatizo la kujidharau na kuona kuwa wao si kitu na wengine wameruhusu hata miili yao kuchezewa katika ngono kwa tatizo hili la kujidharau na kuona kuwa hawana uthamani ila kama wangefahamu uthamani wao isingekuwa ni vyepesi kufanya hivyo. Na wengine wameshawahi kutamkiwa maneno ya kudharauliwa na wengine na kufika mahali pa kusema kuwa hawana thamani kabisa katika maisha yao.

Wewe ni mtu wa thamani sana katika hii dunia hata kama watu wana kudharau na jua kuwa Yesu Kristo ndivyo akuonavyo na ndiyo maana akatoa uhai wake ili apate mtu kama wewe. Usijidharau kwa kuwa mwanadamu yeyote aliyeumbwa na Mungu ameumbwa na kitu cha tofauti sana ndani yake na amepewa uwezo wa kufanya mambo mengi yakatokea hivyo amini kuwa unaweza wala usitie hofu wala shaka maana wewe ni wa thamani sana na unaweza sana.

Hesabu 13:30 “Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”

Kujidharau ni siraha kubwa sana ambayo adui utumia kumfanya mwamini kutofikia hatima yake, wapelelezi wanafika mahali wanajidharau na kujiona kama mapanzi ndani yao na ukishajiona dhaifu ni lazima itakuwa tu kwako. Ttizo ni wewe kujiona katika hali mbaya na tatizo si kwa wale wanaokuona, kwa sababu kama unajiamini hata wakudharauje ni lazima hautakubaliana na utazamaji wao kwako.

Paulo katika kitabu cha Wafilipi 4:13 anajiamini wazi kwa kusema kuwa “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”

Kujidharau kunatokana pia na kutokujitambua kuwa wewe ni nani na umebeba kusudi la namna gani ndani yako na pia kutojua Mungu anakutazamaje na anakutazama kama nani. Usipojifahamu wewe ni nani ni rahisi sana ukajidharau na hata kufungua mlango kwa wengine kukudharau na kukuona ni mtu wa kawaida sana.

Nilipogundua kuwa Mungu ananitazama kama ‘mungu’ kama anenavyo katika Zaburi 82:6 “Mimi nimesema, Ndinyi miungu na wana wa aliye juu nyote pia” ilinibadilisha sana mtazamo wangu na kunifanya nijiamini zaidi kwa kuwa nimepewa uwezo ndani yangu wa kutosha ambao kwa huo naweza nikafanya mambo mengi na yakadhihirika katika uhalisia wake; na pia neno katika Yohana 1:12  inasema “bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu; ndio wale waliaminio jina lake” kwa maandiko haya ujasiri wa mtu uzidishwa haswa kwa kujifahamu wewe ni nani na Mungu anakutazama kama nani na kama umepewa uwezo ndani yako basi unaweza mambo yote katika yeye akutiaye nguvu. Umepewa uwezo wa Kiungu ni lazima uwe mtu wa tofauti na walivyo watu wengine.

Kudharauliwa na watu wengine.

Huwezi kumzuia mtu anayetaka kukudharau ila unaweza kutokubaliana na dharau zake.

Mathayo 13:54-58 “Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? 55 Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? 56 Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? 57 Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. 58 Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao”

Watu walikuwa wanamfahamu Yesu kama seremala na walipoona anafanya mambo makubwa kuliko wao walivyomuona kama seremala tu wakaanza kumshangaa na wengine kumdharau, ila Yesu hakuwakataza wao kumdharau bali hakuchukulia maanani yale madharau yao kwake.

Usijidharau maana wewe ni zaidi ya watu wakuonavyo na hata wasemavyo kuhusu wewe, hakuna akujuaye wewe ni nani ila muumbaji wako ndiye akujuaye wewe ni nani. 

Kudharau vitu vidogo vidogo. 

Mambo yote makubwa yalitoka katika vitu vidogo dogo ambavyo mara zote huonekana ni vitu vya kawaida sana. Mwanadamu alitoka kwenye mavumbi ya ardhini, msitu mkubwa ulitokea kwenye mbegu ndogo sana na pia waweza kuangamizwa kwa njiti ndogo sana ya kiberiti, mti wa haradari ulitoke kwenye mbegu ndogo sana lakini uwa mkubwa hata kuwafaa ndege na hata wanadamu. Watu wakubwa duniani nao walianza sehemu ndogo sana na ya chini sana kuliko uliyonayo wewe leo japo waweza pungua au kuzidi kwa sehemu tu, ila tofauti yao na watu wengine ni kwa namna ile ya kuyachukulia hayo mambo madogo. Yupo tajiri mkubwa sana duniani ambaye alianza kwa kuuza bigijii ‘bub gum’ chuoni ila leo ni mtu mkubwa sana.

Watu wengi sana wamekuwa na kasumba ya kuyadharau mambo madogo madogo na kuona kuwa hayana maana kwao labda wangeanzia kwenye mambo makubwa ambayo yangewafanya na wao kuonekana watu wenye thamani. Historia ya tajiri mkubwa kuliko wote Afrika kwa wakati huu aitwaye Dangote alianzia na biashara ya kuuza unga kwa mtaji wa kukopa kwa ndugu yake ila alijiongeza siku hadi siku hata kufikia ukubwa huo.

Suala la kudharau mambo madogo madogo ni kubwa sana haswa kwa watu wa Mungu pia kwa kuamini kuwa watu watawadharau watakapowaona wanafanya biashara ndogo ndogo na wengine uamini ni kujipotezea utu wao ila ni muhimu sana kufahamu kuwa hata walio juu walianza chini ila walikuwa na lengo la kuwa juu na ndiyo maana mpaka leo wapo juu. Wengine huamini kuwa “mimi nimebarikiwa na Mungu itakuwaje nifanye kazi za watu wa hali ya chini” hii ni mbaya sana na ni vyema kujifunza kwa Yusufu aliyekubali kuwa mtumwa/mfanyakazi wa ndani ila badae akawa waziri mkuu na pia Yakobo alianza kama kibarua wa kuchunga mifugo ya Labani ila ndipo alipopatia utajiri mkubwa sana aliokuwa nao.

Nimejifunza sana katika eneo hili kwa kuwa Mungu anapenda watu wachakarikaji na ilinilazimu kwa wakati mwingine kuajiliwa kama muuza duka la mtu, mtunza mifugo ya mtu, kubeba mikaa na kufanya kazi za hali ya chini sana ila nikijua kuwa naelekea mahali pa juu sana na yale ninayoyaona leo sitoyaona tena, ngoja nikukumbushe habari za Yusufu ya kuwa baada ya kuinuliwa na Bwana hakuwa mtumwa/mfanya kazi wa ndani tena ila yeye aliajiri wa kumfanyia hizo kazi na pia Yakobo yeye hakuchunga yeye tena ila alikuwa akichungiwa. 

Kwenye kitu ambacho wewe unakidharau wenzio wanaona fursa ya kuwapeleka mahali wanapotaka kwenda. Usidharau vitu vidogo vidogo kwa kujitia moyo kuwa mimi ni mbarikiwa siwezi kufanya vitu vya aibu namna hiyo kwa kuwa yupo Yakobo ambaye alitoka kwenye familia ya kitajiri sana pengine zaidi yako na pia alikuwa ni mbarikiwa wa BWANA na kuahidiwa mambo makubwa pengine kuliko wewe leo ila hakuona ule utajiri kama ni kitu cha kufungamana nacho hata kikamfanya abweteke na kudharau kazi ila alianza kuangaika na mambo madogo madogo ambayo yalimuongeza na kumfanya awe mtu mkubwa sana ila naye kabla ya utumwa huo alitamkiwa kuwa ni mbarikiwa na pia jifunze kwa Musa aliyechunga mifugo kule Midiani alikuwa anatokea kwenye nyumba ya kifalme. Ndivyo walivyo watu wa Mungu halisi.

Wengine hawataki kujishughulisha katika madogo madogo kwanza na utegemea sana kusaidiwa mitaji mikubwa ili waanzie juu, hii ni dhana mbovu kwa kuwa waweza anza na padogo sana ambapo pana dharauliwa na watu wengi ila ukapanda juu siku hadi siku. Kuna aina mbili tofauti za watu katika kupambana na maisha hata kufikia viwango vya juu; aina ya kwanza ni watu wale waliowekewa ngazi tayari na watu waliowatangulia ambao waweza kuwa wazazi, ndugu wa karibu na hata marafiki wa karibu, yaani wao huikuta ngazi na kazi yao kubwa huwa ni kuanza kupanda ngazi hiyo ili kufika juu: aina nyingine ni watu ambao huanza wao kama wao kwa kutafuta mbao, na kila dhana ya kutengenezea ngazi na huanza kuitengeneza ngazi wao wenyewe hata ikikamilika huiweka mahali pa kupandia wao wenyewe na kuanza kuipanda wao wenyewe, aina hii ndiyo inabeba watu wengi wa jamii ya Kiafrika. Aina hizi mbili za watu huwa tofauti na kila mmoja anapaswa kupambana kwa namna yake ili kufika pale juu apaswapo kufika ila umakini na juhudi kubwa kote yatakiwa na ule upande wa pili unahitaji juhudi kubwa zaidi ya kupambana na kuijiamini kuwa unaweza katika kupambana hata ukafanikiwa kufika juu katika eneo ambalo uhitaji kufika. 

Mchwa wadogo uangusha nguzo kubwa. 

Rafiki yangu mmoja anapenda sana kusisitiza mara nyingi katika msemo huu ambao nimekuwa nikijifunza sana kwa msemo huu. Nguzo inapokuwa imesimama huonekana ni nzuri na imara ila nguzo hiyo huweza angushwa na mdudu mdogo sana aitwaye mchwa. Ikiwa imesimama mchwa wanaisogolea hili kuanza kuitafuna ila kama imekingwa na vidhibiti vya mchwa si rahisi kuweza kuliwa. Ndivyo ilivyo kuna mambo watu huyaona ni madogo madogo sana ila ndiyo mambo hayo hayo yaliyo kwazo la kufanikiwa kwa mtu na zaidi huweza mnyima mtu nafasi ya kuziingia mbingu. Ukimtazama mtu ambaye anguko limetokea wengi waweza shangaa sana ila ukweli ni kwamba kuna mchwa walikuwa wanakula ndani kwa ndani na mtu huyo hakuweza kuwazuia wasiendelee sasa wamekula mpaka kuozesha nguzo hiyo na ndiyo maana imeanguka kwa kuwa imeoza na imeshindwa kujimudu.

Ni vyema sana kutodharau mambo madogo madogo kwa kuwa hata shetani anajua kuwa hawezi kukupata kwenye makubwa na ndiyo maana anaweza kutumia vitu vidogo na kuvilemba sana hata ukavitetea na kuviona vyafaa sana ila mwisho wake ni kukupeleka katika maangamizo makubwa. Waswahili usema “usipoziba ufa utajenga ukuta” tazama kwa umakini sana na usiruhusu kabisa madogo kupata nafasi ya kukuangusha. 

Maangamizo makubwa uletwa na vitu vidogo. 

Kwa kuitazama njiti ya kiberiti ni njiti ndogo sana ila inauwezo wa kuchoma msitu mkubwa uliokaa kwa kitambo kirefu ndani ya masaa machache sana uteketea kwa matokeo ya njiti hiyo. Pia magonjwa yanayomsumbua mwanadamu hutokana na wadudu wadogo sana kwa kuutazama mfano wa mbu ni kiumbe kidogo sana ila ueneza malaria ambayo uua watu wengi sana ila cha msingi ni “kinga ni bora kuliko tiba” jikinge kwa kila tahadhari na kwa gharama yoyote kabla ya hatari na ni bora watu wakaona wewe ni muoga ila kwako si uoga bali ni usalama. Wengine huikimbia sana zinaa na kuitwa waoga na washamba ila hawa sivyo kama watazamavyo ila wameepuka hatari na kufuata usalama.

Mfano mwingine wakuona ni mfano wa nzi kuwa ni mdogo sana ila usababisha ugonjwa mkubwa wa kipindu pindu ila kinga yake ni kutumia chakula cha moto na kisafi ambacho hushindwa mudu kukisogelea na vivyo hivyo kwa mwamini ni bora kuwa safi na wa moto ili kuepuka hatari. Ukiwa safi na wa moto vitu vichafu haviwezi kupata fursa ya kuwa karibu na wewe na kukufanyia maangamizo makubwa.

–Kelvin Kitaso

Advertisements

2 thoughts on “Kudharau vitu vidogo kutatuletea maangamizo makubwa!!

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s