Kula mezani na adui!!

pastormbwambo

Utangulizi:

Katika kitabu cha Mwanzo, tunasoma vile Mungu alivyomuumba mwanadamu na sababu za uumbaji huo. Kulingana na maandiko katika kitabu hicho, tunaelewa wazi kuwa aliumba ili awe mwangalizi wa uumbaji wake, sambamba na kuwa na ushirika naye. Kutokana na ukweli huu, tunaweza kusema kuwa, aliumbwa ili awe mkuu (master) kuliko vitu chini ya mbingu. Kuonyesha vile alivyomheshimu mwanadamu, Mungu alimuweka mahali ambapo hata Sulemani katika fahari zake zote, hakuwahi kuishi sehemu kama hiyo. Makazi haya yalikuwa na kila aina ya matunda, wanyama, mito na dhahabu iliyo safi. Kwa lugha nyingine tunaweza kusema kuwa, kila kitu kilikuwa ni chema katika Edeni ya Adamu wa kwanza, hadi pale dhambi ilipoingia katika bustani ya Edeni. Baada ya anguko hili, mwanadamu aliweza kupoteza si tu ushindi katika mambo ya kiroho bali alipoteza ushindi katika mambo ya mwilini pia.

Hata hivyo kutokana na upendo wa Mungu wa kumpenda mwanadamu, alitoa ahadi ya kuuletea ulimwengu mbegu itakayourudishia yale yote waliyoyapoteza baada ya kuhiari kuwa chini ya ufalme wa Ibilisi. Wakati wa kuingojea ahadi hii, Mungu aliliinua taifa la Israeli ili kuifundisha dunia vile watoto wake wanavyotakiwa kuishi. Tunapoliangalia taifa hili, tunaweza kuona kuwa kila wakati, Mungu alihakikisha kuwa anakutana na mahitaji yao ya msingi ya kila siku. Hata pale janga la njaa lilipokuwa likiinyemelea dunia, alimnyakua Yusufu kutoka kwa Yakobo, ili kuwa mlango wa shibe kwa taifa lake alilolichagua.

Utoshelevu wa Mungu kwa taifa hili, unaonekana pia katika maneno yaliyonenwa na Mungu kwa Musa juu ya taifa hili. Mungu alimwambia kuwa, atawatoa wana wa Israeli mikononi mwa Farao katika maisha yasiyo na kitu, na kuwapeleka katika nchi inayobubujika maziwa na asali. Pamoja na ukweli huu, wa Mungu kukutana na mahitaji ya kimsingi ya watu wake, uko wakati ambao wana wa Israeli waliishi kwa kula vichwa vya punda, mavi ya njiwa pamoja na kuwala watoto wao! Unachokiona hapa ni kuwa, badala ya maziwa na asali, wana wa Israeli waliishia kula vitu visivyoliwa kutokana na hali ngumu ya kimaisha iliyokuwa ikiwakabili. Neno la Mungu linatuambia kuwa, upungufu huu ulisababishwa na mfalme Ben Hadadi na jeshi lake. Mfalme huyu alikuwa ameliweka jeshi lake nje ya mji wa Samaria ili kuzuia kitu chochote kisiingie au kutoka katika mji wa Samaria.

Kupitia mbinu hii ya Ben Hadadii, biashara za Israeli zilisimama, waliotaka kwenda Yerusalemu kuabudu walishindwa kufanya hivyo, wagonjwa waliotakiwa kutibiwa nje ya Samaria, hawakuweza kufanya hivyo, masomo yalisimama na maghala ya chakula yalibakiwa kuwa matupu. Kwa maneno mengine tunaweza kusema kuwa, Israeli ilikuwa imeporomoka kiroho, kimwili na kiuchumi pia.

Mbinu hii ya mfalme Ben Hadadi, ndiyo inayotumiwa mara kwa mara na Ibilisi, kuyazuia mahitaji ya msingi ya watoto wa Mungu. Kupitia huduma ya Yesu Kristo hapa duniani, Mungu tayari ametoa baraka za kiroho na kimwili kwa kanisa lake, ila mara nyingi kanisa limeishi bila ya baraka hizo kutokana na Shetani kuzikalia baraka hizo. Leo katika somo letu, tutaona vile Mungu alivyolipeperusha jeshi la mfalme Ben Hadadi, na kuuruhusu tena mzunguko wa maisha katika taifa Israeli uliokuwa umesimamishwa na mfalme Ben Hadadi. Kwa vile Mungu habadiliki, ni wazi kuwa yale yaliyobadilisha uteka wa Israeli, yanaweza kutusaidia pia, kuishi kama vile Mungu alivyotukusudia kuishi. Mambo yaliyochangia kurudisha maisha katika Israeli, ni pamoja na haya yafuatayo:-

NENO KUTOKA KWA MUNGU

“Elisha akasema, Lisikieni neno la BWANA; BWANA asema hivi, Kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri, kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria.” 2 Wafalme 7:1

Tunapozungumza juu ya neno analohitaji mtu ili kuzichukua haki zake zinazokaliwa na adui, tunapaswa kufahamu njia mbili zinazotumiwa na Mungu pale anapotaka kufikisha ujumbe wake kwa wanadamu. Njia ya kwanza ni ile tunayoweza kuiita neno la msingi la wakati wote kwa ulimwengu mzima, kwa Kiyunani ‘logos’, au maandiko matakatifu. Neno hili la kijumuiya, ni ufunuo wa Mungu uliotolewa zamani na hatimaye kuandikwa katika vitabu 66, vinavyojulikana kama Biblia takatifu. Njia ya pili ya kupokea ujumbe kutoka kwa Mungu, ni ile ya Mungu kufunua mapenzi yake au kile anachotaka kukifanya kwa mtu au kikundi, kwa wakati maalum. Neno la Mungu linalowajia wanadamu kwa njia hii, linajulikana  kwa Kiyunani kama, rhema.

Kutokana na njia hizi mbili za Mungu kusema na watu wake, yako mambo tunayoweza kuyatarajia kwa kusimamia maandiko peke yake, na yako yale yanayohitaji njia zote mbili. Kwa mfano,hatuhitaji ufunuo maalum ili kuwashuhudia watu habari njema za wokovu, ila tunahitaji ufunuo maalum ili kutangazia idadi ya watakaompa Yesu maisha yao, kutokana na ushuhuda huo. Hali kadhalika, hatuhitaji ufunuo maalum ndipo tuhubiri injili ya uponyaji ya Bwana Yesu, ila tunahitaji ufunuo maalum kutamka idadi ya watakaofunguliwa kutokana na maombi yetu. Tunachojifunza kutokana na mifano hii miwili ni kuwa, tunapokuwa katika tatizo fulani zito na la muda mrefu, njia hizi mbili za kupokea kutoka kwa Mungu zinahitajika, ili kutuumbia imani itakayotuinua. Maandiko yatatusaidia kupima pale ufunuo wa kibinafsi utakapotujia, hali kadhalika ufunuo maalum wa kibinafsi, utatuwezesha kutambua kuwadia kwa wakati wa Mungu wa kufanya jambo fulani.

Hiki ndicho kilichotukia wakati maadui walipokuwa wamekalia haki za Israeli. Katikati ya tatizo hili, Elisha alipata neno kutoka kwa Bwana kwa niaba ya taifa la Israeli, kuhusiana na tatizo lililokuwa likiwakabili. Kama mtumishi wa Mungu alikuwa anazijua ahadi za Mungu katika torati vile Mungu anavyoweza kukutana na shida za watu wake, ila ufahamu huu wa maandiko, haukumpatia ujasiri wa kutoa tamko la kumalizika kwa njaa katika Israeli. Ni pale tu alipopokea neno maalum kutoka kwa BWANA kuhusiana na tatizo hilo, ndipo alipoutamkia umma kuwa, “kesho panapo saa hii, kipimo cha unga mzuri, kitauzwa kwa shekeli, na vipimo viwili vya shayiri kwa shekeli, langoni pa Samaria.”

KUKUBALIANA NA NENO LA MUNGU

“Basi yule Akida, ambaye mfalme alikuwa akitegemea mkono wake, akamjibu yule mtu wa Mungu, akisema, Tazama, kama BWANA angefanya madirisha mbinguni, je! Jambo hili lingewezekana? Akamwambia, Angalia, wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula.” 2 Wafalme 7:2

Jambo lingine lililowasaidia wana wa Israeli wakati wa Elisha, kutwaa haki zao zilizokuwa zinakaliwa na maadui, ni imani yao juu ya neno la Mungu lililowajia kupitia kwa mtumishi wake. Kama wasingeliamini kile kilichosemwa na Mungu kuhusiana na tatizo lililokuwa likiwakabili, ni wazi wasingeliweza kukutana na matunda ya neno hilo.

Katika hili, wako wanaoweza kuhoji na kusema, “ kama  wakati wa Mungu umefika, kuna haja gani ya kumsaidia kwa kuamini?” Ninachotaka ukione hapa ni kuwa,kila wakati Mungu hutenda kazi sawasawa na kanuni za maisha zinazopatikana katika maandiko matakatifu. Wakati wake wa kufanya jambo unapofika, kile alichokusudia kukifanya, kitafanyika kupitia barabara ya ufunuo wake, unaopatikana katika maandiko matakatifu. Ufunuo huu ni pamoja na zile kanuni za maisha zijulikanazo kama, “kanuni za imani.”   Neno la Mungu kuhusiana na kanuni hizo linatufundisha kuwa, “Mwenye haki wa Mungu ataishi kwa imani.” Warumi 1:17. Kwa kuwa maisha ni kutoa na kupokea, ni pale tu tunapounganisha imani yetu na neno la Mungu, ndipo tunapoweza kupokea kutoka kwake. Kwa maneno mengine, Mungu anapotaka kutufanyia jambo lolote lile, ni lazima jambo hilo lipitie katika barabara ya imani.

Mara nyingi imekuwa vigumu kwa baadhi ya watoto wa Mungu kukutana na haki zao za kimsingi za kimaisha, kutokana na kutoweka bidii kukubaliana na neno lililotoka kinywani mwa Mungu. Hata wana wa Israeli waliweza kuangamia jangwani kutokana na kutokubaliana na neno la Mungu.Waebrania 4:2. Mungu anaposema na wewe ukashawishika kuwa hilo ni neno lake kwako, ni lazima ufikie hatua ya kuamini kuwa, itafanyika kwako sawasawa na neno hilo. Kinyume cha hapa, utakuwa na neno la Mungu katikati yako, ila halitakusaidia.

Katika andiko linalotawala kipengele chetu tunaona kuwa, Afisa katika Ikulu ya mfalme wa Israeli alivuna uharibifu kutokana kutoamini kile kilichonenwa na Mungu kupitia kwa mtumishi wake. Mungu alipoona kutokuamini kwake, alimwambia yule ofisa kupitia mtumishi wake kuwa, “ wewe utaliona kwa macho yako, lakini hutakula.” Kweli siku ya tukio ilipofika, neno la Mungu lilitimia kwake, pale watu walipokanyaga kutokuamini kulikokuwa ndani yake, mpaka akafa!  Wafalme 7:20

LAZIMA KUSEMA, SASA BASI

“Basi walikuwepo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo, nasi tukikaa hapa, tutakufa vilevile. Haya! Twende kukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai, tutaishi; wakituua, tutakufa tu.” 2 Wafalme 7:3-4

Wakati maadui walipokuwa wanaendelea kuzikalia haki za wana wa Israeli na njaa kuwa kali katika Samaria, aandiko letu hapo  juu kwa sehemu, linatueleza kwa sehemu vile maisha ya watu yalivyokuwa. Miongoni mwa watu waliokuwa wakiteseka kutokana na haki zao kukaliwa na maadui, ni wakoma wanne, waliokuwa wakiomba katika lango la mji wa Samaria. Hawa nao kama ilivyokuwa kwa wenzao, nao waliishia kula makombo ya mavi ya njiwa pamoja na mifupa ya vichwa vya punda! Jambo la kutia moja ni kuwa, baada ya kipindi kirefu cha kuteseka, wakoma hawa walifikia mahali pa kusema, “sasa basi.” Mara zote Mungu hutenda kazi pamoja na watu waliofikia hatua ya kuchoshwa kuishi nje ya mapenzi ya Mungu.

Kama kanisa la siku hizi za mwisho linataka kuzitwaa haki zake zinazokaliwa na adui, ni lazima lifikie mahali pa kuchoshwa na hali hiyo na kuanza kutafuta namna ya kuondokana na hali hiyo. Inasikitisha kuona vile baadhi ya waamini, wanavyochukuliana na Shetani kwa kile kinachoonekana kama ‘kuyapalilia’ matatizo waliyo nayo! Katika miaka tuliyo nayo, si jambo geni kumwona mwamini asiye na muda wa kuomba kutokana na kuzidiwa na usingizi, licha ya kuwa analalia  godoro la maboksi!   Ni wazi mwamini wa jinsi hii, bado hajafikia hatua ya kuchukia hali hii ya kukosa godoro. Kama tunahitaji kuishi maisha ambayo Mungu ametukusudia tuishi, ni lazima tuungane na wale wenye ukoma wanne, ambao katika taabu yao, walifikia mahali pa kusema, “sasa basi!”

KUWE NA HALI YA KUKUBALIANA

Haya! Twende kukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai, tutaishi; wakituua, tutakufa tu.” 2 Wafalme 7:3-4

Kwa kuwa idadi ya wakoma ilikuwa wanne, ni wazi wazo la kuiendea kambi ya Washami halikuwa wazo la pamoja, mmojawao alitoa wazo hilo na wengine wakakubaliana naye. Hivi ndivyo ilivyo ndani ya ufalme wa Mungu, kila mara yuko atakayetoa wazo fulani jema, litakalohitaji kuungwa mkono na wananchi wengine katika ufalme huo. Kama kusingelikuwa na kukubaliana katika kambi hii ya wakoma, ni wazi hata yule aliyelitoa wazo hilo, angelikata tamaa na ushindi usingelipatikana.

Mambo mengi yanatatizika katika maeneo mengi ndani na nje ya ufalme wa Mungu, kutokana na kukosekana kwa mhimili huu wa makubaliano. Kiongozi wa kiroho anaweza kutamka neno jema, ila siku ya kulitendea kazi neno hilo, ni waamini kiduchu watakaoonekana. “Njoni kwenye maombi”, mchungaji atasema, siku ya maombi, hakuna watu. “Njoni ibada za katikati”, siku ikifika patupu. “Wekeni bidii kushuhudia”, hakuna wa kufanya hivyo. Nionyeshe familia iliyopiga hatua kiroho na kimwili, nami nitakuonyesha hali ya makubaliano, ndani ya jamii hiyo. Makubaliano yalikifanya kishindo cha kazi ya ujenzi wa mnara wa Babeli kufika mbinguni, lakini makubaliano yalipokosekana, kazi ya ujenzi iliweza kusimama! Mwanzo 11:1-9

Kama wana wa Mungu tunataka kula mema ya nchi, ni lazima tuhakikishe kuwa, tunakubaliana na; neno la Mungu, viongozi wanaotuongoza na Roho Mtakatifu. Hali kadhalika, tunatakiwa kukubaliana na waamini wenzetu katika kila neno linaloujenga ufalme wa Mungu.

FANYA UAMUZI WA BUSARA

“Basi walikuwepo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo, nasi tukikaa hapa, tutakufa vilevile. Haya! Twende kukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai, tutaishi; wakituua, tutakufa tu.” 2 Wafalme 7:3-4

Andiko letu hapa juu linaonyesha mtihani mkubwa wa kimaamuzi uliokuwa ukiikabili kambi ya wakoma, katika lango la Samaria. Uchaguzi wa kwanza uliokuwa mbele zao, ulikuwa ni ule wa kuiacha kambi yao na kuhamia ndani ya mji. Kama wangeliamua kufanya hivyo, katika ulimwengu wa roho, wangelikuwa wanakwenda kufia mbali na haki zao. Uamuzi wa pili waliokuwa nao, ni ule wa kuendelea na ndoa yao ya mateso katika lango la mji. Hapa tena, wangelikufa licha ya kuwa karibu sana na jeshi la Washami, lililokuwa likizishikilia haki zao. Uamuzi wa tatu waliokuwa nao, ni ule wa kuwaendea maadui wanaozishikilia haki zao. Ingawa kibinadamu uamuzi huu ulionekana kuwa wa hatari zaidi, ulikuwa umebeba mwanya wa kuhurumiwa na Washami. Baada ya kuichunguza milango hii mitatu, walichagua kuiendea kambi ya maadui.

Mara kwa mara maisha ya wanadamu chini ya jua yanakabiliwa na mitihani ya aina hii ya kimaamuzi, kumchagua Kristo ukose mali ya dunia hii au kuchagua mali ya dunia hii, umkose Kristo. Wakati mwingine, kuna mtihani wa kumchagua Kristo upoteze nafasi ya kazi iliyokuwa mbele zako, au kuichagua nafasi ya kazi, uukose uzima wa milele. Wakati wa mitihani ya jinsi hii, upenyo utapatikana pale mwamini atakapofanya uamuzi ulio na busara za Mungu ndani yake. Mwamini anaweza kufanikiwa mtihani huu wa uchaguzi, pale atakapoomba ushauri wa kiongozi wake wa kiroho pale atakapokabiliwa na mitihani hii ya kimaamuzi.

Kama kanisa la siku za mwisho linataka kuzitwaa haki zake zilizofunuliwa katika maandiko matakatifu, linatakiwa kufanya maamuzi yenye busara hata kama kutakuwa na hatari katika kufanya hivyo. Mafanikio ya mtu ya sasa na yale yajayo, kwa kiwango kikubwa yanategemea busara yake katika maamuzi anayoyafanya siku kwa siku katika maisha yake.

USIANGALIE UDHAIFU ULIO NAO

“Basi walikuwepo watu wanne wenye ukoma, penye lango la mji; wakasemezana, Mbona tunakaa hapa hata tufe? Tukisema, Tutaingia mjini, mjini mna njaa, nasi tutakufa humo, nasi tukikaa hapa, tutakufa vilevile. Haya! Twende kukaliendee jeshi la Washami; wakituhifadhi hai, tutaishi; wakituua, tutakufa tu.” 2 Wafalme 7:3-4

Kabla ya kuzama ndani katika kukielezea kipengele hiki, ni vema tukumbuke kuwa, taabu iliyokuwa ikiukabili ufalme wa Israeli, ilitokana na mji wao kuzingirwa na maadui. Ingawa Israeli ilikuwa mojawapo ya mataifa yenye jeshi lenye nguvu miaka hiyo, jeshi hilo lilinyong’onyea kutokana na nguvu za kijeshi za Washami. Hofu hii iliyokuwa imeliangukia jeshi la Israeli, zilizokuwa zimeenea katika maeneo yote ya mji na kila mtu katika taifa lile, alikuwa katika hofu kubwa. Hata wale wenye ukoma wanne walikuwa wanaelewa juu ya mfadhaiko huu uliokuwa juu ya wote waliokuwa wakiishi ndani ya Samaria.

Kitu cha kutia moyo ni kuwa, pamoja na viungo vyao kuliwa na ukoma kiasi cha kuwaondolea kasi ya kutembea au kukimbia, bado wakoma hawa, waliamua kuiendea kambi ya Washami! Kama wasingelikuwa na ukoma, ingelikuwa rahisi kuiendea kambi ya Washami na pia ingelikuwa rahisi kwao, kukimbia pale neno la shari litakapotokea. Watuhawa walikataa kukubaliana na milango yao ya fahamu na kujitamkia kuwa, “pamoja na udhaifu tulio nao, tunaiendea kambi ya maadui!”

Tunachokigundua hapa ni kuwa, kama tunahitaji kuwa kama vile Mungu anavyotaka tuwe, ni lazima tuwe tayari kung’ang’ana na uamuzi wa busara tulioufanya bila kuangalia udhaifu wetu. Udhaifu wetu unaweza kuwa umaskini, kukosa elimu, hali ya kutoka katika familia isiyo na jina, udhaifu wa kiafya na kadhalika. Ndio, udhaifu huu unaweza kuwa dhahiri, ila kamwe hautakiwi uwe kikwazo cha kutuzuia kuishi katika mapenzi ya Mungu. Ukiangalia watu ambao Mungu aliwatumia kufanya mambo makubwa katika siku za Biblia, walikuwa ni watu waliokuwa na udhaifu fulani katika maisha yao.

Fanny Crossby, alikuwa kipofu, ila aliweza kuandika zaidi ya nyimbo 3,000. Smirth Wigglesworth, alikuwa seremala asiye na kisomo ila alitumiwa na Mungu kwa kiwango kilichowafanya wengine wamwite, mtume wa imani! Naye Musa alikuwa na kigugumizi, ila aliweza kumtetemesha Farao na ufalme wake, naye Gideoni, alikuwa ni mtu kutoka familia maskini, ila aliweza kuliongoza jeshi la Israeli kulishinda jeshi lenye nguvu la Wamidiani. Watu hawa walitumiwa na Mungu kufanya mambo makubwa, pale waliposukuma mbele pasipo kuangalia udhaifu uliokuwa ukiwakabili.

Inasikitisha kusema kuwa, watoto wengi wa Mungu wameshindwa kuishi maisha waliyokusudiwa na Mungu, kutokana na kukubaliana na kilio kinachofanywa na udhaifu wao wa kiroho na ule wa kimwili. Wakati umefika kwa watoto wa Mungu kupambana na chochote kile kinachozizuia haki zao, bila kuangalia udhaifu walio nao. Hivi ndivyo walivyofanya wale wenye ukoma wanne, udhaifu wao ulikuwa halisi, ila walichoshwa na matatizo yao na kusema, “tunaiendea kambi ya Washami.

WALIAMKA KABLA YA KUPAMBAZUKA

“Basi wakaondoka kabla ya mapambazuko, ili waende mpaka kituo cha Washami.” 2 Wafalme 7:5

Biblia haisemi hasa sababu zilizowafanya wakoma hawa waamke mapema kabla ya giza kutoweka, ila kudamka kwao kulileta matokeo makubwa mawili. Kwanza, kuliepusha kukutana na watu katika kusafiri kwao. Kulingana na torati ya Musa, wenye ukoma walitakiwa kupaza sauti za unajisi wakati wanapotoka eneo moja kwenda lingine. Pamoja na uzuri wa agizo hili katika torati, kitendo hiki hakikuwa cha kufurahisha kwa yule aliyehesabika kuwa najisi katika jamii. Unafahamu kama una tatizo, na ukawekwa utaratibu wa kulipigia mbiu tatizo hilo mara kwa mara, kamwe utaratibu huo, hautakuwa baraka kwako. Hata wataalam wanasema kuwa, jinsi mtu anavyotamka mara kwa mara juu ya tatizo lake, ndivyo makali ya tatizo hilo yanavyozidi kuongezeka. Kutokana na ukweli huu, uamuzi uliofanywa na wakoma wa kuanza safari kabla ya kupambazuka, uliwafanya wasikutane na watu, hivyo kuwaondolea kero ya kupiga kelele za unajisi.

Jambo la pili, kule kudamka kwao usiku, kuliondoa uwezekano wa kukatishwa tamaa na watu, pale watakapoulizwa kule walikokuwa wakielekea. Jamii ilizoea kuwakuta katika lango la mji, hivyo kuwaona wakiwa mbali na lango hilo pamoja na mizigo yao, kungelizusha dodoso kuhusiana na kilele cha safari yao. Kama wangeanza safari yao mapema na kukutana na watu, swali kubwa lingekuwa,“mnakwenda wapi?”, na hapo wangelikutana na maneno ya kukatisha tamaa pale watakapojibu kuwa, “tunaliendea jeshi la Washami.” Tunachokiona hapa ni kuwa, kama tunahitaji kukifikia kilele tulichokusudiwa na Mungu tukifikie katika maisha yetu, tunatakiwa kuiruhusu imani itusahaulishe mto wa matatizo yanayoyasonga maisha yetu. Kama tutakuwa watu wa kutumia muda mwingi kushika tama kutokana na matatizo yanayotusonga, tutaufanya mto wa matatizo uzidi kufurika katika maisha yetu, na hapo hatutaona ushindi.

Sambamba na kuondoa macho na vinywa vyetu katika matatizo yanayotusonga, tunatakiwa kuamka kungali giza ili kuwakwepa watu waliobeba sumaku ya kukatisha tamaa. Mara nyingi tunaongea juu ya kushirikiana hatupaswi kushirikiana na kila mtu ndani ya kanisa la Mungu.   Mtu mmoja alitamka mahali fulani kuwa, katika kanisa kuna makundi mawili ya watu. Kundi la kwanza ni lile la wabeba maono (vision carriers) na la pili ni la wauaji wa maono (vision killers). Kama ni kushirikiana, tutashirikiana na wabeba maono, ila kwa wale wanaoua maono, ni lazima tuhakikishe kuwa tunaamka kungali giza ili tuwakwepe.

TARAJIA MUUJIZA

“Na walipofika mwanzo wa kituo cha Washami, kumbe! hapana mtu. Kwa maana BWANA alikuwa amewasikizisha Washami kishindo cha miendo ya magari, na kishindo cha farasi, kama kishindo cha jeshi kubwa wakaambiana, Tazama, mfalme wa Israeli amewaajiri wafalme wa Wahiti, na wafalme wa Wamisri, waje wapigane nasi. Kwa hiyo, wakaondoka wakakimbia kungali giza bado, wakaziacha hema zao, na farasi zao, na kituo chao vile vile   kama kilivyokuwa, wakakimbia wapate kuziponya nafsi zao. 2 Wafalme 7:5-8

Ingawa kulikuwa na uwezekano wa kuuawa au kuhurumiwa na Washami, kulingana na maneno ya wenye ukoma, naamini kuwa, walikiendea kituo cha Washami huku wakitarajia uzima badala ya umauti. Kama wangelikuwa tu wakitarajia kifo, ni wazi wangelichagua kufia katika kambi yao katika lango la mji. Ingawa kulikuwa na uwezekano wa kuangamizwa na Washami, wakoma hawa waliiendea kambi ya adui huku wakitarajia kuhurumiwa na wale waliokuwa wakiwataabisha. Kama tunahitaji kuzikamata haki zetu zilizokaliwa na adui na hatimaye kula mezani pa adui, ni vema tufanye kila lililo katika uwezo wetu na tukisha kufanya hivyo, tukae mkao wa kutarajia muujiza kutoka kwa Mungu.

Mara zote wakati wa Mungu wa kutenda jambo fulani unapofika, ni lazima mhusika naye ashirikiane na Mungu kwa kuweka imani yake katika lile linalokusudiwa kutendwa na Mungu. Hivi ndivyo ilivyotukia wakati wa njaa iliyolipata taifa la Israeli wakati wa Elisha. Kwanza, lilitangulia neno la Mungu kuashiria wakati wa Mungu wa kugeuza uteka wa Israeli na kisha, wakawepo wenye ukoma walioamua kuwaendea wale walioisababisha njaa hiyo. Kama wenye ukoma hawa wasingeliamua kuiendea kambi ya Washami, huenda muujiza huo usingelitokea. Hili nalisema kwa kuwa neno la Mungu linatuambia kuwa, Washami waliziachia haki za wana wa Israeli, pale Mungu alipotenda muujiza kupitia kishindo cha miguu ya wale wakoma wanne. Wakati mwingine limeuelezea muujiza huu kwa kutumia maneno yafuatayo; ‘Mungu alikichukua kishindo cha miguu ya wakoma wanne, akakiingiza kwenye amplifaya ya mbinguni na kukitupa katika spika  zilizofungwa katika kambi ya Washami!’

Mpendwa, naamini kuwa umepokea kitu kupitia fundisho hili, unachotakiwa kufanya, ni kuanza kuyaweka mafundisho haya katika vitendo, huku ukimwomba Roho wa Mungu kukuongoza. Kama ukiyatendea kazi mafundisho haya, naamini kuwa yatatoa mchango mkubwa kukufanya uishi sawasawa na vile Mungu alivyokukusudia. Wewe fanya yale yaliyo katika uwezo wako na Mungu atakitumia kishindo kitakachozaliwa na bidii yako kuwafanya maadui waziachilie haki zako! AMENI

Na Askofu Rodrick Mbwambo

Advertisements

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s