SADAKA IGUSAYO MOYO WA MUNGU!- Part I

“Utoaji ulio mwema ni mlango wa mafanikio na uponyaji wa kimwili, kiuchumi, na kiroho”

 Dhabihu igusayo moyo wa Mungu ni mlango wa baraka yako.

 Watu wengi wamekuwa wakitamani sana kubarikiwa na Mungu ila si wepesi kutaka kujua ni kwa namna gani au zipi ni kanuni za Mungu kwa mafanikio yao. Wengine kwa kutojua utaratibu wa Mungu wameamua hata kuvutwa na makanisa yanayotangaza kuwa wana ibada za kuombea watu Baraka na utajiri, ila Mungu yeye ni wa utaratibu na ukimgusa katika maeneo yake aliyoamuru yafanywe ni lazima utabarikiwa hata pasipo kuombewa na mitume na manabii, Ni muhimu sana kwa kila mtu kujifunza njia za Mungu na kujua ni kwa namna gani Mungu anawabarika watu wake.

 Nyakati za leo ni rahisi sana kukuta mtu anamdai Mungu mambo mengi na Baraka ila ukitazama maisha yake jinsi yalivyo hakuna utoaji na si mwepesi kufanya mambo yanayobariki moyo wa Mungu.

 Vipo vitu vinavyougusa moyo wa Mungu moja kwa moja, na vipo vitu vinafanyika na vimebeba sura nzuri ila si vyote vinavyougusa moyo wa Mungu. Katika sadaka kuna sadaka inayougusa moyo wa Mungu moja kwa moja na kuna dhabihu itolewayo katika madhabahu ya Mungu ila haina sifa ya kugusa moyo wa Mungu.

 Maandiko matakatifu yanatueleza kuwa utoaji ulio wa moyoni pasipo kushinikizwa ni sababu ya watu kubarikiwa na pia kukosa roho ya utoaji ubaki kuwa sababu ya watu kutobarikiwa.

 Kitabu cha Marko 5:30-32 “Mara Yesu, hali akifahamu nafsini mwake kwamba nguvu zimemtoka, akageuka kati ya mkutano, akasema, Ni nani aliyenigusa mavazi yangu? Wanafunzi wake wakamwambia, je! Wawaona makutano wanavyokusonga-songa, na wewe wasema ni nani aliyenigusa?” Watu wengine waliokuwa katika eneo lile walimpapasa Yesu ila hakuona mguso wowote, tofauti ni kwa Yule mama ambaye aligusa kwa mguso wa kudhamilia ambao uligusa moyo wa Mungu moja kwa moja na ukamfanya Mungu aingilie kati suala la Yule mama na kumponya.

 Si kila agusaye ana mguso wa kugusa moja kwa moja, kuna wengine wanapapasa tu ila hawagusi ila kuna wengine wanagusa kabisa mpaka wanatoa mshituko na muitikio wa tofauti kwa mguswaji, mpapasaji hana athari yoyote ile ila mgusaji anaathari kubwa sana, na mgusaji aweza patiwa mambo mengi sana kwa kule tu kugusa kwake.

 Marko 12:44-44 “Naye akaketi kulielekea sanduku la hazina, akatazama jinsi mkutano watiavyo mapesa katika sanduku. Matajiri wengi wakatia mengi. 42 Akaja mwanamke mmoja, mjane, maskini, akatia senti mbili, kiasi cha nusu pesa. 43 Akawaita wanafunzi wake, akawaambia, Amin, nawaambia, Huyu mjane maskini ametia zaidi kuliko wote wanaotia katika sanduku la hazina; 44 maana hao wote walitia baadhi ya mali iliyowazidi; bali huyu katika umaskini wake ametia vyote alivyokuwa navyo, ndiyo riziki yake yote pia.” Suala si kutoa ila suala ni kutoa dhabihu igusayo moyo wa Mungu kwa moja kwa moja, mtu unayeweza kumpima kwa viwango vyako vya kawaida kuwa yuko chini sana ndiye anaweza kuwa mtu afanyaye mambo yanayougusa moyo wa Mungu na kumfanya ajisikie vizuri.

 Aidha katika eneo la sadaka kuna watu wengi watatoa dhabihu zao kama wapapasaji, ila kuna mmoja atatoa dhabihu ambayo itaugusa moyo wa Mungu moja kwa moja na kumfanya Mungu asiwe na kimya na ashuke na kusababisha uponyaji wa maeneo yote kwa huyo mtu.

 Dhabihu itolewayo kwa moyo na kupenda mbele za Mungu uwa inasema na kumkumbusha Mungu mara zote kwa habari yetu na maisha yetu. Ni kweli kuwa maombi tuyaombayo uzungumza sana mbele za Mungu, ila dhabihu tuzitoazo kwa moyo zinapaza sauti njema sana mara zote mbele za Mungu huku zikimkumbusha Mungu kuwa imempasa hatubariki. Kweli kuna wakati aweza kaa kimya kabisa ila akitazama moyo wako wa kumtolea na kujitoa mbele zako ni lazima aitike na kufanya hata zaidi ya yale uyaombayo. Maandiko usema yeye ufanya zaidi ya yale tuyaombayo, ushawahi kujihoji ndani yako kuwa ni nini kinamshawishi afanye zaidi ya yale tuyatamkayo katika kuomba kwetu? Ni kweli kuwa kuna neema ila pia dhabihu uzitoazo zinadai ulinzi, uponyaji, utajiri na mali, na heshima mbele za Mungu kwa maisha yako.

 Mfano Kornelio sadaka alizokuwa akitoa kuwasaidia watu wengi wenye shida zilifika mbele za Mungu na kumkumbusha Mungu kuwa inapaswa afanye jambo kwa mtu wake Kornelio.

 Mwanzo 4:3-5 “Ikawa hatimaye Kaini akaleta mazao ya ardhi, sadaka kwa BWANA. 4 Habili naye akaleta wazao wa kwanza wa wanyama wake na sehemu zilizonona za wanyama, BWANA akamtakabali Habili na sadaka yake; 5 bali Kaini hakumtakabali wala sadaka yake, Kaini akagadhabika sana, uso wake ukakunjamana.” Suala si kutoa tu ila suala ni kutoa dhabihu yenye kupendeza mbele za Mungu. Kaini alikuwa anatoa tena sana ila tatizo alikuwa anatoa ziada za vile alivyonavyo na tena si vile vizuri, nadhani hakufahamu kuwa, “kipimo kile kile upimacho  ndicho utapimiwa”. Tofauti kwa Habili ni ya kuwa yeye alitoa kila kilicho bora mbele za Mungu, kile ambacho ni kizuri na chenye kupendeza ndicho alichochagua kumpa BWANA, maandiko yanaeleza kuwa Mungu aliikubali na kuipokea sadaka ya Habili na akaikataa sadaka ya Kaini.

 Kama si mtoaji au unatoa sadaka mbovu usijadili sana kwa nini mambo yako hayako vizuri. Jawabu unalo kuwa Mungu anakubali sana sadaka itolewayo kwa moyo na yenye kupendeza.

 Ni dhahiri kuwa kukosa roho ya utoaji na kuwa na tabia ya kumkadiria Mungu katika yale tuyatoayo ni sababu kubwa sana ya kutopokea baraka za Mungu.

 Watu wengi sana huwa na tabia njema ya kupenda kutoa kama ilivyokuwa kwa Kaini na Habili, ila katika kupenda huko wengi hutoa ziada ya vile walivyonavyo na wakati mwingine uchagua vitu ambavyo wanaona kwao vimepoteza thamani na ndivyo uvitoa kwa wengine. Kutoa ziada ya vitu ulivyonavyo na kuchagua kibovu katika vizuri kamwe hakuwezi kugusa moyo wa Mungu hata akageuka kama alivyogeuka kwa mama Yule aliyemgusa.

 Wengine usema kuwa mimi ninatoa sana ila naona kama sibarikiwi, jiulize kama unatoa kwa namna njema inayoweza kumgusa moyo wa Mungu.

 Nakumbuka siku moja nikiwa nimesafiri kuelekea mahali pa faragha kwa ajili ya maombi binafsi, nikiwa huko nilipata mguso wa tofauti sana wa kutoa mavazi yote ya thamani niliyokuwa nayo nimpatie mtu wa Mungu ambaye nilimkuta katika eneo hilo, suala hili lilikuwa gumu sana, haswa ukizingatia nami sikuwa na mavazi mazuri na ya kupendeza zaidi ya yale, nilishindana na ile sauti ya kufanya jambo hili, ila mwisho nikaona ni vyema niitii ile sauti na kutoa, haikuchukua muda mrefu kuna mama mmoja alikuja nyumbani na kuleta nguo nyingi zaidi ya zile nilizotoa na kupata viatu vizuri, kwangu hii ni uaminifu wa Mungu asemaye, “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa kifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakacho pimiwa”

 Dhabihu inayougusa moyo wa Mungu ni dhabihu inayouma katika moyo wa mwanadamu, yaani kutoa kitu ukipendacho na ukionacho kuwa bora kuliko vyote na wapenda kukitumia ila kwa ajili ya BWANA unaamua kutoa si jambo rahisi na kufanya hivyo ni ishara ya upendo sana kwa Mungu na huonyesha kuwa unamjua unayemtumikia. Yaani dhabihu ambayo yaweza kuugusa moyo wa Mungu hata wewe mwenyewe ukitoa unaona umetoa kitu mbele za BWANA na wakati mwingine hata nafsi yako yagoma kabisa kwa kuwa nafsi ina tabia ya kujipenda yenyewe.

 Mwanzo 22:2 “Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka, ukaende zako mpaka nchi ya Moria, ukamtoe sadaka ya kuteketezwa huko juu ya mlima mmojawapo nitakaokuambia.” Mungu anamtaka Ibrahimu atoe mtoto pekee aliye naye na ampendaye, si jambo rahisi kwa watu walio wengi kufanya hivi. Kwa mfano huu ni sawa na umeangaika kupanga miaka mingi sana halafu unapata tu nyumba yako mwenyewe ukasikia Mungu anakuambia nataka utoe hiyo nyumba uliyonayo umpatie mtu Fulani, au umetembea muda mrefu sana kwa miguu halafu umepata gari zuri la pekee na ulipendalo sana halafu ukasikia Mungu anakuambia toa hilo gari umpatie mtu Fulani si jambo rahisi.

 Kumtii Mungu ni jambo la msingi sana katika maisha yetu, akisema hata kama jambo ni gumu sana wewe tii tu kwa kuwa kamwe hafanyi jambo hili kumkomoa mwanadamu, ila yeye ufanya yote kwa utukufu wake na hili kumfanya mwanadamu afurahie wema wake. Kwa Ibrahimu ukiendelea kusoma utaona kuwa Mungu anamuambia kwa kuwa hakumzuilia mwanae pekee ni lazima ambariki.

 Sauti ya Mungu wakati mwingine inakuja kinyume na wewe ulivyo na waweza jiuliza mbona mimi nina vichache sana kwa nini amechagua mimi nitoe na si wale wenye navyo, ila jawabu ni kuwa Mungu amekuheshimu na amechagua kukubariki ndiyo maana amekuchagua wewe kati ya wengi.

 Kijana mmoja katika Mathayo 19:21-22 “Yesu akamwambia, Ukitaka kuwa mkamilifu, enenda ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, Nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo unifuate. 22 Yule kijana aliposikia neno lile, akaenda zake kwa huzuni; kwa sababu alikuwa na mali nyingi.” Kutoa na kuacha unavyomiliki kwa ajili ya Mungu ni suala la kujikana, kwa yule kijana alipoambiwa atoe alivyonavyo awape maskini aliondoka kwa kuhuzunika na akaona kuwa Mungu hamtakii mema kwa kumuagiza kutoa vitu vyake, ila laiti angejua siri iliyomkuta Ibrahimu na mjane wa Sarepta basi angetoa naye kwa kuwa angepata maradufu ya vile alivyokuwa navyo.

 Mfano mwingine ni kitabu cha 1 Wafalme 17:13-16 “Eliya akamwambia, Usiogope; enenda ukafanye kama ulivyosema; lakini unifanyie kwanza mkate mdogo ukaniletee; kisha ujifanyie nafsi yako na mwanao. 14 Kwa kuwa BWANA, Mungu wa Israeli, asema hivi, Lile pipa la unga halitapunguka, wala ile chupa ya mafuta haitaisha, hata siku ile BWANA atakapoleta mvua juu ya nchi. 15 Basi akaenda, akafanya kama alivyosema Eliya; na yeye mwenyewe, na Eliya, na nyumba yake, wakala siku nyingi. 16 Lile pipa la unga halikupunguka, wala ile chupa ya mafuta haikuisha, sawasawa na neno la BWANA alilonena kwa kinywa cha Eliya.”

 Kutoa si kuwa navyo vitu vingi sana ila hata vile vidogo ulivyonavyo Mungu anataka umtumikie navyo, mjane wa Sarepta alidhani kuwa kutoa kwa ajili ya mtumishi wa Mungu ni mpaka awe na vitu vingi sana ila sivyo Mungu anavyotaka kwa watu wake. Kutoa ni moy na wala si wingi wa vitu ulivyo navyo.

 Kutoa ni muhimu sana kwa kuwa ni kujiwekea hazina mbinguni ambapo nondo na kutu hawali, kama isemavyo katika Mathayo 6:19-21 “Msijiwekee hazina duniani, nondo na kutu viharibupo, na wevi huvunja na kuiba; 20 bali jiwekeeni hazina mbinguni, kusikoharibika kitu kwa nondo wala kutu, wala wevi hawavunji wala hawaibi; 21 kwa kuwa hazina yako ilipo, ndipo utakapokuwapo na moyo wako.”

 Kutoa mbele za Mungu unajiwekea hazina mbinguni mahali ambapo utakuwa ukiishi milele, mfano mmoja aliutoa mzee Moses Kulola kwa kusema “unakuta mtu anajisifu kuwa ana milioni kumi (10) benki ana mali nyingi sana ila hana hazina yoyote mbinguni na ni bahiri katika kutoa, ukimuuliza mtu huyu anaenda mbinguni, akifika bila shaka hata mahali pake kama atapata bahati hiyo hakutakuwa na hazina halizojiwekea.” Ukifahamu kuwa wewe duniani unapita kuelekea mbinguni weka juhudi katika siri hii pia. Kutoa katika hali ya kawaida ni kama kupoteza ila ni njia ya kujazwa vingi zaidi, ndiyo maana biblia usema kuwa “amfadhiliye/amsaidiaye maskini amkopesha BWANA”

Mungu anataka watu wake kujitoa kwa ajili ya kuifanya kazi ya injili na ana thamini sana wote wanaojitoa kwa ajili ya injili. Hagai 1, Na BWANA uumizwa sana na watu wanaothamini mambo ya nyumba zao na kusahau kazi ya nyumba ya BWANA.

Alisema nami mama yangu kuwa imenipasa kujisikia vibaya na kuona aibu sana pale napopendeza na kuonekana nipo vizuri sana huku wakitazama familia yangu na wazazi wangu hata kwa sehemu ndogo sana hatufananii, yaani nimewaacha mbali sana na hata aibu kutambulisha kuwa ni wazazi wangu. Lengo la nasaha hii kwangu ni kunihimiza kuwa nina wajibu wa kuwafanya wazazi wangu wang’ae na kupendeza hata watu wakitazama waone namna ninavyo jali.

Itaendelea sehemu ya pili

Na Mwl Kelvin Kitaso

 

 

10 thoughts on “SADAKA IGUSAYO MOYO WA MUNGU!- Part I

 1. Thanks for the sweet Word jaman,mana unasoma mpka mwili unasisimka,Mungu awabariki mno mmefungua kitu na kuniongezea kwangu,kwakweli mnafanyika baraka bila nyinyi kujua pia,asanteni sana kaka @Kalvin na @Mabinza LS upo vizuri sana,stay blessd

 2. Ubarikiwe mtu wa Mungu.nimebarikiwa na somo lako.leo naenda kutoa nguo zangu nilizozipenda na kuzileta kanisani kiukweli nilikuwa nssita sita kama sauti uloongelea hapo juu licha yaukweli kwamba niliwahi kupata somo na kunfundishika kuwa ile nguo ulonayo ambayo umekaa zaidi ya mwezi mmoja hujaivaa hiyo si nguo yako igawe kwa wasio na nguo lakini nimekuwa nikiwa mzito na nina nguo za namna hyo nyingi, ila umenitia nguvu.Mungu akutie nguvu.

 3. shalom mimi ni muchungaji nimefurahiya mafundisho haya basi mubarikiwe na Mungu wetu asante.

 4. shalo0m, mpendwa kwa kutoa elimu ya imani juu ya watu ambao wnajaribu kumjaribu Mungu na kunung’unika kuwa Mungu hawaoni lakini ni kuwa IMANIkwao imepungua.
  ubarikiweMTumishi.

 5. Asante kwa maneno yote hakika nimeguswa sana kama kijana mungu hawabariki wote naningependa kuwasiliana nanyi ili niweze kupata masomo zaidi kwani nahisi kubarikiwa nakufanikiwa sana kutokana na somo hili

 6. Mpendwa Kelvin, nimevutiwa na mafundisho yako, kiasi kwamba yamenivuta nitake kuchangia mambo kadhaa na kujifunza zaidi juu ya kubarikiwa kimwili na kiroho.

  Umegusia mambo kadhaa yafaayo mtu wa Mungu ayafanye ili kupata baraka za mali na vitu, kimsingi sipingani nawe. Mifano na mistari uliyoinukuu ni kweli ndivyo inavosomeka na kujieleza, lakini niseme tu kwamba, yule mama mwenye kutokwa damu si kwmba alifanya mguso fulani tofauti ambao ulimfanya Bwana Yesu kuuona uhitaji wake, kama ulivyosema wewe nikirejea ulivyosema hapa kwamba, “Watu wengine waliokuwa katika eneo lile walimpapasa Yesu ila hakuona mguso wowote, tofauti ni kwa Yule mama ambaye aligusa kwa mguso wa kudhamilia ambao uligusa moyo wa Mungu moja kwa moja na ukamfanya Mungu aingilie kati suala la Yule mama na kumponya.” Na pia si kwamba matoleo na sadaka pekee ndizo zinasababisha mtu kubarikiwa! Nikiifuatia sana hiyo habari ya huyo mama mwenye kutokwa damu, ninachokiona hapo ni IMANI aliyokuwa nayo moyoni mwake, maana ukiuangalia ule mstari wa 28 katika sura hiyohiyo ya 5, inaeleza wazi kuwa, “28maana alisema moyoni mwake, “Kama nikiweza kuligusa vazi Lake tu, nitapona.” Kwa hiyo, hapo naona kuwa kilichomshtua Yesu hata kuona kuwa huo ulikuwa mguso wa kipekee ni ile Imani iliyokuwa ndani ya yule mwanamke, na wala si mguso kama mguso kwenye vazi la Yesu pekee.

  Kule kukusudia moyoni mwake na kuamini kuwa kukugusa tu vazi lile kungesababisha uponyaji, ilikuwa ni IMANI na kule kuchukua hatua ya kwenda hadi kuligusa pindo la vazi lile ilikuwa ni KITENDO; lakini tunajua kwamba Tendo huthibitisha kiasi cha imani ya mtu, imani na matendo vyote kwa pamoja ndivyo vilivyompa haki ya kupata ombi lake, Imani na Tendo kwa pamoja husababisha NGUVU ya msababishaji ASABABISHE! Ndiyo maana katika mstari wa 34 kwenye sura hiyohiyo ya 5 panasomeka hivi, “34Yesu akamwambia, ‘‘Binti, imani yako imekuponya. Nenda kwa amani, upone kabisa ugonjwa wako.”

  Katika utoaji wa Yule mama masikini katika ile Marko 12:44 hiyo ni sawa na kile alichokifanya Ibrahimu, Mwanzo 22:2 “Akasema, Umchukue mwanao, mwana wako wa pekee, umpendaye, Isaka,……….” Kwa maana hiyo, ni kwamba, tunathibitisha Imani yetu kwa Mungu kwa kufanya matendo ya utoaji ama kujitoa katika hali yenye uthabiti, na uthaminifu mkuu wa moyo na upendo wa hali ya juu, yaani huko ndiko kuthibitisha Imani kupitia matendo, ukamilifu huo ndiyo unaompa mwombaji haki ya kupata mahitaji yake. ‘Neno vyote ulivyonavyo’ mimi binafsi naweza kusema kuwa, huko ni kumaanisha ‘utayari na ukamilifu wa imani ya mhitaji’. Yaani kuwa tayari hata kutoa chote ama chote ulicho nacho bila majuto! Ndiyo maana Yule kijana tajiri, alipoambiwa kauuze vyote ulivyonavyo kisha uje unifuuate, akaenda zake kwa huzuni! Kwa nini aliondoka kwa huzuni? Ni kwa sababu moja tu kwamba, ‘ALIIPENDA MALI YAKE ZAIDI NA HIVYO KUKOSA “TENDO” AMBALO NI LA UTOAJI KWA UPENDO MKUU!’ Kwa kifupi mtu huyu alikuwa na IMANI isiyo na MATENDO. Imani isiyo na Matendo ‘IMEKUFA’ ili iwe Imani hai lazima iwe na matendo. Yesu akamwambia akauze vyote alivyo navyo kisha aje amfuate. Naweza kusema, ‘ni kama’ Yesu alimwambia kuwa, Imani yako nimeiona lakini imekufa, na mimi sifuatani na wafu, kijana, fufuka ki imani kwanza, ndipo unifuate (uwe na Imani hai kwanza – Yakobo 2:18-19).! Neno linasema “…….mwenye kusitsita sia haja naye”. Niwaambie kwamba, Yesu kwa uvumilivu anaweza kukaa karibu na wenye imani haba, lakini si wenye imani Mfu!

  Kwa Ibrahim kumtoa Isaka mwanaye wa pekee, tendo hilo nalo lilikuwa si la kijasiri tu kwa maana ya ujasiri,au kutoa kitu bora kuliko vyote. Kilichokuwa kitu cha ‘PEKEE’ ndani yake ni ile IMANI aliyokuwa nayo juu ya Mungu mkuu, na kiwango cha Imani aliyokuwa nayo Ibrahimu ndiyo kilichofanya awe Rafiki wa Mungu, na Mungu akamuona Ibrahim kuwa ni Rafiki yake (Yakobo 2:23). Naweza kusema kwamba, Ibrahimu alikuwa ni mtu wa imani iliyokamilika tangu mwanzo, na ukamilifu wa Imani yake ulithibitika kwa ‘KITENDO’ cha kumtoa Mwanaye wa ‘PEKEE’ hicho ndicho kilichomfanya aitwe Baba wa Imani’ Tendo la kumtoa mwanaye wa ‘PEKEE’ ndilo tendo pekee lililokuwa kubwa la kuthibitisha imani yake, tendo ambalo na Mungu alilifanya, Neno linasema, “……Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda Ulimwengu hata akamtoa Mwanaye wa ‘PEKEE’……”. Kwa hiyo, Imani ya Ibrahimu haingefanya lolote bila matendo, maana Mtu hupata haki kwa Imani, na imani huthibitika kwa matendo (Yakobo 2:21). Na kwa hiyo Ibrahimu akawa mtu mkamilifu kwa Imani, hata kufanya mataifa yote yabarikiwe ama yalaaniwe kupitia yeye!

  Sipingani nawe kuwa watu wasitoe matoleo, lakini kwanza wajue namna ya kutoa na kitu ambacho ni lazima kiambatane sawa kwa sawa na kutoa huko, wala si kuwa Mungu hupendezwa kwa uthamani, ukubwa, aina za sadaka zitolewazo ama kwa namna inavyomgusa mtoaji mwenyewe sadaka anayokwenda kuitoa, kwa mawazo kuwa ndiyo itasababisha mtu kubarikiwa ama kupata majibu ya mahitaji yake! Lakini kujulikane kwanza kwa mtoaji kuwa, kumtolea Mungu ni nini? Yaani kutoa huko ndiko kufanya nini, na unatoa kitu gani? Wala kutoa si kwa kuwa unatoa kitu kitakachokufanya ujute, ama uumie moyoni mwako, ama kutoa kitu chako cha thamani sana kulikoni ulivyonavyo, ama kutoa Akiba ama hazina yako yote upeleke kanisani huku moyo haujapenda.

  Unatakiwa kujua kuwa kutoa ni kuthibitisha imani yako kwa vitendo, ndiyo maana utoavyo ndivyo ubarikiwavyo, kwa maana nyingine ndiyo kusema, uthaminivu, upendo na hamu ya utoaji na ule utoaji wenyewe ndiyo imani yenyewe!. Wingi, ukubwa ama thamani ya vitu uvitoavyo visipofanyika kwa UPENDO MKUU, kamwe si kipimo cha kiwango cha imani yako! Cha Musingi unatakiwa kutoa kwa UPENDO mkuu kwa Mungu na kutoa kwa Mungu kuliko bora ni kuwapa watu! Luka 6:38 inasema, “38Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa. Kipimo cha kujaa na kushindiliwa na kusukwasukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho, ndicho mtakachopimiwa.” Na Dhabihu aipendayo Mungu ni ile iliyotajwa katika Waebrania 13:16 ambayo inasema, “16Msiache kutenda mema na kushirikiana vile mlivyo navyo, kwa kuwa dhabihu kama hizo ndizo zinazompendeza Mungu”. Ndiyo maana atakachokuuliza wakati atakapokuwa akiwabagua kondoo na mbuzi wa kiroho, atataka tu kujua ulitoa ama hukutoa kwa watu, kama una nafasi isome ile Mathayo 25:34-46

  Mungu ni Baba yetu, hayupo baba mwema mwenyekufurahia kupokea matoleo toka kwa watoto wake waliokuja kumpa matoleo kisha, wakarudi makwao kwa huzuni, wengine kwenda kulala njaa ama wakawa hawana hata nauri ya kuwarudisha makwao, ati wamempa baba yao vyote walivyo navyo, huo ni ujinga! Hayupo baba wa namna hiyo mwenye kufurahia wanawe wanaompa matoleo yenye kuwahuzunisha ama kujutia; baba wa watoto kama hao, akiwa mwema atawaambia njia na namna stahiki ya kutoa matoleo, la hawawezi kufuata ushauri wake basi atawambia waache wala wasije kumtolea, na huo ndiyo utakuwa mwisho wa Baraka kwao! Na hicho ndicho kilichomtokea kaini, Kaini sadaka yake si kwamba haikuwa vitu vinavyofaa kwa kutolewa sadaka, maana hata Mafarisayo, Yesu aliwambia kuwa, kutoa mbogamboga kama matoleo si vibaya ila walitakiwa kufanya hivyo kwa upendo. Kwa hiyo Kaini hakuujua wakati na aina ya sadaka na namna impasayo kuitoa sadaka, kwa maana hiyo alitoa matoleo yake ‘VIBAYA’ kwa sababu inaonyesha wazi kuwa yeye hakuwa na ufunuo wa Mungu ndani yake na kabisa hakuutaka, na hakuutaka kwakuwa hakuwa mwana wa Mungu!

  Ziko SABABU KUU mbili zinazofanya mtu asipate Baraka za kimwili na Kiroho, Moja ni IMANI MFU (Imani isiyo na matendo) lakini sababu ya pili, ambayo watu hawaiangalii na mara nyingi nasikitika hawaizungumzii au kuifundisha sana ni, KUWAHESHIMU WAZAZI. Huwezi KAMWE kubarikiwa kama huna heshima, adabu ama utii kwa wazazi wako, hata kama unaimani ya kufanya milima ing’oke! Maana hiyo ni ‘zawadi’ waliyopewa wazazi kwa ahadi, tunajua kuwa Mungu Neno lake hulichunguza ili apate kulitimiza, kwa kujidanganya kuwa unaombewa ili upate ‘HERI’ wakati haupo sawa kwa wazazi wako ni bure, maana maombi hujibiwa na Mungu yakiwa yamezingatia Neno lake lote!. Vilevile uelewe kwamba, Kuwaheshimu huko si kwa maneno (Imani) pekee, ni lazima kuandamane na MATOLEO (Matendo) kiasi cha kuwafanya wakutamkie neno la Baraka. Ipo mifano mingi sana katika Biblia inayozungumzia jambo hilo yaani wazazi kuwaita watoto wao na kuwatamkia ‘MANENO’ la Baraka!, kwa sasa sitaitaja.

  (Ufahamu ni chembe ya Uhai!)

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s