HEKIMA YA MFINYANZI!

Yeremia ni mmoja wa manabii wakubwa tunaokutana nao katika Biblia. Aliishi katika karne ya sita KK. Wakati wa uhai wake, taifa la Israeli lilipokuwa limegawanyika kutokana na kosa lililofanywa na Rehoboamu. Katika kipindi cha unabii wake, upande wa kaskazini uliokuwa unajulikana kama Israeli, ulikuwa umechukuliwa mateka na kupelekwa katika nchi ya Ashuru. Ashuru leo hii ni nchi inayojulikana kama Syria.

Baada ya Israeli kuchukuliwa utumwani, Mungu alimwinua nabii Yeremia ili kulionya taifa ya Yuda lililokuwa limebakia katika nchi ya ahadi, kuhusu hukumu inayolingojea pale litakapokataa kutubu. Maandiko tutakayojifunza leo, ni sehemu ya ujumbe ambao Mungu alimpatia Yeremia kuwapelekea watu wa Yuda. Kwa kuwa neno la Mungu ni la siku zote, kupitia ujumbe huu wa Yeremia kwa Yuda, kanisa la kizazi cha leo linaweza kujengwa, kuimarishwa, kuuelewa moyo wa Mungu na kupokea tumaini jipya katika kumwishia Mungu.

MUNGU WA KWELI ANAZUNGUMZA
Ndipo BWANA akamwambia Yeremia…(Yeremia 18:1). Siku moja nilipokuwa nikiwaeleza watu habari njema za Kristo, mtu mmoja alinijia na kuniambia: “Waislamu wanasema kuwa mungu wao ndiye wa kweli, Wabuda nao wanasema Buda ndiye wa kweli na Wahindu nao wanasema miungu yao ndiyo sahihi. Leo hii wewe nawe unasema kuwa Mungu wa Biblia ndiye wa kweli, sasa ni yupi anayesema ukweli?” Nilichomweleza ndugu huyu ni kuwa, mimi simwabudu Mungu wa historia. Mungu wa historia ni yule aliyetenda na kusema zamani, ila sasa hatendi wala kusema! Na ieleweke wazi kuwa Mungu anayetenda pia anazungumza. Mimi nimemwamini Mungu kwa kuwa anazungumza na mimi kila iitwapo leo. Mara zote Mungu wa kweli ni yule anayeendelea kuzungumza na watu wake kwa sauti ya wazi.

Kama mtu anataka kumjua Mungu wa kweli, anachotakiwa ni kupiga magoti na kuomba ombi lifuatalo: “Muumba wa mbingu na nchi, nimesikia yale yanayozungumzwa na Waislamu, Wabuda, Wahindu na Wakristo kukuhusu wewe. Ni wazi wako walio sahihi katika hili na wako waliopotoka, kwa kuwa haiwezekani wote wawe sahihi. Naomba uzungumze nami na kunionyesha upande ulio sahihi.” Mungu aliye hai ni Baba anayependa kuongea na watoto wake wa kizazi cha leo, kama alivyofanya kwa Yeremia.

MUNGU HUENDELEA KUZUNGUMZA
“…Ondoka shuka mpaka nyumbani kwa mfinyanzi, nami nitaongea na huko nitaongea nawe” (Yeremia 18:2)NLT. Mungu anapozungumza mara ya kwanza na mtu, hufanya hivyo kwa neema. Kutokana na ukweli huu, anaweza kuzungumza na mwuaji kama Sauli na anaweza kusema na mtu mwema kama Kornelio.
Ili kuisikia sauti ya Mungu kwa mara ya kwanza, sio lazima mtu awe na imani au moyo mkamilifu. Kinachohitajika katika hili, ni neema na mapenzi ya Mungu ya kutaka kuzungumza na mtu. Hata hivyo, baada ya mtu kuisikia sauti ya Mungu kwa neema, ni lazima mahusiano yake na Mungu yaimarike, ili kumwezesha kuendelea kuisikia sauti ya Mungu.

Huu ndio ukweli tunaokutana nao, pale tunapofuatilia maneno yanayoongoza kipengele hiki. Katika andiko hili, Mungu alimwagiza Yeremia kwenda nyumbani kwa Mfinyanzi na akaahidi kuzungumza naye akiwa huko. Baada ya Yeremia kufika nyumbani kwa mfinyanzi kama alivyokuwa ameagizwa, kwa mara nyingine Mungu aliongea naye. Ili Mungu aendelee kuongea nawe, ni lazima utii kile alichokuambia mara ya kwanza. Kama Yeremia asingelitii na kushuka nyumbani mwa mfinyanzi, ni wazi Mungu hangemwambia maneno yaliyoandikwa katika mstari wa tano na kuendelea.

Leo ndani ya kanisa, kuna watu wengi sana waliovunjika mioyo kutokana na kutoendelea kusikia sauti ya Mungu. Mungu aliongea nao zamani, ila sasa haendelei kuongea nao. Hali kama hii inasababishwa na kitu gani. Je, Mungu amebadilika? Jibu ni hapana kwa kuwa neno la Mungu linasema wazi kuwa Mungu ni yeye yule jana, leo na hata milele. Ni Mungu asiyebadilika. Ukichunguza maisha ya wokovu wa watu hawa, utaona kuwa kuna wakati ambapo walizembea katika kutendea kazi yale Mungu aliyoongea nao wakati wa kwanza.

PICHA NDANI YA MOYO WA MFINYANZI
“…Hivyo nikafanya kama nilivyoambiwa, nikamkuta mfinyanzi akifanya kazi yake kwa kutumia gurudumu” (Yeremia 18:3). Baada ya Yeremia kuwasili katika nyumba ya mfinyanzi, alimkuta akifanya kazi yake kwa gurudumu. Baada ya kipindi fulani cha kumtazama mfinyanzi akifanya kazi yake, Yeremia alishangaa pale mfinyanzi alipogeuza udongo wa mfinyanzi uliokuwa mikononi mwake, kuwa chombo kizuri na cha kupendeza.
Wakati Yeremia akishangaa chombo hicho, mambo yalikuwa tofauti kwa mfinyanzi. Kwake chombo hicho kilikuwa matokeo ya picha iliyokuwa moyoni mwake. Kabla ya kutengeneza chombo hicho kipawa kutoka kwa Mungu kilikuwa kimeumba picha hiyo, ndani ya moyo wake.

Hapa ndipo tunapokutana na ukweli wa kwanza kuhusiana na hekima ya mfinyanzi. Kila mara hufanya kazi kwa kuongozwa na picha iliyoumbika ndani ya moyo wake. Kwa maneno mengine, kabla ya kazi ya kutengeneza chombo kuanza, iliumbika picha ya chombo hicho ndani ya moyo wake. Wakati mwingine zoezi la kuumba picha ndani ya moyo wa mtu ni gumu, kuliko kutendea kazi picha hiyo.

Katika hili wako wanaoweza kuinuka na kusema, “kwangu kuumba picha ni jambo rahisi, kuliko kutendea kazi picha hiyo!” Maneno haya yanaweza kuwa ya kweli pale mtu anapoumba picha kwa kutumia akili zake. Hata hivyo iko tofauti kati ya picha zinazoumbwa na akili za kibinadamu na picha zinazotokana na wazo la Mungu. Picha zinazoinua viwango vya maisha ya mwanadamu, ni zile zinazotokana na Mungu.

Ili mtu awe na picha zinazotokana na wazo la Mungu, ni lazima awe na uhusiano mzuri na Mungu. Ni katika kushirikiana na Mungu katika maombi, kusoma neno lake na kutumika, ndipo Mungu anapoweka mionjo ya maisha ya mtu ya baadaye ndani ya moyo wa mtu. Mara zote mtu anapokuwa na ushirika mzuri na Mungu, ndani yake kutakuwa na picha njema zinazohusu maisha yake.

Waamini wengi wanaishi nje ya duara la mapenzi ya Mungu kutokana na kutokuwa na picha ndani yao zinazotokana na kusikia kutoka kwa Mungu. Kumbuka kuwa Biblia inasema wazi kuwa imani chanzo chake ni kusikia neno la Kristo. Kutokana na ukweli huu, mwamini anatakiwa kuimarisha ushirika wake na Mungu ili kuruhusu kuchipua ndani yake picha zinazohusu maisha yake ya baadaye.

MFINYANZI HUIKAGUA KAZI YAKE
“Lakini kama chombo alichokuwa akikitengeneza hakikutokea kama alivyotarajia…” (Yeremia 18:4). Wakati Yeremia alipokuwa akishangaa uzuri wa chombo mikononi mwa mfinyanzi, ghafla alimwona mfinyanzi akikizungusha chombo chake taratibu kwa lengo la kukikagua. Huu ni ukweli wa pili unaohusu hekima ya mfinyanzi, huchunguza kazi ya mikono yake. Mtu yeyote anayehitaji kufanikiwa katika maisha yake ya sasa na yale yajayo, ni lazima ajenge utamaduni wa kukagua kazi yake.

Mara zote uhusiano kati ya chombo kilichotengenezwa na mfinyanzi na picha iliyoumbika moyoni mwake, ndio unaomwongoza mfinyanzi wakati wa kuikagua kazi yake. Kama umbile la chombo linapingana na picha iliyoko moyoni mwake, kamwe mfinyanzi hatavumilia kuendelea kuwa na chombo hicho. Maisha ya watu wengi yamekuwa ya kudharaulika, kutokana na kutokuwa na utamaduni wa kukagua shughuli wanazozifanya. Ukaguzi ndio unaomhakikishia mwamini kuhusu usahihi wa utendaji wake na ikiwa anafanya kwa faida au hasara.

MFINYANZI HUZINGATIA UBORA
“…Alikiponda na kukifanya kuwa udongo tena” (Yeremia 18:4). Baada ya mfinyanzi kumaliza kukagua chombo chake kilichoonekana kuwa waridi machoni mwa Yeremia, mfinyanzi alifanya jambo lililoonekana kuumiza moyo wa Yeremia. Alikiponda kile chombo na kukirudisha katika hali yake ya awali ya udongo!

Kwa nini afanye hivyo baada ya kufanya kazi kubwa na ya kuchosha? Yawezekana hili ndilo lililousonga moyo wa Yeremia. Kwa mfinyanzi kile kilichomshangaza Yeremia, kilikuwa sehemu ya maono na utumishi wake wa kila siku. Aliharibu chombo alichokitengeneza ili kurekebisha kasoro aliyoigundua ndani ya chombo hicho.
Ingawa kasoro hiyo ilikuwa ndogo kiasi cha kutoonekana machoni mwa Yeremia, alitambua jinsi madhara yake yatakavyokuwa makubwa pale kitakapoingia sokoni. Kikiingia sokoni na kasoro hiyo, kitaharibu soko lake, jina lake na maisha yake. Mara zote hekima ya mfinyanzi, inafanya mambo kwa kuzingatia ubora.

Wakati mwingine katika maisha haya, wako watu watakaokushambulia na kuwa kinyume na nawe, kwa vile tu hawaelewi umuhimu wa kufanya mambo kwa kuzingatia ubora. Mungu tunayemwabudu na kumtumikia, ni Mungu anayefanya mambo kwa kuzingatia ubora. Alifanya hivyo wakati wa uumbaji, wakati wa kutengeneza safina na wakati wa kutengeneza hema ya kukutania jangwani.

Mwalimu mmoja alisema wazi kuwa, hakuna mwanadamu anayeishi leo, anayeweza kutengeneza yale yaliyotengenezwa na Bezaleli, kwa kutumia vifaa alivyokuwa navyo!

Tatizo kubwa linalodidimiza maisha ya kiroho na kimwili ya waamini, ni tabia ya kufanya mambo pasipo kuzingatia ubora. Ndiyo wanakuwa na picha zinazotokana na wazo la Mungu, ila wanafanya mambo kwa kulipua. Kama waamini watageuka na kuamua kufanya mambo kwa kuzingatia ubora, ni wazi wangekuwa vichwa badala ya kuwa mkia!

Ni huzuni kuiona familia ya Mungu ikiwa mkia huku familia za Molecki na Dargoni zikiwa vichwa! Ili kuibadili hali hii, amua kufanya mambo kwa kuzingatia ubora katika, kufanya kazi ya Mungu, katika kula, kuvaa, kazi yako, masomo na katika mahusiano na watu wengine.

MFINYANZI HAOGOPI KUANZA TENA
“…Kisha alianza kukifanyiza tena” (Yeremia 18:4). Baada ya kukiponda chombo chake na kukirudisha katika hali yake ya awali ya udongo, huenda Yeremia alitarajia kumwona mfinyanzi akiwa amekata tamaa ya kutoendelea na kazi. La kushangaza ni kuwa mfinyanzi alifanya kinyume, badala ya kutundika kinubi chake kama walivyofanya wana wa Israeli wakiwa Babeli, alizungusha gurudumu lake na kuanza kufinyanga chombo kingine!

Watu wengi wataingia jehanamu na wengine wataishia kuishi maisha tofauti na yale waliyokusudiwa kuyaishi, kutokana na kuogopa kuanza upya, pale mambo yanapokuwa yameharibika. Kama wezi wamevunja na kuifilisi biashara yako, anza upya, chuo kimekutupa nje wakati wa kuchukua shahada ya kwanza, anza tena. Uchumba wa kwanza umevunjika, mwangalie Mungu na uanze tena. Hata kama umeanguka katika wokovu, anza tena!

Ndio mfinyanzi alikuwa amepoteza muda mwingi kutengeneza chombo chake, ila hekima yake iliishinda roho ya kukata tamaa. Kupitia hekima yake ya kutoogopa kuanza upya, aliukamata udongo na kulizungusha gurudumu ili kutengeneza chombo kingine kisicho na hitilafu.

Kama unahitaji kuingia na kuishi katika mduara wa maisha ya ushindi, ondoa neno la kukata tamaa katika ubongo wako. Kama maisha yako ya kiroho na kimwili yatashindwa kuzaa tunda linalofanana na picha iliyojengeka ndani yako, anza tena. Amen.

Advertisements

3 thoughts on “HEKIMA YA MFINYANZI!

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s