MASHAKA NA UOGA NI VIKWAZO VYA KUKUFIKISHA MAHALI UNAPOPASWA KUFIKA.

woga

Usipoweza kujikana na kuthubutu, hutoweza kamilisha mambo makubwa” C,S Lewis

Watu wengi wamekuwa wanatamani sana kuwa na maisha yaliyo bora na kuwa na hali njema kiroho lakini miongoni mwa vikwazo vya kuwa hivyo licha ya kile cha watu wa karibu yao/marafiki, changamoto nyingine ni uoga/mashaka.  

Uoga ni ile hali ya kusitasita kuthubutu kufanya mambo na kuweka mashaka kama matokeo yatarajiwayo yanaweza kutokea. Mara zote hali hii uambatana na maneno kama;

 • Sidhani.

 • Siwezi

 • Sijui.

 • Labda.

 • Nitajaribu badala ya nitafanya.

Kibiblia hii ni hali ya kukosa uhakika na ubayana juu ya mambo yatarajiwayo na mambo yasiyoonekana; yaani ni kukosa imani. Na kitendo hiki kinamfanya mtu wa Mungu kuishi maisha yanayomfanya Mungu asiwe na furaha kwa kuwa haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo kuwa na imani.

Waebrania 10:38-39 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. 39 Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.”

Waebrania 10:6a “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza;……..”

                Uoga ni kitendo cha kupungukiwa imani kwa kuingiwa na wasiwasi.

Marko 4:40 “Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?”

Yesu anaweka uwiano wa maneno mawili ya ‘kuwa waoga’ na ‘kukosa imani’ Kwa kumaanisha kuwa wanafunzi waliogopa kwa kuwa hawakuwa na imani bado na kama wasingekuwa waoga ni matokeo ya kuwa na imani na kama wangekuwa hivyo Yesu angeweza kunena nao na kusema “hamkuwa waoga, mmekuwa na imani sasa”.

Wakati mmoja nikiwa natafakari neno pamoja na rafiki yangu tukafika mahali pa kutafakari ‘flexibility’ (kubadilika) kwa Mungu na kutafakari kuwa Mungu ni Mungu anayeweza kubadilika na uwezo wa kumfanya asibadilike (static) umewekwa mikononi mwetu wenyewe. Jinsi tunavyoweza enenda ndivyo tunaweza kumfanya Mungu atende yale aliyoahidi au asitende. Wana wa Israeli walipotolewa na Mungu katika nchi ya utumwa (Misri) waliambiwa wanaelekea Kanani (nchi ya ahadi) ila si kwamba  Mungu akupenda wao wafike Kanani bali ni wao wenyewe ndio waliuokuwa sababu ya kutofika kwao.

Waebrania 3:11-19 “ Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu.

12 Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.

16 Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?

17 Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?

18 Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi?

19 Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.”

Kuna jambo Mungu anaapa tena kwa hasira na sababu kuu inayomfanya aape kwa hasira ni kukosa imani/uoga/kusitasita kwa watu wake hii ni kwa sababu alisema watu wake wanapaswa kuishi kwa imani na wakisitasita moyo wake hauna furaha nao.  

Watu wengi wamekuwa wakijifariji kuwa Mungu ameniahidia ni lazima itatimia ila ukweli ni kwamba ukiweka uoga na mashaka kamwe mambo hayo hayatatimia kamwe na itakuwa historia tu kama ilivyo historia ya wana wa Israeli kuwa waliahidiwa lakini hawakuweza kuingia Kanani isipokuwa uzao wao pamoja na Joshua na Kalebu.

Mpaka mtu anaogopa zipo sababu zinazomsababisha akaogopa na pengine zikawa ni sababu nzito, ngumu na za msingi sana za kumfanya mtu aogope, mara nyingi sababu hizo uwa kwa namna ya mazingira yanayomzunguka mtu kwa kutokuwa rafiki na yale ayatamaniyo, au jamii inayomzunguka si rafiki na hali aiendeayo na pengine unenewa maneno mabaya na kusikia mambo mengi ambayo yanamfanya yeye aogope.

maneno ya wanadamu mara nyingi uleta uoga nakubomoa imani ila neno la Mungu uimarisha imani na kumpa mtu ujasiri”

Marko 4:35-40 “Siku ile kulipokuwa jioni, akaawaambia na tuvuke mpaka ng’ambo. 36 Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwa pamoja naye. 37 Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. 38 Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? 39 Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. 40 Akawaambia, mbona mmekuwa waoga? Hamna imani

Wanafunzi walizungukwa na mazingira yasiyotabiri kama watafika ng’ambo lakini wakasahau kuwa utendaji wa Mungu haufungwi na mazingira ambayo wapo.

Kumbukumbu la Torati 7:17-23 “Nawe kama ukisema moyoni mwako,mataifa haya ni mengi kunipita mimi;nitawatoaje katika miliki yao? 18 Usiwaogope; kumbuka sana Bwana Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote; 19 uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyooka, aliokutolea nje BWANA, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya BWANA, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa. 20 Tena BWANA, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.  21 Usiingie na kicho kwa sababu yao;kwa kuwa BWANA, Mungu wakoyu katikati yako, Mungu mkuu mwenye utiisho. 22 Naye BWANA, Mungu wako, atayatupia nje mataifa yale mbele yako kidogo kidogo; haikupasi kuwaangamiza kwa mara moja, wasije wakaongezeka kwako wanyama wa mwitu. 23 Ila BWANA, Mungu wako, atawatoambele yako, atawatia mashaka, mashaka makuu, hata waishe kuangamizwa”

Unaweza ukaona vita ni vikubwa sana kuliko vile ulivyo na wanaosimama kinyume nawe ni wengi kuliko ulivyo na hali hii ikatia uoga.

2 Wafalme 6:15,16 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake Yule mtu wa Mungu alipoondoka na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyaje? 16 Akamwambia, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”

Sababu ya kutokuogopa ni kuu sana ya zaidi ya sababu za kuogopesha, ikiwa Mungu yu upande wako uwezekano wa kushindwa ni asilimia 0% na kushinda ni 100%.

Hesabu 13:30-33 “Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. 31 Bali wale waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi, 32 Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya nchi waliyoipeleleza, wakasema, ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. 33 Kisha huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”

Ni kweli uhalisia na muonekano wa adui zao ilikuwa ni sababu kubwa sana ya kuwasababisha kuogopa ila ule uzoefu wao waliowahi kumwona Mungu akifanya kazi toka Misri ilikuwa ni sababu kuu ya kuwafanya wasioogope, japo kuogopa kwa wale wengine kuliwasababisha wajione kama mapanzi na ndivyo walivyokuwa kwa kuwa ajionavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo. Uonaji wa Mungu uko tofauti kwa kuwa Yeye aliwatazama kama mashujaa ila tatizo lilikuwa ni katika wao wenyewe kujiona kama mapanzi.

1 Samweli 17:8-11 “Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupinga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu akanishukie mimi. 9 Kama akiweza kupigana na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; name nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. 10 Yule Mfilisti akasema, nipeni mtu tupigane. 11 Basi Sauli na Israeli waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”

Pindi tu unapoingiwa na uoga ndipo unatoa mwanya wa kushindwa kwako. Ni vyema ukafahamu kuwa hakuna muoga ambaye alishawahi kufanikiwa katika maisha haya kwa kuwa waoga wote uogopa kuthubutu kufanya mambo kwa kuhofia kushindwa ila waliowahi kushinda ni watu waliokubali kufanya mambo pasipo kuogopa kushindwa na hata waliposhidwa walitumia kushindwa kwao kama fursa ya kuwapeleka katika hatua nyingine ya juu sana.

Wengine uogopa kufanya mambo kwa sababu tu walishawahi kuwaona watu wengine wanashindwa katika mambo hayo na katika fahamu zao wamekubaliana na mambo hayo, hii ni sawa na yale mawazo ya wale wapelelezi walioogopa kabla hawajaenda kutamalaki kwa wanefili. Waoga mara nyingi usema nitajaribu labda nitashinda lakini washindi mara zote usema nitafanya na nitashinda bila shaka kama walivyosema Joshua na Kalebu kuwa “tupande tukatamalaki kwa kuwa tutashinda bila shaka” lakini muoga ni rahisi kusema “siendi” au akasema “twendeni labda twaweza kushinda na sisi.”

Tofauti kati ya muoga na mtu jasiri ipo katika mitazamo yao juu ya mambo yanayowazunguka, katika jambo moja jasiri atafanya na kushinda ila mtu muoga ataogopa na akija ona matokeo ya mwenzie ubaki kutaamaki na kumwona menzie kuwa ni mtu wa tofauti sana ila siri ipo katika kuthubutu kufanya na si kukimbia kufanya.

Hakuna muoga yeyote aliyewahi kufanikiwa ila ni majasiri tu ambao uthubutu kugusa katika sehemu ambazo wengine hawagusi. Kwa mfano katika maeneo ya siasa wengi wamekuwa wakiogopa kuthubutu hata kugombea nafasi za ngazi mbali mbali kwa kuogopa kushindwa na wengine pia uogopa kuwa ni ngumu sana na zipo kwa ajiri ya watu wa tabaka fulani tu na uamini kuwa watu wa chini ni vigumu sana kuweza katika mambo ya siasa; ila uoga wa mtu ndio kushindwa kwa mtu mbona wapo wanaoweza kwa hiyo mtu muoga yeye ushindwa hata kabla hajaingia kwenye ushindani na jasiri ushinda hata kabla hajaingia kwenye mashindano.

Mfano kwenye mpira zikiwa zinacheza timu mbili kuna timu ambayo inacheza ili ishinde na kuna timu ambayo inacheza isishindwe, timu ambayo inacheza ishinde wachezaji wake wanakuwa na hali ya ushindi mara zote na ucheza kwa kushambulia wapinzani mara zote na ndiyo timu inayotazamiwa kushinda kwa kuwa ushindi wao ni hali iliyopo ndani yao kabla hawajaanza mchezo; ila mambo uwa tofauti kwa timu inayocheza ili isifungwe yenyewe ucheza kwa kujilinda sana kuliko kushambulia na wachezaji wake hali yao ni kujilinda wasije kufungwa na mara nyingi si watu wa kushinda. Ni vyema kujifunza kwa timu ichezayo kushinda.

Mambo ya msingi ili kuweza kuishinda hali ya uoga:

 1. Usiogope.

2 Wafalme 6:15-16 “…………………………, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyaje? Akamwambia, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”

Neno usiogope ni neno lenye maana kubwa sana nimeelezea kwa undani katika kitabu cha ‘uungu wa mwanadamu na maisha yenye kibari mbele za Mungu’ na popote ulionapo neno hili limetumika ujue nyuma yake ipo/zipo sababu za kuogopa japo vijana wengi upenda tumia kama neno la kawaida katika mazungumzo yao ila matumizi sahihi ni pale kunapokuwa na sababu za kuogopesha.

Na Mungu anaposema neno hili usiogope umaanisha mengi na haina maana kuwa haoni kuwa yapo yanayoogopesha ila yeye anaona sababu za kukufanya wewe usiogope ni nyingi na kubwa kuliko zikufanyazo uogope nazo ni kama:

 • Yupo pamoja nawe nyakati zote hata ukamilifu wa dahari.

 • Anaweza juu ya jambo linalokusumbua.

 • Hakuna neno gumu asiloliweza.

 • Ameona na kutazama kuteseka kwako na yupo apate kukusaidia.

 • Hakuna liwezalo kusimama mbele zako likafanikiwa.

 • Tulia tu ili atende kwa uweza wake, n.k

Pia neno hili usiogope lina maana sawa na ile ya kuwa hodari na moyo wa ushujaa. Ni taarifa njema kufahamu kuwa neno usiogope kwenye biblia lipo kwa hesabu za siku za mwaka mzima kwa maana ya kwamba kila siku ina ‘usiogope’ moja, kila uamkapo lipo neno la BWANA lisemalo usiogope  kwa kuwa waweza kutana na yaogopeshayo ila kila siku tumia moja hata mwaka uishapo na kuanza mwingine kwa namna hiyo hiyo.

 1. Usienende kwa kuona bali enenda kwa imani.

2 Wakorinto 5:7 “(Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona)”

Kwa maana nyingine ni kusema kuwa mazingira usema kuwa haiwezekani ila imani ambayo chanzo chake ni kusikia neno la Mungu usema kuwa “nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu, Filipi 4:13.” Ni vyema kutoangalia kwa macho ya damu na nyama na kukubaliana na ile hali uliyonayo ila ni busara sana kutazama nini Mungu anatazama kwako.

Kwa kutazama Yese alimwona Daudi kama kijana mdogo sana na hakuona kile kitu kilicho ndani ya Daudi ila Mungu yeye hakumtazama Daudi kama mchunga kondoo tu, bali aliona zaidi kwa kumwona mtu mkubwa na mpakwa mafuta wake wa kusimama kama mfalme.

Usikatishwe tamaa na mazingira uliyonayo leo pengine ni magumu sana na yanakupa mashaka kama utakuja kuwa mtu mkubwa fahamu kwamba hayo uonekana tu ila kwa imani utakuwa kama vile Mungu akuonavyo. Ni vyema sana kujifunza kwa ndugu zetu walio tangulia katika biblia nao walianza sehemu mbaya sana lakini hawakutazama mazingira yanatabiri nini kwa habari yao bali walitazama nini Mungu anasema kwa habari ya maisha yao.

Watu watakutazama kama mtu mdogo sana kama walivyo mtazama Daudi ila Mungu anakutazama kama mtu mkubwa na mfalme juu ya watu wake; watakuona mfungwa ila Mungu anaona waziri mkuu kama alivyomuona Yusufu. Kamwe usikubaliane na watu wakutazamavyo kwa kuwa akuonavyo Mungu si kama watu waonavyo, wao wanaweza kukuona wa kawaida ila Mungu anakuona mtu mkubwa.

I Samweli 16:7 “Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa, BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje bali BWANA huutazama moyo”

Mungu kamwe hatazami umbo, historia, mali za mtu bali uangalia moyo wa mtu. Alipotazama kule porini na machungani alimuona Mfalme mkubwa wa taifa la Israeli japo Yesse aliona mchunga wanyama aliye na thamani ndogo kuliko ndugu zake wengine. Alipotazama gerezani alitazama na kuona mtu mkubwa wa kuwa waziri mkuu japo Potifa yeye aliona mfungwa na mtumwa. Alipoangalia Midiani aliona mkombozi wa wana wa Israeli kutoka Misri aitwaye Musa japo Yethro kuhani wa Midiani aliona mchunga mifugo. Aonavyo Mungu si kama vile wanadamu wengine wawezavyo kuona kwa kuwa wao waweza kukuona si kitu ila Mungu akaona mtu mkubwa sana ndani yako.

Mungu kamwe haangalii umezaliwa kwenye familia ya namna gani au ulitoka kwenye tumbo la mama wa namna gani au viuno vya baba wa namna gani ila anaangalia kusudi lake juu yako ambalo lilikuwepo kabla ya uwepo wako katika tumbo la mama yako.

Mithali 23:7a “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.”

Ona vyema kama Mungu aonavyo huku ukitambua ya kuwa uonaji wako ndicho kipimo cha hatima yako, kwa maana ya kuwa utakuwa kwa namna ile ujionavyo nafsini mwako. Kuna msemo wa Kiswahili usemao “mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake” na ndivyo ilivyo kwa sisi wanadamu ya kuwa mtu uwa kwa upana wa utazamaji wake na kamwe mtu hawezi kuvuna asichopanda kwa kuwa apandacho mtu ndicho avunacho ni rahisi kusema alichokibeba mtu ndani yake ndicho atakacho kitoa kwa kuwa haiwezekani mtu atoe kitu kisichokuwa ndani yake na pia ni wazi sana kuwa yamtokayo mtu ni yale yaujazayo moyo wake na si yalio nje yake.

Mazingira na watu pia uweza sema  wewe hauwezi kufanikiwa, kupata kazi, kuwa mtu mkubwa, kuwa na ndoa nzuri, kupata mchumba,nakadharika ila Mungu naye usema kuwa mambo yote hayo kwake yanawezekana na hakuna lisilowezekana kwake na anahitaji uwe na imani tu kwa kutotia shaka.

Matendo ya mitume 4:19 “Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe”

Ni bora kumsikiliza Mungu katika mambo magumu unayoyapitia maana kwa kusikiliza watu ni rahisi sana ukarudi nyuma na kushindwa kuyatimiza makusudi ya Mungu.

Marko 10:27 “Yesu akawakazia macho, akasema, kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yanawezekana kwa Mungu”

Wakikukatisha tamaa wewe sema “kwa wanadamu kama nyinyi/wewe haiwezekani lakini kwa Mungu inawezekana”

Luka 1:37 “Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu”

Wewe fanya yale yakupasayo kufanya ili upate kufanikiwa kwa kuwa hakuna limshindalo Mungu.

Kwenye hili eneo la Imani bado watu wengi wamekuwa na mtazamo hafifu na si wa kiMungu kwa kuwa wengine usema kuwa namwamini Mungu atatenda tu ila hawafanyi kazi yoyote ili wapate kufanikiwa, ni jambo jema kufahamu sana kuwa Mungu hapendi watu wasioshughulika kwa kuwa yeye hafanyi kazi na mkono mlegevu kwa hiyo hata kama utakiri sana kuwa itakuwa ila kama haufanyi juhudi zozote usidhanie kuwa utapata kufanikiwa. Mungu ameahidi kubariki kazi za mikono ya watu wamchao na ni vyema kufahamu kuwa kama ukifanya kazi ndipo Baraka za Mungu ukutana na wewe huko ili apate kuzidisha yale uyafanyayo.

 1. Dharau tatizo na kuliona kuwa dogo kwa kuwa aliye upande wako ni mkuu kuliko tatizo lililo kinyume nawe.

Hesabu 14:7-9 “wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuipitayo kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. 8 Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. 9 Lakini msimwasi BWANA, wala msiogope wala wenyeji wan chi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope.”

Sehemu hii ya maandiko nimekuwa nikiipenda sana na kuifurahia kila wakati napoitazama kwa kina zaidi. Joshua na Kalebu wanaonyesha ushujaa wa hali ya juu sana ambao kama ukisoma kwa kawaida tu hauwezi pata undani mkubwa wa yale waliyoyasema, cha kwanza wanaliona taifa kubwa lililotia uoga na mashaka taifa la Israeli kuwa kama chakula kwao yaani kwa maana nyingine ni kuona kuwa ni kitu kidogo sana ambacho unaweza kukila si kikudhuru bali kikutie nguvu ya kusonga mbele, Joshua na Kalebu wao waliona mbali zaidi ya kuwa wanasafari ndefu sana na kama wasipopata chakula kama wanefili ambacho ni chakula chenye nguvu watateseka na njaa katika safari waiendeayo. Wao waliona fursa katika matatizo, chakula katika matatizo na sina maana ya kwamba walimaanisha kuwa wawale nyama yao ila waliona ni kitu kidogo sana kwao. Lakini jambo jingine wanaona ule uvuli uliokuwa ndani yao umeondolewa, yaani ule utiisho au kile kinachowafanya waogopeshe kimeondolewa ni sawa na kumwona simba atishaye sana ila hana meno na kucha ambazo zaweza kukudhuru ndivyo walivyoona Joshua na Kalebu kwa wale Wanefili.

Kwako leo inawezekana wapo wanefili wasumbuao ila ni vyema kuona kama mashujaa hawa walivyoona. Yaani kuona fursa katika tatizo na si kuona adha katika tatizo lililo mbele zako na kujua katika kila tatizo linalojitokeza mbele zako ipo fursa (chakula chako) ila ni swala la wewe kuwa jasiri na kutumia fursa hiyo.

Mithali 28:1b “……Bali wenye haki ni wajasiri kama simba” Wenye haki wa Bwana ni majasiri kama simba na hakuna la kuwatisha.

1 Samweli 17: Inaelezea kwa kina sana mwanzo wa tatizo na hata mwisho wa tatizo na jinsi kijana Daudi anavyopambana vyema na kuzidi hata kwa mfalme Sauli.

Tofauti ya Sauli na Daudi katika tatizo lililotokea ni:

 • Sauli alitazama tatizo kama lilivyo na kulitukuza; ila Daudi aliona tatizo ni dogo sana na kumshusha sana mfilisti.

 • Sauli alipomtazama Goliathi akaona kama ‘giant’ (shujaa/shupavu) asiyepigika; ila Daudi akamtazama kama ndege ndo mana akabeba silaha za kuulia ndege. Ni bora angemtazama kama dubu au simba angebeba mkuki na siraha kubwa ila yeye alimuona kama ndege.

 • Sauli alitegemea akili zake mwenyewe bali Daudi alimtegemea Bwana.

 • Sauli alikwenda kwa kuona ila Daudi alikwenda kwa Imani, 1 Wakorinto 5:7.

 • Daudi alimsikiliza Bwana na kumtii kwa kile Bwana aonavyo ila haikuwa hivyo kwa Sauli, Matendo 4:19.

Hata kama tatizo ni kubwa kiasi gani kwako, kwa Mungu ni dogo tu, wewe mwamini Mungu na umtarajie yeye naye atafanya.

Zaburi 37:5 “Umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini naye atafanya.”

 1. Inuka na utende uyaogopayo kwa imani bila kuogopa.

Jitie ujasiri juu ya hicho kitu ukiogopacho, na uinuke na kukifanya kwa ujasiri huku ukimuomba Mungu akusaidie.

Kuna wengine wamekuwa wakisema kuwa hawawezi hata kama bado hawajajaribu kufanya. Mara nyingi kitu ambacho unaona uwezi kwanza ni vigumu sana kukifanya ukafanikiwa ni kwa sababu:

Kumbukumbu la torati 7:17 “Nawe kama ukisema moyoni mwako,mataifa haya ni mengi kunipita mimi;nitawatoaje katika miliki yao?”

Ukiona kushindwa usidhani kama Mungu atasimama. Mungu utenda kazi katika mazingira na viwango ulivyomwekea na ukimwekea mazingira madogo madogo ufanya kwa mazingira hayo hayo na ukiweka makubwa aweza fanya kwa viwango hivyo.

2 Wafalme 4:3-6 “Akasema nenda ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. 4 Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, nay eye akamimina. 6 Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma”

Katika chombo cha mama mjane mafuta yalijaa kwa kadiri alivyoandaa vyombo angeandaa vidogo angepata vidogo na angeandaa vingi zaidi bila shaka angepata vingi zaidi. Ni vyema kwa mtu wa Mungu kumjengea Mungu mazingira ya kutenda mambo makubwa hata kama u mtu mdogo sana. Ikiwa ni biashara, kazi, masomo, inuka na utende kwa ujasiri maana Mungu anatenda kazi na majasiri na wasioogopa. Fanya tu ukishindwa mara ya kwanza usikate tamaa rudia kufanya tena na tena hata ukafanikiwa huku ukikumbuka kuwa mkono wenye juhudi utawandishwa.  

 1. Amini kuwa unaweza.

Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”

Ikiwa watu wenye mafanikio makubwa duniani na walio na hali ya chini sana hapa duniani wote wana masaa 24 kwa siku, swali ni je, Nini kinaleta tofauti kati yao?

Hii pia ni sababu kubwa ya wao kufanikiwa kwa kuamini kuwa wanaweza wakafanya na hatimaye wakafanikiwa kuthubutu na kutenda.

Ukijenga imani ya kuamini kuwa unaweza kufanya una nafasi kubwa sana ya kufanikiwa katika lile ulitendalo.

Dr Mayles Munroe anasema “watu waliofanikiwa katika ulimwengu huu ni watu waliotoa kabisa neno haiwezekani katika kamusi zao na kuliacha neno inawezekana.”

Hii ni kuonyesha kuwa katika kuamini kuwa inawezekana hapo ndipo mafanikio ya mtu yamewekezwa. Lipo neno jema sana Bwana Yesu alisisitiza na kusema kuwa “mambo yote yanawezekana kwake yeye aaminiye”

–Mwl Kelvin Kitaso

Advertisements

7 thoughts on “MASHAKA NA UOGA NI VIKWAZO VYA KUKUFIKISHA MAHALI UNAPOPASWA KUFIKA.

 1. Barikiwa Kelvin,

  Mimi nianze hivi, kinachokosekana kwa wanaoshindwa ni DETERMINATION ( Shauku thabiti), au nawezasema kuwa ni yale maandalizi yakinifu juu ya jambo wanalotaka kutimiza.

  Huwezi ukaanza tu kuamini juu ya jambo ambalo hujalifanyia maandalizi kifikra ili hayo maandalizi yakusaidie kuweka shauku thabiti.

  Mahali palipo na “determination” ndipo mahali ambapo imani hufanya kazi kwa matokeo chanya mtu akiamua kuamini.

  Kuna kitu kinaitwa “kuhesabu gharama” Yesu aliwahi kukisema. Alisema kuwa mtu akitaka kuvamia mji lazima apige kwanza mahesabu, hasa aangalie uwezo wake wa kijeshi.

  Tena alisema unapotaka kujenga mji lazima upige kwanza mahesabu yakusaidie kujua uwezo wako wa kukamilisha huo ujenzi, ili usipate aibu ya kukomea njiani ukachekwa.

  Hayo mahesabu ndo mm nayaita shauku thabiti iliyojengwa katika msingi imara ndani ya fikra ya mwenye kuamini.

  Ili ujue kuwa wakristo wanazo imani waangalie vile wanavyoweza kumwamini Mungu ktk mambo ambayo huwapata bila kupita kwenye fikra zao, na kuwafanya wasiwe na cha kufanya ispokuwa kumwamini Mungu.

  Eg, wakivamiwa na mapepo gafla, au ugonjwa.

  Na hiyo determination lazima ipate msingi wake kutoka katika neno la Mungu kwa mktisto.

  Ahadi pekee ya Mungu inayoweza kutimia kwa mkristo bila yeye kuweka determination ni ile ambayo iko ktk aina ya mapenzi ya Mungu ambayo hayahitaji uhusika wa mtu ndipo yatimie.

  Kuamini tu bila kuwa na determination ni ngumu sana kutimiza malengo!

 2. lakini mimi ningependa kuongezea hivi: tukilipa nafasi kubwa kwa kulisoma na kulitafakari neno la Mungu vichwani mwetu, ndipo kwa msaada wa neno hilo, tutajikuta hatuna huo woga na wasiwasi wa kibinadamu, kwa kuwa hilo neno la Mungu ndilo huyo roho, kweli na uzima litupalo nguvu na ujasiri wa kutoogopa nk…lakini kama tukijifunza kielimu ili tusiogope bila ya neno la kristo kuwa kwa wingi ndani yetu, basi hatutafanikiwa kuushinda uoga ijapokuwa tutakuwa tunaelimu au tunajua, kwa kuwa neno la Mungu ndiye kristo mwenyewe, nae alikwishatuambia kwamba “pasipo yeye sisi hatuwezi kitu” naye ndiye hilo neno akaaye ndani yetu na kutusaidia kutupa ujasiri kwa njia hiyo!.

 3. ni moja kati ya masomo mazuri sana ya kuzingatia kiundani (kiroho). Wakristo wengi hawafanikiwi na kuifaidi dunia hii kwa sababu ya kukosa ufahamu wa neno la Mungu kwa namna hii. ..na hapo ndipo penye mwanya ambao, shetani amekuwa akiutumia , kuwaweka watoto wengi wa Mungu utumwani!.Mungu akubariki mtumishi kwa mchango wako mzuri sana.

 4. AMEN Mtumishi Kelvin Kitaso umenibariki sana kwa somo hili. MUngu azidi kukujaza Neno lake zaidi na zaidi. Ubarakiwe mno.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s