MUNGU ANATAFUTA WAMWABUDUO HALISI.

Yohana 4:24  Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

Mpendwa wangu, ubarikiwe sana kwa kupita mara kwa mara kwenye huu ukuta kujichotea mafundisho yenye uzima ambayo Mungu wa mbinguni ananijalia kuyaweka kwa kadiri Roho Wake anavyonisukuma kwenye utu wangu wa ndani sawa sawa na neema Yake niibebayo maishani mwangu.

Katika somo hili nataka tuangalia kwa sehemu kuhusiana na hili jambo muhimu na nyeti sana kwa mwamini, Kumwabudu Mungu.

Kama umeshawahi kupata fursa au bahati ya kuwepo mahali watu wanapomwabudu Mungu kiukweli kuna mambo ambayo lazima umekuwa ukiyaona katikati ya watu wanao mwabudu Mungu katika uhalisi wake ambayo yamekusaidia kuanza kupata mwanga kidogo juu ya kuabudu.

Mara nyingi ukikuta watu wanamwabudu Mungu utaona wamenyanyua mikono yao juu. Unaweza ukaona watu wakiwa wamenyanyua nyuso za kuelekea juu na wakati mwingine kuna machozi yanawatoka lakini sio kila kunyayua uso juu na kutokwa machozi ni kumwabudu Mungu. Unaweza ukawaona watu katika kumwabudu Mungu wamepiga magoti lakini sio kila kupiga magoti ni kumwabudu Mungu. Unaweza ukawaona watu wamesujudu au kulala kifudi fudi mbele za Bwana lakini sio kila kusujudu au kulala kifudi fudi ni kumwabudu Mungu.

Kwa maneno rahisi sana kueleweka na kila mtu, kuabudu ni kila kinachotokea kwa mwanadamu aliyekombolewa uwepo wa Mungu unapojidhihirisha kwake.

Kinyume na fikra za wengi, uwepo wa Mungu hauletwi na kuabudu bali kuabudu ni mwitikio wa mwanandamu kwa uwepo wa Mungu uliyodhihirishwa. Uwepo wa amungu ukijidhihirisha mwitikio wa mwanadamu kwa uwepo huu ndiko kuitwako kuabudu. Sasa sio kuabudu kunakoleta uwepo wa Mungu bali ni sifa ndiyo huleta uwepo wa Mungu.

Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. (ZAB. 22:3 SUV).

Israeli au watu Wake Mungu wakimsifu, ndiko kunakoleta uwepo Wake katika maisha yao au mahali pale walipo.

Unaweza ukamfundisha mtu kusifu lakini huwezi ukamfundisha mtu kuabudu. Kusifu kwafundishika bali kuabudu hukamatika tu maana ni kitu ambacho kinafanya na roho yako japo hujidhihirisha kwenye nafsi na mwili wako lakini mahali hasa ambapo ibada ya kweli huanzia ni kwenye roho yako.

Mungu hawatafuti tu wamwabuduo bali anawatafuta wamwabuduo halisi. Hii ni dhahiri kuwa kuwa waabudu halisi na kuna waabudu wa kuegeza. Wa kuegeza wanajua kila kitu ambacho inabidi kifanyike ili kuabudu. Wanajua nyimbo za kutumia, wanajua jinsi ya kujiweka ili tu waonekane wanaabudu. Lakini bila uwepo wa Mungu kujidhihirisha kwanza hapawezi kuwa na kuabudu halisi hata siku moja.

Kunaweza kuwepo mfano wa kuabudu lakini hapawezi kuwa na kuabudu halisi.

Moja ya vitu ambavyo vinasababisha kuabudu kwako na kwangu kuboreke zaidi ni kiasi ambacho binafsi unamjua Mungu naye mwabudu. Ukimjua Mungu unaye mwabudu utajua jinsi sahihi ya kumwitikia anapojidhIhirisha na uwepo Wake. Ndo maana Yesu akamwambia yule mwanamke Msamaria, Nyie mnaabudu msichokijua, sisi tunaabudu tukijuacho kwa maana wokovu watoka kwa Wayahudi.

Kumjua kwako unayemwabudu itaongeza sana uwezo wako wa kumwabudu katika Roho na Kweli. Hapa cha kuelewa hapa kumwabudu Mungu katika Roho na Kweli ni kumwabudu kwa msaada wa Roho Wake na Kweli Yake na vyote viwili hivi vinakusaidia kuongeza kumjua kwako unayemwabudu. Kwa kadiri umuuavyo ndivyo utakavyojua ikupasavyo kuitika anapojidhihirisha kwako. Hilo hawezi kukufundisha mtu ni jambo linatokea tu uwepo Wake ukidhihirishwa.

Sasa nisilimalize hili nilisemalo bila kutaja mambo yanayoweza kukuzuia usimwabudu Mungu. Yapo kadhaa lakini leo naomba niyasemee mawili.

1. Utumwa au kifungo kinaweza kukuzuia usimwabudu Mungu.

Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu,
Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote. (LK. 1:73-75 SUV).

Ina maana kwa mujibu wa andiko hilo hapo juu kama asipotujalia kuokoka mikononi mwa adui zetu hatutaweza kumwabudu Mungu pasipo hofu. Au hatutamwabudu kabisa au kama tukimwabudu tunamabudu katika hofu ya hao maadui na palipo na hofu pana adhabu na yeye aogopaye hajakamilishwa katika upendo.

Ona maneno ambayo Mungu alimwambia Musa.

Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu. (KUT. 3:12 SUV).

Mungu anamwambia Musa kuwa dalili kuwa yeye ndo amemtuma ni kwamba watakapokwisha kutoka Misri watamwabudu katika Mlima ule. Kwa maneno mengine kama upo Misri huwezi kumwabudu Mungu. Lazima utolewe huko kwanza ndipo uweze kumwabudu Mungumkwa uhuru. Misri ni mahali pa utumwa, mateso, kifungo, kutumikishwa. Vikiwo hivi maishani mwako vitazuia uwezo wako wa kumwabudu Mungu.

2. Dhambi inaondoa ujasiri ndani yako wa kumwabudu Mungu.

Mungu huabudiwa katika uzuri wa utakatifu.

Mpeni BWANA utukufu wa jina lake;
Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu. (ZAB. 29:2 SUV).

Utakatifu ndo mazingira muafaka kabisa ya kuachilia ibada yako kwa Mungu.

Kunapokuwa na dhambi maishani dhamiri yako inakuzuia usimwabudu Mungu kwa uhuru.

Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai? (EBR. 9:13, 14 SUV).

C unaona inavyosema kwenye huo mstari hapo juu? Dhamiri iliyonajisiwa kwa dhambi haina uwezo wa kumwabudu Mungu na ndo maana damu ya Yesu hutakasa dhamiri zetu na kazi mfu tupate kumwabudu Mungu aliye hai. Kumbuka tulisema kuwa kuabudu ni mwitikio wetu kwa uwepo wa Mungu uliyodhihirishwa.

Embu tusome haka kakipande ka maandiko.

Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi. (ISA. 6:1-5 SUV).

Unaona hapa uwepo wa Mungu ulijidhihirisha kwa Isaya lakini kwa sababu Isaya alikuwa ana dhambi nyemelezi maishani mwake badala ya kuabudu alitumia fursa hiyo kutengeneza na Mungu japo uwepo wa Mungu ulidhihirishwa ili aabudiwe.

Sio kila mtu anayeonekana kama anaanudu uwepo wa Mungu ukija anaabudu kweli. Wengine ndo wanatumia fursa hiyo kutengeneza na Mungu maana ndo keshakuja. Sio kila chozi ni chozi la moyo uliyoguswa na uwepo wa Mungu katika kuabudu. Machozi mengine ni machozi ya toba. Kusujudu kwingine ni kusujudu kwa toba. Kupiga magoti kwingine ni kupiga magoti katika toba. Ni Mumgu tu na yule mtu mdo wanajua uhalisi wa kinachoendelea pale.

Ndo maana ni muhimu kutengeneza na Mungu kabla hajajidhihirisha ili akijidhihirisha kutumii huo muda kumalizana nae bali kumfurahia kwa uwepo Wake aliyoudhihirisha.

 Mungu akubariki sana sana sana.

 Mwl.Conrad C
Advertisements

One thought on “MUNGU ANATAFUTA WAMWABUDUO HALISI.

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

w

Connecting to %s