UMOJA

ünity

Magreth na Joseph wako kwenye mazungumzo:

MAGRETH: Kati ya mambo yanayonikera ni kutokuwepo umoja baina ya madhehebu ya watu waliookoka.

JOSEPH: Kwa nini unasema hivyo?

MAGRETH: Wewe huoni kila kanisa linafanya mambo kivyake. Angalia mikutano ya injili, kila dhehebu linaandaa kivyake. Hata ushirikiano baina ya wachungaji wa makanisa hayo hauko kwa kiwango cha kuridhisha. We hali hiyo unaiona iko sawa?

JOSEPH: Mhh, kama wote wanahubiri injili ya Yesu Kristo mie sioni kama kuna tatizo.

MAGRETH: Tatizo lipo bwana! Yesu alituombea umoja. Madhehebu yote hayo yalipaswa yawe na umoja wenye nguvu, yawe na sauti moja, sio kila watu na lwake! Nafikiri ipo haja ya kufanya maombi ya mzigo tuwe na umoja katika makanisa yetu.

Ni kweli Bwana Yesu Kristo kabla hajaenda kutolewa dhabihu pale msalabani, aliwaombea wanafunzi wake umoja. Hebu tusome lile andiko maarufu kuhusu hii mada ya umoja:

“Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.” (Yohana 17:11, SUV)

Je umoja aliokuwa akiuzungumzia Bwana Yesu ni umoja wa jinsi gani?

Hebu tusome tena pale katika muktadha (context) wake:

“Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, WAKUJUE WEWE, MUNGU PEKEE WA KWELI, NA YESU KRISTO ULIYEMTUMA. Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye. Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako. Jina lako nimewadhihirishia WATU WALE ULIONIPA KATIKA ULIMWENGU; walikuwa wako, ukanipa mimi, na NENO LAKO WAMELISHIKA. Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako. Kwa kuwa MANENO ULIYONIPA NIMEWAPA WAO; NAO WAKAYAPOKEA, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, WAKASADIKI YA KWAMBA WEWE NDIYE ULIYENITUMA. MIMI NAWAOMBEA hao; siuombei ulimwengu; bali HAO ULIONIPA, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; NAMI NIMETUKUZWA NDANI YAKO. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, KWA JINA LAKO ULILONIPA UWALINDE HAWA, ILI WAWE NA UMOJA KAMA SISI TULIVYO. NILIPOKUWAPO PAMOJA NAO, mimi NALIWALINDA KWA JINA LAKO ULILONIPA, nikawatunza; WALA HAPANA MMOJA WAO ALIYEPOTEA, ILA YULE MWANA WA UPOTEVU, ili andiko litimie. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali UWALINDE NA YULE MWOVU. WAO SI WA ULIMWENGU, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Wala SI HAO TU NINAOWAOMBEA; LAKINI NA WALE WATAKAONIAMINI KWA SABABU YA NENO LAO. WOTE WAWE NA UMOJA; KAMA WEWE, BABA, ULIVYO NDANI YANGU, NAMI NDANI YAKO; HAO NAO WAWE NDANI YETU; ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI YA KWAMBA WEWE NDIWE ULIYENITUPA.

Nami UTUKUFU ule ULIONIPA NIMEWAPA wao; ILI WAWE NA UMOJA KAMA SISI TULIVYO UMOJA. MIMI NDANI YAO, NAWE NDANI YANGU, ILI WAWE WAMEKAMILIKA KATIKA UMOJA; ILI ULIMWENGU UJUE YA KUWA NDIWE ULIYENITUMA, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.” (Yohana 17:1-23, SUV, msisitizo wangu)

Kuna mambo kadhaa tunayaona katika kifungu hicho cha Maandiko Matakatifu:

1. Bwana Yesu Kristo alikuwa anawaombea wale waliokuwa wamemwamini wakati ule na wale ambao wangekuja kuamini baadaye (hivyo mimi na wewe ambaye umeamini tumejumuishwa humo). Hao ndio watu ambao Mungu amempa (waweza kusoma pia Yohana 6:39).

2. Sifa kuu ya watu hao ambao Yesu alikuwa anawaombea ni kwamba wamelipokea na kulishika Neno lake na Yeye ametukuzwa ndani yao; hakuwa akimwombea kila mtu ulimwenguni.

3. Alikuwa anawaombea Mungu awatakase kwa kweli ya Neno lake.

4. Alikuwa anawaombea Mungu awalinde dhidi ya yule mwovu muda ambao watu wa Mungu wakiwa bado wapo ulimwenguni, asipotee hata mmoja, ILI WAWE NA UMOJA.

5. Waliomwamini Kristo Yesu wakiwa na umoja, utapelekea ulimwengu kumwamini.

Mtume Paulo naye aliandika yafuatayo katika waraka wake kwa jamii ya waamini waliokuwa wakiishi kule Efeso:

“Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, MWENENDE KAMA INAVYOUSTAHILI wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na KUJITAHIDI KUUHIFADHI UMOJA WA ROHO katika KIFUNGO CHA AMANI. Mwili MMOJA, na Roho MMOJA, kama na mlivyoitwa katika tumaini MOJA la wito wenu. Bwana MMOJA, imani MOJA, ubatizo MMOJA. Mungu MMOJA, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.” (Waefeso 4:1-6, SUV, msisitizo wangu)

Na kisha akaendelea:

“Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia UMOJA WA IMANI na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini TUISHIKE KWELI katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.” (Waefeso 4:11-15, SUV, msisitizo wangu)

Hebu tusome na Maandiko mengine:

“Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu. Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote MNENE MAMOJA; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika NIA MOJA na SHAURI MOJA. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?” (1 Wakorintho 1:9-13, SUV, msisitizo wangu)

“Basi ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na NIA MOJA, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja. MSITENDE NENO LO LOTE KWA KUSHINDANA wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.” (Wafilipi 2:1-4, SUV, msisitizo wangu)

Kwa kuzingatia Maandiko hayo hapo juu pamoja na mengine, naomba tujadili mambo yafuatayo kuhusiana na swala hili la UMOJA miongoni mwa jamii ya waaminio:

1. Je umoja ambao Bwana Yesu Kristo aliwaombea wanafunzi wake ni umoja miongoni mwa makanisa au madhehebu ya Kikristo au ni umoja wa jinsi gani hasa?

2. Je umoja huo unafikiwa vipi?

3. Ni mambo gani yakiwepo miongoni mwa jamii ya waaminio inadhihirisha kuwa kuna umoja miongoni mwao?

4. Je umoja huo upo au haupo hivi leo katika Kanisa la Yesu Kristo?

Karibuni tujadili.

Joel Msella

Advertisements

7 thoughts on “UMOJA

 1. Siyi;
  Naona umejitahidi kusema kweli kuwa haya Madhehebu likiwemo la kwako lengo lake ni baya na Mwisho wake ni Mauti.Kwa kweli Madhehebu ni miradi ya watu.
  BWANA YESU na WANAFUNZI WAKE hawajawahi kuwa na DHEHEBU lolote.
  MATENDO 11:26″……..Na wanafunzi waliitwa Wakristo kwanza hapo Antiokia”
  Majina mengine tofauti na kuwa Wakristo yanatoka kwa Ibilisi.
  Ahsante kwa mchango mzuri.

 2. Binafsi nakubaliana na Mile. Utitiri wa madhehebu leo, ni kudanganyana na kupotezeana muda, fedha na hata maisha yenyewe baada ya haya! Mungu atusaidie tuisome Biblia kwa jicho pevu.

 3. Kilichotugawa wakristo ni kuchanganya biblia na mawazo ya watu,Hivyo kila moja anawavuta watu kwake kwa maslahi yake.

  MATENDO 20:28-29

  28. NAJUA MIMI YA KUWA BAADA YA KUONDOKA KWANGU MBWA-MWITU WAKALI WATAINGIA KWENU, WASILIHURUMIE KUNDI;
  29. TENA KATIKA NINYI WENYEWE WATAINUKA WATU WAKISEMA MAPOTOVU, WAWAVUTE HAO WANAFUNZI WAWAANDAMIE WAO.

  Yesu anayeitwa Neno ndiye anaeunganisha watu wakimtii kama asemavyo
  watajikuta chini ya mwamvuli mmoja.

 4. Biblia iko bayana kwenye suala la upendo unaotufungamanisha kama wakristo wa kanisa moja tu ulimwenguni. Paulo anasema, “ Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, mwenende kama inavyoustahili wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na kujitahidi kuuhifadhi umoja wa roho katika kifungo cha amani. Mwili mmoja, na Roho mmoja, kama na mlivyoitwa katika tumaini moja la wito wenu. Bwana mmoja, imani moja, ubatizo mmoja. Mungu mmoja, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.” Wakolosai 4:1-6.

  Kwa hiyo, kuna kanisa moja tu linalowapeleka watu mbinguni. Na watu wanaosali katika kanisa hilo, ndio wanaopaswa kuwa na UMOJA wa kiuelewa wa neno. Mikusanyiko ya kimadhehebu katika masuala ya ibada au mashirikiano mbalimbali ya kiimani, huo sio UMOJA wala upendo unaozungumzwa na Kristo. Ungekuwa ni UMOJA au UPENDO wa Kristo, jumuia hizo za kimadhehebu, zingeungana na kukaa pamoja na kuunda kanisa moja lenye ubatizo mmoja, imani moja, Bwana mmoja na siku moja tu ya kuabudu. “… Mimi ndimi njia, na kweli, na uzima; mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.” Yohana 14:6. Hatuna mayesu wengi kama tulivyo na madhehebu mengi leo! Yesu ni mmoja tu, na mume wa mke (kanisa) mmoja tu. Sharti na watu wake (kanisa lake), liwe moja tu lenye umoja wa kiulewa katika Neno; zaidi ya hapo, ni kudanganyana!

  UMOJA na UPENDO unaoshabikiwa hivi leo na madhehebu ya Kikristo, kimsingi siyo upendo au umoja unaotokana na matakwa ya madhehebu hayo. Ni sera za mpinga Kristo kutoka Rumi, zinazoingizwa kisiasa ndani ya madhehebu hayo. Zamani (naam na hata leo), ilikuwa inajulikana kuwa, mkatholiki alimsema Mlutheri kuwa amepotea kwa imani yake, msabato akawanyoshea vidole wajumapili wote kwa utitiri wa madhehebu yao kuwa wamepotea kwa imani zao n.k. n.k.. Lakini siku hizi, tofauti hizo zimeshaanza kupungua, naam hata kuondolewa kabisa. Watu wanafarijiana kuwa woooote kwa ujumla wao –(umoja wao) huo, wanamwabudu Mungu. Sijui kama Biblia imebadilika!! Wala sijui kama Mungu ana mwana zaidi ya Yesu Kristo!! Na cha ajabu zaidi, watu wanashabikia tu bila ya kufahamu chimbuko hili la counterfeit unity. Ni vyema watu wakafahamu vyema jambo hili ya kuwa, hakuna mfungamano uliopo kati ya waasi na waumini. Biblia inasema “Msifungiwe nira pamoja na wasioamini, kwa jinsi isivyo sawasawa; kwa maana pana urafiki gani kati ya haki na uasi? Tena pana shirika gani kati ya nuru na giza? Tena pana ulinganifu gani kati ya Kristo na Beliari? Tena pana mapatano gani kati ya hekalu la Mungu na sanamu? Kwa maana sisi tu hekalu la Mungu aliye hai; kama Mungu alivyosema, ya kwamba, Nitakaa ndani yao, na kati yao nitatembea, nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu. Kwa hiyo, Tokeni kati yao, Mkatengwe nao, asema Bwana, Msiguse kitu kilicho kichafu, Nami nitawakaribisha. Nitakuwa Baba kwenu, Nanyi mtakuwa kwangu wanangu wa kiume na wa kike.” 2 Korintho 6:14-18.

  NB: Nieleweke kuwa, sihamasishi watu watengane, wasisaidiane kimaisha, wasipendane, n.k. Ninachokisema ni kwamba, ni SHARTI watu watofautishe mambo ya Mungu (eg Holy Union) na mambo ya ulimwengu huu.

 5. binadamu ni wengi duniani pote japo kuna tofauti kadha wa kadha baina yao, iwe ktk langi , lugha, mitazamo, umbo, vinasaba n.k.
  lakini pamoja na tofauti hizo bado tunakubariana kuna mambo ya msingi yanayopasawa kuzingatiwa katika kutunza utu wake.
  hitaji la kupendwa, kuthaminiwa, kulindwa, kuheshimiwa ni mahitaji ya msingi kwa mwanadamu.
  kanisa la kristo kama jamii ya watu wanaomwamini kristo nawaliopo duniani ktka maeneo tofauti wanatambuliwa ktika ulimwengu wa roho kama jumuya ya wana wa Mungu .
  hapa duniani licha ya tofauti ya kijiografia bado ziko jumuiya za wakristo ktk maeneo tofautitofauti ikiwemo ktk madhehebu.
  utofauti wa kidhehebu hautupi kibali cha kutoishi maisha ya ukristo hapa duniani.
  hakuna dhehebu la kikristo linalofundisha kutowapenda na kuwachukia binadamu wasioamini ktk yale tunayoyaamini.
  tofauti katika madheebu haitokaa haiondoke ikizingatiwa kila wanachokiamini hudai ni fundisho na mafunuo ya kibiblia.
  ila katika jumuisho la yote, ziweko lugha, kuweko unabii, kuweko mafunuo jumla ya haki ya mungu imejumuishwa katika kweli hii
  MPENDE MUNGU WAKO KWA MOYO WAKO WOTE, KWA ROHO YAKO YOTE NA KWA NGUVU ZAKO ZOTE.
  PIA MPENDE JIRANI YAKO KAMA UNAVYOJIPENDA MWENYEWE.

  katika hayo hakuna hudhehebu wala mafunuo binafsi.
  hivyo utaona dunia ya kuionyesha umoja unaoutamani na wa kimungu ktk kristo yesu ni inayokuzunguka, anza ktk familia yako, na jamii yako inayokuzunguka kisha onyesha umoja huo ktk kanuni ya upendo hapo juu utakuwa unatimiza kweli yote.

  madhehebu na dini ni vyama vilivyojipambanua kumsaidia mwanadamu amjue mungu. basi ikiwa utapata mafundisho na mafunuo sahii ya kubiblia utahitajika ku-apply mafundisho hayo ktk uhalisia wa maisha ktk jamii inayokuzunguka.

 6. Asante saana mtoa hii mada na brother siyi,,kuna mengi nimenjifunza ..God bless you all….

 7. Msella,
  Nikushukuru kwa kuwa mbunifu na mwenye kuleta mada nzito, muhimu na kwa wakati mwafaka. Mambo mengi aliyoyazungumza Yesu Kristo na mitume wake kuhusu UMOJA, watu wengi hudhani ni umoja huu wa kula ugali pamoja, kucheka pamoja, kufurahi pamoja na pengine kufanya kazi au shughuli fulani pamoja! Na hili ndilo kosa kubwa la kifikra tunalolifanya wakristo tulio wengi. Hata makanisani kwetu huko, watu hufundishwa umoja huu wa kidunia na umoja wa kimbingu unaachwa! Na siku si nyingi Mpinga Kristo, naam tayari ameshaanza mchakato wa kuyaunganisha makanisa yooote ya Kikristo kuwa chini ya mwamvuli huu wa UMOJA wa kidunia huku akichomeka mafundisho yake polepole pasi kujua! Na kwa vile ndiye wakala mkuu wa mungu wa dunia hii (shetani), mipango yake hiyo (ya kuwa na umoja wa kiimani) lazima ishinikizwe na sheria za kimataifa. Wale wooote watakaonekana kuwa kinyume na sheria hizo za umoja wa kidini, hatima yao watauwawa!! Nisiseme mengi sana, naomba niende kwenye maswali yako ya mjadala.
  1. “Je umoja ambao Bwana Yesu Kristo aliwaombea wanafunzi wake ni umoja miongoni mwa makanisa au madhehebu ya Kikristo au ni umoja wa jinsi gani hasa?”.
  Jibu
  Inabidi uelewe tafsiri ya makanisa au madhehebu kwanza! Yesu hakuuombea watu wawe na umoja wa makanisa ya Kikristo kama vile Wapentekoste waungane na wasabato, waroma na mashahidi wa Yehova, n.k. Na wala Yesu hakuombea umoja wa kimadhehebu kama vile umoja baina ya wasabato na waroma n.k. Wala hakuombea umoja kati ya imani ZA Kikristo, bali Yesu aliombea UMOJA wa wanafunzi kiroho! Nina maana gani hapa! Nina maana kwamba, Yesu aliwaombea ufanano wa kuielewa Biblia na kuwa na lengo, dhamira na kusudi moja kama alivyokuwa YEYE na BABA yake. Makanisa au madhehebu yanayoitafsiri Biblia tofautitofauti, hayawezi kufikia UMOJA alioukusudia Kristo; na badala yake, wataishia kwenye umoja wa kidunia ambao mwasisi wake ni ibilisi na Lusifa.
  2. “Je umoja huo unafikiwa vipi?”
  Jibu
  Umoja huo wa kiuelewa wa Maandiko, utafikiwa pale tu watu watakaporudi kwenye mafundisho ya Biblia na Biblia Pekee; jambo ambalo kwa sasa, haliwezi kutokea maana kila mchungaji na nabii, anaanzisha kanisa kwa maslahi yake. Tena hufundisha mafundisho yenye kukidhi matakwa ya kimwili tofauti kabisa na mambo ya kiroho yalivyo. Wale watakaoufikia UMOJA wa Kristo, ni wale (individuals), watakaosimama kwenye ukweli wa Biblia na Biblia pekee tu. Umoja wa kiimani tofauti na huu, ni makongamano ya kula ugali na mlenda tu! Tena ni umoja bandia utakaopeleka watu motoni, naam wengi wao bila kujua!
  3. “Ni mambo gani yakiwepo miongoni mwa jamii ya waaminio inadhihirisha kuwa kuna umoja miongoni mwao?”
  Jibu
  Yapo mengi sana ndugu Msella. Mimi nitakutajieni machache tu.
  a. Kama makanisa au madhehebu yanakapofundisha mafundisho yoote ya Kibiblia na kuondoa creeds zote.
  b. Kama yameanza/yataanza kuondoa creeds zote zinazoaminiwa kwa sasa na waumini kana kwamba ni mafundisho ya Kibiblia kumbe sivyo.
  c. Kama yataondoa taratibu zote za uendeshaji wa makanisa au madhehebu zilizotengenezwa na wanadamu na badala yake kurejea taratibu hizo kutoka kwenye neno la Mungu pekee.
  4. “Je umoja huo upo au haupo hivi leo katika Kanisa la Yesu Kristo?”
  Jibu
  Umoja huo leo kwa kiwango kikubwa haupo, ila upo kwa watu wachache sana waliomo ndani ya kanisa la kweli; watu wanaouamini ukweli kama ulivyoandikwa ndani ya Biblia.
  Nisiseme mengi sana nikanyima fursa kwa wengine kuchangia.
  Neema ya Bwana ikufunike.
  Siyi

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out / Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out / Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out / Change )

Google+ photo

You are commenting using your Google+ account. Log Out / Change )

Connecting to %s