Ukishindwa, Ongeza Uwezo!


Nakumbuka ilikuwa ni tar 29/9 mwaka huu, nilipoamka asubuhi, nikiwa ninawaza juu ya baadhi ya mambo ambayo niliyafanya lakini nikashindwa. Nikawa najiuliza ni kwanini nilishindwa ? Je ni kwa vile yale mambo hayawezekani ? Nikasikia sauti ndani yangu inaniambia sio kwamba hayawezekani, kuwezakana yanawezekana ila uwezo wako ni mdogo. Unachotakiwa kufanya ni kuongeza uwezo sawa na neno la Mungu linavyosema “Mtu mwenye hekima ana nguvu; Naam, mtu wa maarifa huongeza uwezo”. (Mithali 24:5) 
Ile sauti ikaendelea kunifundisha, ikaniambia kuwa kulikuwa na watoto wa 3 wa mfalme ambao walikuwa ni mapacha, na mfalme alikuwa anataka mmoja kati ya hao watoto wa 3 arithi kiti chake cha ufalme. Akawapa mtihani wa kubeba mzigo uliokuwa na kilo 300 na kuuweka juu ya ukuta ambao ulikuwa na urefu wa futi 4 kutoka ardhini. Na aliwapa muda wa mwaka mmoja na nusu wawe wamekamilisha hilo zoezi. 
Wale watoto wote walikuwa na urefu wa futi 6 kila mmoja na uzito unaolingana. Mtoto wa kwanza alipoungalia ule mzigo na kugundua kuwa unauzito wa kilo 300, alikata tamaa mapema na kusema kuwa hawezi kuubeba. Akaja wa pili, akajaribu kuunyanyua lakini akashindwa, akajaribu tena akashindwa, akajaribu hadi mara 5 lakini akashindwa kuunyanyua. Akajisemea moyoni huu mzigo ni mzito sana hauwezi kubebeka, hakuna mtu kati yetu anayeweza kuunyanyua. Akaamua kuuacha. Akaja mtoto wa tatu, yeye alijaribu kuunyanyua mara moja tuu, aliposhindwa akaamua kuuacha. Akaanza kuwaza nifanyeje ili huu mzigo niweze kuunyanyua. Akaamua kutafuta majarida yanayoelezea wanyua vitu vizito, kujua ni jinsi gani wanaweza kunyanyua vitu vizito. Katika utafiti wake na kusoma kwake akagundua kuwa wale watu wanaobeba vitu vizito hawakuzaliwa wakiwa na uwezo huo, bali huwa wanafanya mazoezi ya kubeba vitu vizito ili kuifanya misuli yao iwe na nguvu ya kubeba vitu vizito. Alipogundua hilo akasijisemea moyoni kwa kuwa baba ametupa mwaka mmoja na nusu nitaanza kufanya mazoezi ya kubeba vitu vizito. Najua baada ya mwaka mmoja nitakuwa nimeijenga misuli yangu vizuri kuwa na uwezo wa kubeba huu mzigo.
Yule kijana akaanza kufanya mazoezi ya kubeba vitu vizito kila siku jioni baada ya muda wa kazi. Wakati anafanya hayo mazoezi kila baada ya muda wa kazi jioni, wale wenzake wawili walikuwa wanamcheka na kumuona kama mjinga. Wao muda wa jioni baada ya kazi walikuwa wanautumia kustarehe na wanawake. Walishasahau habari ya kubeba ule mzigo wakijua kuwa hakuna hata mmoja kati yao mwenye uwezo wa kuubeba ule mzigo. Na kwa vile hakuna anayeweza, baba ataamua mwenyewe wa kumrithisha kiti chake cha kifalme. 
Yule kijana baada ya kufanya yale mazoezi kwa muda wa mwaka mmoja, mwili wake ulikuwa umejengeka vyema, misuli yake ilikuwa ni mikubwa. Akamfuata baba yake akamwambia nataka nifanye ile kazi uliyotupa ya kubeba ule mzigo wa kilo 300 na kuuweka juu ya ukuta. Basi basi baba yake pamoja na wasaidizi wake wakatoka kwenda kuangalia kama yule kijana ataweza kuubeba ule mzigo. Yule kijana akausogelea ule mzigo, akaunyanyua juu na kuuweka juu ya ukuta. Wenzake na wale watu waliokusanyika kuangalia lile tukio walishangaa sana!! Wakasema imekuwaje huyu aliyeshindwa kuubeba huu mzigo mwaka jana, leo hii ameweza; tena kirahisi tuu!! Baba yake alipoona kuwa ameweza kuubeba ule mzigo na kuuweka juu ya ukuta alifurahi sana. Akamrithisha yule mtoto kiti cha ufalme. Akawaambia watoto wake niliwapa hii kazi nikijua ya kuwa kwa wakati ule mlikuwa hamna uwezo wa kuifanya lakini nilijua kuwa ndani yenu mna uwezo wa kuifanya kazi ile. Mlichotakiwa kufanya ni KUONGEZA UWEZO WENU, na huyu mdogo wenu aligundua hili; ameongeza uwezo kwa kufanya mazoezi ya kunyanyua vitu vizito; na ndio maana ingawa mwanzoni alishindwa kunyanyua ule mzigo lakini sasa ameweza.
NI NINI NINACHOTAKA UJIFUNZE KWENYE HUU MFANO.
Ni kwamba katika maisha tunayoishi watu wengi sana wameacha kufanya vitu ambavyo walipenda kuvifanya na vingewapa faida baada ya kushindwa mara kadhaa. Kushindwa kwao kufanya yale waliyotaka kuyafanya kuliwafanya waamini kuwa hawana uwezo wa kufanya yale waliyotaka kufanya; na wengine kuamini kuwa yale waliyotaka kufanya hayawezekani. Lakini ukweli ni kwamba wameshindwa kufanya sio kwa sababu hawawezi kufanya, ila ni kwa sababu uwezo wao wa kufanya lile jambo kwa wakati ule, ulikuwa ni mdogo. Walichotakiwa kufanya ni kuongeza uwezo kama yule kijana alivyoongeza uwezo kwa kufanya mazoezi ya kunyanyua vitu vizito. Na pia wameshindwa kufanya sio kwa sababu lile jambo walilotaka kufanya haliwezekani, ila ni kwa sababu wao ndio walikuwa hawana uwezo wa kulifanya lile jambo.
Sikia; kuwezekana kwa jambo au kutokuwezakana kwa jambo lolote lile, hakuko kwenye lile jambo, bali katika uwezo wa yule anayetaka kulifanya lile jambo. Ukimpa mtoto wa miaka 5 abebe ndoo ya maji ya lita 20 hataweza kuibeba ile ndoo. Hataweza kuibeba sio kwa sababu ile ndoo haibebeki, ila ni kwa sababu uwezo wake ni mdogo. Kwa hiyo hatuwezi kusema hiyo ndoo haibebeki eti kwa sababu yule mtoto ameshindwa kuibeba. Lakini ndoo hiyo hiyo ukimpa kijana wa miaka 18 ataweza kuibeba. Hii inamaanisha kuwa kubebeka kwa hiyo ndoo au kutokubebeka kwake hakuko kwenye hiyo ndoo, bali katika uwezo wa yule anayetaka kuibeba. Tunaliona hili swala la kuwezekana au kutokuwezekana kwa jambo hata kwa Yesu na wanafunzi wake. Neno linasema:

“14 Nao walipoufikia mkutano, mtu mmoja akamjia, akampigia magoti, akisema, 15 Bwana, umrehemu mwanangu, kwa kuwa ana kifafa, na kuteswa vibaya; maana mara nyingi huanguka motoni, na mara nyingi majini. 16 Nikamleta kwa wanafunzi wako, wasiweze kumponya. 17 Yesu akajibu, akasema, Enyi kizazi kisichoamini, kilichopotoka, nitakaa pamoja nanyi hata lini? Nitachukuliana nanyi hata lini? Mleteni huku kwangu. 18 Yesu akamkemea pepo, naye akamtoka; yule kijana akapona tangu saa ile. 19 Kisha wale wanafunzi wakamwendea Yesu kwa faragha wakasema Mbona sisi hatukuweza kumtoa? 20 Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu. 21 [Lakini namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga.] (Mathayo 17:14-21). 

Wanafunzi wa Yesu walishindwa kutoa pepo. Tusingeweza kusema kuwa pepo lile haliwezi kutoka, eti kwa sababu wanafunzi wale wameshindwa kumtoa. Walishindwa kumtoa si kwa sababu ilikuwa haiwezekani kumtoa yule pepo, ila ni kwa sababu wale wanafunzi walikuwa hawana uwezo wa kumtoa kwa wakati ule. Pepo yule yule ambaye wanafunzi wa Yesu walishindwa kumtoa, pepo huyo huyo Yesu alimtoa. 
Baada ya kushindwa kumtoa yule pepo wanafunzi wa Yesu walimuuliza Yesu; ni kwanini sisi tumeshindwa kumtoa ? Yesu akawajibu ni kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Akawaambia namna hii haitoki ila kwa kusali na kufunga. Kwa maana nyingine alikuwa anawaambia kuwa wanatakiwa waongeze uwezo kwa kusali na kufunga ili waweze kutoa aina ile ya pepo. 
Wanafunzi wa Yesu baada ya kugundua ile siri ya kuwa wanatakiwa kuongeza uwezo waliitendea kazi, na tunaposoma maandiko hatuoni mahali popote tena ambapo wanafunzi wale wakishindwa kutoa tena pepo; ila tunaona wakifanya miujiza mikubwa zaidi ya kutoa pepo. Walifikia hatua ya kufufua maiti. Maandiko yanasema,

“Na mwanafunzi mmoja alikuwako Yafa, jina lake Tabitha, tafsiri yake ni Dorkasi (yaani paa); mwanamke huyu alikuwa amejaa matendo mema na sadaka alizozitoa. 37 Ikawa siku zile akaugua, akafa; hata walipokwisha kumwosha, wakamweka orofani. 38 Na kwa kuwa mji wa Lida ulikuwa karibu na Yafa, nao wanafunzi wamesikia ya kwamba Petro yuko huko, wakatuma watu wawili kwake, kumsihi na kusema, Usikawie kuja kwetu. 39 Petro akaondoka akafuatana nao. Alipofika, wakampeleka juu orofani wajane wote wakasimama karibu naye, wakilia na kumwonyesha zile kanzu na nguo alizozishona Dorkasi wakati ule alipokuwa pamoja nao. 40 Petro akawatoa nje wote, akapiga magoti, akaomba, kisha akaelekea yule maiti, akanena, Tabitha, ondoka. Naye akafumbua macho yake, na alipomwona Petro akajiinua, akaketi. 41 Akampa mkono, akamwinua; hata akiisha kuwaita wale watakatifu na wajane akamweka mbele yao, hali yu hai.” (Matendo 9:36-40).

Kama ambavyo wanafunzi wa Yesu walitakiwa kuongeza uwezo kwa kusali na kufunga ili waweze kutoa aina ile ya pepo; vivyo hivyo na wewe unatakiwa uongeze uwezo ili uweze kufanya yale ambayo yalikushinda huko nyuma. Yalikushinda si kwa sababu hauwezi ila ni kwa sababu uwezo wako ulikuwa mdogo.

Inawezekana wewe ni tabibu(daktari) na umewahi kufanya operesheni kadhaa huko nyuma, na mafanikio ni madogo, umekata tamaa na kujiona kuwa hauko competence, nataka kukuambia kwamba you’re very competence; unachotakiwa kufanya ni kuongeza uwezo kwa kusoma medical journals na kujifunza kwa waliokutangulia waliofanikiwa kwenye field yako. Neurosurgeon Benjamin Carson maarufu kama Ben Carson, ndiye daktari wa kwanza kuwafanyia upasuaji watoto mapacha waliungana vichwa na operation hiyo ikafanikiwa. Kilichomfanya Ben Carson afanikiwe ni kuongeza uwezo kwa kusoma medical journals na kutaka kujua kilichowafanya madaktari wa mwanzo washindwe kuwatenganisha watoto walioungana vichwa ni nini. Alifanikiwa kungundua kuwa kilichokuwa kinasababisha watoto wafe ni kwa sababu ya upoteaji mwingi wa damu wakati wa upasuaji. Alipogundua hilo aliongeza uwezo kwa kujifunza kutoka kwa daktari wa moyo ni jinsi gani ambavyo anaweza kuzuia upoteaji mwingi wa damu wakati wa upasuaji. Matokeo yake ni kuwa alifanikiwa kuwatenganisha wale watoto waliokuwa wameungana vichwa.
Kama wewe ni mwanafunzi na kuna hesabu zimekuwa zikikushinda, usidhani ya kwamba hauwezi hizo hesabu, unachotakiwa ni kuongeza uwezo kwa kufanya mazoezi mengi zaidi kuhusiana na hiyo topic. Si unakumbuka kuhusu kukariri table, mwanzoni ulihisi kama hautaweza kukariri table zote kuanzia ya 1 hadi ya 12; lakini ulipoongeza uwezo kwa kuongeza bidii ya kujifunza hizo table, leo hii ziko kichwani. Hata ukiamshwa usingizini unazitaja bila kigugumizi. 
Kama wewe ni mkulima; ongeza uwezo kwa kujifunza njia za kisasa za ukulima ili uweze kuongeza kipato chako. Tembelea mashamba ya wakulima wengine ambao wako juu yako kiutaalamu na kujifunza kutoka kwao. 
Kama wewe ni mwalimu, ongeza uwezo kwa kusoma sana vitabu mbalimbali vya masomo unayofundisha. Kwa wale ambao A level wamesoma chemistry shule za Dar, au ambao walikuwa wanasoma tuition Dar, miaka ya 2000 kurudi nyuma, naamini jina la Mwalimu Mkandawile, na Mama Shija sio mageni kwao. Hawa ni moja kati ya walimu the best katika somo la chemistry kwa wakati ule. Ni kwanini walikuwa the best ? Ni kwa sababu waliongeza uwezo.
Kama wewe ni mpishi, ongeza uwezo kwa kujifunza aina tofauti tofauti za mapishi. Kama ulikuwa hujui kutengeneza Italian pizza, tafuta mpishi mwenzako mwenye ujuzi huo.

Kama wewe ni mjasiriamali ongeza uwezo kwa kujifunza kutoka kwa waliokutangulia na kusoma majarida yanayohusiana na aina ya bidhaa unazozalisha .
KWA VILE KIMEKUSHINDA, HAIMANISHI KUWA HAUWEZI !! INAMANISHA KUWA UWEZO WAKO NI MDOGO. HIVYO ONGEZA UWEZO KWA KUJIFUNZA ZAIDI NA HATIMAYE UTAWEZA.  
Mungu wangu akubariki.
Mwalimu na Mchungaji Gibson Gondwe.

6 thoughts on “Ukishindwa, Ongeza Uwezo!

  1. MUNGU na awabariki sana kwa ujumbe mzuri

    ujumbe huu unafundisha na kujenga

    2016-10-13 15:05 GMT+03:00 Strictly Gospel :

    > Strictly Gospel posted: ” Nakumbuka ilikuwa ni tar 29/9 mwaka huu, > nilipoamka asubuhi, nikiwa ninawaza juu ya baadhi ya mambo ambayo > niliyafanya lakini nikashindwa. Nikawa najiuliza ni kwanini nilishindwa ? > Je ni kwa vile yale mambo hayawezekani ? Nikasikia sauti ndani yangu in” >

Andika maoni yako

Fill in your details below or click an icon to log in:

WordPress.com Logo

You are commenting using your WordPress.com account. Log Out /  Change )

Google photo

You are commenting using your Google account. Log Out /  Change )

Twitter picture

You are commenting using your Twitter account. Log Out /  Change )

Facebook photo

You are commenting using your Facebook account. Log Out /  Change )

Connecting to %s