Walioteketeza kanisa Israeli wakamatwa!

Polisi wa Israel wamewakamata watu kadha waliochoma kanisa mwezi uliopita katika bahari ya Galilaya ambapo ni eneo linapoaminika Bwana Yesu Kristo aliwalisha watu maelfu mikate na samaki.

Watu hao walipochoma ukuta wa kanisa hilo waliandika maandishi ya kiyahudi kuudhalilisha Ukristo na kwa mujibu wa maafisa wa upelelezi wamesema hao ni Wayahudi wenye msimamo mkali.

–BBC

Raisi wa Gambia atangaza kuwashughulikia mashoga!

Raisi wa Gambia Yahya Jammeh ametangaza hadharani kwamba hataona huruma kwa watu wanaojihusisha na vitendo vya kishoga. Ambapo mwishoni mwaka jana alisaini sheria ya kuwafunga maisha watakaopatikana na hatia.

Hata hivyo, suala la ushoga bado limekuwa gumzo duniani ambapo nchi mbali mbali kuzua mijadala na Imani ya wakristo kuyumbishwa kwa baadhi yetu, watumishi wa Mungu pia wametoa matamko yao hadharani kupinga na kusimama na Neno la Mungu lakini pia kuna wengine ambao wanawatetea mashoga na kuwataka watu wawapende na kutowatenga maana si wao waliojiumba.

Wakati haya yakiendelea, sisi tuzidi kumtazama Bwana Yesu atukute tayari hata ajapo.

 

Mifupa Ya Bwana Yesu Kristo Haiwezi Kupatikana Mahali popote!!!!!!

Shetani hataacha kulishambulia kanisa lakini kama watu tunaoishi kwa Imani na siyo kwa kuona, Imani yetu haitayumba. Hivi sasa kuna majadiliano yanayoendelea kuhusu kupatikana mifupa ya Bwana Yesu na maneno mengi ya kulitikisa kanisa, utakaposikia hayo mwambie shetani imeandikwa “Malaika akajibu, akawaambia wale wanawake, Msiogope ninyi; kwa maana najua ya kuwa mnamtafuta Yesu aliyesurubiwa. Hayupo hapa; kwani amefufuka kama alivyosema. Njoni, mpatazame mahali alipolazwa” Mathayo 285-6

Haitapatikana mifupa ya Bwana Yesu Kristo mahali popote maana Yu Hai….Hakuoza kwenye kaburi bali alifufuka, alikufa akazikwa na siku ya tatu akafufuka. “tena kama Kristo hakufufuka, basi kuhubiri kwetu ni bure na imani yetu ni bure” 1 Wakorintho 15:14

Na tutasikia mengi, lakini kikubwa tusisahau tunaishi kwa Imani na Imani yetu imejengwa kwenye msingi Imara ambao ni Bwana Yesu Kristo mwenyewe.

Raisi Kikwete azungumzia mahakama ya Kadhi!

Rais Jakaya Kikwete akifungua mkutano wa viongozi wa Kamati ya Amani Mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC) jijini Dar es Salaam jana. (Picha na Freddy Maro).

Rais Jakaya Kikwete akifungua mkutano wa viongozi wa kamati ya Amani mkoa wa Dar es Salaam uliofanyika katika ukumbi wa Mikutano wa Kitaifa wa Julius Nyerere (JNICC) Dar es Salaam juzi

 

RAIS Jakaya Kikwete amefafanua msimamo wa Serikali katika mjadala unaoendelea wa Mahakama ya Kadhi, na kuweka wazi kuwa Serikali haina mpango wa kuianzisha, wala kuiendesha.

Mbali na hiyo, Rais Kikwete ambaye jana alizungumza na Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Dar es Salaam, pia alielezea kusikitishwa kwake na tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania, lililowaelekeza waumini wao kupigia Katiba Inayopendekezwa kura ya Hapana.

Akifafanua suala la Mahakama ya Kadhi, Rais Kikwete alisema Serikali ina msimamo wa mambo mawili katika mahakama hiyo.

Kwanza, alisema Serikali haina mpango wa kuianzisha na kuiweka katika Katiba na pili, haihusiki kuiendesha na badala yake, Waislamu wenyewe ndio watakaoiendesha.

Alisema kimsingi, mahakama hiyo ilikuwepo kabla ya Uhuru na kinachotakiwa kuzungumzwa ndani ya Bunge, ni Sheria ya Kutambua Uamuzi Unaofanywa na Kadhi.

Alifafanua zaidi kuwa Mahakama hiyo ya Kadhi, haihusiki na mambo ya jinai, isipokuwa mambo ya kijamii ikiwemo talaka, mirathi na mengine ya aina hiyo.

Alitoa mfano wa Sheria ya Kiislamu, iliyokuwepo tangu zamani, ambayo inatambua chombo hicho na kusisitiza kuwa kinazungumzwa, ni uamuzi unaofanywa na Kadhi utambulike tu.

Katika mfano huo, alisema Muislamu ukigombana na mke wake, kuna mabaraza ya usuluhishi ambayo huyo mwanamke atapaswa kwenda, ila wakishindwa na ataomba talaka ambayo inaidhinishwa na Kadhi, ambaye ndiye msajili wa vyeti vya ndoa kwa Waislmau.

Baada ya kutoa ufafanuzi huo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Shehe Alhad Musa, alimshukuru Rais Kikwete kwa ufafanuzi alioutoa na kusema Wakristo na Waislamu siku zote ni wamoja na wataendelea kuishi kwa amani, furaha na ushirikiano.

Katika hilo, Shehe Alhad alinukuu Biblia katika Kitabu cha Mathayo tano, mstari wa 25, ambao unasema; “Patana na mshitaki wako, mngali njiani, asije akakupeleka kwa Kadhi na Kadhi akakukabidhi kwa Polisi na Polisi akakutupa korokoroni.”

Katiba Pendekezwa

Akizungumzia Katiba Inayopendekezwa, ambayo inasubiri kupigiwa kura na wananchi, Rais Kikwete alisema Katiba hiyo imewakilisha vitu vingi kuliko Katiba iliyopo.

Alifafanua kwamba Katiba Inayopendekezwa, imeweka haki za makundi mbalimbali ya jamii, kuliko iliyopo na kuongeza kuwa yeye binafsi ameisoma na kurudia kuisoma, lakini hajaona mahali popote ambapo ina kasoro.

Alisema isingekuwa rahisi kuweka maoni ya kila mtu katika Katiba, na kufafanua kuwa yale ambayo hayajawekwa sasa hivi, utafika wakati wake na yatawekwa.

Alibainisha kuwa haikuwa rahisi kwa maoni ya kila mtu kuingia katika Katiba Inayopendekezwa, kwani hata CCM ilikuwa na mambo 60 waliyopendekeza, lakini kati ya hayo ni 12 tu yaliyoingia.

Rais Kikwete alisema Katiba sio Msahafu au Kurani, ambayo haiwezekani kubadilishwa hata nukta. Alitoa mfano wa Zanzibar, kwamba wakati kuunda Muungano, yapo mambo yalionekana ni muhimu kubakia katika Muungano, lakini kadri muda ulivyokwenda yameondoka.

Jukwaa la Wakristo

Akizungumzia tamko la Jukwaa la Wakristo Tanzania, Rais Kikwete alisema amehuzunishwa na kufadhaishwa na tamko hilo la viongozi wa dini la kutaka waumini wao wajiandikishe kwa wingi, lakini wapige kura ya Hapana kwa Katiba Inayopendekezwa.

Tamko hilo lilitolewa na jukwaa hilo linaloundwa na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC) na Baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT).

Rais Kikwete alisema, tamko hilo litakuwa pia limekwaza waumini, kwa kuwawekea mipaka ya kidemokrasia na kukwaza hata viongozi wenyewe.

Alitoa mfano kwamba kwa tamko hilo, muumini hataweza kusimama na kumwambia kiongozi wa dini asiwaingilie katika uamuzi, kwa kuwa kupiga kura ni haki ya kikatiba ya kila mtu, na ikitokea hivyo, hata kiongozi husika atakwazika.

Subira kwa NEC

Kuhusu uwezekano wa Kura ya Maoni kufanyika Aprili 30 kama ilivyotangazwa na Serikali, huku kazi ya kuandikisha wapigakura ikiendelea kusuasua, Rais Kikwete alisema Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), inayoratibu uandikishaji wa wapigakura, itazungumza kuhusu walipofikia wakati muafaka ukifika.

Amani Kuhusu amani ya nchi, Rais Kikwete alisema viongozi wa dini pia wa jukumu kubwa la kuimarisha amani ya nchi.

Katika utekelezaji wa jukumu hilo, Rais Kikwete aliwataka viongozi hao wajaribu kuepuka kutumiwa na watu wenye nia mbaya, kwa sababu wanafahamu kuwa viongozi wa dini wana ushawishi katika jamii na wana watu wengi nyuma yao.

Alisema machafuko yatakayotokana na mvurugano wa kidini, hakuna mtu atakayeweza kuyazuia, hivyo ni vyema viongozi hao waendeleze mshikamano.

Alitoa mwito kwa mikoa mingine nchini, kuunda kamati za amani kama ilivyo Kamati ya Amani ya Viongozi wa Dini mkoani Dar es Salaam.

Kadhi yuko Kibiblia

Akitoa neno la shukrani, Makamu wa Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Askofu Valentino Mokiwa wa Kanisa Anglikana Tanzania, alielezea kufurahishwa na maelezo ya kina yaliyotolewa na Rais Kikwete.

Alisema pia alifurahishwa na maneno aliyonukuu Shehe Alhad kutoka Mathayo 5:25 yaliyoonesha kwamba kumbe Mahakama ya Kadhi ni ya Wakristo, maana ipo katika Biblia, na kufanya ukumbi uvunjike kwa kicheko.

CHANZO: HABARI LEO

Askofu Gwajima kufikishwa kwenye vyombo vya sheria!!

ASKOFU GWAJIMA ATAKIWA KUHOJIWA NA JESHI LA POLISI KUHUSU TUHUMA ZA KASHFA NA MATUSI DHIDI YA KALDINARI PENGO.

Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linamtaka Askofu JOSEPHAT GWAJIMA wa Kanisa la Ufufuo na Uzima afike haraka katika kituo cha Polisi cha Kati ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa mahojiano kuhusu tuhuma za  kashfa na matusi.

Tumepokea malalamiko ya kukashifiwa na kutukanwa hadharani Mwadhama Kaldinari Polycarp Pengo ambaye ni kiongozi wa Kanisa Katoliki nchini Tanzania. Kupitia mitandao mbalimbali ya kijamii kama vile WhatsApp na mingineyo kuna sauti iliyorekodiwa (audio) na picha za video (Video Clip) zikimuonyesha Askofu Gwajima akimkashfu na kumtukana kwa maneno makali Kaldinari Pengo katika hali ambayo pia imewaudhi watu wengine.

Baada ya tukio hilo juhudi mbalimbali zimekuwa zikifanyika katika hali ya kawaida ili kumpata Askofu Gwajima bila mafanikio na hivyo yeye mwenyewe sasa anatakiwa aende akaripoti haraka kwa Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam bila kukosa.

Ni muhimu sana kwa Askofu Josephat Gwajima kuripoti yeye mwenyewe badala ya Kutafutwa au kukamatwa ili ajibu tuhuma hizo kutokana na nafasi yake katika jamii.
Jalada la uchunguzi limefunguliwa na upelelezi wa shauri hili unaendelea ili sheria. ichukue mkondo wake.

S. H. KOVA,
KAMISHNA WA POLISI KANDA MAALUM
DAR ES SALAAM

Video iliyoleta matatizo