Injili Ruksa kuhubiriwa vilabu vya pombe

3137de4f-218b-4125-8a76-506085aaa093

Mkuu wa Mkoa Wa Dar es salaam Mhe. Paul Makonda tarehe 8 mwezi Wa tisa ametoa kibali kwa Watumishi wa Mungu wa Dini zote kuhubiri na kutangaza neno la Mungu kwenye Sehemu za Club, Disko na Kumbi za Starehe ili neno la Mungu lizidi kuenea na kuwafikia watu wote jambo litakalosaidia kujenga jamii inayomjua Mungu.
_
RC Makonda amesema Mtumishi wa Mungu atakapohitaji kuhubiri mziki utazimwa kwa muda wa Nusu saa na baada ya hapo watu wataendelea na starehe zao wakiwa tayari wamepokea Neno la Mungu na kuahidi kuwa Mmiliki wa Club atakaemkatalia Mtumishi Kuhubiri RC Makonda atamwombea Mtumishi huyo na ikibidi atamsindikiza.
_
Hatua hiyo ya RC Makonda imekuja baada ya kubaini uwepo wa Idadi kubwa ya watu kwenye sehemu za starehe na pindi watu hao wakienda Makanisani na Misikitini wanaishia kusinzia na wengine wanakuwa wamechoka kiasi cha kushindwa kulisikiliza kwa ufasaha neno la Mungu.
_
Hayo yote yalijiri wakati akizungumza na Waumini wa Kanisa la Arise and Shine linaloongozwa na Mtumishi wa Mungu Apostle Boniface Mwamposa.

Tuukomboe Wakati

WAFU WANAOTEMBEA

wp-1469764099794.png

WATU WA JINSI HII NI WAFU WANAOTEMBEA; INAWEZEKANA NA WEWE NI MMOJA WAO !!

Moja kati ya kauli zenye kutatanisha ambazo Yesu aliwahi kuziongea ni hii ambayo Yesu alimwambia mwanafunzi wake “WAACHE WAFU WAWAZIKE WAFU WAO” (Mathayo 8:22), mara baada ya mwanafunzi yule kumwomba Yesu ruhusa ya kwenda kumzika baba yake. Hii kauli katika akili za kawaida za kibinadamu ni ngumu sana kueleweka, haswa kwa kipindi kile. Sidhani kama yule mwanafunzi alimwelewa Yesu. Nadhani moja kati ya maswali aliyojiuliza ni “inawezekanaje mfu akazika mfu ?” Inawezekanaje maiti ikazika maiti nyenzake ? Hii ilikuwa ni sentensi tata ambayo kwa akili za kawaida za kibinadamu ilikuwa haieleweki. Hii kauli aliyoitoa Yesu inatokana na namna mambo, vitu, na watu wanavyoonekana katika ulimwengu wa roho. Ipo tofauti kubwa kati ya namna mambo, vitu na watu wanavyoonekana katika ulimwengu wa kawaida, na namna mambo, vitu na watu wanavyoonekana katika ulimwengu wa roho.

Ni nini tofauti kati ya ulimwengu wa roho na ulimwengu wa kawaida ? Ulimwengu wa kawaida ni ulimwengu ambao, viumbe vyake, na vitu vilivyomo katika huu ulimwengu vinaonekana kwa macho ya kawaida, vinahisika kwa ngozi, vinaonjeka kwa ulimi, vinanusika kwa pua, na sauti zao zinasikika kwa masikio haya ya kawaida. Ni ulimwengu ambao vitu vilivyomo vinatambulika kwa kutumia milango mitano ya fahamu (pua, macho, masikio, ulimi na ngozi).

Ulimwengu wa roho ni ulimwengu ambao hauonekani kwa macho ya kawaida, wala hauwezi kusikia sauti za viumbe vilivyomo katila ulimwengu huo kwa masikio ya kawaida. Ni ulimwengu ambao Mungu na viumbe vya kiroho vinaishi. Mungu, roho za wanadamu, malaika, shetani, na mapepo wanaishi katika ulimwengu huu. Ndio maana hauwezi kumwona Mungu kwa macho ya kawaida, wala hauwezi kuziona roho za wanadamu kwa macho ya kawaida, wala hauwezi kuwaona malaika kwa macho ya kawaida, wala hauwezi kuyaona mapepo kwa macho ya kawaida, kwa sababu wako katika ulimwengu wa roho.

Namna ambavyo mtu anaonekana katika ulimwengu wa kawaida ni tofauti na namna anavyoonekana katika ulimwengu wa roho. Anaweza akawa anaonekana ni tajiri, ananguvu, ni msafi sana, amevaa vizuri sana lakini lakini katika ulimwengu wa roho akaoneka ni mchafu, maskini, kipofu, na yuko uchi. Neno la Mungu linasema “KWA KUWA WASEMA, MIMI NI TAJIRI, NIMEJITAJIRISHA WALA SINA HAJA YA KITU; NAWE HUJUI YA YA KUWA WEWE U NYONGE, NA MWENYE MASHAKA, MASKINI, NA KIPOFU , NA UCHI” (Ufunuo wa Yohana 3:17) huyu mtu alikuwa anajiona ya kuwa yeye amevaa, ni tajiri, ana macho, ana nguvu lakini katika ulimwengu wa roho anaonekana kuwa ni kipofu, yuko uchi, na maskini, mnyonge, na mwenye mashaka.

Inawezekana mtu akawa anaonekana yuko hai katika ulimwengu wa kawaida, lakini akawa anaonekana amekufa katika ulimwengu wa roho. Neno linasema “NA NINYI MLIPOKUWA MMEKUFA KWA SABABU YA MAKOSA YENU………” (Wakolosai :213).Hawa watu walionekana kuwa wako hai katika ulimwengu wa kawaida lakini kumbe walikuwa wamekufa kwa sababu ya makosa yao  katika ulimwengu wa roho. Hii inawezekanaje? Ni kwa sababu ya jinsi binadamu alivyoumbwa. Binadamu ana aina mbili za utu. Ana utu wa ndani na utu wa nje. Neno linasema, “KWA HIYO HATULEGEI; IJAPOKUWA UTU WETU WA NJE UNACHAKAA; LAKINI UTU WETU WA NDANI UNAFANYWA UPYA SIKU KWA SIKU. (2Wakorintho 4:16). Sasa utu wa nje ni upi na utu wa ndani ni upi ? Biblia inajijibu yenyewe katika 1Wathethasalonike 5:23 neno linasema ” MUNGU WA AMANI MWENYEWE AWATAKASE KABISA; NANYI NAFSI ZENU NA ROHO ZENU NA MIILI YENU……” katika hili neno tunaona kuwa kuna NAFSI, ROHO, na MWILI. Sasa hivi vitatu NAFSI, ROHO, na MWILI, ndivyo vinavyojenga utu wa nje na utu wa ndani wa mwanadamu. Mwili ni utu wa nje, nafsi na roho vinajenga utu wa ndani.

Mwili unamwezsha mwanadamu kutenda kazi na kuwasiliana katika ulimwengu wa kawaida, wakati roho inamwesha kutenda kazi na kuwasiliana katika ulimwengu wa roho.

Wewe halisi sio huo mwili wako (utu wa nje), wewe halisi ni utu wa ndani (nafsi na roho). Ndio maana mtu anapokufa na ndugu zake wakaamua kuisafirisha maiti kuipeleka kijijini kwao utasikia wanasema  “MWILI WA MAREHEMU UTASAFIRISHWA KWENDA KIJIJINI KWAO” ni kwanini wanasema mwili wa marehemu, ni kwa sababu marehemu mwenyewe (roho na nafsi) hayupo, ameondoka na kuucha mwili wake. Uzima wa mwili wako unatokana na roho iliyoko ndani yako, mwili pasipo roho umekufa (Yakobo 2:26). Pia thamani ya mwili wako, haijalishi ni mzuri kiasi gani, au mtanashati (handsome a.k.a HB kiasi gani), thamani yake inatokana na roho iliyoko ndani yako. Siku utakapokufa ndipo na thamani ya mwili wako inaishia hapo; kama uko nje ya nchi ukafia huko na ndugu zako wakaamua kuisafirisha maiti yako, ujue kuwa haitapakiwa kwenye ndege ya abiria, itapakiwa kwenye ndege ya mizigo. Hata kama ikipakiwa kwenye ndege ya abiria, haitakalishwa na abiria wengine, itawekwa kwenye sehemu ya mizigo; kwanini ? Kwa sababu mwili hauna thamani pasipo roho !! Hata kama mumeo anakupenda kiasi gani, au mkeo anakupenda kiasi gani, roho yako ikiondoka na kutengana na mwili wako, na mwili ukageuka kuwa maiti; hawezi kukubali kulala tena na wewe kitanda kimoja; HAIJALISHI ALIKUWA ANAKUPENDA KIASI GANI.!! HAIJALISHI ULIKUWA MZURI KIASI GANI !! Hii ni kwa sababu mwili wako hauna thamani pasipo roho. Maiti hazihitajiki katika dunia hii, sehemu yao ni chini ya udongo !! Roho inapotengana na mwili tunasema mtu AMEKUFA. Huyo mtu ni MFU !! Upende mwili wako, ulishe vizuri, uvishe vizuri, lakini ROHO YAKO NDIO UNATAKIWA UIJALI ZAIDI YA UNAVYOUJALI HUO MWILI WAKO KWA SABABU HIYO NDIYO ITAKAYO SIMAMA MBELE YA KITI CHA HUKUMU SIKU MWISHO.

Kama ambavyo mwili hufa hata roho nayo huwa inakufa. Neno la Mungu linasema “NANYI MLIKUWA WAFU KWA SABABU YA MAKOSA NA DHAMBI ZENU”(Waefeso 2:1) Wafu hawa wanaozungumziwa hapa ni wale waliokufa kiroho, ni wale ambao roho zao zimekufa. Ni watu ambao hawana uzima wa milele ndani ya roho zao. Mtu yeyote ambaye hajaokoka, huyo mtu amekufa kiroho, roho yake imekufa.Tafauti ya kifo cha roho na kifo cha mwili ni kuwa, kifo cha mwili kinatokea pale roho ya mtu inapotengana na mwili wa mwanadamu,  wakati kifo cha roho kinatokea pale Roho wa Mungu (Roho Mtakatifu), anapotengana na roho ya mwanadamu. Kama ambavyo mwili ulio hai unauzima ndani yake unaotokana na roho ya mwanadamu iliyoko ndani yake, vivyo hivyo, roho iliyo hai inauzima wa milele ndani yake unaotokana na Roho Mtakatifu. Neno la Mungu linasema “NA HUU NDIO USHUHUDA, YA KWAMBA MUNGU ALITUPA UZIMA WA MILELE; NA UZIMA HUU UMO KATIKA MWANAWE. YEYE ALIYE NAYE MWANA ANAO HUO UZIMA; YEYE ASIYE NAYE MWANA WA MUNGU HANA HUO UZIMA” (1Yohana 5:11,12). Neno linasema aliye naye mwana anao huo uzima, asiye naye mwana hana huo uzima. Mtu ambaye hana uzima huyo mtu amekufa, ni mfu. Katika ulimwengu wa kawaida anaonekana yuko hai lakini katika ulimwengu wa roho anaonekana amekufa. Yesu aliwaita wale watu waliokuwa wanakwenda kuzika maiti ni wafu kwa sababu ingawa miili yao ilikuwa ina uhai uliotokana na roho zilizomo ndani yao, lakini roho zao zilikuwa zimekufa kwa sababu walikuwa hawana Roho Mtakatifu ndani ya Roho zao na hivyo kutokuwa na uzima wa milele ndani yao. Mtu yeyote ambaye hana Roho Mtakatifu ndani yake, huyo amekufa kiroho;  ni mfu kwa sababu hana uzima wa milele ndani yake. Ni maiti inayotembea!! Kuna wafu wanaotembea bungeni, ni wabunge lakini ni wafu, kuna wafu wanaotembea ikulu, wanafanya kazi ikulu lakini ni wafu, kuna wafu wanaotembea mahakamani, ni majaji, mahakimu, lakini ni wafu, kuna wafu walioko vyuoni na mashuleni, ni wanafunzi lakini ni wafu. Kama wewe hauna Roho Mtakatifu ndani yako, kwa mujibu wa neno la Mungu wewe ni mfu anayetembea. Na kwa sababu wewe ni mfu hauwezi kwenda mbinguni, mbinguni hawaingii wafu, mbinguni haziingii maiti, kwa sababu mbinguni hakuna mochwari utaishia jehanamu ya moto!!

Jiulize; kama wewe ni mfu unayetembea au la !! Kama haujaokoka basi kwa mujibu wa maandiko wewe ni mfu unayetembea, kwa sababu hauna Roho Mtakatifu ndani yako ambaye anatupa uzima wa milele; hivyo hauna uzima  wa milele ndani yako. Na kwa sababu hauna huu uzima wewe ni mfu unayetembea. Dawa ya kufufuka katika hali ya ufu ni kwa njia ya kumpokea Yesu Kristo awe Bwana na mwokozi wa maisha yako. Ukimpokea Yesu;  Roho Mtakatifu anakuja na kufanya makazi ndani ya Roho yako na hivyo unakuwa umeupata uzima wa milele katika roho yako. KWANI UZIMA HUU WA MILELE UNATOKANA NA ROHO MTAKATIFU, AMBAYE YESU ALISEMA ATAKUJA NA KUKAA NDANI YETU (Yohana 14:15-17).

Mungu akubariki !!

Mchungaji na Mwalimu Gibson Gondwe.

WAKRISTO WA JUMAPILI

mfungwa

Wakristo Wa jumapili: Hawa ni wale wanaomkumbuka Mungu siku ya Jumapili na kwenye nyumba ya ibada tu. Akitoka kanisani anamuacha Mungu anamuacha mlangoni. Anakuwa mpagani Wa kawaida mpaka Jumapili nyingine.

Hapa katikati ya wiki michanganyo kama kawaida; akifanya mambo yasiyompendeza Mungu na kutarajia kuungama ibadani Jumapili.

Ushauri:: Mpokee Kristo na umruhusu afanye makazi ndani yako,awe Bwana na mokozi wako,hapo Mungu atafanyika kuwa Wa kila siku maana atakuwa anaishi ndani yako,hautamuacha Tena pale kwenye geti la jengo la Kanisa.

Acha kuwa mkristo wa Jumapili,Bwana anakuita uende kwake. Mkabidhi maisha yako leo. Na Mungu akubariki!

Samson Chitalika

KIBURI CHA UZIMA

way-of-the-world-pride-of-life-450x450.png

Ukitaka kujua sisi binadamu ni waajabu kuliko maajabu yote duniani…kuna watu tumelewa na KIBURI CHA UZIMA.

Wakati unasaka kazi huku na kule, ulikuwa mtiifu na mnyenyekevu mbele za Bwana, huku ukimwomba na kuhudhuria kila ibada za kanisani na maombi.

Kipindi unamwomba Mungu akupe mke/mume, ulikuwa mtiifu sana mbele za Mungu. Kwa kujitoa kwake kwa kila kazi itakayojitokeza kanisani ama kwenye vikundi vya vijana/wamama.

Ukiwa unasaka mtoto huku na kule, umetembea hospitali nyingi ukitafuta suluhisho, lakini ilishindikana mpaka ukapata ushauri wa kumwomba Mungu. Kufanya hivyo ukapata mtoto kweli.

Ulipokuwa maisha yamekuvuruga, ulikuwa mwema na mwaminifu mbele za Mungu. Na uliheshimu kweli watumishi wa Mungu, na kuwaomba wakuombee kwa Mungu maana ulishaomba sana na ukaona mambo bado hayaendi. Baada ya kukusaidia kubeba mzigo huo wa kukuombea ulifanikiwa.

Ulipokuwa unanyanyaswa na maisha ya ndoa, ulikuwa mnyenyekevu na mcha Mungu mzuri sana. Na uliheshimu sana kumpa Mungu muda wako, na ilipofika siku, Mungu akasikia kilio chako.

Ulipokuwa na cheo cha chini kazini kwako, na kuishia kutukanwa ovyo na wafanyakazi wenzako. Ulikuwa mpole na mwenye huzuni nyingi, huku ukimwona Mungu amekusahau…ila uliponyenyekea mbele zake uliona mafanikio makubwa ya kuwa kiongozi kwa wale waliokuonea na kukucheka.

Ulipokuwa shule, ulikosa tumaini kweli la kuendelea na masomo yako, na kuona ndoto zako ndio zimezimika kama watoto wengine walioishia darasa la Nne C kwa kukosa pesa ya kununulia hata pencil.

Lakini wewe Mungu alikuinulia mtu wa kukusaidia kutimiza ndoto zako.

Ulipokuwa kwenye nyumba za kupanga, na kutolewa vyombo kila siku. Kwa kukosa kodi ya nyumba, ulikuwa mnyenyekevu na mtu mwenye kutia huruma sana sana. Lakini Mungu alikupa maarifa ya namna ya kuondokana na hiyo hali, na sasa upo ndani ya nyumba yako.

Cha kushangaza na kusikitisha, leo hii umeachana na mambo ya Mungu. Na kuona ni ushamba na kupoteza muda kusali sali, na kuomba omba.

Umefika kipindi umeanza kuwakejeli wengine kuwa wanaomba omba, kwa sababu wana shida sana.

Binafsi hukumbuki mara ya mwisho ulimpa lini Mungu muda wako wa kukaa naye katika maombi na kusoma na kusikiliza neno lake. Umebaki na maombi ya kwenye Radio na Tv.

Nyakati zile ulikuwa unafunga tatu kavu, ila sasa hivi hata maombi ya masaa 12 yanakushinda. Ukiulizwa unasema huna muda, na huwezi kujitesa bure na njaa.

Baada ya mafanikio, familia yako huikumbuki tena..wala mke/mume wako huna habari naye. Mwanaume hujui mke wako anakula nini na watoto wenu, kazi yako imebaki kuruka viwanja vya starehe.

Neno la Mungu, linatusihi sasa usimsahau Mungu wako wakati wa mafanikio yako. Usiinue mabenga na kusema ulifanikiwa kwa akili zako, na nguvu zako.

Geuka umrudie Mungu wako, kabla nyakati mbaya hazijaja.

Omba msamaha kwa familia yako, na Mungu wako. Acha mafanikio yako yamtukuze Mungu, kwa kuwabariki wengine.

Mungu atusaidie kuelewa haya.

Ndg. Samson Ernest