KUMJUA MUNGU

PhotoGrid_1568106704690

KUMJUA MUNGU NI CHANZO CHA MAFANIKIO YAKO YOTE
21 Mjue sana Mungu, ili uwe na amani; Ndivyo mema yatakavyokujia.
Ayubu 22:21

Kumjua Mungu ni kuwa na ufahamu wakutosha kumuhusu Mungu.Unafamu yeye ni nani ,ana nguvu kiasi gani, uweza alonao nk hii inatufanya tujiweke chini ya utawala wake Na kutoa Maisha yetu yote kwa kwake .

Kufanikiwa kibiblia ni kuwa vizuri maeneo yote kwenye maisha Na wanadamu wengi tunapenda kufanikiwa, kila mmoja yupo busy eneo Lake kuhakikisha anafanikiwa ila kutokana na andiko hapo juu tunapaswa kumjua Mungu sana sio kidogo na mafanikio yatakuja tu sio kuyatafuta.
Ni vizuri kujua kuwa Mungu ametuandalia kila tunachohitaji kwenye maisha yetu na kinapatikana kwaajili yetu ila tunavielewa na kuvipata kwa kumjua Mungu.
3 Kwa kuwa uweza wake wa Uungu umetukirimia vitu vyote vipasavyo uzima na utauwa, kwa kumjua yeye aliyetuita kwa utukufu wake na wema wake mwenyewe.
2 Petro 1:3

Uweza wa uungu umetukirimia (Umetupatia) kila tunachohitaji kwaajili ya uzima(maisha yetu ya mwilini) na utauwa(maisha yetu ya Rohoni) kwa kumjua yeye. Hii inamaana hivi vitu hatuwezi kuvipata kama hatamjua yeye aliyetuita kwaajili ya utukufu wake mwenyewe.

Weka shauku, matamanio yako kumjua sana huyu Mungu mwenye vitu vyako vyote unavyovihitaji. Usiweke jitihada kutafuta vitu weka jitihada ya kumtafuta Mungu mwenye vitu.
#ZaidizaidinikufahamuYesunijuependolakonawokovuwakokamili

Na mchungaji Imani Boaz

Kufurahia thawabu ya kashfa ya uongo….

_32

Amini usiamini! Kumbe kuna thawabu kwa ajili ya kutungiwa kashfa za uongo! Haya si maneno yangu binafsi. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyesema haya kama ilivyoandikwa hapa chini: “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.” (MT.5:11-12) Maneno mazito ni haya ya “watakapowashutumu…….na kuwaudhi……..na kuwanenea……. Kila NENO BAYA kwa UONGO….”

Kuna kushutumiwa na kulaumiwa na kunenewa vibaya lakini kwa mambo ya kweli, kwa makosa ya kweli. Hii ni kawaida kila mkosaji kulaumiwa kwa makosa yake. Lakini si rahisi, na si kawaida, mtu asiye na hatia kabisa, kushutumiwa, kulaumiwa na kunenwa vibaya kwa tuhuma za kashfa za uongo. Tena tuhuma ambazo wahusika wanaweka mikakati ya makusudi huku wamepania kwa makusudi kumdhalilisha, kumvunjia heshima yake, huyo asiye na hatia “maskini wa Mungu” ili tu aabike, aadhirike, aharibikiwe, na ikiwezeka afilie mbali!!! Kisa ni nini? Ati kwa kuwa tu yeye ni “mchaji Mungu”! Ati anawakera mno kwa kuwa ni “mshika maadili ya kibiblia”! Ati kwa kuwa kajitoa mhanga kutangaza habari za imani yake aliyo nayo kwa Mungu wake!!! Tena wengine wamemkasirikia kwa madai ati “anajifanya mtakatifu sana, hataki kushiriki maovu; hatoi wala kupokea rushwa; kajitenga na ufisadi kwa sababu ya imani yake kwa Yesu!” Basi, kwa ajili hiyo tu, zinasukwa njama na kutengenezwa tuhuma za kashfa za uongo dhidi yake; ili tu kumkomoa na kumkomesha asiendelee na msimamo wake wa kimaadili. Haya ndiyo Yesu alimaanisha aliposema, “….na kuwanenea kila neno baya kwa uongo KWA AJILI YANGU..”

Sasa uzito wa ujumbe huu sio kusingiziwa na kuzushiwa kwa ajili ya imani. Uzito wa ujumbe huu ni jinsi “mtendewa, msingiziwa, mzushiwa,” anavyoagizwa jinsi ya kuchukuliana na hali ya namna hii. Anaagizwa na Yesu kwamba AFURAHI NA KUSHANGILIA AKITUNGIWA KASHFA ZA UONGO KWA AJILI YA KRISTO! Hapooooo!!! Kufurahi na kushangilia!!!! “Ee Bwana Yesu nisaidie miye mtu dhaifu sanaa naomba unirehemu tu katika hili! Ninatamani kupata thawabu zako, ila kwa thawabu hii ninahitaji neema yako. Maana udhaifu wangu huu unaweza kunikosesha hata thawabu nyingine nisipokuwa makini sana katika eneo hili..AMINA”

Duh! Samahani kwa kusali hadharani lakini najua ujumbe huu una walengwa wake. Napenda kuhitimisha kwa kusema ya kwamba, tuache unafiki, ukweli inauma sanaaaa kunenwa vibaya kwa uongo. Lakini ni kwa sababu ya maumivu ya jinsi hii ndiyo maana Yesu naye kaweka njia ya kupona maumivu hayo. Anatutaka tuwe na mtazamo tofauti pale tunapopatwa na majaribu ya jinsi hii. Kwanza kila unaposingiziwa kwa uongo, na wewe unajua kuwa huo ni uzushi, kumbuka shahidi wako wa kwanza ni Mungu. Wakati watu wengine wasiojua ukweli wanatapokuwa wanakulaumu na kukutukana kwa kashfa ambazo chanzo chake sio wewe; kumbuka, laana zao zitageuka kuwa baraka kwako mbele za Mungu. Lakini ili baraka hizo zidumu lazima kwanza uishinde hisia ya uchungu na maumivu ya nafsi, kwa kuwasamehe bure wale wanaokuudhi. Unaishindaje hisia hiyo hasi ya uchungu? Kwa kuruhusu hisia chanya ya furaha, na hata kushangilia kwa ajili ya THAWABU KUBWA INAYOKUSUBIRI MBINGUNI.

Msomaji wangu, usikubali kumaliza mwaka huu ukiwa na uchungu moyoni kwa sababu ya kashfa za uongo. Sisi sote tutakutana siku moja mbele za Kiti cha hukumu cha Kristo na ukweli utajulikana wakati huo. Hivi sasa furahi na kumshukuru Mungu kwa kila jambo kwa kuwa hayo ndiye mapenzi yake pale tunapoteswa isivyo haki….. “Maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivya haki.” (1 Pet.2:19) Nakutakia baraka za mwaka mpya. Ubarikiwe sana

– Pastor Imori

MANENO ya KINYWA CHAKO ni CHAKULA CHAKO!

“Ee BWANA, uweke mlinzi kinywani pangu, Mngojezi mlangoni pa midomo yangu” (Zaburi 141:3).

“Mtu hulifurahia jibu la kinywa chake; Na neno linenwalo wakati wa kufaa ni jema kama nini!” (Mithali 15:23)

“7 Kinywa cha mpumbavu ni uharibifu wake, Na midomo yake ni mtego wa nafsi yake…. 20Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake” (Mithali 18: 7, 20).

“Maana twajikwaa sisi sote pia katika mambo mengi. Mtu asiyejikwaa katika kunena, huyo ni mtu mkamilifu, awezaye kuuzuia na mwili wake wote kama kwa lijamu” (Yakobo 3:2).

Nimesoma maombi ya Daudi kwa Mungu wake nikaona jambo la muhimu maishani mwa mwanadamu; Maneno ya kinywa!

Kumbe kuna uhusiano mkubwa kati ya MAFANIKIO ya mtu na MANENO yake? Naam, hili ni dhahiri, japo mara nyingi watu wanadhani kujinenea maneno ya laana tu ndio shida, kumbe, hata kunena jambo jingine hovyohovyo linaweza kuathiri hatma yako! Japo hukujilaani ila umefungua kinywa chako kwa upumbavu.

Basi nikaangalia na kuona jinsi ambavyo mara nyingi watu hufanya mzaha, na kufumbua vinywa vyao bila kufikiri, kumbe, maneno yao ni chakula chao! Wengi wana njaa hata sasa kwa sababu ya maneno yao tu!

Ndipo Daudi akaomba ULINZI wa Mungu kinywani mwake, naam, na mwanaye Suleiman akasema siri hii kwamba, “Tumbo la mtu litajazwa matunda ya kinywa chake; Atashiba mazao ya midomo yake”.

Basi nikatazama tena nakujiuliza kwanini neno la kinywa liwe mtego? kwanini limkamate mtu na kumwangusha? Je! Utalipimaje kila neno kwamba lafaa? Nikaona mambo mawili: Kwanza, muda wa kulisema jambo (Mithali 15:23), na pili, kusudi la kulisema hilo jambo.

Kama UKAMILIFU wa mtu hupimwa kwa maneno yake (Yakobo 3:2), basi nikaona thamani katika maneno kama ilivyo katika matendo; yote mawili yanahitaji MLINZI ambaye ni Mungu. Lakini je! Waweza kulinda maneno na matendo bila kulinda mawazo ya moyo wako? Nikaona jambo hili, aliyefanikiwa kulinda MAWAZO ya moyo wake, ameweza vyote.

Frank P. Seth

MUNGU ANATAFUTA WAMWABUDUO HALISI.

Yohana 4:24  Mungu ni Roho, nao wamwabuduo yeye imewapasa kumwabudu katika roho na kweli.

Mpendwa wangu, ubarikiwe sana kwa kupita mara kwa mara kwenye huu ukuta kujichotea mafundisho yenye uzima ambayo Mungu wa mbinguni ananijalia kuyaweka kwa kadiri Roho Wake anavyonisukuma kwenye utu wangu wa ndani sawa sawa na neema Yake niibebayo maishani mwangu.

Katika somo hili nataka tuangalia kwa sehemu kuhusiana na hili jambo muhimu na nyeti sana kwa mwamini, Kumwabudu Mungu.

Kama umeshawahi kupata fursa au bahati ya kuwepo mahali watu wanapomwabudu Mungu kiukweli kuna mambo ambayo lazima umekuwa ukiyaona katikati ya watu wanao mwabudu Mungu katika uhalisi wake ambayo yamekusaidia kuanza kupata mwanga kidogo juu ya kuabudu.

Mara nyingi ukikuta watu wanamwabudu Mungu utaona wamenyanyua mikono yao juu. Unaweza ukaona watu wakiwa wamenyanyua nyuso za kuelekea juu na wakati mwingine kuna machozi yanawatoka lakini sio kila kunyayua uso juu na kutokwa machozi ni kumwabudu Mungu. Unaweza ukawaona watu katika kumwabudu Mungu wamepiga magoti lakini sio kila kupiga magoti ni kumwabudu Mungu. Unaweza ukawaona watu wamesujudu au kulala kifudi fudi mbele za Bwana lakini sio kila kusujudu au kulala kifudi fudi ni kumwabudu Mungu.

Kwa maneno rahisi sana kueleweka na kila mtu, kuabudu ni kila kinachotokea kwa mwanadamu aliyekombolewa uwepo wa Mungu unapojidhihirisha kwake.

Kinyume na fikra za wengi, uwepo wa Mungu hauletwi na kuabudu bali kuabudu ni mwitikio wa mwanandamu kwa uwepo wa Mungu uliyodhihirishwa. Uwepo wa amungu ukijidhihirisha mwitikio wa mwanadamu kwa uwepo huu ndiko kuitwako kuabudu. Sasa sio kuabudu kunakoleta uwepo wa Mungu bali ni sifa ndiyo huleta uwepo wa Mungu.

Na Wewe U Mtakatifu, Uketiye juu ya sifa za Israeli. (ZAB. 22:3 SUV).

Israeli au watu Wake Mungu wakimsifu, ndiko kunakoleta uwepo Wake katika maisha yao au mahali pale walipo.

Unaweza ukamfundisha mtu kusifu lakini huwezi ukamfundisha mtu kuabudu. Kusifu kwafundishika bali kuabudu hukamatika tu maana ni kitu ambacho kinafanya na roho yako japo hujidhihirisha kwenye nafsi na mwili wako lakini mahali hasa ambapo ibada ya kweli huanzia ni kwenye roho yako.

Mungu hawatafuti tu wamwabuduo bali anawatafuta wamwabuduo halisi. Hii ni dhahiri kuwa kuwa waabudu halisi na kuna waabudu wa kuegeza. Wa kuegeza wanajua kila kitu ambacho inabidi kifanyike ili kuabudu. Wanajua nyimbo za kutumia, wanajua jinsi ya kujiweka ili tu waonekane wanaabudu. Lakini bila uwepo wa Mungu kujidhihirisha kwanza hapawezi kuwa na kuabudu halisi hata siku moja.

Kunaweza kuwepo mfano wa kuabudu lakini hapawezi kuwa na kuabudu halisi.

Moja ya vitu ambavyo vinasababisha kuabudu kwako na kwangu kuboreke zaidi ni kiasi ambacho binafsi unamjua Mungu naye mwabudu. Ukimjua Mungu unaye mwabudu utajua jinsi sahihi ya kumwitikia anapojidhIhirisha na uwepo Wake. Ndo maana Yesu akamwambia yule mwanamke Msamaria, Nyie mnaabudu msichokijua, sisi tunaabudu tukijuacho kwa maana wokovu watoka kwa Wayahudi.

Kumjua kwako unayemwabudu itaongeza sana uwezo wako wa kumwabudu katika Roho na Kweli. Hapa cha kuelewa hapa kumwabudu Mungu katika Roho na Kweli ni kumwabudu kwa msaada wa Roho Wake na Kweli Yake na vyote viwili hivi vinakusaidia kuongeza kumjua kwako unayemwabudu. Kwa kadiri umuuavyo ndivyo utakavyojua ikupasavyo kuitika anapojidhihirisha kwako. Hilo hawezi kukufundisha mtu ni jambo linatokea tu uwepo Wake ukidhihirishwa.

Sasa nisilimalize hili nilisemalo bila kutaja mambo yanayoweza kukuzuia usimwabudu Mungu. Yapo kadhaa lakini leo naomba niyasemee mawili.

1. Utumwa au kifungo kinaweza kukuzuia usimwabudu Mungu.

Uapo aliomwapia Ibrahimu, baba yetu,
Ya kwamba atatujalia sisi,
Tuokoke mikononi mwa adui zetu,
Na kumwabudu pasipo hofu,
Kwa utakatifu na kwa haki
Mbele zake siku zetu zote. (LK. 1:73-75 SUV).

Ina maana kwa mujibu wa andiko hilo hapo juu kama asipotujalia kuokoka mikononi mwa adui zetu hatutaweza kumwabudu Mungu pasipo hofu. Au hatutamwabudu kabisa au kama tukimwabudu tunamabudu katika hofu ya hao maadui na palipo na hofu pana adhabu na yeye aogopaye hajakamilishwa katika upendo.

Ona maneno ambayo Mungu alimwambia Musa.

Akasema, Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu. (KUT. 3:12 SUV).

Mungu anamwambia Musa kuwa dalili kuwa yeye ndo amemtuma ni kwamba watakapokwisha kutoka Misri watamwabudu katika Mlima ule. Kwa maneno mengine kama upo Misri huwezi kumwabudu Mungu. Lazima utolewe huko kwanza ndipo uweze kumwabudu Mungumkwa uhuru. Misri ni mahali pa utumwa, mateso, kifungo, kutumikishwa. Vikiwo hivi maishani mwako vitazuia uwezo wako wa kumwabudu Mungu.

2. Dhambi inaondoa ujasiri ndani yako wa kumwabudu Mungu.

Mungu huabudiwa katika uzuri wa utakatifu.

Mpeni BWANA utukufu wa jina lake;
Mwabuduni BWANA kwa uzuri wa utakatifu. (ZAB. 29:2 SUV).

Utakatifu ndo mazingira muafaka kabisa ya kuachilia ibada yako kwa Mungu.

Kunapokuwa na dhambi maishani dhamiri yako inakuzuia usimwabudu Mungu kwa uhuru.

Kwa maana, ikiwa damu ya mbuzi na mafahali na majivu ya ndama ya ng’ombe waliyonyunyiziwa wenye uchafu hutakasa hata kuusafisha mwili; basi si zaidi damu yake Kristo, ambaye kwamba kwa Roho wa milele alijitoa nafsi yake kwa Mungu kuwa sadaka isiyo na mawaa, itawasafisha dhamiri zenu na matendo mafu, mpate kumwabudu Mungu aliye hai? (EBR. 9:13, 14 SUV).

C unaona inavyosema kwenye huo mstari hapo juu? Dhamiri iliyonajisiwa kwa dhambi haina uwezo wa kumwabudu Mungu na ndo maana damu ya Yesu hutakasa dhamiri zetu na kazi mfu tupate kumwabudu Mungu aliye hai. Kumbuka tulisema kuwa kuabudu ni mwitikio wetu kwa uwepo wa Mungu uliyodhihirishwa.

Embu tusome haka kakipande ka maandiko.

Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu. Juu yake walisimama maserafi; kila mmoja alikuwa na mabawa sita; kwa mawili alifunika uso wake, na kwa mawili alifunika miguu yake, na kwa mawili aliruka. Wakaitana, kila mmoja na mwenzake, wakisema, Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, ni BWANA wa majeshi; dunia yote imejaa utukufu wake. Na misingi ya vizingiti ikatikisika kwa sababu ya sauti yake aliyelia, nayo nyumba ikajaa moshi. Ndipo niliposema, Ole wangu! Kwa maana nimepotea; kwa sababu mimi ni mtu mwenye midomo michafu, nami ninakaa kati ya watu wenye midomo michafu; na macho yangu yamemwona Mfalme, BWANA wa majeshi. (ISA. 6:1-5 SUV).

Unaona hapa uwepo wa Mungu ulijidhihirisha kwa Isaya lakini kwa sababu Isaya alikuwa ana dhambi nyemelezi maishani mwake badala ya kuabudu alitumia fursa hiyo kutengeneza na Mungu japo uwepo wa Mungu ulidhihirishwa ili aabudiwe.

Sio kila mtu anayeonekana kama anaanudu uwepo wa Mungu ukija anaabudu kweli. Wengine ndo wanatumia fursa hiyo kutengeneza na Mungu maana ndo keshakuja. Sio kila chozi ni chozi la moyo uliyoguswa na uwepo wa Mungu katika kuabudu. Machozi mengine ni machozi ya toba. Kusujudu kwingine ni kusujudu kwa toba. Kupiga magoti kwingine ni kupiga magoti katika toba. Ni Mumgu tu na yule mtu mdo wanajua uhalisi wa kinachoendelea pale.

Ndo maana ni muhimu kutengeneza na Mungu kabla hajajidhihirisha ili akijidhihirisha kutumii huo muda kumalizana nae bali kumfurahia kwa uwepo Wake aliyoudhihirisha.

 Mungu akubariki sana sana sana.

 Mwl.Conrad C

MASHAKA NA UOGA NI VIKWAZO VYA KUKUFIKISHA MAHALI UNAPOPASWA KUFIKA.

woga

Usipoweza kujikana na kuthubutu, hutoweza kamilisha mambo makubwa” C,S Lewis

Watu wengi wamekuwa wanatamani sana kuwa na maisha yaliyo bora na kuwa na hali njema kiroho lakini miongoni mwa vikwazo vya kuwa hivyo licha ya kile cha watu wa karibu yao/marafiki, changamoto nyingine ni uoga/mashaka.  

Uoga ni ile hali ya kusitasita kuthubutu kufanya mambo na kuweka mashaka kama matokeo yatarajiwayo yanaweza kutokea. Mara zote hali hii uambatana na maneno kama;

 • Sidhani.

 • Siwezi

 • Sijui.

 • Labda.

 • Nitajaribu badala ya nitafanya.

Kibiblia hii ni hali ya kukosa uhakika na ubayana juu ya mambo yatarajiwayo na mambo yasiyoonekana; yaani ni kukosa imani. Na kitendo hiki kinamfanya mtu wa Mungu kuishi maisha yanayomfanya Mungu asiwe na furaha kwa kuwa haiwezekani kumpendeza Mungu pasipo kuwa na imani.

Waebrania 10:38-39 “Lakini mwenye haki wangu ataishi kwa imani; Naye akisita-sita, roho yangu haina furaha naye. 39 Lakini sisi hatumo miongoni mwao wasitao na kupotea, bali tumo miongoni mwa hao walio na imani ya kutuokoa roho zetu.”

Waebrania 10:6a “Lakini pasipo imani haiwezekani kumpendeza;……..”

                Uoga ni kitendo cha kupungukiwa imani kwa kuingiwa na wasiwasi.

Marko 4:40 “Akawaambia, Mbona mmekuwa waoga? Hamna imani bado?”

Yesu anaweka uwiano wa maneno mawili ya ‘kuwa waoga’ na ‘kukosa imani’ Kwa kumaanisha kuwa wanafunzi waliogopa kwa kuwa hawakuwa na imani bado na kama wasingekuwa waoga ni matokeo ya kuwa na imani na kama wangekuwa hivyo Yesu angeweza kunena nao na kusema “hamkuwa waoga, mmekuwa na imani sasa”.

Wakati mmoja nikiwa natafakari neno pamoja na rafiki yangu tukafika mahali pa kutafakari ‘flexibility’ (kubadilika) kwa Mungu na kutafakari kuwa Mungu ni Mungu anayeweza kubadilika na uwezo wa kumfanya asibadilike (static) umewekwa mikononi mwetu wenyewe. Jinsi tunavyoweza enenda ndivyo tunaweza kumfanya Mungu atende yale aliyoahidi au asitende. Wana wa Israeli walipotolewa na Mungu katika nchi ya utumwa (Misri) waliambiwa wanaelekea Kanani (nchi ya ahadi) ila si kwamba  Mungu akupenda wao wafike Kanani bali ni wao wenyewe ndio waliuokuwa sababu ya kutofika kwao.

Waebrania 3:11-19 “ Kama nilivyoapa kwa hasira yangu, Hawataingia rahani mwangu.

12 Angalieni, ndugu zangu, usiwe katika mmoja wenu moyo mbovu wa kutokuamini, kwa kujitenga na Mungu aliye hai.

16 Maana ni akina nani waliokasirisha, waliposikia? Si wale wote waliotoka Misri wakiongozwa na Musa?

17 Tena ni akina nani aliochukizwa nao miaka arobaini? Si wale waliokosa, ambao mizoga yao ilianguka katika jangwa?

18 Tena ni akina nani aliowaapia ya kwamba hawataingia katika raha yake, ila wale walioasi?

19 Basi twaona ya kuwa hawakuweza kuingia kwa sababu ya kutokuamini kwao.”

Kuna jambo Mungu anaapa tena kwa hasira na sababu kuu inayomfanya aape kwa hasira ni kukosa imani/uoga/kusitasita kwa watu wake hii ni kwa sababu alisema watu wake wanapaswa kuishi kwa imani na wakisitasita moyo wake hauna furaha nao.  

Watu wengi wamekuwa wakijifariji kuwa Mungu ameniahidia ni lazima itatimia ila ukweli ni kwamba ukiweka uoga na mashaka kamwe mambo hayo hayatatimia kamwe na itakuwa historia tu kama ilivyo historia ya wana wa Israeli kuwa waliahidiwa lakini hawakuweza kuingia Kanani isipokuwa uzao wao pamoja na Joshua na Kalebu.

Mpaka mtu anaogopa zipo sababu zinazomsababisha akaogopa na pengine zikawa ni sababu nzito, ngumu na za msingi sana za kumfanya mtu aogope, mara nyingi sababu hizo uwa kwa namna ya mazingira yanayomzunguka mtu kwa kutokuwa rafiki na yale ayatamaniyo, au jamii inayomzunguka si rafiki na hali aiendeayo na pengine unenewa maneno mabaya na kusikia mambo mengi ambayo yanamfanya yeye aogope.

maneno ya wanadamu mara nyingi uleta uoga nakubomoa imani ila neno la Mungu uimarisha imani na kumpa mtu ujasiri”

Marko 4:35-40 “Siku ile kulipokuwa jioni, akaawaambia na tuvuke mpaka ng’ambo. 36 Wakauacha mkutano, wakamchukua vile vile alivyo katika chombo. Na vyombo vingine vilikuwa pamoja naye. 37 Ikatokea dhoruba kuu ya upepo, mawimbi yakakipiga chombo hata kikaanza kujaa maji. 38 Naye mwenyewe alikuwapo katika shetri, amelala juu ya mto; wakamwamsha, wakamwambia, mwalimu, si kitu kwako kuwa tunaangamia? 39 Akaamka, akaukemea upepo, akaiambia bahari, Nyamaza utulie. Upepo ukakoma, kukawa shwari kuu. 40 Akawaambia, mbona mmekuwa waoga? Hamna imani

Wanafunzi walizungukwa na mazingira yasiyotabiri kama watafika ng’ambo lakini wakasahau kuwa utendaji wa Mungu haufungwi na mazingira ambayo wapo.

Kumbukumbu la Torati 7:17-23 “Nawe kama ukisema moyoni mwako,mataifa haya ni mengi kunipita mimi;nitawatoaje katika miliki yao? 18 Usiwaogope; kumbuka sana Bwana Mungu wako, alivyomfanya Farao na Misri yote; 19 uyakumbuke hayo majaribu makuu yaliyoyaona macho yako, na hizo ishara, na maajabu, na mkono wa nguvu, na mkono ulionyooka, aliokutolea nje BWANA, Mungu wako; ndivyo atakavyowafanya BWANA, Mungu wako, mataifa yote unaowaogopa. 20 Tena BWANA, Mungu wako, atampeleka mavu kati yao, hata hao watakaosalia, hao wajifichao, waangamie mbele zako.  21 Usiingie na kicho kwa sababu yao;kwa kuwa BWANA, Mungu wakoyu katikati yako, Mungu mkuu mwenye utiisho. 22 Naye BWANA, Mungu wako, atayatupia nje mataifa yale mbele yako kidogo kidogo; haikupasi kuwaangamiza kwa mara moja, wasije wakaongezeka kwako wanyama wa mwitu. 23 Ila BWANA, Mungu wako, atawatoambele yako, atawatia mashaka, mashaka makuu, hata waishe kuangamizwa”

Unaweza ukaona vita ni vikubwa sana kuliko vile ulivyo na wanaosimama kinyume nawe ni wengi kuliko ulivyo na hali hii ikatia uoga.

2 Wafalme 6:15,16 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake Yule mtu wa Mungu alipoondoka na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyaje? 16 Akamwambia, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”

Sababu ya kutokuogopa ni kuu sana ya zaidi ya sababu za kuogopesha, ikiwa Mungu yu upande wako uwezekano wa kushindwa ni asilimia 0% na kushinda ni 100%.

Hesabu 13:30-33 “Kalebu akawatuliza watu mbele ya Musa, akasema, Na tupande mara, tukaitamalaki; maana twaweza kushinda bila shaka. 31 Bali wale waliopanda pamoja naye wakasema, Hatuwezi kupanda tupigane na watu hawa; kwa maana wana nguvu kuliko sisi, 32 Wakawaletea wana wa Israeli habari mbaya ya nchi waliyoipeleleza, wakasema, ile nchi tuliyopita kati yake ili kuipeleleza, ni nchi inayowala watu wanaoikaa; na watu wote tuliowaona ndani yake ni watu warefu mno. 33 Kisha huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”

Ni kweli uhalisia na muonekano wa adui zao ilikuwa ni sababu kubwa sana ya kuwasababisha kuogopa ila ule uzoefu wao waliowahi kumwona Mungu akifanya kazi toka Misri ilikuwa ni sababu kuu ya kuwafanya wasioogope, japo kuogopa kwa wale wengine kuliwasababisha wajione kama mapanzi na ndivyo walivyokuwa kwa kuwa ajionavyo mtu nafsini mwake ndivyo alivyo. Uonaji wa Mungu uko tofauti kwa kuwa Yeye aliwatazama kama mashujaa ila tatizo lilikuwa ni katika wao wenyewe kujiona kama mapanzi.

1 Samweli 17:8-11 “Naye akasimama, akawapigia kelele majeshi ya Israeli akawaambia, Mbona mmetoka kupinga vita? Je! Mimi si Mfilisti, na ninyi si watumishi wa Sauli? Jichagulieni mtu akanishukie mimi. 9 Kama akiweza kupigana na kuniua, sisi tutakuwa watumwa wenu; name nikimshinda yeye na kumwua, ninyi mtakuwa watumwa wetu, na kututumikia. 10 Yule Mfilisti akasema, nipeni mtu tupigane. 11 Basi Sauli na Israeli waliposikia maneno hayo ya Mfilisti, wakafadhaika na kuogopa sana.”

Pindi tu unapoingiwa na uoga ndipo unatoa mwanya wa kushindwa kwako. Ni vyema ukafahamu kuwa hakuna muoga ambaye alishawahi kufanikiwa katika maisha haya kwa kuwa waoga wote uogopa kuthubutu kufanya mambo kwa kuhofia kushindwa ila waliowahi kushinda ni watu waliokubali kufanya mambo pasipo kuogopa kushindwa na hata waliposhidwa walitumia kushindwa kwao kama fursa ya kuwapeleka katika hatua nyingine ya juu sana.

Wengine uogopa kufanya mambo kwa sababu tu walishawahi kuwaona watu wengine wanashindwa katika mambo hayo na katika fahamu zao wamekubaliana na mambo hayo, hii ni sawa na yale mawazo ya wale wapelelezi walioogopa kabla hawajaenda kutamalaki kwa wanefili. Waoga mara nyingi usema nitajaribu labda nitashinda lakini washindi mara zote usema nitafanya na nitashinda bila shaka kama walivyosema Joshua na Kalebu kuwa “tupande tukatamalaki kwa kuwa tutashinda bila shaka” lakini muoga ni rahisi kusema “siendi” au akasema “twendeni labda twaweza kushinda na sisi.”

Tofauti kati ya muoga na mtu jasiri ipo katika mitazamo yao juu ya mambo yanayowazunguka, katika jambo moja jasiri atafanya na kushinda ila mtu muoga ataogopa na akija ona matokeo ya mwenzie ubaki kutaamaki na kumwona menzie kuwa ni mtu wa tofauti sana ila siri ipo katika kuthubutu kufanya na si kukimbia kufanya.

Hakuna muoga yeyote aliyewahi kufanikiwa ila ni majasiri tu ambao uthubutu kugusa katika sehemu ambazo wengine hawagusi. Kwa mfano katika maeneo ya siasa wengi wamekuwa wakiogopa kuthubutu hata kugombea nafasi za ngazi mbali mbali kwa kuogopa kushindwa na wengine pia uogopa kuwa ni ngumu sana na zipo kwa ajiri ya watu wa tabaka fulani tu na uamini kuwa watu wa chini ni vigumu sana kuweza katika mambo ya siasa; ila uoga wa mtu ndio kushindwa kwa mtu mbona wapo wanaoweza kwa hiyo mtu muoga yeye ushindwa hata kabla hajaingia kwenye ushindani na jasiri ushinda hata kabla hajaingia kwenye mashindano.

Mfano kwenye mpira zikiwa zinacheza timu mbili kuna timu ambayo inacheza ili ishinde na kuna timu ambayo inacheza isishindwe, timu ambayo inacheza ishinde wachezaji wake wanakuwa na hali ya ushindi mara zote na ucheza kwa kushambulia wapinzani mara zote na ndiyo timu inayotazamiwa kushinda kwa kuwa ushindi wao ni hali iliyopo ndani yao kabla hawajaanza mchezo; ila mambo uwa tofauti kwa timu inayocheza ili isifungwe yenyewe ucheza kwa kujilinda sana kuliko kushambulia na wachezaji wake hali yao ni kujilinda wasije kufungwa na mara nyingi si watu wa kushinda. Ni vyema kujifunza kwa timu ichezayo kushinda.

Mambo ya msingi ili kuweza kuishinda hali ya uoga:

 1. Usiogope.

2 Wafalme 6:15-16 “…………………………, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyaje? Akamwambia, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.”

Neno usiogope ni neno lenye maana kubwa sana nimeelezea kwa undani katika kitabu cha ‘uungu wa mwanadamu na maisha yenye kibari mbele za Mungu’ na popote ulionapo neno hili limetumika ujue nyuma yake ipo/zipo sababu za kuogopa japo vijana wengi upenda tumia kama neno la kawaida katika mazungumzo yao ila matumizi sahihi ni pale kunapokuwa na sababu za kuogopesha.

Na Mungu anaposema neno hili usiogope umaanisha mengi na haina maana kuwa haoni kuwa yapo yanayoogopesha ila yeye anaona sababu za kukufanya wewe usiogope ni nyingi na kubwa kuliko zikufanyazo uogope nazo ni kama:

 • Yupo pamoja nawe nyakati zote hata ukamilifu wa dahari.

 • Anaweza juu ya jambo linalokusumbua.

 • Hakuna neno gumu asiloliweza.

 • Ameona na kutazama kuteseka kwako na yupo apate kukusaidia.

 • Hakuna liwezalo kusimama mbele zako likafanikiwa.

 • Tulia tu ili atende kwa uweza wake, n.k

Pia neno hili usiogope lina maana sawa na ile ya kuwa hodari na moyo wa ushujaa. Ni taarifa njema kufahamu kuwa neno usiogope kwenye biblia lipo kwa hesabu za siku za mwaka mzima kwa maana ya kwamba kila siku ina ‘usiogope’ moja, kila uamkapo lipo neno la BWANA lisemalo usiogope  kwa kuwa waweza kutana na yaogopeshayo ila kila siku tumia moja hata mwaka uishapo na kuanza mwingine kwa namna hiyo hiyo.

 1. Usienende kwa kuona bali enenda kwa imani.

2 Wakorinto 5:7 “(Maana twaenenda kwa imani, si kwa kuona)”

Kwa maana nyingine ni kusema kuwa mazingira usema kuwa haiwezekani ila imani ambayo chanzo chake ni kusikia neno la Mungu usema kuwa “nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu, Filipi 4:13.” Ni vyema kutoangalia kwa macho ya damu na nyama na kukubaliana na ile hali uliyonayo ila ni busara sana kutazama nini Mungu anatazama kwako.

Kwa kutazama Yese alimwona Daudi kama kijana mdogo sana na hakuona kile kitu kilicho ndani ya Daudi ila Mungu yeye hakumtazama Daudi kama mchunga kondoo tu, bali aliona zaidi kwa kumwona mtu mkubwa na mpakwa mafuta wake wa kusimama kama mfalme.

Usikatishwe tamaa na mazingira uliyonayo leo pengine ni magumu sana na yanakupa mashaka kama utakuja kuwa mtu mkubwa fahamu kwamba hayo uonekana tu ila kwa imani utakuwa kama vile Mungu akuonavyo. Ni vyema sana kujifunza kwa ndugu zetu walio tangulia katika biblia nao walianza sehemu mbaya sana lakini hawakutazama mazingira yanatabiri nini kwa habari yao bali walitazama nini Mungu anasema kwa habari ya maisha yao.

Watu watakutazama kama mtu mdogo sana kama walivyo mtazama Daudi ila Mungu anakutazama kama mtu mkubwa na mfalme juu ya watu wake; watakuona mfungwa ila Mungu anaona waziri mkuu kama alivyomuona Yusufu. Kamwe usikubaliane na watu wakutazamavyo kwa kuwa akuonavyo Mungu si kama watu waonavyo, wao wanaweza kukuona wa kawaida ila Mungu anakuona mtu mkubwa.

I Samweli 16:7 “Lakini BWANA akamwambia Samweli, Usimtazame uso wake, wala urefu wa kimo chake; kwa maana mimi nimemkataa, BWANA haangalii kama binadamu aangaliavyo; maana wanadamu huitazama sura ya nje bali BWANA huutazama moyo”

Mungu kamwe hatazami umbo, historia, mali za mtu bali uangalia moyo wa mtu. Alipotazama kule porini na machungani alimuona Mfalme mkubwa wa taifa la Israeli japo Yesse aliona mchunga wanyama aliye na thamani ndogo kuliko ndugu zake wengine. Alipotazama gerezani alitazama na kuona mtu mkubwa wa kuwa waziri mkuu japo Potifa yeye aliona mfungwa na mtumwa. Alipoangalia Midiani aliona mkombozi wa wana wa Israeli kutoka Misri aitwaye Musa japo Yethro kuhani wa Midiani aliona mchunga mifugo. Aonavyo Mungu si kama vile wanadamu wengine wawezavyo kuona kwa kuwa wao waweza kukuona si kitu ila Mungu akaona mtu mkubwa sana ndani yako.

Mungu kamwe haangalii umezaliwa kwenye familia ya namna gani au ulitoka kwenye tumbo la mama wa namna gani au viuno vya baba wa namna gani ila anaangalia kusudi lake juu yako ambalo lilikuwepo kabla ya uwepo wako katika tumbo la mama yako.

Mithali 23:7a “Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.”

Ona vyema kama Mungu aonavyo huku ukitambua ya kuwa uonaji wako ndicho kipimo cha hatima yako, kwa maana ya kuwa utakuwa kwa namna ile ujionavyo nafsini mwako. Kuna msemo wa Kiswahili usemao “mbuzi hula kwa urefu wa kamba yake” na ndivyo ilivyo kwa sisi wanadamu ya kuwa mtu uwa kwa upana wa utazamaji wake na kamwe mtu hawezi kuvuna asichopanda kwa kuwa apandacho mtu ndicho avunacho ni rahisi kusema alichokibeba mtu ndani yake ndicho atakacho kitoa kwa kuwa haiwezekani mtu atoe kitu kisichokuwa ndani yake na pia ni wazi sana kuwa yamtokayo mtu ni yale yaujazayo moyo wake na si yalio nje yake.

Mazingira na watu pia uweza sema  wewe hauwezi kufanikiwa, kupata kazi, kuwa mtu mkubwa, kuwa na ndoa nzuri, kupata mchumba,nakadharika ila Mungu naye usema kuwa mambo yote hayo kwake yanawezekana na hakuna lisilowezekana kwake na anahitaji uwe na imani tu kwa kutotia shaka.

Matendo ya mitume 4:19 “Petro na Yohana wakawajibu wakawaambia kwamba ni haki mbele za Mungu kuwasikiliza ninyi kuliko Mungu, hukumuni ninyi wenyewe”

Ni bora kumsikiliza Mungu katika mambo magumu unayoyapitia maana kwa kusikiliza watu ni rahisi sana ukarudi nyuma na kushindwa kuyatimiza makusudi ya Mungu.

Marko 10:27 “Yesu akawakazia macho, akasema, kwa wanadamu haiwezekani, bali kwa Mungu sivyo; maana yote yanawezekana kwa Mungu”

Wakikukatisha tamaa wewe sema “kwa wanadamu kama nyinyi/wewe haiwezekani lakini kwa Mungu inawezekana”

Luka 1:37 “Kwa kuwa hakuna neno lisilowezekana kwa Mungu”

Wewe fanya yale yakupasayo kufanya ili upate kufanikiwa kwa kuwa hakuna limshindalo Mungu.

Kwenye hili eneo la Imani bado watu wengi wamekuwa na mtazamo hafifu na si wa kiMungu kwa kuwa wengine usema kuwa namwamini Mungu atatenda tu ila hawafanyi kazi yoyote ili wapate kufanikiwa, ni jambo jema kufahamu sana kuwa Mungu hapendi watu wasioshughulika kwa kuwa yeye hafanyi kazi na mkono mlegevu kwa hiyo hata kama utakiri sana kuwa itakuwa ila kama haufanyi juhudi zozote usidhanie kuwa utapata kufanikiwa. Mungu ameahidi kubariki kazi za mikono ya watu wamchao na ni vyema kufahamu kuwa kama ukifanya kazi ndipo Baraka za Mungu ukutana na wewe huko ili apate kuzidisha yale uyafanyayo.

 1. Dharau tatizo na kuliona kuwa dogo kwa kuwa aliye upande wako ni mkuu kuliko tatizo lililo kinyume nawe.

Hesabu 14:7-9 “wakanena na mkutano wote wa wana wa Israeli wakasema, Nchi ile tuipitayo kati yake ili kuipeleleza, ni nchi njema mno ya ajabu. 8 Ikiwa BWANA anatufurahia, atatuingiza katika nchi hii atupe iwe yetu, nayo ni nchi yenye wingi wa maziwa na asali. 9 Lakini msimwasi BWANA, wala msiogope wala wenyeji wan chi, maana wao ni chakula kwetu; uvuli uliokuwa juu yao umeondolewa, naye BWANA yu pamoja nasi; msiwaogope.”

Sehemu hii ya maandiko nimekuwa nikiipenda sana na kuifurahia kila wakati napoitazama kwa kina zaidi. Joshua na Kalebu wanaonyesha ushujaa wa hali ya juu sana ambao kama ukisoma kwa kawaida tu hauwezi pata undani mkubwa wa yale waliyoyasema, cha kwanza wanaliona taifa kubwa lililotia uoga na mashaka taifa la Israeli kuwa kama chakula kwao yaani kwa maana nyingine ni kuona kuwa ni kitu kidogo sana ambacho unaweza kukila si kikudhuru bali kikutie nguvu ya kusonga mbele, Joshua na Kalebu wao waliona mbali zaidi ya kuwa wanasafari ndefu sana na kama wasipopata chakula kama wanefili ambacho ni chakula chenye nguvu watateseka na njaa katika safari waiendeayo. Wao waliona fursa katika matatizo, chakula katika matatizo na sina maana ya kwamba walimaanisha kuwa wawale nyama yao ila waliona ni kitu kidogo sana kwao. Lakini jambo jingine wanaona ule uvuli uliokuwa ndani yao umeondolewa, yaani ule utiisho au kile kinachowafanya waogopeshe kimeondolewa ni sawa na kumwona simba atishaye sana ila hana meno na kucha ambazo zaweza kukudhuru ndivyo walivyoona Joshua na Kalebu kwa wale Wanefili.

Kwako leo inawezekana wapo wanefili wasumbuao ila ni vyema kuona kama mashujaa hawa walivyoona. Yaani kuona fursa katika tatizo na si kuona adha katika tatizo lililo mbele zako na kujua katika kila tatizo linalojitokeza mbele zako ipo fursa (chakula chako) ila ni swala la wewe kuwa jasiri na kutumia fursa hiyo.

Mithali 28:1b “……Bali wenye haki ni wajasiri kama simba” Wenye haki wa Bwana ni majasiri kama simba na hakuna la kuwatisha.

1 Samweli 17: Inaelezea kwa kina sana mwanzo wa tatizo na hata mwisho wa tatizo na jinsi kijana Daudi anavyopambana vyema na kuzidi hata kwa mfalme Sauli.

Tofauti ya Sauli na Daudi katika tatizo lililotokea ni:

 • Sauli alitazama tatizo kama lilivyo na kulitukuza; ila Daudi aliona tatizo ni dogo sana na kumshusha sana mfilisti.

 • Sauli alipomtazama Goliathi akaona kama ‘giant’ (shujaa/shupavu) asiyepigika; ila Daudi akamtazama kama ndege ndo mana akabeba silaha za kuulia ndege. Ni bora angemtazama kama dubu au simba angebeba mkuki na siraha kubwa ila yeye alimuona kama ndege.

 • Sauli alitegemea akili zake mwenyewe bali Daudi alimtegemea Bwana.

 • Sauli alikwenda kwa kuona ila Daudi alikwenda kwa Imani, 1 Wakorinto 5:7.

 • Daudi alimsikiliza Bwana na kumtii kwa kile Bwana aonavyo ila haikuwa hivyo kwa Sauli, Matendo 4:19.

Hata kama tatizo ni kubwa kiasi gani kwako, kwa Mungu ni dogo tu, wewe mwamini Mungu na umtarajie yeye naye atafanya.

Zaburi 37:5 “Umkabidhi BWANA njia yako, pia umtumaini naye atafanya.”

 1. Inuka na utende uyaogopayo kwa imani bila kuogopa.

Jitie ujasiri juu ya hicho kitu ukiogopacho, na uinuke na kukifanya kwa ujasiri huku ukimuomba Mungu akusaidie.

Kuna wengine wamekuwa wakisema kuwa hawawezi hata kama bado hawajajaribu kufanya. Mara nyingi kitu ambacho unaona uwezi kwanza ni vigumu sana kukifanya ukafanikiwa ni kwa sababu:

Kumbukumbu la torati 7:17 “Nawe kama ukisema moyoni mwako,mataifa haya ni mengi kunipita mimi;nitawatoaje katika miliki yao?”

Ukiona kushindwa usidhani kama Mungu atasimama. Mungu utenda kazi katika mazingira na viwango ulivyomwekea na ukimwekea mazingira madogo madogo ufanya kwa mazingira hayo hayo na ukiweka makubwa aweza fanya kwa viwango hivyo.

2 Wafalme 4:3-6 “Akasema nenda ukatake vyombo huko nje kwa jirani zako wote, vyombo vitupu; wala usitake vichache. 4 Kisha uingie ndani, ukajifungie mlango wewe na wanao, ukavimiminie mafuta vyombo vile vyote; navyo vilivyojaa ukavitenge. Basi akamwacha akajifungia mlango yeye na wanawe; hao wakamletea vile vyombo, nay eye akamimina. 6 Ikawa, vilipokwisha kujaa vile vyombo, akamwambia mwanawe, Niletee tena chombo. Akamwambia, hakuna tena chombo. Mafuta yakakoma”

Katika chombo cha mama mjane mafuta yalijaa kwa kadiri alivyoandaa vyombo angeandaa vidogo angepata vidogo na angeandaa vingi zaidi bila shaka angepata vingi zaidi. Ni vyema kwa mtu wa Mungu kumjengea Mungu mazingira ya kutenda mambo makubwa hata kama u mtu mdogo sana. Ikiwa ni biashara, kazi, masomo, inuka na utende kwa ujasiri maana Mungu anatenda kazi na majasiri na wasioogopa. Fanya tu ukishindwa mara ya kwanza usikate tamaa rudia kufanya tena na tena hata ukafanikiwa huku ukikumbuka kuwa mkono wenye juhudi utawandishwa.  

 1. Amini kuwa unaweza.

Wafilipi 4:13 “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu.”

Ikiwa watu wenye mafanikio makubwa duniani na walio na hali ya chini sana hapa duniani wote wana masaa 24 kwa siku, swali ni je, Nini kinaleta tofauti kati yao?

Hii pia ni sababu kubwa ya wao kufanikiwa kwa kuamini kuwa wanaweza wakafanya na hatimaye wakafanikiwa kuthubutu na kutenda.

Ukijenga imani ya kuamini kuwa unaweza kufanya una nafasi kubwa sana ya kufanikiwa katika lile ulitendalo.

Dr Mayles Munroe anasema “watu waliofanikiwa katika ulimwengu huu ni watu waliotoa kabisa neno haiwezekani katika kamusi zao na kuliacha neno inawezekana.”

Hii ni kuonyesha kuwa katika kuamini kuwa inawezekana hapo ndipo mafanikio ya mtu yamewekezwa. Lipo neno jema sana Bwana Yesu alisisitiza na kusema kuwa “mambo yote yanawezekana kwake yeye aaminiye”

–Mwl Kelvin Kitaso

Kukosa Nidhamu ya Maisha!!

“Fanya kitu sahihi, wakati sahihi na mahali sahihi” Shauri

Mara nyingi tumekuwa tukifahamu nidhamu kwa kuzingatia sana masuala ya nje kama vile utii, heshima,unyenyekevu na mengine mengi yafananayo na hayo na kwamba kuwapo na dharau, kiburi, ufanywaji wa mambo ya aibu, unyama na mengine ni matokeo ya ukosefu wa nidhamu ya ndani ya mtu binafsi (mental discipline). Lakini hapa tutazungumzia masuala ya nidhamu katika Nyanja zote za maisha yaani nidhamu binafsi, kimasomo,kikazi, katika mambo ya Mungu, kifamilia, muda n.k. Nidhamu ya ndani ya mtu ndio inayoweza kufanya mabadiliko katika ufanisi wa kazi au utendaji wa mambo ya mtu na kubadilisha mfumo mzima wa Maisha.

Nidhamu ni neno dogo sana kulitamka ila ni kitu kikuu mno kumfanya mtu kufikia malengo yake na kuwa mtu wa tofauti na watu wengine wamzungukao. Kinachotofautisha mtu huyu na Yule ni nidhamu yao katika kuishi kwao.

Maana ya neno nidhamu.

Nidhamu ni ile hali ya mtu kuwa makini katika kufuata uongozi sahihi au kanuni sahihi ili kufikia malengo yaliyotarajiwa. Na nidhamu ya ndani ni ile nguvu ya ndani ya mtu ambayo imejengeka, imeimarika kiasi cha kufanya mambo katika ufanisi na ujuzi wa hali ya juu yaani kufanya kitu sahihi, wakati sahihi na mahali sahihi ili kufikia kusudi sahihi.

Ni wazi ya kwamba watu tumekuwa tukitafuta matokeo mazuri kiafya, kimasomo, kikazi, kifamilia, kibiashara, kijamii yaani kimaisha kwa ujumla lakini imekuwa ni kazi nzito, ngumu na inayochosha

kufikia malengo hayo, Jiulize je, ninafuata kanuni sahihi na kwa umakini? kwani mipango tu na juhudi nyingi hazitoshi kuleta matokeo mazuri. Kunahitajika kitu cha muhimu kinachofuatwa mara kwa mara ili kurahisisha ufikiaji wa lengo hilo, kitu hicho ni nidhamu.

Pia nidhamu tunaweza kulinganisha na egemeo katika kurahisisha utendaji wa kazi yaani katika nyenzo.  Tujikumbushe fizikia

Nyenzo ni kitu ambacho kinatumika katika kurahisisha kazi. Nyenzo ina sehemu kuu tatu yaani mzigo, egemeo na jitihada.  Mzigo pekee pamoja na jitihada haviwezi kurahisisha kazi, na muda mwingine kazi huonekana ni ngumu sana kwa kukosekana kwake kwani lazima kuwepo na kitu cha muhimu sana ambacho ni egemeo.

Vivyo hivyo ili kurahisisha utendaji kazi, au ufikiwaji wa malengo husika ya mtu, lazima kuwe na vitu vikuu vitatu vinavvyo ambatana, ambavyo ni malengo, nidhamu pamoja na juhudi. Kuwa na mipango tu, au maono tu  pamoja na juhudi nyingi haviwezi kurahisisha kufikia mafanikio yako, lazima kuwe na kitu kimoja cha muhimu kinachotegemewa kurahisisha kazi ambacho ni nidhamu.

Hebu tuangalie kwa upana kidogo kuhusu vipengele mbalimbali vya ukosefu wa nidhamu

 1. Ukosefu wa nidhamu katika muda

Huyu kwa kweli ndiye adui mkubwa ambaye anazuia mafanikio makubwa ya watu wengi, kwani ana uwezo wa kupoteza, kuharibu na hata kufanya mipango ya mtu isitimie, kama tulivyomtazama kwa undani wake katika sura zilizotangulia.

Kusipokuwa na umakini katika kutumia muda, yaani kuwa mahali sahihi, ukifanya kitu sahihi kwa wakati sahihi lazima kunakuwa na upungufu katika kupata matokeo yaliyokusudiwa. Kama maandiko matakatifu yanavyo sema katika kitabu cha Mhubiri 3:1Kwa kila jambo kuna majira yake, na wakati kwa kila kusudi chini ya mbingu.”

Kwa hiyo tangu mbingu na nchi ziumbwe, mwanadamu aliumbwa ili afanye mambo yake yote kwa kufuata utaratibu. Mtume Paulo aliwaonya waefeso kuhusu kuutunza muda , alisema  “Basi angalieni sana jinsi mnavyoenenda; si kama watu wasio na hekima bali kama watu wenye hekima; Mkiukomboa wakati kwa maana nyakati hizi ni za uovu” Waefeso 5:15-16

Na pia kuna usemi wa kiingereza usemao “you can choose to be the manager of time or the servant of time” it is your choice, ikimaanisha ya kwamba ni wewe tu mwenye maamuzi ya kutumia muda kwa kuuongoza (ukawa meneja) au ukaongozwa na muda (ukawa mtumwa). Hivyo ni vema kupata moyo wa hekima katika kuyafanyia kazi mafundisho haya nawe utakuwa mwenye hekima. Weka nidhamu ya hali ya juu katika kutumia muda wako.

 1. Ukosefu wa nidhamu katika mambo ya Mungu

Mungu wetu ni Mungu ambaye yuko makini na anayefuata utaratibu katika kufanya mambo yake yote. Katika siku sita za uumbaji aliumba kwa mpangilio thabiti na ndio matokeo mpaka sasa vitu vilivyoumbwa vipo. Vivyo hivyo kama wana wa Mungu aliye hai imetupasa kutii na kufuata maagizo anayotuagiza kila siku ili tuwe kama alivyotukusudia.

Wakristo wengi wamekuwa ni watu ambao wanapenda matokeo mazuri tu katika uhusiano wao na Mungu na kufikiri kwamba unakuja kiurahisi rahisi. Lahasha! Kuna juhudi zinatakiwa ikiwa na kufuata uongozi kwa ufasaha ndipo matokeo yanakuja.   katika kila jambo linahitaji kufuata uongozi wa neno la Mungu ambayo ndiyo nidhamu. Ni kweli yote yanawezekana kwa Mungu tukiamini na zaidi tukiwa na nidhamu kwa mambo yake.

 1. Ukosefu wa nidhamu katika kula/kunywa.

Unaweza dharau na kuona ni jambo dogo sana kutazama masuala ya afya ila hili ni jambo kubwa sana kwa kuwa mafanikio yako yanategemea sana afya yako ilivyo, kama afya yako si njema si rahisi kufikia malengo uliyonayo.

Tatizo si chakula ila tatizo ni wewe umekosa nidhamu katika matumizi ya chakula, kama una nidhamu nzuri utajua ni nini ukile kwa wakati fulani na nini usile kwa wakati fulani, ukifahamu kuwa kitu fulani kinaweza kuleta hatari ya afya yako nidhamu inakufundisha uache ili kuitunza afya yako iwe njema kukusaidia kutimiza malengo uliyonayo katika maisha yako. Mfano kuna watu wanavuta sigara na kunywa pombe wakifahamu kuwa ni hatari kwa afya zao na jamii iwazungukayo, jawabu rahisi kutoka kwao ni wamekosa nidhamu ambayo ingewasaidia kukwepa kwa kuwa nidhamu yatufunza kuwa makini kufanya mambo ya faida kwetu wenyewe.

Nidhamu katika mfumo mzima wa afya ni wa muhimu sana katika kuyafikia malengo au ndoto zako. Mungu wetu mwenyewe anataka tuwe na afya njema wakati wote ndio maana kwa kupigwa kwake msalabani sisi tumepona yaani tu wazima.

Ili tuweze kuwa na afya njema inatakiwa tujali afya za miili yetu kwa kutumia chakula bora pamoja na maji safi na salama.

Hapa nitatilia mkazo sana katika suala la kunywa maji, kwani mwili wetu umejengwa kwa asilimia 100 ambapo 60% ni maji na 40% ni chakula, kumaanisha ya kwamba  ya mwili ni maji tu na  ni chakula. Kwa hiyo inatakiwa tunywe maji kwa wingi na kwa kufuata utaratibu ili tuikinge miili yetu dhidi ya magonjwa, cha kushangaza watu wengi wanatumia chakula kwa wingi na maji yanatumiwa kama ya ziada tu, na zaidi utafiti unaonyesha ya kwamba 90% ya magonjwa yote huanzia kwenye mfumo wa mmeng’enyo wa chakula hivyo ni wazi kwamba kutozingatia kanuni sahihi za utumiaji wa lishe bora unapelekea kuibuka kwa magonjwa mengi.

Kwa kawaida kila mtu anapaswa kunywa maji yasiyopungua lita 3 kwa siku, lakini swali ni hili; je? Unakunywa kiwango sahihi, wakati sahihi, mahali sahihi ili uweze kupata matokeo sahihi? au matokeo yoyote? Unaweza ukasema huyu mwandishi anaongea nini, jibu ni kwamba kama unataka upate matokeo sahihi ni lazima ufuate kanuni sahihi. Hapa nitakufundisha kanuni rahisi sana itakayokusaidia kunywa maji na kupata matokeo mazuri maana imefanyiwa utafiti, kujaribiwa na hata kutumiwa kwa miaka mingi na matokeo unayaona.

Kwanza unapoamka alfajiri kwa ajili ya maombi, mazoezi au kujiandaa ni lazima unywe 150cl ambayo ni sawa na lita 1  kwa muda wa dakika 2  ̶ 5. Na muda unaofaa ni (saa 10, 11 na 12) alfajiri kulingana na muda unaoamka ukichelewa sana saa 1 asubuhi. Imethibitishwa kwamba maji yanayonywewa muda huu yana umuhimu mkubwa sana katika ufanisi wa kazi zako za siku nzima.

Pili mchana saa moja kabla, au baada ya chakula kati ya saa7, 8 hadi 9 unakunywa 75cl ambazo ni sawa na   ya lita. Vivyo hivyo na jioni kati saa (12,1 na  2 )usiku unakunywa robo tatu ya lita yaani .  Maji yanayoshauriwa kutumiwa ni ya kawaida usipende kutumia maji ya baridi.

Asubuhi

(10,11,12,1)

Mchana( 7,8.9)

Jioni (12,1,2)

Ukianza kuifuata kanuni hii itakusaidia kufanya kazi kwa ufanisi, kwa muda mrefu na kuufanya ubongo wako ufanye kazi vizuri, pia itakukinga dhidi ya maradhi kwani kila sehemu ya mwili imepata kiasi chake cha maji kinachotakiwa. Sio hivyo tu bali utalala kwa wakati unaostahili kulala na utaamka kwa muda unaopaswa hivyo kuzuia kusinzia wakati wa kazi/ibaada/mikutano n.k.  Kwa wiki mbili za kwanza unapoanza unaweza ukaona ni kazi sana kwani unakunywa maji kwa muda usio na kiu bali kuanzia wiki ya tatu itakuwa ni tabia yako iliyojengeka na kuimarika na utayafurahia matokeo yake.

Pia kuhusu umuhimu wa maji katika Maisha ya mtu, naomba utafakari sana kuhusu UUMBAJI katika kitabu cha Mwanzo 1:2 “Nayo nchi ilikuwa ukiwa,tena utupu,na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji” Hivi? Kwanini roho wa Mungu alikaa juu ya maji na sio chini kwenye vilindi au mbinguni? Hii ni kuonyesha kwamba alikuwa anaatamia uumbaji (kuumbwa kwa nchi) hivyo hata kama hali uliyonayo ni ya ukiwa kiasi gani, maji ni ya muhimu sana katika kuumba afya njema.

Kwa kuwa afya njema ni ya muhimu sana kwa mafanikio ya mtu, Big Results Now (BRN) yaani matokeo makubwa sasa kwa afya yako yanawezekana kwa kufuata utaratibu sahihi ulioelekezwa. Wewe andaa maji yako tu, na uyatumie.

Daudi anamuomba Mungu na kumwambia “Basi utujulishe kuzihesabu siku zetu, Tujipatie moyo wa hekima” na katika tafsiri ya The Living Bible usema “Teach us to number our days. And recognize how few they are, help us to spend them as we should,” utafsiri maneno haya kwa Kiswahili chake kuwa “Utufundishe kuhesabu siku zetu. Tujue ni jinsi zilivyo chache, utusaidie kuzitumia jinsi itupasavyo.” Zaburi 90.12. Daudi kwa kuwa na hekima alifahamu kuna umuhimu sana wa kujua siku zake kuwa zi chache na kuna umuhimu mkubwa sana wa kuishi kwa hekima katika siku hizo. Ni dhahiri kuwa kama hujui kuwa una siku chache za kuishi duniani ni kazi kwako kuishi kwa hekima na hata kujua ni namna gani unapaswa kufanya hili afya yako iwe chache sana.

Kwa kujua kuwa una maono ya kufanya ni lazima umuombe Mungu akufunze kuzitumia siku zako vizuri ili uweze kufikia malengo yako ukiwa na afya njema. Ukiwa na maono ya maisha yako ni lazima uwe makini na namna unavyoyaishi maono yako, angalia aina ya vyakula unavyotumia na jiepushe na vitu hatarishi kwa afya yako. Zingatia sana matumizi ya maji ya kutosha maana ni ya msingi sana kwa afya yako iliyo msingi wa maono yako, epuka matumizi ya vyakula vya kemikali ambazo zinachangia mwili wako kuchoka mapema na tumia hata mazoezi kwa kuwa ni muhimu sana. Usitumie vitu ambavyo vitaufanya mwili wako uremae na kukufanya kuwa mzembe.

–Kelvin Kitaso

Itaendelea sehemu ya pili