Kudharau vitu vidogo kutatuletea maangamizo makubwa!!

  • kitaso picha

    Katika mfululizo wa makala zilizopita tuliangalia maadui wa mafanikio ya mwanadamu kwa kuanza na kukosa maono, na kukata tamaa. Wiki hii tunaendelea na adui wa tatu ambaye ni dharau. Karibu katika mwendelezo wa maadui wa mafanikio kwa kuangalia dharau.

 “Hakuna atakayekuona dhaifu pasipo ruhusa yako.” Eleanor Roosevelt

 Dharau ni kikwazo kikubwa pia cha mafanikio kwa mtu yeyote anayetaka kufanikiwa; na dharau hapa haina maana moja ya kuwadharau wengine ila inaenda juu zaidi ya hapo kwa kutazama kujidharau mtu kama mtu, kudharau vitu vinavyomzunguka na pia kujidharau yeye mwenyewe kuwa hawezi kufikia mafanikio na kuona kuwa hawezi kabisa.

 Kujidharau 

Ni wewe tu unayeweza kuwafanya watu au jamii ikuzungukayo ikudharau au ikuheshimu.

Mtu anayejidharau ni vigumu sana kukubalika na watu wengine na pia ni vigumu sana kwa yeye mwenyewe kufanya mambo makubwa kwa kuwa ujidharau na kuona kuwa hawezi kufanya mambo hayo. Ni kweli kuwa zipo sababu nyingi ambazo zinaweza kumsababisha mtu akajidharau ila ya kutojitambua kuwa yeye ni nani inakamata maeneo yote kwa kuwa mtu anayejitambua na uthamani wake hata kama hana vitu ila kamwe hatokaa kujidharau kwa vile alivyo na hata kama watu wengine wanamdharau lakini yeye hawezi kukubaliana nao na kuanza kujidharau kama wengine wajionavyo.

Watu wengi sana wameuza utu wao kwa tatizo la kujidharau na kuona kuwa wao si kitu na wengine wameruhusu hata miili yao kuchezewa katika ngono kwa tatizo hili la kujidharau na kuona kuwa hawana uthamani ila kama wangefahamu uthamani wao isingekuwa ni vyepesi kufanya hivyo. Na wengine wameshawahi kutamkiwa maneno ya kudharauliwa na wengine na kufika mahali pa kusema kuwa hawana thamani kabisa katika maisha yao.

Wewe ni mtu wa thamani sana katika hii dunia hata kama watu wana kudharau na jua kuwa Yesu Kristo ndivyo akuonavyo na ndiyo maana akatoa uhai wake ili apate mtu kama wewe. Usijidharau kwa kuwa mwanadamu yeyote aliyeumbwa na Mungu ameumbwa na kitu cha tofauti sana ndani yake na amepewa uwezo wa kufanya mambo mengi yakatokea hivyo amini kuwa unaweza wala usitie hofu wala shaka maana wewe ni wa thamani sana na unaweza sana.

Hesabu 13:30 “Kisha, huko tuliwaona Wanefili, wana wa Anaki, waliotoka kwa hao Wanefili; tukajiona nafsi zetu kuwa kama mapanzi; nao ndivyo walivyotuona sisi.”

Kujidharau ni siraha kubwa sana ambayo adui utumia kumfanya mwamini kutofikia hatima yake, wapelelezi wanafika mahali wanajidharau na kujiona kama mapanzi ndani yao na ukishajiona dhaifu ni lazima itakuwa tu kwako. Ttizo ni wewe kujiona katika hali mbaya na tatizo si kwa wale wanaokuona, kwa sababu kama unajiamini hata wakudharauje ni lazima hautakubaliana na utazamaji wao kwako.

Paulo katika kitabu cha Wafilipi 4:13 anajiamini wazi kwa kusema kuwa “Nayaweza mambo yote katika yeye anitiaye nguvu”

Kujidharau kunatokana pia na kutokujitambua kuwa wewe ni nani na umebeba kusudi la namna gani ndani yako na pia kutojua Mungu anakutazamaje na anakutazama kama nani. Usipojifahamu wewe ni nani ni rahisi sana ukajidharau na hata kufungua mlango kwa wengine kukudharau na kukuona ni mtu wa kawaida sana.

Nilipogundua kuwa Mungu ananitazama kama ‘mungu’ kama anenavyo katika Zaburi 82:6 “Mimi nimesema, Ndinyi miungu na wana wa aliye juu nyote pia” ilinibadilisha sana mtazamo wangu na kunifanya nijiamini zaidi kwa kuwa nimepewa uwezo ndani yangu wa kutosha ambao kwa huo naweza nikafanya mambo mengi na yakadhihirika katika uhalisia wake; na pia neno katika Yohana 1:12  inasema “bali wote waliompokea aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu; ndio wale waliaminio jina lake” kwa maandiko haya ujasiri wa mtu uzidishwa haswa kwa kujifahamu wewe ni nani na Mungu anakutazama kama nani na kama umepewa uwezo ndani yako basi unaweza mambo yote katika yeye akutiaye nguvu. Umepewa uwezo wa Kiungu ni lazima uwe mtu wa tofauti na walivyo watu wengine.

Kudharauliwa na watu wengine.

Huwezi kumzuia mtu anayetaka kukudharau ila unaweza kutokubaliana na dharau zake.

Mathayo 13:54-58 “Na alipofika nchi yake, akawafundisha katika sinagogi lao, hata wakashangaa, wakasema, Huyu amepata wapi hekima hii na miujiza hii? 55 Huyu si mwana wa seremala? Mamaye si yeye aitwaye Mariamu? Na nduguze si Yakobo, na Yusufu, na Simoni, na Yuda? 56 Na maumbu yake wote hawapo hapa petu? Basi huyu amepata wapi haya yote? 57 Wakachukizwa naye. Yesu akawaambia, Nabii hakosi kupata heshima, isipokuwa katika nchi yake, na nyumbani mwake mwenyewe. 58 Wala hakufanya miujiza mingi huko, kwa sababu ya kutokuamini kwao”

Watu walikuwa wanamfahamu Yesu kama seremala na walipoona anafanya mambo makubwa kuliko wao walivyomuona kama seremala tu wakaanza kumshangaa na wengine kumdharau, ila Yesu hakuwakataza wao kumdharau bali hakuchukulia maanani yale madharau yao kwake.

Usijidharau maana wewe ni zaidi ya watu wakuonavyo na hata wasemavyo kuhusu wewe, hakuna akujuaye wewe ni nani ila muumbaji wako ndiye akujuaye wewe ni nani. 

Kudharau vitu vidogo vidogo. 

Mambo yote makubwa yalitoka katika vitu vidogo dogo ambavyo mara zote huonekana ni vitu vya kawaida sana. Mwanadamu alitoka kwenye mavumbi ya ardhini, msitu mkubwa ulitokea kwenye mbegu ndogo sana na pia waweza kuangamizwa kwa njiti ndogo sana ya kiberiti, mti wa haradari ulitoke kwenye mbegu ndogo sana lakini uwa mkubwa hata kuwafaa ndege na hata wanadamu. Watu wakubwa duniani nao walianza sehemu ndogo sana na ya chini sana kuliko uliyonayo wewe leo japo waweza pungua au kuzidi kwa sehemu tu, ila tofauti yao na watu wengine ni kwa namna ile ya kuyachukulia hayo mambo madogo. Yupo tajiri mkubwa sana duniani ambaye alianza kwa kuuza bigijii ‘bub gum’ chuoni ila leo ni mtu mkubwa sana.

Watu wengi sana wamekuwa na kasumba ya kuyadharau mambo madogo madogo na kuona kuwa hayana maana kwao labda wangeanzia kwenye mambo makubwa ambayo yangewafanya na wao kuonekana watu wenye thamani. Historia ya tajiri mkubwa kuliko wote Afrika kwa wakati huu aitwaye Dangote alianzia na biashara ya kuuza unga kwa mtaji wa kukopa kwa ndugu yake ila alijiongeza siku hadi siku hata kufikia ukubwa huo.

Suala la kudharau mambo madogo madogo ni kubwa sana haswa kwa watu wa Mungu pia kwa kuamini kuwa watu watawadharau watakapowaona wanafanya biashara ndogo ndogo na wengine uamini ni kujipotezea utu wao ila ni muhimu sana kufahamu kuwa hata walio juu walianza chini ila walikuwa na lengo la kuwa juu na ndiyo maana mpaka leo wapo juu. Wengine huamini kuwa “mimi nimebarikiwa na Mungu itakuwaje nifanye kazi za watu wa hali ya chini” hii ni mbaya sana na ni vyema kujifunza kwa Yusufu aliyekubali kuwa mtumwa/mfanyakazi wa ndani ila badae akawa waziri mkuu na pia Yakobo alianza kama kibarua wa kuchunga mifugo ya Labani ila ndipo alipopatia utajiri mkubwa sana aliokuwa nao.

Nimejifunza sana katika eneo hili kwa kuwa Mungu anapenda watu wachakarikaji na ilinilazimu kwa wakati mwingine kuajiliwa kama muuza duka la mtu, mtunza mifugo ya mtu, kubeba mikaa na kufanya kazi za hali ya chini sana ila nikijua kuwa naelekea mahali pa juu sana na yale ninayoyaona leo sitoyaona tena, ngoja nikukumbushe habari za Yusufu ya kuwa baada ya kuinuliwa na Bwana hakuwa mtumwa/mfanya kazi wa ndani tena ila yeye aliajiri wa kumfanyia hizo kazi na pia Yakobo yeye hakuchunga yeye tena ila alikuwa akichungiwa. 

Kwenye kitu ambacho wewe unakidharau wenzio wanaona fursa ya kuwapeleka mahali wanapotaka kwenda. Usidharau vitu vidogo vidogo kwa kujitia moyo kuwa mimi ni mbarikiwa siwezi kufanya vitu vya aibu namna hiyo kwa kuwa yupo Yakobo ambaye alitoka kwenye familia ya kitajiri sana pengine zaidi yako na pia alikuwa ni mbarikiwa wa BWANA na kuahidiwa mambo makubwa pengine kuliko wewe leo ila hakuona ule utajiri kama ni kitu cha kufungamana nacho hata kikamfanya abweteke na kudharau kazi ila alianza kuangaika na mambo madogo madogo ambayo yalimuongeza na kumfanya awe mtu mkubwa sana ila naye kabla ya utumwa huo alitamkiwa kuwa ni mbarikiwa na pia jifunze kwa Musa aliyechunga mifugo kule Midiani alikuwa anatokea kwenye nyumba ya kifalme. Ndivyo walivyo watu wa Mungu halisi.

Wengine hawataki kujishughulisha katika madogo madogo kwanza na utegemea sana kusaidiwa mitaji mikubwa ili waanzie juu, hii ni dhana mbovu kwa kuwa waweza anza na padogo sana ambapo pana dharauliwa na watu wengi ila ukapanda juu siku hadi siku. Kuna aina mbili tofauti za watu katika kupambana na maisha hata kufikia viwango vya juu; aina ya kwanza ni watu wale waliowekewa ngazi tayari na watu waliowatangulia ambao waweza kuwa wazazi, ndugu wa karibu na hata marafiki wa karibu, yaani wao huikuta ngazi na kazi yao kubwa huwa ni kuanza kupanda ngazi hiyo ili kufika juu: aina nyingine ni watu ambao huanza wao kama wao kwa kutafuta mbao, na kila dhana ya kutengenezea ngazi na huanza kuitengeneza ngazi wao wenyewe hata ikikamilika huiweka mahali pa kupandia wao wenyewe na kuanza kuipanda wao wenyewe, aina hii ndiyo inabeba watu wengi wa jamii ya Kiafrika. Aina hizi mbili za watu huwa tofauti na kila mmoja anapaswa kupambana kwa namna yake ili kufika pale juu apaswapo kufika ila umakini na juhudi kubwa kote yatakiwa na ule upande wa pili unahitaji juhudi kubwa zaidi ya kupambana na kuijiamini kuwa unaweza katika kupambana hata ukafanikiwa kufika juu katika eneo ambalo uhitaji kufika. 

Mchwa wadogo uangusha nguzo kubwa. 

Rafiki yangu mmoja anapenda sana kusisitiza mara nyingi katika msemo huu ambao nimekuwa nikijifunza sana kwa msemo huu. Nguzo inapokuwa imesimama huonekana ni nzuri na imara ila nguzo hiyo huweza angushwa na mdudu mdogo sana aitwaye mchwa. Ikiwa imesimama mchwa wanaisogolea hili kuanza kuitafuna ila kama imekingwa na vidhibiti vya mchwa si rahisi kuweza kuliwa. Ndivyo ilivyo kuna mambo watu huyaona ni madogo madogo sana ila ndiyo mambo hayo hayo yaliyo kwazo la kufanikiwa kwa mtu na zaidi huweza mnyima mtu nafasi ya kuziingia mbingu. Ukimtazama mtu ambaye anguko limetokea wengi waweza shangaa sana ila ukweli ni kwamba kuna mchwa walikuwa wanakula ndani kwa ndani na mtu huyo hakuweza kuwazuia wasiendelee sasa wamekula mpaka kuozesha nguzo hiyo na ndiyo maana imeanguka kwa kuwa imeoza na imeshindwa kujimudu.

Ni vyema sana kutodharau mambo madogo madogo kwa kuwa hata shetani anajua kuwa hawezi kukupata kwenye makubwa na ndiyo maana anaweza kutumia vitu vidogo na kuvilemba sana hata ukavitetea na kuviona vyafaa sana ila mwisho wake ni kukupeleka katika maangamizo makubwa. Waswahili usema “usipoziba ufa utajenga ukuta” tazama kwa umakini sana na usiruhusu kabisa madogo kupata nafasi ya kukuangusha. 

Maangamizo makubwa uletwa na vitu vidogo. 

Kwa kuitazama njiti ya kiberiti ni njiti ndogo sana ila inauwezo wa kuchoma msitu mkubwa uliokaa kwa kitambo kirefu ndani ya masaa machache sana uteketea kwa matokeo ya njiti hiyo. Pia magonjwa yanayomsumbua mwanadamu hutokana na wadudu wadogo sana kwa kuutazama mfano wa mbu ni kiumbe kidogo sana ila ueneza malaria ambayo uua watu wengi sana ila cha msingi ni “kinga ni bora kuliko tiba” jikinge kwa kila tahadhari na kwa gharama yoyote kabla ya hatari na ni bora watu wakaona wewe ni muoga ila kwako si uoga bali ni usalama. Wengine huikimbia sana zinaa na kuitwa waoga na washamba ila hawa sivyo kama watazamavyo ila wameepuka hatari na kufuata usalama.

Mfano mwingine wakuona ni mfano wa nzi kuwa ni mdogo sana ila usababisha ugonjwa mkubwa wa kipindu pindu ila kinga yake ni kutumia chakula cha moto na kisafi ambacho hushindwa mudu kukisogelea na vivyo hivyo kwa mwamini ni bora kuwa safi na wa moto ili kuepuka hatari. Ukiwa safi na wa moto vitu vichafu haviwezi kupata fursa ya kuwa karibu na wewe na kukufanyia maangamizo makubwa.

–Kelvin Kitaso

NGUVU zako WAKATI wa MAJARIBU!!

“Nguvu zangu ni zipi, hata ningoje? Na mwisho wangu ni nini, hata nisubiri? Je! Nguvu zangu ni nguvu za mawe? Au mwili wangu, je! Ni shaba? Je! Si kwamba sina msaada ndani yangu. Tena kwamba kufanikiwa kumeondolewa mbali nami? Kwake huyo atakaye kuzima roho inapasa atendewe mema na rafiki; Hata kwake huyo aachaye kumcha Mwenyezi” (Ayubu: 6:11-14).

Nimesoma tena habari za Ayubu nikaona jambo. Kuzimia roho maana yake ni kukata tamaa au kuishiwa nguvu za kuendelea na msimamamo au jambo unalofanya. Ayubu alifika mahali pa kuzimia roho wakati anapita kwenye JARIBU ambalo lengo lake ni KUPIMA kile ambacho Mungu aliona ndani yake, yaani “mkamilifu, mwelekevu, mcha Mungu na aliyejiepusha na uovu” (Ayubu 1:1). Kwa sababu ya UBORA wa Ayubu, Mungu akajisifu juu ya Ayubu lakini Ibilisi aliona kwamba Ayubu alikuwa na SABABU nyingine ya kuishi hicho kiwango bora cha maisha na wala sio kwa sababu ya kumcha Mungu tu. Angalia hapa, “Ndipo Shetani akamjibu BWANA, na kusema, Je! Huyo Ayubu yuamcha BWANA bure? Wewe hukumzingira kwa ukigo pande zote, pamoja na nyumba yake, na vitu vyote alivyo navyo? Kazi za mikono yake umezibarikia, nayo mali yake imeongezeka katika nchi” (Ayubu 1:9, 10).

Kuna tofauti ya kumcha BWANA kwa sababu ya sheria, watu wanaokuzunguka, hofu ya matokeo ya uovu wako kwa jamii, hofu ya mume au mkeo, hofu ya kupoteza kazi, hofu ya kupata aibu, hofu ya magonjwa, hofu ya kufa, nk. na kumcha Mungu kwa sababu UNAMHESHIMU na KUMPENDA tu. Iko tofauti kubwa, na hii sababu ya kumcha Mungu kwa sababu umeamua kumheshimu na kumpenda, ni jambo ambalo ni bora na la kumvutia Mungu sana. Angalia, Mungu anasema “hakuna aliye kama Ayubu duniani” (Ayubu 1:8), inamaana Mungu aliangalia na kuona viwango tofauti ndani ya “watakatifu walioko duniani” kisha akaona “ni yupi anampendeza zaidi”. Safari hii, BWANA aliamua kusema habari za Ayubu kwa maana viwango vyake vilikuwa vya juu kuliko wenzake wote juu ya nchi.

Angalia tena jambo hili, akili za kawaida za mke wa Ayubu hazikujua kwamba hata walio wakamilifu na wacha Mungu hupatwa na mambo magumu! Ona tena hapa Ayubu anamjibu mkewe, “Lakini yeye akamwambia, Wewe wanena kama mmoja wa hao wanawake wapumbavu anenavyo. Je! Tupate mema mkononi mwa Mungu, nasi tusipate na mabaya? Katika mambo hayo yote Ayubu hakufanya dhambi kwa midomo yake” (Ayubu:2:10). Angalia tena, kama jambo halikufikishi mahali pa kutenda dhambi hilo sio jaribu. Ayubu hakutenda dhambi hata kwa hatua hii ambayo mkewe alimfikisha, yaani hata kumwazia Mungu vibaya licha ya kufanya dhambi kwa matendo yake.

Angalia jambo hili tena, wakati Ayubu anajua na kutarajia kutiwa moyo, kufarijiwa na kupata bega la kuegemea wakati wa shida yake, hakupata sio kwa mkewe wala marafiki zake! Ndipo akasema, “Kwake huyo atakaye kuzima roho inapasa atendewe mema na rafiki; Hata kwake huyo aachaye kumcha Mwenyezi”. Ndipo nikajua, kumbe! Watu wengi wanakata tamaa, kuchoka au hata kumtenda Mungu dhambi, eti, hawajatiwa moyo! Au kuna mtu amewakatisha tamaa au kuwavuruga? Na sasa WAMEAMUA kufanya dhambi tu! Je! Umeona kiwango hiki cha kumcha Mungu? Yaani mtu anamcha Mungu kwa sababu “ametendewa mema”, akitendewa asivyotarajia “anaacha kumcha Mungu”! Basi nikajifunza jambo hili. Katika shida zangu na majaribu yangu, wapo watu ambao kazi yao itakuwa kuondoa tegemeo langu kwao, au kunikatisha tamaa, au kuweka vikwazo zaidi, au kuja na namna mbali mbali za kunisukuma ili kuniangusha. Ole wake ambaye nguvu zake ziko katika “wema wa wanadamu” na kusaidiwa nao! Maana kama Ayubu naye angekuwa hivyo, jina lake lisingetajwa kamwe japo alifanya mengi mazuri huko nyuma, ila jaribu hili asingevuka kwa sababu “rafiki na watu wake hawakumtendea wema”.

Angalia jambo hili la rafiki wataabishaji wa Ayubu, “Kumbuka, tafadhali, ni nani aliyeangamia akiwa hana hatia? Au hao waelekevu, walikatiliwa mbali wapi? Kama mimi nilivyoona, hao walimao maovu, Na kupanda madhara, huvuna yayo hayo.” (Ayubu 4:7,8). Mawazo yao ni kama ya wale wasiojua njia za Mungu. Wanajaribu kumwambia Ayubu kwamba anapata mabaya kwa sababu ametenda dhambi, kumbe! Ni kinyume chake. Ayubu anapata majaribu kwa sababu ya ubora wake sio kwa sababu ya uovu wake! Naye Ayubu akajibu na kusema, “Nifunzeni, nami nitanyamaa kimya; Mkanijulishe ni jambo gani nililokosa. Jinsi yafaavyo maneno ya uelekevu! Lakini kuhoji kwenu, je! Kumeonya nini? (Ayubu 6:24,25). Kila Ayubu akiangalia na kujitathimini haoni jambo, ndipo anasema jamani, niambieni nimekosa nini sio kunisomesha tu maneno, niambieni mimi nijue maana kuhoji kwenu hakunisaidii kitu, niambieni nimekosea wapi?

Angalia tabia ya Ayubu. Sio tu kwamba alikuwa hatendi dhambi ila “alijiepusha na uovu” kwa kiwango kwamba hata alitoa sadaka na toba kwa watoto wake ili isije ikawa wanatenda dhambi au kumkufuru Mungu wakati yeye hajui! (Ayubu 1:5). Ayubu alifika kiwango cha kufanya toba hata kwa dhambi ya kudhaniwa achilia mbali aijuayo, leo anaambiwa “mabaya haya ni kwa sababu umetenda dhambi”! jambo hili likamsumbua Ayubu. Hata leo, mbona wanadamu wanazidi kuwaza namna hii? Yaani mmoja wetu akipatwa na mabaya akili zinakimbilia kufikiri ni kwa sababu ya uovu wake, na sasa analipwa sawa na matendo yake! Kwanini tusijifunze kwa Ayubu?

Katika mambo yote, yaani yalikuwa mengi, Ayubu hakutenda dhambi. Mara nyingi Jaribu linakuwa moja ila linakuwa na awamu zake nyingi. Kwa mfano, mtu anaweza asizini, ila katika mchakato wa kuepuka zinaa, kashatukana, tamani, laani, pigana, kusema uongo, nk. umeona hapo? Je! Huyo naye kashinda jaribu? Kwanini kuruka majivu na kukanyaga moto? Sasa angalia tena kwa Ayubu, haya ndio majaribu ya Ayubu, alipewa majaribu mawili, kwanza kuguswa mali zake na pili, kuguswa mwili wake, lakini ukiangalia utaona wanakuja watu hapo, mkewe na rafiki zake ili Ayubu akosee na kutenda dhambi NYINGINE. Lengo la Ibilisi ni utende dhambi, na usimche Mungu, haijalishi ni dhambi ipi au humchi Mungu kwa mtindo gani. Katika mambo yote, Ayubu hakutenda dhambi kwa matendo, kinywa wala mawazo.

Jifunze kujua na kutambua majaribu yako. Jifunze kujua jinsi ya kushinda kwa halali, na jifunze kusimama peke yako bila kumlaumu mwingine kwa kushindwa kwako kwa maana hatukuitwa kwa makundi bali mmoja mmoja. Jifunze kujua mchakato na vipengele vya muhimu kujilinda ujaribiwapo ili upate ushindi kamili. Nguvu zako zinatoka wapi wakati wa Majaribu?

Heri mtu yule ambaye anamcha Mungu kwa sababu AMEAMUA kumcha bila kujali kupungukiwa, kuwa na vingi wala kufanyiwa mema au mabaya na mtu awaye yote. Huyo ni kivutio kikubwa cha Mungu Baba.

Frank Philip Seth.

The Power of God in You!

Luke 10:19 “Behold, I give unto you power…”

I’m sure that you, like me, have read many inspirational stories over the years. The children of this generation are told stories all the time followed by the words “You can do anything if you put your mind to it.” I like that people are inspired. It’s better than being told “You are good for nothing and you won’t amount to anything.” Positive and encouraging words spoken over others is something God’s word encourages us to do but, those words are meant to be rooted in the promise of the Holy Spirit working in us and helping us reach our dreams. That is where the power to overcome comes from! To think we can do anything that is significant in His eyes without His guidance and direction and help is futile thinking.

Any power within us is only the power of God.  Before you give your life to Jesus Christ, God’s Word makes it clear that you are stuck in Satan’s grip and power. No one wants to hear that. You might think, “How could that be possible? I’m not under Satan’s power.” I remember thinking that when someone was sharing Jesus with me before I gave my life to Him. God’s Word makes it clear that when we receive Jesus into our hearts as Lord and Savior – we change kingdoms and are rescued from Satan’s power and brought under and given God’s power. Col. 1:13 says, “God who has delivered us from Satan’s power – the power of darkness, and has translated us into the kingdom of His dear Son Jesus..” Acts 1:8 then says, “But you will receive power when the Holy Spirit comes on you; and you will be my witnesses…”

If you want to see a world that is under Satan’s power but does not recognize it, go watch the movie-documentary “Super Size Me.” If you were to look into stats on the amount of money gambled and lost, the amount of money spent on alcohol and recreational drugs and the addictions and the problems and deaths they’ve caused, if you will look into the amount of money spent on cigarettes and the health issues and deaths they have caused, if you will look into the amount of money it takes police to catch, prosecute, and jail or imprison criminals, or the amount of money spent on our military to defend our country from enemies, you will find that we squander, waste, and spend the majority of the world’s wealth – literally trillions on evil or the protection from it. Surely this world is under Satan’s grip and his power. People don’t have the power do to do anything they want. They don’t even have the power to stop evil thinking and actions in their lives without the power of Jesus.

To most people the thought of power is more of a fantasy or a game, but not something they really give all that much thought to. God wanted us to not only know of His power but to experience it at the most base level of our lives – the power to make sound godly moment-by-moment decisions with the courage and strength to carry them out. Remember that the next time you begin something as simple as a diet! Forget what you’ve been taught by television and movies when you think of power.

Instead, think of it as the supernatural and inward strength of God working within you to actually live godly and upright in thought and actions in a world of corruption and evil. Think of it as the power bringing you courage and boldness to stand up for your faith in God and what you believe. Think of it as the supernatural power of God working behind the scenes to work through your prayers and to guide your steps and life. Think of it as strength from God to say “yes” to right choices and “no”to temptations!

“Behold, I give unto you power…”If you are a believer, God has made His power available to you. If you walk in faith believing in it because you know God promises it to you, then it becomes tangible to you. To be inspired is good, but motivation can be a flash in the pan – quick in coming and quick in departing. Faith in God’s power working within you should become the core of your belief system and a blessing and strength that you draw from day in and day out!

2 Peter 1:4 “And by that same mighty power, God has given us all of his rich and wonderful promises. He has promised that you will escape the decadence all around you caused by evil desires and that you will share in His divine nature.”

In His Love,
Pastor Tim Burt

Sababu saba zitakazokufanya kuwa mshindi…

Glory to GOD watu wa MUNGU, leo ninataka nizungumze na wewe Sababu saba zitakazokufanya kuwa Mshindi Duniani…Zifuatazo ni Sababu hizo..

1.NENO LA MUNGU LIWE KWA WINGI NDANI YAKO..
Neno la MUNGU likiwa kwa wingi ndani yako ni Dhahili utakuwa Mshindi lakini ndani yako kukiwa na Maneno mengine kinyume na Neno la MUNGU unaweza ukatikiswa na adui na kujikuta umeanguka, ndio Maana Mfalme Daudi akasema “Moyoni Mwangu nimeliweka Nno lako nisikutende dhambi” Zaburi 119:11,Je moyoni mwako wewe umeweka Neno la namna gani??

2.MAOMBI/KUOMBA….
Daniel,Eliya,Mussa,Bwana YESU,nk Hawa wote walihakikisha wanaishi katika Maombi,Wakati Mwingine kwa kufunga,Bwana Yesu kuna sehemu aliwaambia wanafunzi wake hamkuweza kukesha name hata saa moja

Mathayo 26:40 “Akawaendea wale wanafunzi, akawakuta wamelala. Akamwambia Petro, Ndiyo kusema hamkuweza kukesha pamoja nami hata saa moja? 41 Kesheni na kusali ili msije mkaingia katika majaribu. Roho i tayari lakini mwili ni dhaifu.”

3.MAONO..
Hakikisha katika maisha yako Duniani unakuwa na maono, (Yaani mtazamo wa Mbeleni) hata kama wenzako hawajafika wewe unasema nitafika, usiishi bila maono, ukiwa na maono mipango yako inakuwa inaenda vizuri pasipo na shida.

Bila ya kuwa na maono ya wapi unaelekea ni rahisi kuchukuliwa na upepo na kupelekwa usikokutazamia. Maono yatakufanya ujue ni nini ufanye kwa ajili ya Mungu na maisha yako kwa ujumla.

Mithali 29: 18 Pasipo maono, watu huacha kujizuia; Bali ana heri mtu yule aishikaye sheria.

4.KUTOKUWA NA TAMAA YA VITU VISIVYOFAA
Kuna watu wanatamani vitu visivyofaa ambavyo ni kinyume na agizo la MUNGU, Ndiyo maana MUNGU akasema usitamani mke wa jirani yako,wengine wanatamani mali za wengine bila kujua chanzo chake na wengi wamepotea kwa namna hiyo

Zaburi 119:37 Unigeuze macho yangu nisitazame yasiyofaa, unihuishe katika njia yako.

5.AMBATANA NA MARAFIKI WEMA..
(Mithali 27:17) Chuma hunoa chuma. ni dhahili chuma hakiwezi kunoa embe angalia marafiki zako wanakunoa au?? angalia mtazamo wao, kuwaza kwao,nk..Wao waliokutana na Marafiki wabaya, ambao wamesababisha mpaka maono yao kufa na kurudi nyuma kwa kumuacha BWANA YESU KRISTO..Wapo waliokutana na marafiki wabaya waliokuwa na lugha chafu na kusabadilisha..Je una marafiki wa aina gani??

6.KUTOMWEKEA MUNGU MIPAKA

Hii ni hali ya mwanadamu kuamini kuwa Mungu anaweza hili na hili hawezi…kitendo hiki Mungu anakiita kuwa ni ‘DHARAU’ kwake… Zaburi 78:41 inasema, “Wakarudi nyuma wakamjaribu MUNGU; Wakamwekea MPAKA Mtakatifu wa Israel” Mstari huu wa Zaburi unaelezea maisha ya wana wa Israel njiani toka Misri kwenda nchi ya Maziwa na Asali-Kanaani. Biblia inaeleza jinsi Musa alivyowatuma wapelelezi 12 kwenda kuipeleleza nchi ya ahadi waone kama kama kweli ni nchi ya ‘Maziwa na Asali’…10 kati yao Waliporudi walirudisha ripoti ya kuwa kweli ile nchi ni ya maziwa na asali, ila inakaliwa na Wanefili-wana wa Anaki…majitu na ya kwamba wao ni kama panzi tu na hawawezi kwenda na kuimiliki. Joshua na Kalebu walileta habari njema…waliona kwa macho lakini wakazungumza kile ambacho ni ‘UHAKIKA WA MAMBO YATARAJIWAYO’ wakamwamini Mungu kuwa aweza kuwapa ile nchi kuwa milki yao sawa na alivyomwapia Ibrahim (Hesabu sura ya 13 na ya 14) na wote waliomwekea Mungu mpaka walikufa huko jangwani, hawakuingia nchi ya ahadi…WALIFUPISHA MAISHA YAO KWA KUTOKUAMINI KWAO…Ila Kalebu aliishi muda mrefu sana, alikuwa na nguvu kama za mtu wa miaka 40 hata alipokuwa na miaka 85( soma Joshua 14:6-14) na inaeleza pia ya kuwa Joshua alikuwa MZEE SANA, alikufa akiwa na miaka 110 lakini alikuwa na nguvu zake kamili mpaka pale BWANA alipompumzisha(Joshua24:1-29)Kama unataka kuwa na maisha marefu, na unataka kuziongeza siku zako…ishi maisha ya IMANI…Usimwekee Mungu mipaka, kumbuka, “Njia zake zi juu mno na fahamu zake pia” Isaya 55:8-11

7.KUACHA DHAMBI

Dhambi ni mbaya…inakutenga mbali na Mungu (Isaya 59:1-2) lakini kibaya zaidi inapunguza maisha yako…inakufanya ufe kabla ya muda wako…Unafurahia kuishi maisha ya dhambi? ni mzinzi, mwongo, msengenyaji, usiyesamehe,mwenye kinyongo, kisasi nk? Unajipeleka kaburini kabla ya wakati wako…unafanya kazi ambayo mshahara uitwao ‘MAUTI’ utaupata.Katika Warumi 6:23 Biblia inasema, “Kwa maana mshahara wa DHAMBI ni MAUTI(KIFO), bali karama ya Mungu ni uzima wa Milele katika Kristo Yesu Bwana wetu” pia Biblia inasema, “Roho itendayo DHAMBI ndiyo itakayokufa”Maisha ya dhambi yanakata muda wa mtu wa kuishi…Ni wangapi waliokufa wakiwa vijana wadogo kwa sababu ya UKIMWI kwa kutoikwepa dhambi ya Uzinzi? au ni Wezi wangapi wamekufa wakiwa katika harakati za kuiba?Dhambi ni adui mkubwa kwangu na kwako!

–Mwl.Conrad..

Kukosa maono ni sababu ya kushindwa kwako – II

maono

Inaendelea kutoka https://strictlygospel.wordpress.com/2015/01/27/kukosa-maono-ni-sababu-ya-kushindwa-kwako-i/

Kutokuwa na vipaumbele katika maisha.

Kukosa maono kunapelekea mtu kushindwa kujizuia na huku kushindwa kujizuia ndikokutokuwa na vipaumbele. Mtu yeyote mwenye maono ni lazima atakuwa na vipaumbele vyamsingi  katika maisha yake na vipaumbele  hivyo umpelekea kufikia utimilifu wa maonoaliyonayo.

Vipaumbele ni vitu ambavyo upewa umuhimu wa hali ya juu na upewa umakini mkubwazaidi ya vitu vingine vyote. Na vitu hivi uweza chukua muda mwingi wa mtu kuliko vituvingine  vyote  na  mtu  uwa  makini  sana  kutoruhusu  vitu  vingine  ambavyo  vitaharibuutaratibu uliopo. Vipaumbele upelekea utimilifu wa maono aliyonayo mtu na umfanya mtukuzingatia kuwa sehemu sahihi, wakati sahihi na watu  sahihi.

Kwa mfano mwanafunzi  awapo shuleni  ni  lazima awe na vipaumbele  vya msingi  kamakumtumikia Mungu kama balozi wa Yesu katika eneo asomalo na kusoma kwa bidii zotekwa kuwa ni jukumu la msingi pia lililompa kuwepo mahali hapo. Na si kwa wanafunzi tubali  hata  aliyepo  kazini  ni  lazima  awe  na  vipaumbele  vya  msingi  vitakavyompelekeakufanikiwa katika kufikia hatima yake iliyo njema.

Hasiye  na  vipaumbele  ufanya  mambo  yake  pasipo  mpangilio  na  uwa  ni  mtu  asiye  namisimamo juu ya yale ayafanyayo na ukosa kujitoa kikamilifu katika mambo ayafanyayo.

Katika vipaumbele ni vyema kuzingatia kuwa kila jambo katika ulimwengu huu lina majirayake, na nyakati zake na utambuzi huu utamfanya mtu kufanya kitu sahihi katika wakatisahihi na kuepuka kufanya jambo ambalo lipo nje ya wakati.

MAMBO YA MSINGI KATIKA KUFANIKISHA VIPAUMBELE VYAKO.

– Chagua marafiki sahihi.

– Kuwa mahali sahihi, sehemu sahihi na ukifanya jambo sahihi.

– Kila  jambo ulifanyalo zingatia  wakati  kwa kuwa kila  jambo lina  wakati  wake namajira yake/ukomboe wakati.

– Ishi kwa malengo, timiza malengo yako.

– Usiishi maisha ya kuigiza, ishi maisha yako.

– Tumia vyema fedha uzipatazo hata kuweka akiba ya kukusaidia baadae.

– Kuwa hodari na moyo wa ushujaa/ usiogope kwa kuwa yapo mengi yaogopeshayo ilasababu ya kutoogopa ni kuu zaidi ya hayo yote.

– Mwamini Mungu.

– Jiamini wewe mwenyewe kuwa unaweza.

Matumizi mabaya ya muda.

Kukosa maono pia kunamsababisha mtu kutotumia muda wake vizuri hii ni kwa sababuhana  kitu  kinachomchochea  kutumia  vizuri  muda  wake  kwa  kuwa  maono  ni  kamamuongozo  unaomchochea  mtu  kufanya  kazi.  Kuna  msemo  unasema,  ‘Time  wasted,  lifewasted’ kwa kumaanisha kuwa kupoteza muda ni kupoteza maisha, hii ni kwa sababu mudakamwe hauwezi  kujirudia yaani  ukienda umeenda.  Kila saa tulipatalo hapa chini  ya juatwapaswa kulitumia vyema kwa kuwa halitokuja kurudi tena na haliwezi kukusubiri wewekutokana na uzembe au kutojitambua kwako.

Matumizi  mabaya  ya  muda  ni  pamoja  na  kujishughulisha  na  kufanya  mambo  ambayohayatakusaidia  kufikia  malengo  yako,  kwa  mfano  kutumia  muda  mwingi  kuangaliatamthilia,  filamu  na  kufanya  michezo  mingi  isiyo  na  mchango  wowote  wa  kukufanyaufanikiwe katika maisha yako.

Hii  utokea  kwa  vijana  wengi  sana  kuwa  na  matumizi  mabaya  ya  muda  kwa  kutazamamifululizo ya matamthilia kwa muda mwingi na wengine utumia hata muda wa kusoma au kazi na muda wa kumfanyia Mungu ibada, wengine pia umaliza muda wao mwingi kuchezamagemu ambayo uchukua muda mwingi pia sana, na wengine utumia muda mwingi katikamitandao ya kijamii. Vitu vyote hivi uwa na uzuri wake na ubaya wake na uweza msaidiamtu au kumuharibu kabisa;  ila ni  vyema kuzingatia sana muda kwa kufanya mambo yamsingi zaidi  ambayo usaidia katika kufikia mambo ya msingi na hata kugundua mambomakubwa. Wengine wamekuwa wakiamini kuwa hawawezi kugundua mambo makubwa ilatatizo moja wapo ni matumizi mabaya ya muda.

“ukitaka  kufanya  mambo  makubwa  na  yakatokea  na  kuushangaza  ulimwengu,hata  kuweka  historia  ya  kuishi  kwako  kwa  kugundua  na  kufanya  mambomakubwa ambayo wengine hawayafanyi ni lazima uwe makini katika matumizi yamuda wako kwa faida na kwa busara kwa kukwepa kila kitu kisicho na faida”

Kwa Waafrika suala la matumizi mabaya ya muda kwao limekuwa ni kawaida sana na watuwengi  wamekuwa  na  tatizo  la  kutoheshimu  muda.  Kuna  msemo  ambao  umekuwa  nikichocheo kikubwa cha watu kushindwa kutumia muda wao vizuri, na kichocheo hiko nineno ambalo upendwa sana kutumiwa haswa nchini Tanzania lisemalo, “muda wa kizungu,na muda wa Kiswahili/Kiafrika,”  maneno haya yamesababisha watu wengi kuendelea natabia ya matumizi mabaya ya muda katika miadi/mapatano yao na mambo mengine mengitu.  Katika matumizi  ya muda waswahili  wakitaka kuanza shughuli  saa 3:00 utoa taarifakuwa tukio litaanza saa 3:00 ya kizungu na uamini kuwa saa 3:00 ya Kiswahili katika miadini sawa na saa 4:00 ya Kiswahili au utoa taarifa kuwa tukio linaanza saa 2:00 wakijua kuwawatu watachelewa mpaka saa 3:00 ndo waanze. Tiba ya tabia hii ni kuanza katika muda wamapatano hata kama watu wamechelewa kwa kufanya hivyo siku nyingine itafanya wawahizaidi. Matumizi mabaya ya muda umfanya mtu kutofikia mambo mengi na kuyafanya kwausahihi. Si kweli kuwa kuna muda wa kizungu na muda wa Kiswahili, ni vyema kwa kilammoja kuzingatia matumizi ya muda na kuheshimu matumizi hayo.

Mungu Anaona Ambayo Wengine hawaoni juu yako.

Ikiwa Mungu aliona taifa kubwa ndani ya Yakobo mchunga mifugo wa Labani, akaonaWaziri Mkuu ndani ya Yusufu mfanya kazi wa ndani na mfungwa kule Misri, akaonamkombozi wa Israeli kwa Musa mchunga mifugo kule Midihani kwa Kuhani Yethro,Akamwona  Mwamuzi  wa  Israeli  Gideoni  yeye  Ambaye  alikuwa  dhaifu  na  kutokakatika familia ya hali ya chini sana, Akamwona Yefta aliyekataliwa na ndugu zake nakumfanya kuwa mwamuzi wa wana wa Israeli, Akaona Mfalme wa Israeli ndani yaDaudi Mchunga mifugo na hakutazamiwa hata na baba yake, Akaona Mwokozi waulimwengu na Mfalme wa mataifa katika Zizi la Ng’ombe (Yesu), Leo hazuiwi na haliuliyonayo  wewe  kukufanya  mtu mkubwa,  usiache  kumtumaini  ni  lazima atafanyaalichokusudia kwako.

–Na: Mwl. Kelvin Kitaso

Kukosa maono ni sababu ya kushindwa kwako!! – I

maono

“Pasipo maono watu hushindwa kujizuia”

Maono ni kama kesho ya mtu.

Kesho ni siku ambayo utarajiwa na haijaonekana bayana bado, na hakuna mwanadamu yeyote chini ya jua aijuaye kesho yake ipoje isipokuwa amejuzwa na Mungu ajuaye mambo yote kabla hayajatukia. Kesho ni siku ambayo ni matokeo ya kile kitu ambacho kimefanyika leo; kesho uandaliwa ndani ya leo, Mungu ndiye utoa jawabu kama iwe kama vile ulivyoiandaa.
Kuna msemo wa kiingereza usemao, “Yesterday has passed, today is here, tomorrow never come” hii inaonyesha kuwa katika maisha yote ya mwanadamu kuna siku tatu tu yaani jana, leo na kesho na mwanadamu anapaswa kuzitumia siku zote hizo kwa faida yake mwenyewe na kunufaisha jamii inayomzunguka pia.

Jana ni siku ambayo imepita na ukutengenezea uzoefu (CV) ambao waweza kuwa mzuri au mbaya na kamwe hautoweza kurudi jana kuibadilisha jana yako ila unaweza kuitumia Leo kuifanya kesho isijekuwa kama jana. Jenga tabia njema ya kutojisifia kwa mazuri uliyofanya jana kwa kuwa kujisifia kutakufanya ujisahau kuwa unapaswa kusababisha mambo makubwa kutokea tena na tena kamwe usijaribu kujilaumu kwa vile ulivyoshindwa jana kwa kuwa itakufanya uwe muoga wa kujaribu kufanya mambo makubwa leo. Lakini mazuri ya jana yanaweza kutumika kama marejeo kuwa kama jana nilishinda basi na leo pia naweza kushinda kama ilivyokuwa kwa Daudi aliporejea kuua simba na dubu alipotaka kupambana na Goliathi.

Kesho ni mimba ambayo imetungwa leo na yapaswa kujifungua ni muhimu sana kuzingatia ili kuweza kujifungua mtoto aliye mzuri na hii inatokana na mimba hiyo imetungwaje na katika hali gani. Kujifungua mimba hii kunahitaji nguvu ya mbeba ujauzito na pia Mungu akusaidie kujifungua salama.

Kesho ni ahadi ambayo imetoka kwa Bwana kwa kuwa ahadi ni mambo yatarajiwayo na hayajaonekana bayana bado, hapa ninazungumzia zaidi ndoto au maono ya mtu ambayo ndiyo kesho yenyewe na utarajiwa kutimia na hayajaonekana bayana bado.Kitu chochote unachokifanya leo kinaonyesha kuwa kesho yako itakuwaje.

Ni lazima uione kesho yako ukiwa leo kwa kuwa kesho yako inategemea sana na wewe unaona nini ndani yako mwenyewe ukiwa leo na si kuona tu pia unakiri nini kwa kuwa kuna nguvu katika ukiri wa maneno na si ukiri tu bali ni nini ukifanyacho leo kinaweza kuitimiza kesho yako. Kitu ukionacho ndani yako, ukikiricho na hata kukifanya ugeuka kuwa tabia na kikiwa tabia mwishoni uja katika uhalisia wa utimilifu wake.

Kesho yako haitakuja kama muujiza yaani umeamka na kuiona tu inatimia, hapana ni mchakato mrefu ambao unakuitaji mwamini kutia juhudi za kutosha ili iingie kwenye utimilifu wake. Kama haujaanza kuwaza kuwa kesho yako itakuja kuweje kamwe usijedhania kama kitakuja kutimia kwako kitu ambacho hujawahi kukiwaza hata siku moja, mtu anaweza kuhangaika na kitu ambacho amewahi kukiwaza hapo awali kuliko kile kitu ambacho hajawahi kuwaza kabisa.

Lazima uione ndani yako kwanza. Mwanadamu huwa vile anawaza ndani yake kwa kuwa lile wazo humpa hamasa ya kufanya kazi ili litokee na wazo pia la ndani yake uweza mfanya kukata tamaa ya kufika mbali. Mtu mmoja akasema kuwaza ni kuwaza tu kama umewaza mambo makubwa au madogo ni bora ukawaza vitu vikubwa labda waweza kuwa mtu mkubwa. Lakini kuwaza tu pasipo kuchukua hatua hakufai.

Mithali 23:7 “7 Maana aonavyo nafsini mwake, ndivyo alivyo.” Yaani ukitangulia tu kuona kuwa wewe ni maskini mkubwa ni lizima uwe, ni lazima ujifunze kuona vyema. Watu wakubwa duniani kabla ya kuwa vile walivyo, walitangulia kuona ukubwa ndani yao kwanza na kisha wakaanza kufanya kazi kwa kuwa ile picha waliyoiona ndani yao uwatesa kuifikia.

Katika biblia neno ‘unaona nini?’ limeonekana mara saba na siku za wiki zipo saba, ina maana ya kusema kila asubuhi BWANA uweza kukuuliza ‘unaona nini?’ mpaka zikaisha siku saba za wiki na itakapoanza jumatatu ataanza na unona nini? tena mpaka Ijumaa huku akiunganisha na neno usiogope kwa kila siku uionayo katika uwepo wako duniani.

Kofi Anan ambaye ni katibu mkuu wa zamani wa umoja wa mataifa baada ya kuingia UN katika nafasi ya kawaida tu akamwandikia mama yake ujumbe na kumtaarifu kuwa siku moja ni lazima aje kuwa katibu wa umoja wa mataifa. Alivyoona ndivyo ilikuja kutokea na kule kuona kwake kulimlazimu kutotulia na kuwa na juhudi kubwa sana ili badae aje kuwa katibu mkuu wa umoja wa mataifa.

Kama kuna picha tayari unaiona ndani yako ya jinsi vile unavyopaswa kuwa ni muhimu sana kuzingatia kuwa picha ile ni nguvu ya kukufanya upigane hata kuitimiza; ila mbaya zaidi ni kwa mtu asiye na maono kwa kuwa hana picha ndani yake ni vigumu kwa yeye kufanya kitu cha msingi.

Maandiko yanasema katika Mithali 28:19 kuwa “18 Pasipo maono, watu huacha kujizuia”, tafsiri ya asili ya kiebrania kutoka katika neno ‘hazon’ utafsiri maandiko haya kwa kumaanisha mafunuo ya neno la Mungu, na uendelea kwa kumaanisha kuwa pasipo neno la Mungu kufunuliwa kwa watu ni lazima watu waende katika njia ya upotevuni. Mahali popote ambapo neno la Mungu halijafunuliwa ni lazima watu waangamie na kuendelea katika njia zao wenyewe kwa kuwa bado uwa kwenye mabano ya wafanye kipi na kuacha kipi.

Kwa kuangalia maono pia mtu yeyote ambaye hajafunuliwa ni maono gani alionayo ni kazi sana kuwa katika njia sahihi. Jamii inayotuzunguka watu wengi hukosa maono na ndiyo maana huishia kufanya vitu vya ajabu sana. Maono ni ile picha ya ndani aionayo mtu kwa habari ya kesho yake na kama mtu haoni picha yoyote ndani yake ni vigumu kufanya vitu vya msingi vya kimaendeleo.

Mtu mwenye maono hata kama anaonekana maskini kwa wakati huo ni mtu wa tofauti kwa kuwa maono ni muongozo wa utendaji kazi wa mtu huyo na ni lazima afanye mambo ambayo yanapelekea utimilifu wa maono hayo na uishi maisha ya kujizuia katika mambo yoyote ambayo hayamsaidii kufikia mwisho wake. Mtu mwenye maono hawezi kutulia hata maono yake yawe yametimia. Maono utoa muongozo wa jinsi mtu apasavyo kuwa na hata jamii ya kushirikiana nayo.

Nikiwa sehemu Fulani nahudumu baada ya huduma nikamuuliza kijana mmoja unatakakuja kuwa nani? yule kijana akanambia nataka kuja kuwa dereva na alikuwa anasoma na nilipomuuliza kwa nini anataka kuja kuwa dereva akanambia ni kwa sababu wazazi wake hawana uwezo wa kumuendeleza kimasomo, nilitafakari kuwa mtu huyu anataka kuja kuwa dereva kwa ajili ya hali ngumu ya kiuchumi ni vizuri ila katika mazungumzo nikagundua kuwa amekata tamaa ya kufanikiwa zaidi kwa sababu ya hali yake ila mwenye maono hata kama ana hali ngumu kamwe hatoacha kuukiri ushindi wake kuwa pamoja na ugumu uliopo ninaweza nikafika pale napokusudia na hata kama nitachelewa kulingana na vikwazo vya hali niliyonayo sasa ila nitahakikisha nimefika.

Pamoja na kuwa mfanya kazi wa ndani kwa Potifa na kisha kupelekwa gerezani na kuwa mfungwa, bado Yusufu aliendelea kuitazama na kuikili ndoto yake ya kuja kuwa mtu mkubwa, mazingira mabaya na ya kukatisha tamaa hayakumfanya Yusufu akate tamaa na kubadilisha aina ya ndoto. Ni ukweli sana kuwa ugumu wa maisha ni sababu kuu sana ya kusababisha watu kuyaacha maono yao ya uhalisia na kuingia katika mengine ambayo si maono yao.

Mtu asiye na maono ni lazima mambo yake yawe ovyo ovyo kwa kuwa hakuna mwongozo sahihi unaoweza kumzuia asifanye yale ambayo anataka kufanya. Maono ni muongozo kwa mtu mwenye nayo katika mambo yote na umuongoza kuwa sehemu sahihi kwa wakati sahihi na kuwa na watu sahihi. Na ni nadra sana kumkuta mtu mwenye maono anafanya mambo ambayo hayawezi kumsaidia kufikia utimilifu wa maono yake.

Ni muhimu sana kwa mtu kuiona kesho yake ndani yake na aione katika uzuri ndipo anaweza tumia muda wake vizuri kutimiza yale ayaonayo. Kuona ni jambo jema sana ila mtu aweza ogopa kuwaza mambo makubwa na hii utokana na mtu kujidharau na kuona kuwa ana uwezo mdogo sana ndani yake, hili ni tatizo la kiimani, kutojitambua na kujidharau; ni lazima utoke kwenye eneo hili la kukosa kutokujiamini na uanze kuona kuwa unaweza.

Maono makubwa, uleta taabu kubwa, (The greater the revelation, the greater tribulation)

Wakati Fulani nikiwa na rafiki yangu akanena na kunambia “the greater revelation, the greater tribulation,” akimaanisha kuwa ‘maono makubwa uambatana na taabu kubwa). Ukifuatilia kwenye biblia utaona kuwa watu wote waliobeba maono makubwa ndio watu waliopata taabu kubwa hata utimilifu wa maono yao. Usikate tamaa unapoona majaribu yamekuwa ni makubwa sana kwa upande wako, kaa utulie huku ukitafakari kuwa ni uzito wa maono uliyonayo ndiyo sababu kuu ya kuteseka kwako.

Mfano ni Mtume Yohana aliyepata maono ya kitabu cha ufunuo akiwa katikati ya mateso makubwa na kuwekwa katika kisiwa cha Patmo na Mtume Paulo ambaye alipata mateso makubwa kulingana na ukubwa wa maono aliyokuwa amebeba. Kwani wao waweze wana nini na sisi tushindwe tuna nini?

Katika jamii ya waswahili huu ni msemo ambao umekuwa ukitumika sana na ni miongoni mwa misemo ambayo imejipatia umaarufu mkubwa sana. Ni kweli kuwa wapo watu wafanyao mambo makubwa na yakatokea lakini wengine ushindwa kufanya mambo hayo. Wafanikiwao nao ni watu kama walivyo watu wengine ila utofauti mkubwa ujengwa katika namna ya kufikiria na pia katika namna ya kufanya mambo, watu wote walio juu ukifuatilia historia zao utakuta walikuwa ni watu wa kawaida sana, ila ndani yao waliweka nia na kuamua kupambana kufikia hatua kubwa na za juu, na watu wa namna hii hata walipopata mafanikio madogo hawakubweteka na kujisahau bali uzidi kusonga mbele kupata mafanikio makubwa zaidi. Kama wao wamejaribu wakaweza kwa kutia nia na wewe ukitia nia kwa lolote ufanyalo ni lazima utaweza tu.

Mfumo wa kuzaa kwa viumbe
Nikiwa na rafiki yangu tunazungumza na kutiana moyo kwa habari ya safari tuliyonayo akazungumza neno jema sana kuhusu maono kwa kufananisha na wanyama kuwa wanyama wadogo ubeba mimba na kujifungua kwa muda mfupi; wengine uwa miezi mitatu(3), wengine ni sita(6) na wengine ni tisa(9), tofauti uwa kwa wanyama wakubwa kama tembo wao ubeba mimba yao kwa muda mrefu sana ukilinganisha na wanyama wengine, hii ni kwa sababu ya ile asili yao ya ukubwa ambayo Mungu amewawekea.

Kwa kuutazama mfano huu ndivyo ilivyo kwa sisi wanadamu ya kuwa maono makubwa uweza chukua muda mrefu sana kabla ya kutoka na mtu mwenye maono makubwa uchukua muda mrefu pia kufikia utimilifu wa maono yale. Usiumie kwa nini wengine wanatoka upesi na wewe unapambana ila bado; fahamu aina ya maono uliyobeba pengine ni mazito kama mimba ya tembo na kama ndivyo yaweza kaa muda mrefu hata utimilifu wake ila yatatokea tu kwa kuwa maono ni kama mimba.

Mbali na wanyama pia kwa mimea kuna neno jema la kujifunza kwa kuwa kuna miti ambayo upandwa na kukua kwa muda mfupi na uvunwa ndani ya muda mfupi huo ila kuna mimea ambayo ukaa sana na uchukua miaka mingi sana hata kufikia utimilifu wake, kwa kuchukulia mifano kama mnazi, hata mbuyu ukaa kwa kitambo kirefu sana hata kuja kutoa matunda yake.

Hii inaonyesha kuna utofauti mkubwa sana wa utimilifu wa maono ya mtu mmoja mpaka mwingine, kuna wengine ambao ushuhudia utimilifu wa maono yao kwa haraka sana ukilinganisha na wengine. Muda wa kuchelewa kwa maono ya mtu Ibilisi uhutumia sana kuwa shawishi watu kuona kuwa Mungu hayupo pamoja nao, na uweza sema, mbona hujabarikiwa kama Fulani na Fulani na wewe unamtumikia Mungu kama wao, au ulimaliza nao chuoni au shuleni au ni marafiki wa karibu ukishiriki nao mengi sana ila wao wamekupita kufanikiwa kwa kuwa Mungu hajali mambo yako na uwapenda wenzako kuliko wewe; wewe usikatishwe tamaa na sauti ya kinyonge namna hiyo songa mbele maana utimilifu wako unakuja na ufanikiwaji wa mtu mmoja na mwingine uwa tofauti na kwa nyakati tofauti tofauti.

Mtu mwenye maono hawezi kutulia hata atimize maono aliyonayo na hata akishindwa mara moja uinuka na kujitia nguvu na kutokata tamaa na ni maono ambayo umsaidia mtu kuishi kwa kuukomboa wakati, kuweka vipaumbele vya maisha ambavyo vitampelekea kufikia utimilifu wa maono nhayo, kuchagua watu sahihi wa kuambatana nao ambao watamsaidia kufikia hatima ya maisha yake.

Itaendelea sehemu ya pili

–Kelvin Kitaso