Kuonyeshwa Mbinguni

heaven.jpg

Hebu Tujadili jambo hili.

Yawezekana umeshasikia ushuhuda wa mtu ambaye alisimulia jinsi ALIVYOPELEKWA MBINGUNI kisha akarudi tena hapa Duniani. Au pengine ni mmoja wao wa watu waliopata ujuzi wa namna hiyo.

Jambo linalosababisha mjadala huu ni kwamba katika Shuhuda hizi kila anayesimulia husimulia mambo tofauti na mwingine! Yaani mmoja akisimulia jinsi alivyoingia na Mambo aliyoyaona huko Mbinguni huwa TOFAUTI na asimuliavyo mwingine.

Mfano:  Mmoja anaweza kusema aliowaona kule Sura zao zinafanana, mwingine akasema sura hazifanani. Mmoja anaweza kusema walifika mahali wakala vitu fulani, Mwingine akasema kule hakuna wala kunywa; na mambo mengine mfano wa hayo!!

Mambo ya kujadili ni pamoja na yafuatayo:

Je, Suala hili la watu kuchukuliwa katika Roho kisha akapelekwa Mbinguni lipo kweli? Na usahihi wake ni upi? Twaweza kulipata katika Biblia?

Kama kweli Mbingu ni moja ni kwa nini kila anayeshuhudia kwamba alifikishwa Mbinguni masimulizi yake hutofautiana na mwingine, ambaye naye husimulia habari za huko huko Mbinguni?

Je, Inawezekana mtu kwenda akaonana na Mungu kisha akarudi tena hapa Duniani kuishi?

Kuna watu wamekuwa wakizinduka akielezea ushuhuda wake anasema Amepewa ujumbe aje awaambie watu, mfano, juu ya kutubu na kuacha dhambi au ujumbe mwingine. Je, Hii haipingani na maneno ambayo aliambiwa Tajiri kwamba Watu yawapasa kusikiliza maneno ya watumishi wa Mungu walioko Duniani, maana hata akitumwa mtu kutoka kwa wafu haiwezi kusaidia kitu? (Kisa cha Tajiri na Lazaro masikini)

Karibu katika mjadala kuhusiana na hayo, pamoja na mengine yatakayojitokeza!

 

Kuenenda Kwa Imani (2Kor. 5:7)

 

images-3.jpeg

Kadri siku zinavyokwenda ndivyo mambo MAPYA yanaibuliwa ili kusindikiza imani!

Katika suala la maombezi, hasa nchini Tanzania, ilikuwa mtu anaombewa tuu kwa kuwekewa mikono na kwa IMANI anapokea uponyaji na anaondoka amepona.

Mambo yaliendelea hadi ikafikia mtu anapewa kitambaa, mafuta, bangiri au kitu chochote kinachobebeka kwa urahisi, kwamba UPONYAJI WAKE UKO NDANI YA HICHO KITU. Anapewa na kuelekezwa namna ya kukitumia!

Mambo yameendelea na sasa, kwa mfano, Watu inabidi Wapite, wakanyage mafuta au wapite kwenye beseni la maji, kwamba kwa kufanya hivyo watapokea UPONYAJI au Majibu ya mahitaji yao. Na mengine mengi!

Jee, Katika Hali ya namna hii bado kweli IMANI IPO au sasa TUNAENENDEA KWA KUONA?

Ni wapi ambako Ukristo Unaelekea?

Haya mambo yanayofanyika wakati wa maombi, mfano wa hayo yaliyotajwa hapo juu, LENGO LAKE NI ZURI au BAYA?

 

UMOJA

ünity

Magreth na Joseph wako kwenye mazungumzo:

MAGRETH: Kati ya mambo yanayonikera ni kutokuwepo umoja baina ya madhehebu ya watu waliookoka.

JOSEPH: Kwa nini unasema hivyo?

MAGRETH: Wewe huoni kila kanisa linafanya mambo kivyake. Angalia mikutano ya injili, kila dhehebu linaandaa kivyake. Hata ushirikiano baina ya wachungaji wa makanisa hayo hauko kwa kiwango cha kuridhisha. We hali hiyo unaiona iko sawa?

JOSEPH: Mhh, kama wote wanahubiri injili ya Yesu Kristo mie sioni kama kuna tatizo.

MAGRETH: Tatizo lipo bwana! Yesu alituombea umoja. Madhehebu yote hayo yalipaswa yawe na umoja wenye nguvu, yawe na sauti moja, sio kila watu na lwake! Nafikiri ipo haja ya kufanya maombi ya mzigo tuwe na umoja katika makanisa yetu.

Ni kweli Bwana Yesu Kristo kabla hajaenda kutolewa dhabihu pale msalabani, aliwaombea wanafunzi wake umoja. Hebu tusome lile andiko maarufu kuhusu hii mada ya umoja:

“Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, kwa jina lako ulilonipa uwalinde hawa, ili wawe na umoja kama sisi tulivyo.” (Yohana 17:11, SUV)

Je umoja aliokuwa akiuzungumzia Bwana Yesu ni umoja wa jinsi gani?

Hebu tusome tena pale katika muktadha (context) wake:

“Maneno hayo aliyasema Yesu; akainua macho yake kuelekea mbinguni, akasema, Baba, saa imekwisha kufika. Mtukuze Mwanao, ili Mwana wako naye akutukuze wewe; kama vile ulivyompa mamlaka juu ya wote wenye mwili, ili kwamba wote uliompa awape uzima wa milele. Na uzima wa milele ndio huu, WAKUJUE WEWE, MUNGU PEKEE WA KWELI, NA YESU KRISTO ULIYEMTUMA. Mimi nimekutukuza duniani, hali nimeimaliza kazi ile uliyonipa niifanye. Na sasa, Baba, unitukuze mimi pamoja nawe, kwa utukufu ule niliokuwa nao pamoja nawe kabla ya ulimwengu kuwako. Jina lako nimewadhihirishia WATU WALE ULIONIPA KATIKA ULIMWENGU; walikuwa wako, ukanipa mimi, na NENO LAKO WAMELISHIKA. Sasa wamejua ya kuwa yote uliyonipa yatoka kwako. Kwa kuwa MANENO ULIYONIPA NIMEWAPA WAO; NAO WAKAYAPOKEA, wakajua hakika ya kuwa nalitoka kwako, WAKASADIKI YA KWAMBA WEWE NDIYE ULIYENITUMA. MIMI NAWAOMBEA hao; siuombei ulimwengu; bali HAO ULIONIPA, kwa kuwa hao ni wako; na wote walio wangu ni wako, na walio wako ni wangu; NAMI NIMETUKUZWA NDANI YAKO. Wala mimi simo tena ulimwenguni, lakini hawa wamo ulimwenguni, nami naja kwako. Baba mtakatifu, KWA JINA LAKO ULILONIPA UWALINDE HAWA, ILI WAWE NA UMOJA KAMA SISI TULIVYO. NILIPOKUWAPO PAMOJA NAO, mimi NALIWALINDA KWA JINA LAKO ULILONIPA, nikawatunza; WALA HAPANA MMOJA WAO ALIYEPOTEA, ILA YULE MWANA WA UPOTEVU, ili andiko litimie. Na sasa naja kwako; na maneno haya nayasema ulimwenguni, ili wawe na furaha yangu imetimizwa ndani yao. Mimi nimewapa neno lako; na ulimwengu umewachukia; kwa kuwa wao si wa ulimwengu, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Mimi siombi kwamba uwatoe katika ulimwengu; bali UWALINDE NA YULE MWOVU. WAO SI WA ULIMWENGU, kama mimi nisivyo wa ulimwengu. Uwatakase kwa ile kweli; neno lako ndiyo kweli. Kama vile ulivyonituma mimi ulimwenguni, nami vivyo hivyo naliwatuma hao ulimwenguni. Na kwa ajili yao najiweka wakfu mwenyewe, ili na hao watakaswe katika kweli. Wala SI HAO TU NINAOWAOMBEA; LAKINI NA WALE WATAKAONIAMINI KWA SABABU YA NENO LAO. WOTE WAWE NA UMOJA; KAMA WEWE, BABA, ULIVYO NDANI YANGU, NAMI NDANI YAKO; HAO NAO WAWE NDANI YETU; ILI ULIMWENGU UPATE KUSADIKI YA KWAMBA WEWE NDIWE ULIYENITUPA.

Nami UTUKUFU ule ULIONIPA NIMEWAPA wao; ILI WAWE NA UMOJA KAMA SISI TULIVYO UMOJA. MIMI NDANI YAO, NAWE NDANI YANGU, ILI WAWE WAMEKAMILIKA KATIKA UMOJA; ILI ULIMWENGU UJUE YA KUWA NDIWE ULIYENITUMA, ukawapenda wao kama ulivyonipenda mimi.” (Yohana 17:1-23, SUV, msisitizo wangu)

Kuna mambo kadhaa tunayaona katika kifungu hicho cha Maandiko Matakatifu:

1. Bwana Yesu Kristo alikuwa anawaombea wale waliokuwa wamemwamini wakati ule na wale ambao wangekuja kuamini baadaye (hivyo mimi na wewe ambaye umeamini tumejumuishwa humo). Hao ndio watu ambao Mungu amempa (waweza kusoma pia Yohana 6:39).

2. Sifa kuu ya watu hao ambao Yesu alikuwa anawaombea ni kwamba wamelipokea na kulishika Neno lake na Yeye ametukuzwa ndani yao; hakuwa akimwombea kila mtu ulimwenguni.

3. Alikuwa anawaombea Mungu awatakase kwa kweli ya Neno lake.

4. Alikuwa anawaombea Mungu awalinde dhidi ya yule mwovu muda ambao watu wa Mungu wakiwa bado wapo ulimwenguni, asipotee hata mmoja, ILI WAWE NA UMOJA.

5. Waliomwamini Kristo Yesu wakiwa na umoja, utapelekea ulimwengu kumwamini.

Mtume Paulo naye aliandika yafuatayo katika waraka wake kwa jamii ya waamini waliokuwa wakiishi kule Efeso:

“Kwa hiyo nawasihi, mimi niliye mfungwa katika Bwana, MWENENDE KAMA INAVYOUSTAHILI wito wenu mlioitiwa; kwa unyenyekevu wote na upole, kwa uvumilivu, mkichukuliana katika upendo; na KUJITAHIDI KUUHIFADHI UMOJA WA ROHO katika KIFUNGO CHA AMANI. Mwili MMOJA, na Roho MMOJA, kama na mlivyoitwa katika tumaini MOJA la wito wenu. Bwana MMOJA, imani MOJA, ubatizo MMOJA. Mungu MMOJA, naye ni Baba wa wote, aliye juu ya yote na katika yote na ndani ya yote.” (Waefeso 4:1-6, SUV, msisitizo wangu)

Na kisha akaendelea:

“Naye alitoa wengine kuwa mitume, na wengine kuwa manabii; na wengine kuwa wainjilisti na wengine kuwa wachungaji na waalimu; kwa kusudi la kuwakamilisha watakatifu, hata kazi ya huduma itendeke, hata mwili wa Kristo ujengwe; hata na sisi sote tutakapoufikia UMOJA WA IMANI na kumfahamu sana Mwana wa Mungu, hata kuwa mtu mkamilifu, hata kufika kwenye cheo cha kimo cha utimilifu wa Kristo; ili tusiwe tena watoto wachanga, tukitupwa huku na huku, na kuchukuliwa na kila upepo wa elimu, kwa hila ya watu, kwa ujanja, tukizifuata njia za udanganyifu. Lakini TUISHIKE KWELI katika upendo na kukua hata tumfikie yeye katika yote, yeye aliye kichwa, Kristo.” (Waefeso 4:11-15, SUV, msisitizo wangu)

Hebu tusome na Maandiko mengine:

“Mungu ni mwaminifu ambaye mliitwa na yeye mwingie katika ushirika wa Mwanawe, Yesu Kristo Bwana wetu. Basi ndugu, nawasihi, kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo, kwamba nyote MNENE MAMOJA; wala pasiwe kwenu faraka, bali mhitimu katika NIA MOJA na SHAURI MOJA. Kwa maana, ndugu zangu, nimearifiwa habari zenu na wale walio wa nyumbani mwa Kloe, ya kwamba iko fitina kwenu. Basi, maana yangu ni hii, ya kwamba kila mtu wa kwenu kusema, Mimi ni wa Paulo, na, Mimi ni wa Apolo, na, Mimi ni wa Kefa, na, Mimi ni wa Kristo. Je! Kristo amegawanyika? Je! Paulo alisulibiwa kwa ajili yenu? Au je! Mlibatizwa kwa jina la Paulo?” (1 Wakorintho 1:9-13, SUV, msisitizo wangu)

“Basi ikiwako faraja yo yote katika Kristo, yakiwako matulizo yo yote ya mapenzi, ukiwako ushirika wo wote wa Roho, ikiwako huruma yo yote na rehema, ijalizeni furaha yangu, ili mwe na NIA MOJA, wenye mapenzi mamoja, wenye roho moja, mkinia mamoja. MSITENDE NENO LO LOTE KWA KUSHINDANA wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake. Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.” (Wafilipi 2:1-4, SUV, msisitizo wangu)

Kwa kuzingatia Maandiko hayo hapo juu pamoja na mengine, naomba tujadili mambo yafuatayo kuhusiana na swala hili la UMOJA miongoni mwa jamii ya waaminio:

1. Je umoja ambao Bwana Yesu Kristo aliwaombea wanafunzi wake ni umoja miongoni mwa makanisa au madhehebu ya Kikristo au ni umoja wa jinsi gani hasa?

2. Je umoja huo unafikiwa vipi?

3. Ni mambo gani yakiwepo miongoni mwa jamii ya waaminio inadhihirisha kuwa kuna umoja miongoni mwao?

4. Je umoja huo upo au haupo hivi leo katika Kanisa la Yesu Kristo?

Karibuni tujadili.

Joel Msella

MILIMA, MITO, BAHARI na Uhusiano wa Kiroho

Lakes and Rivers Desktop Wallpapers001

Je, Kuna uhusiano gani wa KIROHO na Milima, Mito na Bahari?

Amri Kumi zilitolewa Mlimani – Kutoka 31:18.

Yesu alisulubiwa Golgotha, Mlimani – Marko 15:22

Wale majini waliowaingia Nguruwe waliwapeleka Baharini – Mathayo 8:32

Kuna maneno mengi mitaani na shuhuda nyingi makanisani zinazohusisha Milima, Mito na Bahari na mambo ya Kiroho, ya kiMungu au ya Shetani.

Je, maeneo hayo yana uhusiano gani na mambo ya rohoni?

UTABIRI kuhusu Viongozi wa Kisiasa

bible-sunset-2

Huku vuguvugu la Uchaguzi mkuu likiwa linaendelea, kuna jambo ambalo linafaa tukalitafakari na Kulijadili:

Wakati wa Utangazaji nia wa Wagombea nafasi ya Urais walisikika baadhi ya viongozi wa kiroho wakitaja majina, ya mtu ambaye kila mmoja aliona anafaa. Wengine walikwenda mbali hata kusema kuwa “Kaonyeshwa na Mungu” kwamba mtu fulani ndiye “Chaguo la Mungu”

Sambamba na viongozi kuyasema hayo, baadhi ya Waimbaji wa nyimbo za Injili nao Walitunga nyimbo za kusifia au Kutangaza kwamba huyo wanayeimba habari zake ” Ni chaguo la Mungu” na ndiye Rais ajaye!

Baada ya Chama Cha Mapinduzi kukamilisha taratibu za kumchagua atakayegombea nafasi hiyo ya Urais, Wote waliokuwa wakitajwa na kusifiwa na ama Viongozi wa Kikristo au Waimbaji wa Injili hawajachaguliwa!

Je, Nini maana ya Utabiri huo kutoka Viongozi na Wanamuziki wa Injili?

Je, Ni kwa kiasi gani NENO likitamkwa na mtu anayesema “Kaonyeshwa na Mungu” litapewa Uzito ikiwa ni kweli itakiwa kaonyeshwa na Mungu?

Je, Nini nafasi ya Mkristo katika kufanikisha upatikanaji wa Vingozi wa nchi wanaofaa?

Ubatizo kwa watoto wadogo ~ inaendelea

Mbarikiwe sana wana wa Mungu kwa michango yenu ya mawazo kuhusu mada ya. Mchango wangu kuhusu mada hii ni wa jumla kwa kusema kuwa, Ni vizuri kutenganisha namna Mungu alivyojifunua kwa watu katika nyakati tofauti ili kujua jinsi watu wa nyakati hizo walivyo mfuata Mungu. 1. wakati wa agano la kale 2. wakati wa agano jipya Grace period). 3.wakati wa kanisa la mwanzo (matendo ya mitume).4. wakati wa utawala wa kanisa la Roma. 5. wakati wa uamsho . 6. wakati wa uamsho wa kipentekoste kule azusa street USA. na 7. wakati wa sasa( naita wakati wakanisa huria). Ukidadisi vizuri kuhusu namna ubatizo ulivyofanyika katika nyakati utagundua wapi ubatizo ulipoteza mwelekeo na hasa jinsi Mungu alivyokusudia ubatizo uwe.

Nimeshitushwa sana na maelezo ya mch Malisa kwa kuharalisha ubatizo wa watoto wachanga kuwa ni sahihi. Inawezekana mchungaji ni miongoni mwa wachungaji ambao hawajasoma vyuo vya kichungaji na amejikuta ameitwa kuwa mchungaji bila kupata vyuo kama ilivyo kwa baadhi ya watumishi wa Mungu. Na ninahisi mch Malisa kwa makusudi kabisa umeweka fundisho hilo ili kuwavutia watu katika kujiunga na kanisa lako na iko siku utaruhusu na jambo lingine kwa kusudi hilo hilo.

Nawabariki sana wachangiaji wengine endeleeni kutafuta elimu ya Mungu kwa manufaa a kujenga wokovu wetu ili tuimalike na kufikia kimo cha utimilifu wa kristo jiepusheni na fundisho hili la mch Malisa kwa habari ya ubatizo wa watoto wachanga hilo sio sahihi nawaambia bila kusita sita. Amina.

Kennedy Simtowe

kusoma zaidi kuhusu ubatizo https://strictlygospel.wordpress.com/2008/07/16/swali-8/