Lijue Neno kwa ajili yako Mwenyewe!

biblia

Jitahidi (Jifunze) ili kujionesha kuwa umekubaliwa na Mungu,  mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukitumia kwa usahihi Neno la kweli (2 Timotheo 2:15),

Kwa wewe kuishi maisha ya furaha, na kuwa udhihirisho kamilifu wa mapenzi, haki, na utukufu wa Mungu, unatakiwa kulijua Neno wewe mwenyewe na kuishi kwa Neno. Wale wasiolijua Neno la Mungu ni kwa tabu sana wanaweza timiza ile shauku na mipango ya Mungu katika maisha yao. Neno la Mungu lilikufanya wewe (1 Petro 1:23), hivyo usipoishi kwa Neno, hautokuwa yule “wewe” Mungu aliyemtazamia, wala hautotimiza hatma Yake Kwako. Hii ndio sababu tunafundisha Neno na kuwatia moyo watoto wa Mungu kuwa wanafunzi wa Neno. Ni lazima ulijue Neno kwa ajili yako mwenyewe (lijue wewe mwenyewe).

 Usiishi katika viwango vya kudhania.  Usiache watu wakuhamasishe (wakushawishi) na mitazamo yao ya “kidini” kuhusu Mungu. Usikubali kwamba kitu fulani kinatoka kwa Mungu kwa sababu tu kinasikika kama chema, kizuri ama cha kidini.

Yesu Alisema katika Yohana 5:39, “Chunguzeni maandiko…” ; Paulo alisema katika 2 Timotheo 2:15, “Jitahidi (Jifunze) ili kujionesha kuwa umekubaliwa na Mungu, mtenda kazi asiye na sababu ya kutahayari, ukilitumia kwa usahihi Neno la kweli.” Neno la Mungu ni ufahamu wa Mungu uliodhihirishwa; ni mapenzi Yake katika maandishi na yaliyoelezewa kwa ajili yetu. Ni faida ya ajabu namna gani hii, kwamba unaweza jifunza Neno wewe mwenyewe, ukalielewa, na kuliishi! Ni baraka kuu.

Kipimo cha maisha yako ya kitukufu na ushindi kitakua ni, kiwango gani cha maanifa ya Mungu unacho, na ni kiasi gani unakitendea kazi. Si umekuwa Mkristo muda mrefu kiasi gani; bali ni unajua Neno vizuri kiasi gani na kulitumia. Shukurani kwa Mungu tunayo faida isiyolinganishwa ya uwepo wa Roho Mtakatifu ukaaoa ndani yetu, Ambaye Hutupatia uelewa wa Neno! Yeye Ndiye mtunzi wa maandiko; hivyo unapojifunza, unaweza kumtegemea Yeye ili kukuongoza, na kukupatia kuona katika mafumbo na siri za ki-Ungu.

 Lipatie Neno umakini na muda wako. Jifunze na uliwekee moyo wako. Kama unataka kuishi maisha yaliyopita ukawaida, ni kwa Neno, kupitia nguvu ya Roho Mtakatifu.

Imetafsiriwa kutoka kwa Mchungaji Chris Oyakhilahome

KUTIMILIZA TORATI

 

law2

 

UTANGULIZI

Neema ya Bwana wetu Yesu Kristo iwe pamoja nawe mdau wa SG. Tunaishi katika kipindi ambacho kuna namna nyingi za injili, na usipokuwa makini unaweza kufikiri kuwa uko katika injili ya Yesu Kristo kumbe mtu ulishahama – kwa wale wanamuziki, wanasema umetoka “nje ya key”! Hata enzi za Kanisa la kwanza, jambo kama hili lilipata kutokea kule Galatia (soma Wagalatia 1:6-9).

Ukisoma Mathayo 5:20 unakutana na maneno haya toka katika kinywa cha Bwana wetu Yesu Kristo:

“Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu isipozidi hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni.”

Andiko hili limekuwa likitumiwa na wengi kusisitiza kwamba, ili kuingia ufalme wa mbinguni hatuna budi kufanya matendo mema au mazuri na mengi zaidi ya vile ambavyo mafarisayo walikuwa wanafanya. Je mafarisayo walikuwa wanafanya nini?

“Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa mimi si kama watu wengine, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza ushuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote.” (Luka 18:11-12)

Hivyo, hoja hiyo husisitiza, tunapaswa kufunga zaidi ya mafarisayo na kutoa zaka na kufanya mambo mengine zaidi yao vinginevyo haki yetu haitazidi ile haki ya mafarisayo na hivyo hatutaweza kuingia ufalme wa mbinguni.

Je, ni kweli Bwana Yesu alimaanisha hivyo? Twende pamoja. Kanuni yetu, kama kawaida, ni kujenga hoja na kujadili kwa kuzingatia kile ambacho Maandiko Matakatifu yanasema.

BWANA YESU NA TORATI

Ili kuelewa ujumbe wa Bwana Yesu alipowaambia watu waliokuwa wakimsikiliza kuwa haki yao isipozidi ya mafarisayo hawataingia katika ufalme wa mbinguni, inabidi kusoma mstari huo katika muktadha wake.

“Msidhani ya kuwa nalikuja kuitangua torati au manabii; la, sikuja kutangua, bali KUTIMILIZA. Kwa maana, amin, nawaambia, Mpaka mbingu na nchi zitakapoondoka,yodi moja wala nukta moja ya torati haitaoondoka ,hata YOTE YATIMIE. Basi mtu ye yote atakayevunja amri moja katika hizi zilizo ndogo, na kuwafundisha watu hivyo, ataitwa mdogo kabisa katika ufalme wa mbinguni; bali mtu atakayezitenda na kuzifundisha, huyo ataitwa mkubwa katika ufalme wa mbinguni. Maana nawaambia ya kwamba, Haki yenu ISIPOZIDI hiyo haki ya waandishi na Mafarisayo, hamtaingia kamwe katika ufalme wa mbinguni. Mmesikia watu wa kale walivyoambiwa, USIUE, na mtu akiua, itampasa hukumu. Bali mimi nawaambieni, Kila AMWONEAYE ndugu yake HASIRA itampasa hukumu; na mtu AKIMFYOLEA ndugu yake, itampasa baraza; na mtu AKIMWAPIZA, itampasa jehanum ya moto.” (Mathayo 5:17-22, SUV, msisitizo wangu)

Yesu alikuwa akiongea na makutano (Mathayo 5:1), katika kipindi ambacho torati ilikuwa imeshika hatamu maana bado kilikuwa ni kipindi cha agano la kale. [Kuzungumzia kwa undani maswala ya agano la kale na lile jipya haiko katika lengo (scope) la mjadala huu, ila kwa ufupi sana niseme tu kuwa agano la kale Mungu aliliweka na wana wa Israeli pale alipowatoa kule Misri (soma Waebrania 8:8-9), na katika kipindi hicho wana wa Israeli walipewa torati waishi kwa hiyo. Agano jipya lilikuja kuanza Bwana Yesu alipotolewa dhabihu pale msalabani (soma Waebrania 9:11-15).] Bwana Yesu aliweka bayana kuwa alikuwa amekuja duniani “kutimiliza” torati. Je “kutimiliza” huku kulikuwa ni kufanya nini hasa, na hayo “yote” ambayo Yesu alisema kwamba yalikuwa hayana budi “kutimia” yalikuwa ni yapi?

Yesu alikuja KUTIMILIZA yale YOTE yaliyokuwa yamenenwa na torati na manabii. Yesu alilifafanua jambo hilo kwa wanafunzi wake baada ya kufufuka maana katika kitambo chote alichokuwa nao hawakumwelewa.

“Kisha akawaambia, Hayo ndiyo maneno yangu NILIYOWAAMBIA nilipokuwa nikali pamoja nanyi, ya kwamba NI LAZIMA YATIMIZWE YOTE niliyoandikiwa katika TORATI YA MUSA, na katika MANABII na ZABURI. Ndipo AKAWAFUNULIA AKILI ZAO wapate kuelewa na maandiko. Akawaambia, NDIVYO ILIVYOANDIKWA, KWAMBA KRISTO ATATESWA NA KUFUFUKA SIKU YA TATU; na kwamba MATAIFA YOTE WATAHUBIRIWA KWA JINA LAKE HABARI YA TOBA NA ONDOLEO LA DHAMBI, kuanza tangu Yerusalemu.” (Luka 24:44-47, SUV, msisitizo wangu)

Kwa hivyo, Yesu aliposema kuwa hakuja kuitangua torati na manabii bali kuitimiliza, alikuwa anamaanisha kuwa alikuwa amekuja duniani ili YALE YOTE YALIYOTABIRIWA katika torati na manabii kuhusu kuteswa, kufa na kufufuka kwake, na hatimaye injili ihubiriwe duniani kote YATIMIE. Ni vema tukumbuke kuwa torati ilikuwa ni kiongozi wa kutuleta kwa Yesu Kristo, maana tunasoma, “Lakini KABLA ya kuja ile IMANI tulikuwa tumewekwa chini ya sheria, tumefungwa mpaka ije ile imani itakayofunuliwa. Hivyo TORATI IMEKUWA KIONGOZI kutuleta kwa Kristo, ILI TUHESABIWE HAKI KWA IMANI. Lakini, IWAPO IMANI IMEKUJA, HATUPO TENA CHINI YA KIONGOZI.” (Wagalatia 3:23-25, SUV, msisitizo wangu)

HAKI YA MAFARISAYO NA HAKI ANAYOITAKA MUNGU KWETU

Baada ya kuona kile ambacho Bwana Yesu alimaanisha aliposema kuwa hakuja kuitangua torati bali kuitimiliza, tunaweza sasa kuelewa kile alichomaanisha alipozungumzia kuwa haki ya mtu inapaswa kuizidi ile ya mafarisayo ili kuingia katika ufalme wa mbinguni. Neno lililotafsiriwa kama “haki” katika Mathayo 5:20 limetokana na neno la Kiyunani “dikaiosune¯” linalomaanisha “the character or quality of being right or just”, yaani, ile hali au tabia ya kuwa sawa (bila kosa lolote) au mwenye haki.

Tafsiri ya Kiingereza ambayo inafafanua zaidi maana za maneno inasema:

“For I tell you, unless your righteousness (your uprightness and your right standing with God) is more than that of the scribes and Pharisees, you will never enter the kingdom of heaven” (Matthew 5:20, Amplified)

Mafarisayo na waandishi walikuwa wakijihesabia haki (yaani, walijihesabu kuwa wako sawa) mbele za Mungu kwa kujipima ni kwa jinsi gani walikuwa wanafanya yaliyoandikwa katika torati. Ndio maana tunasoma:

“Akawaambia mfano huu watu WALIOJIKINAI YA KUWA WAO NI WENYE HAKI, WAKIWADHARAU WENGINE WOTE. Watu wawili walipanda kwenda hekaluni kusali, mmoja Farisayo, wa pili mtoza ushuru. Yule Farisayo akasimama akiomba hivi moyoni mwake; Ee Mungu, nakushukuru kwa kuwa MIMI SI KAMA WATU WENGINE, wanyang’anyi, wadhalimu, wazinzi, wala kama huyu mtoza shuru. Mimi nafunga mara mbili kwa juma; hutoa zaka katika mapato yangu yote. Lakini yule mtoza ushuru alisimama mbali, wala hakuthubutu hata kuinua macho yake mbinguni, bali alijipiga-piga kifua akisema, Ee Mungu, uniwie radhi mimi mwenye dhambi. Nawaambia, HUYU ALISHUKA KWENDA NYUMBANI KWAKE AMEHESABIWA HAKI KULIKO YULE; kwa maana kila ajikwezaye atadhiliwa, naye ajidhiliye atakwezwa.” (Luka 18:9-14, SUV, msisitizo wangu)

Bwana Yesu katika hotuba yake ya mlimani alifafanua kuwa, katika torati iliandikwa “usiue” (yaani wasifanye tendo ambalo linaonekana kwa macho – kuua – na ambalo lilikuwa limeandikwa katika torati) lakini yeye akawatajia mambo ambayo mtu akiyafanya itampasa adhabu – kumwonea hasira mwenzake, kumfyolea, au kumwapiza. Hayo aliyowatajia hayakuandikwa katika torati yao, lakini yalikuwa ni mwanzo wa hasira ambayo mtu anakuwa nayo kabla ya kufikia hatua ya kumwua mwenzake. Nitatoa mfano mwingine.

“Mmesikia kwamba imenenwa, Usizini; lakini mimi nawaambia, Kila mtu atazamaye mwanamke kwa kumtamani, amekwisha kuzini naye moyoni mwake.” (Mathayo 5:27-28, SUV)

Yesu aliwaambia mafarisayo waliokuwa wakijihesabia haki kwa kuwa hawakuzini kwamba, hata kama hawakuzini lakini kama waliwaangalia wanawake kwa kuwatamani kingono tayari walikuwa wamezini nao. Tamaa ya kutaka kufanya ngono na mwanamke ndiyo hupelekea mtu kutafuta fursa ya kuzini naye (soma pia Yakobo 1:13-15). Mafarisayo walijihesabia haki kwa kuwa hawakufanya lile tendo la ngono, lakini Yesu akawasisitizia kuwa kutamani kufanya ngono na mwanamke – hata bila ya kufanya tendo lenyewe – tayari ilikuwa ni uzinzi.

Kupitia mifano hiyo, Bwana Yesu alikuwa anawaeleza kiwango cha juu cha haki ambacho Mungu alikuwa anakitarajia kwa wanadamu – si tu kufuata vile torati ilivyokuwa ikisema (usiue, usizini, usiibe, nk), bali kwenda kushughulikia kwenye MZIZI wa hayo maovu, yaani kwenye moyo ambako mawazo ya kufanya maovu hayo huanzia. Huko kukishashughulikiwa, mtu hatahitaji tena kuwa na orodha ya mambo ya kutokufanya bali atajikuta anaenenda katika njia iliyo sawa na hafanyi yasiyopasa. Kwa maneno mengine, Yesu alikuwa anawaeleza namna ya haki ambayo ilikuwa ni ya KIWANGO CHA JUU, iliyozidi kwa mbali sana namna ile ya haki ambayo mafarisayo walikuwa wanajihesabia.

Mahali pengine Yesu aliwaambia mafarisayo, ambao walijihesabu kuwa ni wenye haki mbele za Mungu kwa zile jitihada zao za kutii torati (japo walichanganya na mapokeo yao ambayo hayakuwemo katika torati (angalia, kwa mfano, Mathayo 15:6)), maneno haya:

“Akasema, Kimtokacho mtu ndicho kimtiacho unajisi. Kwa maana ndani ya MIOYO ya watu hutoka mawazo mabaya, uasherati, wivi, uuaji, uzinzi, tamaa mbaya, ukorofi, hila, ufisadi, kijicho, matukano, kiburi, upumbavu. Haya yote yaliyo maovu YATOKA NDANI, nayo yamtia mtu unajisi.” (Marko 7:20-23, SUV, msisitizo wangu)

Mafarisayo walijihesabia haki kwa kujitahidi kukwepa kufanya matendo maovu na kufanya matendo mema yanayoonekana (angalia Mathayo 6:1-6), lakini Yesu aliweka bayana kwao kuwa walitakiwa kushughulika na mioyo yao ambako matendo yote huanzia huko. Ndiyo maana aliwaambia:

“Ole wenu waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa MNASAFISHA NJE ya kikombe na chano, na NDANI YAKE vimejaa unyang’anyi na kutokuwa na kiasi. Ewe Farisayo kipofu, safisha kwanza NDANI ya kikombe, ILI NJE YAKE NAYO IPATE KUWA SAFI.” (Mathayo 23:25-26, SUV, msisitizo wangu)

Kama haki ya mtu itaishia katika kutii torati au orodha ya makatazo (prohibitions), kwamba usifanye hiki au kile, itakuwa sawa na ile waliyojihesabia mafarisayo na waandishi. Hiyo haitasaidia kitu.

“Basi ikiwa MLIKUFA PAMOJA NA KRISTO mkayaacha yale mafundisho ya awali ya ulimwengu, KWA NINI KUJITIA CHINI YA AMRI, kama wenye kuishi duniani, Msishike, msionje, msiguse; (mambo hayo yote huharibika wakati wa kutumiwa); hali mkifuata MAAGIZO NA MAFUNDISHO YA WANADAMU? Mambo hayo YANAONEKANA KANA KWAMBA YANA HEKIMA, katika namna ya IBADA MLIYOJITUNGIA WENYEWE, na katika kunyenyekea, na katika kuutawala mwili kwa ukali; lakini HAYAFAI KITU kwa kuzizuia tamaa za mwili.” (Wakolosai 2:20-23, SUV, msisitizo wangu)

Haki yetu inatakiwa izidi hiyo – itokane na kushughulikia kule ndani kabisa, kwenye moyo, ambako maovu huanzia. Na hilo haliwezekani pasipo kumpokea Kristo Yesu na kuzaliwa upya, na kujifunza kuongozwa na Roho Mtakatifu katika kufisha mwili pamoja na tamaa zake.

“Na hao walio wa Kristo Yesu wameusulibisha mwili pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.” (Wagalatia 5:24)

NAFASI YA MATENDO MEMA

Baada ya kusema hayo, hebu tuangalie nafasi ya matendo mema katika maisha ya mtu aliyemwamini Kristo Yesu.

Ni muhimu kutambua kuwa Mungu alituumba ili tutende yaliyo mema kwa wengine:

“Maana tu kazi yake, tuliumbwa katika Kristo Yesu, tutende MATENDO MEMA, ambayo TOKEA AWALI MUNGU ALIYATENGENEZA ILI TUENENDE NAYO.” (Waefeso 2:10, SUV, msisitizo wangu)

Kama wana wa Mungu, tunatarajiwa kufanya yaliyo mema (soma pia Mathayo 5:16, 1 Timotheo 2:8-10, Tito 2:7-14; 3:14), lakini SI MATENDO HAYO yanayotufanya tuhesabiwe haki mbele za Mungu (angalia Warumi 3:23-24, Waefeso 2:8-9, Warumi 11:6, Wagalatia 2:21, ). Tukitarajia au kutafuta kuhesabiwa haki kwa sababu ya matendo yetu mema tunarudi kule kwenye torati na kuachana na neema.

Matendo mema tunayoyatenda ni matunda ya mabadiliko yanayotokana na utendaji au uhai wa ile imani katika Kristo Yesu iliyo ndani yetu. Ndiyo maana Yakobo aliandika:

“Ndugu zangu, yafaa nini, mtu akisema ya kwamba anayo imani, lakini hana matendo? Je! Ile imani yaweza kumwokoa? Ikiwa ndugu mwanamume au ndugu mwanamke yu uchi na kupungukiwa na riziki, na mtu wa kwenu akawaambia, Enendeni zenu kwa amani, mkaote moto na kushiba, lakini asiwape mahitaji ya mwili, yafaa nini? Vivyo hivyo na imani, ISIPOKUWA INA MATENDO, IMEKUFA NAFSINI MWAKE. Lakini mtu atasema, Wewe unayo imani, nami ninayo matendo. Nionyeshe imani yako pasipo matendo, nami NITAKUONYESHA IMANI YANGU KWA NJIA YA MATENDO YANGU.” (Yakobo 2:14-18, SUV, msisitizo wangu)

Uhai wa imani yetu katika Kristo Yesu unaonekana kwa nje kupitia matendo yetu. Kama hakuna mabadiliko, Maandiko yako wazi kabisa kuwa imani hiyo imekufa.

KWA KUMALIZIA

Nisisitize kuwa, Bwana Yesu alikuja duniani akafa msalabani na kupata mateso mengi, damu yake ikamwagika, ili ashughulikie mzizi wa dhambi unaotufanya tuwaze na hatimaye kutenda maovu. Kama tutang’ang’ania kutaka kuishi kwa kufuata mlolongo wa sheria na kujihesabia haki kwa umahiri wetu wa kuzifuata, tutakuwa tumetoka nje ya mstari na kuifanya kazi yote ya Mwokozi kuwa haina maana. Tunapomwamini, imani ile inapotenda kazi ndani yetu inapelekea sisi kutenda matendo mema yanayoonekana kwa nje na kudhihirisha badiliko lililotokea katika maisha yetu.

Mungu wa mbinguni akubariki.

Joel Msella

Mpende adui yako!

mlk

‘‘Mmesikia kwamba ilinenwa, ‘Mpende jirani yako na umchukie adui yako.’ Lakini mimi ninawaambia, Wapendeni adui zenu na waombeeni wanaowatesa ninyi, ili mpate kuwa watoto wa Baba yenu aliye mbinguni. Kwa maana Yeye huwaangazia jua lake watu waovu na watu wema, naye huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki. Kama mkiwapenda wale wanaowapenda tu, mtapata thawabu gani? Je, hata watoza ushuru hawafanyi hivyo?

Mathayo 5:43-46

Hekima hujenga, upumbavu hubomoa huku ikiona ipo sawa.!!

pst

MIT. 14:1 SUV

Kila mwanamke aliye na hekima hujenga nyumba yake; Bali aliye mpumbavu huibomoa kwa mikono yake mwenyewe.

Hamna wakati ambapo upumbavu unakuwa kileleni kama wakati mtu akiwa na hasira.

MHU. 7:9 SUV

Usifanye haraka kukasirika rohoni mwako, Maana hasira hukaa kifuani mwa wapumbavu.

Unapokuwa na hasira unakuwa kwa kipindi hicho umejawa na upumbavu kifuani. Unaweza ukasukuma maneno toka kifuani yatakuwa maneno ya upumbavu tu. Ni vema ungenyamaza kimya.

MIT. 17:28 SUV

Hata mpumbavu akinyamaza, huhesabiwa hekima; Akifumba midomo yake, huhesabiwa ufahamu.

Katika hasira yako ukiamua kufanya jambo japo litakuwa la kipumbavu lakini wewe kwa sababu ya hasira yako utakuwa unaliona sawa tu.

MIT. 12:15 SUV

Njia ya mpumbavu imenyoka machoni pake mwenyewe; Bali yeye aliye na hekima husikiliza shauri.

Hasira na hasara hazijapishana sana. Tofauti yake ni herufi moja tu.

–Pastor Carlos Kirimbai