Kufurahia thawabu ya kashfa ya uongo….

_32

Amini usiamini! Kumbe kuna thawabu kwa ajili ya kutungiwa kashfa za uongo! Haya si maneno yangu binafsi. Yesu Kristo mwenyewe ndiye aliyesema haya kama ilivyoandikwa hapa chini: “Heri ninyi watakapowashutumu na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.” (MT.5:11-12) Maneno mazito ni haya ya “watakapowashutumu…….na kuwaudhi……..na kuwanenea……. Kila NENO BAYA kwa UONGO….”

Kuna kushutumiwa na kulaumiwa na kunenewa vibaya lakini kwa mambo ya kweli, kwa makosa ya kweli. Hii ni kawaida kila mkosaji kulaumiwa kwa makosa yake. Lakini si rahisi, na si kawaida, mtu asiye na hatia kabisa, kushutumiwa, kulaumiwa na kunenwa vibaya kwa tuhuma za kashfa za uongo. Tena tuhuma ambazo wahusika wanaweka mikakati ya makusudi huku wamepania kwa makusudi kumdhalilisha, kumvunjia heshima yake, huyo asiye na hatia “maskini wa Mungu” ili tu aabike, aadhirike, aharibikiwe, na ikiwezeka afilie mbali!!! Kisa ni nini? Ati kwa kuwa tu yeye ni “mchaji Mungu”! Ati anawakera mno kwa kuwa ni “mshika maadili ya kibiblia”! Ati kwa kuwa kajitoa mhanga kutangaza habari za imani yake aliyo nayo kwa Mungu wake!!! Tena wengine wamemkasirikia kwa madai ati “anajifanya mtakatifu sana, hataki kushiriki maovu; hatoi wala kupokea rushwa; kajitenga na ufisadi kwa sababu ya imani yake kwa Yesu!” Basi, kwa ajili hiyo tu, zinasukwa njama na kutengenezwa tuhuma za kashfa za uongo dhidi yake; ili tu kumkomoa na kumkomesha asiendelee na msimamo wake wa kimaadili. Haya ndiyo Yesu alimaanisha aliposema, “….na kuwanenea kila neno baya kwa uongo KWA AJILI YANGU..”

Sasa uzito wa ujumbe huu sio kusingiziwa na kuzushiwa kwa ajili ya imani. Uzito wa ujumbe huu ni jinsi “mtendewa, msingiziwa, mzushiwa,” anavyoagizwa jinsi ya kuchukuliana na hali ya namna hii. Anaagizwa na Yesu kwamba AFURAHI NA KUSHANGILIA AKITUNGIWA KASHFA ZA UONGO KWA AJILI YA KRISTO! Hapooooo!!! Kufurahi na kushangilia!!!! “Ee Bwana Yesu nisaidie miye mtu dhaifu sanaa naomba unirehemu tu katika hili! Ninatamani kupata thawabu zako, ila kwa thawabu hii ninahitaji neema yako. Maana udhaifu wangu huu unaweza kunikosesha hata thawabu nyingine nisipokuwa makini sana katika eneo hili..AMINA”

Duh! Samahani kwa kusali hadharani lakini najua ujumbe huu una walengwa wake. Napenda kuhitimisha kwa kusema ya kwamba, tuache unafiki, ukweli inauma sanaaaa kunenwa vibaya kwa uongo. Lakini ni kwa sababu ya maumivu ya jinsi hii ndiyo maana Yesu naye kaweka njia ya kupona maumivu hayo. Anatutaka tuwe na mtazamo tofauti pale tunapopatwa na majaribu ya jinsi hii. Kwanza kila unaposingiziwa kwa uongo, na wewe unajua kuwa huo ni uzushi, kumbuka shahidi wako wa kwanza ni Mungu. Wakati watu wengine wasiojua ukweli wanatapokuwa wanakulaumu na kukutukana kwa kashfa ambazo chanzo chake sio wewe; kumbuka, laana zao zitageuka kuwa baraka kwako mbele za Mungu. Lakini ili baraka hizo zidumu lazima kwanza uishinde hisia ya uchungu na maumivu ya nafsi, kwa kuwasamehe bure wale wanaokuudhi. Unaishindaje hisia hiyo hasi ya uchungu? Kwa kuruhusu hisia chanya ya furaha, na hata kushangilia kwa ajili ya THAWABU KUBWA INAYOKUSUBIRI MBINGUNI.

Msomaji wangu, usikubali kumaliza mwaka huu ukiwa na uchungu moyoni kwa sababu ya kashfa za uongo. Sisi sote tutakutana siku moja mbele za Kiti cha hukumu cha Kristo na ukweli utajulikana wakati huo. Hivi sasa furahi na kumshukuru Mungu kwa kila jambo kwa kuwa hayo ndiye mapenzi yake pale tunapoteswa isivyo haki….. “Maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivya haki.” (1 Pet.2:19) Nakutakia baraka za mwaka mpya. Ubarikiwe sana

– Pastor Imori

Usikate Tamaa!

wp-1468997924869.jpg

ELIYA ALIKATAA KUKATISHWA TAMAA

OMBI: Mwenyezi Mungu na Baba yetu mwema wa mbinguni, tunakushukuru sana kwa ajili ya ukuu na upendo Wako kwetu! Asante kwa kutupenda na kutusamehe dhambi zetu. Tunaalika uwepo Wako katika tafakari hii. Tusaidie kulifahamu Neno Lako, tubadilishe ili tufanane Nawe, na pia tupatie uwezo wa kuyatenda mapenzi Yako. Tunaomba na kuamini katika Jina la Yesu Kristo. Amina!

Tuendelee na kutafakari bahari za Eliya:

“Ikawa mara ya saba akasema, Tazama, wingu linatoka katika bahari, nalo ni dogo kama mkono wa mtu. Akanena, Enenda, umwambie Ahabu, Tandika, ushuke, mvua isikuzuie” (1 Wafalme 18:44 ).

Hapa tunapata mafundisho muhimu kutokana na uzoefu wa Eliya. Alipokuwa pale Mlimani Karmeli aliomba mvua inyeshe, imani yake ikajaribiwa, lakini “alidumu katika kufanya maombi yake yajulikane kwa Mungu.”

Aliomba kwa dhati mara sita na bado hapakuwa na ishara iliyoonesha kwamba ombi lake lilikuwa limekubalika, lakini huku imani yake ikiwa na nguvu, alisisitiza ombi lake kuelekea kwenye Kiti cha Enzi cha neema. “Kama angechoka na kukata tamaa mara ya sita ombi lake lisingejibiwa.”

Tunaye Mungu ambaye sikio Lake halijafungwa ili asisikie maombi yetu, na “ikiwa tutalijaribu Neno Lake, ataheshimu imani yetu”. Yeye anataka shauku zetu zote ziwe zinefungamanishwa pamoja na mapenzi Yake na hapo ndipo atatubariki kwa uhakika kabisa, kwani hapo ndipo hatutajitwalia utukufu wakati baraka zitakapokuwa zetu, bali “tutaelekeza sifa zote kwa Mungu.”

Siyo mara zote ambapo Mungu hujibu maombi yetu papo kwa papo tunapomwita kwa mara ya kwanza, kwani akifanya hivi, “tunaweza kukichukulia kirahisi tu kwamba tulikuwa na haki kupata baraka na fadhili zote ambazo alitupatia”.

Mtumishi wa Eliya alikuwa akimtazama Eliya alipokuwa akiomba. Alipokuwa akichunguza moyo wake, alionekana kupungua zaidi na zaidi, kulingana na alivyojitazama mwenyewe na jinsi alivyojiona machoni pa Mungu. llionekana kwake kwamba alikuwa sio kitu na kwamba Mungu ndiye aliyekuwa kila kitu, “na pale alipofikia hatua ya kuikana nafsi, huku akimng’ang’ania Mwokozi kama nguvu na haki yake pekee, jibu lilikuja.”

Hata mtu awe jasiri na mwenye mafanikio kiasi gani afanyapo kazi maalum, “asipodumu kumtazama Mungu” wakati mambo yanapotokea kujaribu imani yake, “atapoteza ujasiri wake”. Hata baada ya Mungu kumpatia vielelezo dhahiri vya uwezo Wake, hata baada ya kuimarishwa kufanya kazi ya Mungu, atashindwa asipomtegemea kikamilifu Yeye aliye na uwezo wote!

Unapokuwa umekwenda mbele za Mungu kwa ajili ya hitaji lako kamwe Usikate tamaa!!

Mchungaji Samuel Imori

USIKIMBIE

mpweke

*Naye Abramu akamwambia Sarai, Tazama, mjakazi wako yu mkononi mwako, mtendee lililo jema machoni pako. Sarai akamtesa, naye akakimbia kutoka mbele yake. Malaika wa BWANA akamwona kwenye chemchemi ya maji katika jangwa, chemchemi iliyoko katika njia ya kuendea Shuri. Akamwambia, Hajiri, wewe mjakazi wa Sarai, unatoka wapi, nawe unakwenda wapi? Akanena, Nakimbia mimi kutoka mbele ya bibi yangu Sarai. Malaika wa BWANA akamwambia, Rudi kwa bibi yako, ukanyenyekee chini ya mikono yake. (MWA. 16:6‭-‬9 SUV)*

Kuna wengine wetu ambao tukiteswa tu kidogo tunaamua kukimbia.

Tukiteswa kazini tunaacha kazi.

Tukipata mapito kanisani tunakimbia kanisa.

Tukipata tu mapito kidogo kwenye urafiki, ushirika, mahusiano tunakimbia.

Hatupendi shida lakini tunasahau shida na mateso huwa mara nyingi vinatumika na Mungu kushape tabia zetu.

Moto ulipowaka kazini kwake, Hajiri aliamua kukimbia lakini malaika wa Mungu akakutana naye akamwambia rudi ukanyenyekee chini ya bibi yako Sarai.

Mara nyingi sana kinachotufanyaga tukimbie ni kiburi.

Mungu kuna wakati ataruhusu mateso ili kushughulika na kiburi, ujeuri na ukaidi wetu.

Daudi anasema, “Kabla sijateswa nalipotea, lakini sasa nimelitii neno Lako.”

Kuna wakati mateso yanakuja kukusaidia kuona ni eneo gani umepotea na kinachotakiwa sio kukimbia bali ni kutii neno la Mungu.

Mara nyingi tunachodai kuwa ni kuumizwa kwa kweli ni kiburi chetu tu ndo kimeumizwa na mimi nasema kisiumizwe tu, kiuawe kabisa.

Daudi anaendelea kusema, “Ilikuwa vema kwangu kuwa naliteswa, nipate kujifunza amri zako.”

Katikati ya mateso yako jifunze amri za Mungu, sio unakimbia.

Isaya akasema, “Nimekuchagua katika tanuru ya mateso.”

Acha kukimbia tanuru ya mateso, tulia maana Bwana atakuchagulia humo.

Sulemani anasema kwenye mhubiri, Roho ya mtawala ikiinuka kinyume chako usiondoke mara mahali pako ulipo kwa maana roho ya upole hutuliza machukizo mengi.

Ukiinukiwa acha kukimbia.

Tuliaaaaaaaaaaa.

Kuwa mpole laa sivyo kuondoka kwako nje ya wakati na utaratibu wa Mungu utainua machukizo mengi sana.

Isaya anasema Maana hamtatoka kwa haraka, wala hamtakwenda kwa kukimbia.

Acha kufanya haraka kusepa.

Acha kukimbia.

Mwangalie Yusufu mateso aliyoyapata Misri.

Je angekimbia angekuwa Waziri Mkuu?

Wakati wa kuinuliwa kwake ungefika lakini angekuwa hayupo ili kuinuliwa.

Isaka alitaka kukimbia nchi ya ahadi kwa sababu ya ukame.

Alitaka kushuka kwenda Misri.

Mungu akamwambia usishuke kwenda Misri.

Kaa katika nchi niliyokuonyesha nami nitakubariki.

Wengi hatujui kuwa tunapokimbia mahali ambapo Mungu ametuweka tunazikimbia baraka za Mungu maana ameahidi kukubariki katika nchi aliyokupa sio uliyojipa.

Natumaini nimezungumza na mtu mahali hapa.

Nyenyekea.

Acha kukimbia.

Mchungaji Imori

Je Mungu Amekunyamazia?

1

I sam 28:6 Lakini Sauli alipouliza kwa Bwana, Bwana hakumjibu, wala kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kwa manabii. Napenda tujifunze kitu hapa, tunaamini kwamba Mungu wetu anasema, na kama tunaamini hivyo ndiyo maana tunamwomba, na tunapomwomba kwa vyovyote huwa tunatarajia, au tunategemea kupokea majibu toka kwake yeye tumwombaye, tumeona Mtumishi wa Mungu Sauli, alikuwa kwenye shida, na akaenda mbele za Mungu kumuomba amsaidie, lakini Biblia inasema Mungu akakaa kimya, nadhani wapo watu wengi wa aina hiyo siku zetu, na wengine hawajui ni kwa nini amekaa kimya, hawasemeshi, wanaomba, majibu hakuna, na wakati mwingine ndiyo mambo yanavyozidi kuharibika, mwisho wengine wanaamua kufanya kama vile Sauli alivyofanya, unajua alifanya nini? Mst 7 Ndipo Sauli akawaambia nitafutieni mwanamke mwenye pepo wa utambuzi, nipate kumwendea na kuuliza kwake, watumishi wake wakamwambia, tazama yuko mwanamke mwenye pepo wa utambuzi huko Endori. Baada ya kuona Mungu hamjibu, akageukia pepo. Ndugu yetu Sauli hakujuwa ni kwa nini alikuwa amekaa kimya, hakujua dawa ambayo angetumia, akaazimu aende akaaguliwe, yawezekana yupo mtu wa hivyo, umeteseka, umeombewa sehemu mbali, watumishi mbali wamekuwekea mikono, lakini tatizo liko pale pale, sasa ufanyeje? Usiende kwa waganga, napenda ufuatane na mimi nitakupatia baadhi ya sababu ambazo zaweza kusababisa Mungu akakaa kimya,

1. Dhambi katika maisha yako. Yoh 9.31 Twajua ya kuwa Mungu hawasikii wenye dhambi, bali mtu akiwa ni mcha Mugu, na kufanya mapenzi yake, humsikia huyo. Tumeona jambo la kwanza kabisa ambalo laweza kumfanya Mungu akanyamaza ni dhambi, hatasikia, 1saya 59..1..3 Tazama mkono wa Bwana haukupunguka, hata usiweze kuokoa, wala sikio lake si zito, hata lisiweze kusikia, lakini maovu yenu yamewafarikisha ninyi na Mungu wenu, na dhambi zenu zimeuficha uso wake msiuone, hata hataki kusikia, kwa maana mikono yenu imetiwa unajisi kwa damu, na vidole vyenu vimetiwa unajisi kwa uovu, midomo yenu imenena uongo, ndimi zenu yenu zimenong’ona ubaya. Unaona hapo ametaja viungo kadhaa vinavyohusika na kitu kinachoitwa dhambi, ametaja Mikono, ulimi, mdomo. Kinachotakiwa ni mtu kuepuka dhambi ya aina yoyote, ndiyo Mtume Paul aliwaandikia Wathesalike hivi. IThes 5..23 Mungu wa Amani mwenyewe awatakase kabisa, Nafsi zenu, na roho zenu, na miili yenu mhifadhiwe muwe kamili, bila lawama, wakati wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo. Kumbe mwandamu kama mwanadamu, anazo nafsi tatu, mwili, Nafsi, na roho zote hizo zinatakiwa kushughulikiwa, kutakaswa, mara nyingi watu wameishia mwilini, maana dhambi nyingi zilizoorodheshwa ni za mwili, zile zinazoonekana kwa macho ya damu na nyama, pia aliwawambia Wakorintho vilevile. 2Kor 7..1. Basi wapenzi wangu, kwa kuwa tuna ahadi hizo, na tujitakase nafsi zetu na uchafu wote wa Mwili na roho, huku tukitimiza utakatifu ktk kumcha Mungu. Kwa sababu mtu ana nafsi tatu, zote zinahitajika kuwa safi, kwa sababu hakuna dhambi kubwa wala ndogo Kumb 23..14 Kwa kuwa Bwana, Mungu wako, yuatembea ktk kituo akuokoe, na kukutolea adui zako mbele yako, kwa hiyo na kiwa kitakatifu kituo chako, asije akaona KITU kwako kisichokuwa safi, akageuka na kukuacha. Unaona kuwa Mungu wetu hakai kimya wakati maadui wanaposogelea, yeye anatembea, aje atuondolee maadui, tuwe tunamwita au hatumwiti, lakini kituo kinatakiwa kiwe safi, kama tulivyoona kuwa ni Mwili, Nafsi, na roho. Japo watu wengi tunasema Mungu hana shughuli na mwili, yeye anaangalia moyo tu, hapana na vyote, Mungu anapenda usafi, na hili limeachwa, ndugu zangu wakati mwingine unapata mgeni, anaingia ndani, viatu anaviacha nje, doh sebule yote inajaa harufu mbaya, na huwa nashangaa mwenye nayo huwa haisikii, mpaka watu mnatazamana, mpaka inafikia mahali mgeni mwingine akifike, inabidi umuwahi tu mlangoni, aa usivue viatu, ingia tu navyo, anadhani ni upendo, umemhurumia asisumbuke kuinama, kuvua, kumbe unaepusha jambo.

Ebu tuwe safi kama Biblia inavyotutaka kama tulivyoona kwamba Mungu anatembelea vituo vyetu, vinatakiwa kuwa safi, asije akaona kitu, mpaka chumbani, wengine nguo chafu zinawekwa uvunguni, na kisha unafunga madirisha, hakuna hewa, inalazimika hewa kuwa nzito, lazima utakoroma tu, mpaka unakosa raha. Ebr 12..1 Basi na sisi pia kwa kuwa tunazungukwa na wingu kubwa la mashahidi namna hii, na tuweke kando kila mzigo mzito, na DHAMBI ILE ituzingayo upesi, na tupige mbio kwa saburi katika yale mashindano yaliyowekwa mbele yetu. Tumeona kuwa Mungu akiona KITU anageuka na kutuacha, napo tumeona ipo le Dhambi inayotuzinga kwa upesi. Nimeeleza kuwa dhambi siyo lazima ziwe nyingi ndipo Mungu asitusikie, pia sio lazima vitu visivyofaa viwe vingi ndiyo Mungu ageuke na kutuacha, hata kama ni kimoja. Dawa ya dhambi ni kuitubia tu, wala siyo kuificha, au kujifanya haipo, kweli wanadamu hawaioni, lakini yeye Mungu anaiona, hakuna kitu tunachoweza kumficha, wanadamu tuta-over look, lakini siyo Mungu, dhambi zipo za aina mbalimbali. Siwezi kuziorodhesha dhambi zote, leo niiseme hii moja inayotesa wengi. Kumb 23..21..22 Utakapoweka Nadhiri kwa Bwana, Mungu wako, usiwe mlegevu katika kuiondoa, kwa kuwa Bwana, Mungu wako, hataacha kuitaka kwako,nayo hivi itakuwa DHAMBI kwako. Lakini ukizuia usiweke Nadhiri, haitakuwa dhambi kwako, yaliyotoka midomoni mwako yashike kuyafanya, kwa mfano wa ulivyomwekea nadhiri Bwana, Mungu wako, NI SADAKA YA HIARI ULIYOAHIDI KWA KINYWA CHAKO. Hii ni dhambi ambayo imetesa wengi, kumbuka, kinywa chako kimewahi kumwambia Mungu nini? Na hivi wengine ni watembeaji sana, wanafika kanisa hili wanaahidi, wanatamka, wanaondoka, wanasema, wanashangiliwa, wanajisikia vizuri, wanaishia hapo, wengi wamefanya hivyo, na bado kesho wataendelea kuahidi, mkoa hata mkoa, wilaya hata wilaya. Halafu kabla mtu huyu hajatimiza anaingia kufunga na kuomba, anamgoja Mungu aseme naye, ngoja nikukumbushe, Biblia inasema unapoenda kutoa sadaka, ukakumbuka kuwa na jambo na mtu usitoe, iache hapo mkapatane.

Sasa wewe unaingia na huku una neno na Mungu, ulimwambia utafanya kile na kile, kheri uache kwanza hayo maombi, upatanane naye, na kupatana naye ni kutimiza vile ulivyo muahidi. 2. Unaomba na huku jibu unalo tayari. Math 26..44 Akawaacha tena akaenda, akaomba mara tatu, akisema maneno yale yale.(yapi) ms 39 Akaendelea mbele kidogo, akaanguka kifuli fuli, akaomba akisema, Baba yangu, ikiwezekana, kikombe hiki kiniepuke, walakini si kama nitakavyo mimi, bali kama utakavyo wewe. Watu wengi wanaomba kulingana na vile wanataka, wanapangilia, wanasema Mungu nataka iwe hivi, nataka nioe huyu, nataka niolewe na huyu, anamalizia kusema Amen. Yaani iwe hivyo, Mungu anashangaa, hakupewa nafasi yoyote, ameshirikishwa jambo ambalo huyu ndugu analitaka, anamalizia najua wewe ni baba, ulisema baba hawezi kumpa mtoto nyoka, wala jiwe, mtu anabeba begi, anaondoka kwenye maombi, akisemda nimeomba Mungu, kumbe angesema nimemwamuru Mungu.

Tumemsikia Yesu Mwana wa Mungu akiomba, Biblia inasema akaenda akisema maneno yale yale, kwamba kikombe hiki kiniepuke, lakini si kama nitakavyo bali MAPENZI YAKO YATIMIZWE. Bila kuweka hilo, angemaliza tu kwamba kikombe hiki kiniepuke, Amen, abebe begi aelekee Kapernaum, na huku nyuma unajua kile ambacho kingetokea? Luka 22..43 Malaika kutoka Mbinguni akamtokea akamtia nguvu. Wacha nikwambie, wapo watu waliomba wakiwa gethseman, na kwa kuwa hawakuruhusu mapenzi ya Mungu walibeba begi wakaenda kapernaum, Malaika alikuja Gethseman hakumkuta, ilibidi arudi na majibu, akaenda akasema nimekuta hayupo, ebu nikuonye ninachosema utanielewa vizuri kabisa. 1say 50..2 Basi, nilipokuja, mbona hapakuwa na mtu? Nilipoita, mbona hapakuwa na mtu aliyenijibu? Je mkono wangu ni mfupi, hata nisiweze kukomboa? Au je mimi sina nguvu za kuponya? Unaona mpaka anashangaa watu wengine, alituma majibu yao Gethseman, akakuta hawapo, kwa kusema hivyo majibu ya wengi yanarudi. Naendelea kuzielezea baadhi ya sababu zinazo weza kumfanya Mungu akamnyamazia mtu.

3. KURUDIWA. Ebr 12..5…8. Tena mmesahau yale maonyo, yasemayo nanyi kama kusema na wana, mwanangu, usiyadharau marudia ya Bwana, wala usizimie moyo ukikemewa naye, Maana yeye ambaye Bwana ampenda, humrudi, Naye HUMPIGA kila mwana amkubaliye.ni kwa ajili ya kurudiwa mwastahimili, Mungu awatendea kama wana, maana ni mwana yupi asiyerudiwa na babaye? Basi kama mkiwa hamna kurudiwa, ambako ni fungu la wote, ndipo mmekuwa wana wa haramu ninyi, wala si wana wa halali. Neno linaeleza vizuri, tunaelewa wote kuwa mzazi hafurahi mtoto wake anapofanya vitu ambavyo si vizuri, wakati mwingine atamwonya kwa maneno, wakati mwingine atamfinya, wakati mwingine atamtandika, wakristo wengi hawalijui, kila kinachowatokea kisicho kizuri, ni kukemea tu, leo nikusaidia, wakati mwingine ni kiboko cha Mungu, na wewe unakemea, atakaa kimya, dawa ni toba tu, wewe sikiliza shuhuda za watu wengi wanaposhuhudia, unasikia wanamlaumu sana shetani, ni sawa kwamba shetani ndiye analeta mabaya kwetu, lakini imekuwaje akuguse? Kwa nini ameruhusiwa akuguse?

Soma hapa 1Yoh 5.18. Twajua ya kuwa kila mtu aliyezaliwa na Mungu hatenda dhambi, bali yeye aliyezaliwa na Mungu HUJILINDA wala yule mwovu hamgusi. Unaona aliyezaliwa na Mungu akijilinda, mwovu wala hawezi kumgusa, na ukiona amemgusa mtu, basi ujue ameruhusiwa, Bwana akasema katika Yoh 15.5 Mimi ni mzabibu, ninyi ni matawi, akaaye ndani yangu, nami ndani yake huyo huzaa sana, maana pasipo mimi ninyi hamwezi kufanya lolote. Mtu asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi na kunyauka, watu huyakusanya na kuyatupa motoni na kuteketea. Ninyi mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu ombeni mtakalo lote nanyi mtatendewa. Tunatakiwa kukaa ndani yake, naye ndani yetu, hii ni kusema kila unalofanya, cheki kwanza Neno linasemaje kuhusu hili ninalotaka kufanya? Vinginevyo, tutaamua uamuzi usio sawa na Neno, yeye atakaa kimya.

Kama tukiomba kitu kilicho nje ya Mapenzi ya Mungu (Neno) atakaa kimya, 1Yoh5..14 Na huu ndio ujasiri tulionao kwake, ya kuwa, tukiomba kitu sawa sawa na mapenzi yake atusikia. Na kama tukijua kwamba atusikia, tuombacho chote, twajua kwamba tunazo zile haja tulizomwomba. Tukimwendea Mungu kwa Neno lake, bila kuliongeza wala kulipunguza, hawezi kukaa kimya, lazima atatimiza, maana yeye hawezi kabisa kusema uongo, sasa kinachotakiwa ni kufanya bidii kulijua Neno, na utajua lipi? Kol 3..16 Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu ktk hekima yote, mkifundishana na kuonyana kwa Zaburi, na nyimbo, na tenzi za rohoni, huku mkimwimbia Mungu kwa Neema mioyoni mwenu. Tutaliwekaje Neno la Mungu mioyoni, ni kwa kulisoma, kulitafakari, kulipa nafasi, siku tulizo nazo Neno halipewi nafasi, nilialikwa mahali, tukakaa masaa 7 watu wakiimba, mwisho nikakaribishwa, mkaribishaji alisema, tunamkaribisha Mhubiri atuletee Neno la Mungu kifupi. Nimekamwambia, hilo silijui, hilo la kifupi. Alishtuka, alinishangaa kusema ati kifupi silijui, unajua wakati mwingi tumempatia Mungu mpaka, tukumbuke kuwa masaa ni yake, akitaka kuyatumia kukushughulikia ni yeye ndiye anajua, wakati tumekuwa na haraka mpaka tukaondoka hata kabla hajaja, na huwa tumetoka majumbani, na tunataka haraka haraka kurudi tena majumbani, zab 78..41 Wakarudi nyuma wakamjaribu Mungu, wakampa mpaka Mtakatifu wa Israel.

Unaona tatizo walilokuwa nalo Wana wa Israel, walimpa mpaka, walimpangia muda, miezi, miaka, yeye ni Mungu, sisi tunachotakiwa ni kumpatia nafasi, kuwa tayari, tusimlazimishe vile tunataka, akikutaka leo kubali, akikutaka mwezi ujao kubali, vinginevyo akikutaka leo, nawe upange siku unayotaka ngoja nikuonyeshe. Mith 1..24…28 Kwa kuwa nimeita nanyi mkakataa, nimeunyosha mkono wangu asiangalie mtu, bali mmebatilisha shauri langu, wala hamkutaka maonyo yangu,Mimi nami nitacheka siku ya msiba wenu nitadhihaki hofu yenu ifikapo, hofu yenu ifikapo kama tufani, na msiba wenu ufikapo kama kisuli suli, dhiki na taabu zitakapowafikia, ndipo watakaponiita. Lakini sitaitika, watanitafuta kwa bidii, wasinione. Kwa kuwa walichukia maarifa, wala hawakuchagua kumcha Bwana. Mungu amejieleza vizuri kwa mwanadamu, tatizo liko kwa mwanadamu, anadhani yeye aliyeumba muda eti haujali, ni yeye aliuumba, anaujali kabisa, utumie vizuri, ameeleza vizuri kabisa hapo juu kuwa kwa muda niliokutaka wewe hukupatikana, ulikuwa busy, na mimi sasa utakapo nitafuta kwa wakati unaotaka wewe, nami nitakuwa busy, wakati huo na shughuli zingine, nilikwambia uache shughuli zako uje, hukuwa tayari, na wakati wewe unanitafuta nitakuwa na shughuli zangu zingine, ndiyo maana wengine amenyamaza, wengine anacheka, wakati wewe unaita, una shida, umemaanisha yeye anacheka, tunatakiwa tufundishwe namna ya kutumia mida yetu, masaa, miezi, miaka, ni vizuri ufike mahali unajiuliza sasa mwaka imeisha nimefanya nini, naplan kufanya nini kwa ajili ya Bwana?. Muda ni tatizo kubwa kwa wanadamu.

Wakati umekuwa ni tatizo, kanisani unakuta mtu anaelewa vizuri saa ya Ibada kuanza, lakini hajali, anaingia imeanza, anatoka haijaisha, unaona jambo la kawaida, Ebr 12..16,17 Asiwepo mwasherati wala asiyemcha Mungu, kama Esau, aliyeuuza urithi wake wa mzaliwa wa kwanza kwa ajili ya chakula kimoja. Maana mwajua ya kuwa hata alipotaka baadae kuurithi baraka, alikataliwa, (maana hakuona nafasi ya kutubu) ijapokuwa aliitafuta sana kwa machozi. Kumbe machozi nayo yapo yasiyo na maana, hata yangetoka bado tatizo liko pale pale, ebu tuwe tayari wakati Mungu anatuhitaji, tusimwambie kesho, Kut 8.8..10. Musa aliimuliza Farao kuwa alikuwa anataka amuombee lini ili vyura wakatoke katika nchi, wakae mtoni. Inasikitisha Faraoh akamwambia Musa KESHO. Ni kwa Faraoh aseme kesho, muombaji ni Musa (yupo) muombwaji ni Mungu(yupo). Watolewaji ni vyura (wapo) sasa kesho inatoka wapi? Leo kuna tatizo gani? Wapendwa wengi ni wa kesho, nawatakia kila la kheri mbarikiwe na Bwana. Amen.

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – XIX

Ndugu zangu, leo tunaendelea na MISINGI ya Mkristo katika sehemu hii ya Kumi na Tisa na ambayo ndiyo ya mwisho katika Somo hili la Mstari unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia.  Katika sehemu iliyopita, ya Kumi na Nane, tuliishia msingi wa Tatu ambao ni Mafundisho ya Mabatizo. Sasa tuendelee…

4.Kufufuliwa Kwa Wafu. Jambo tunalopaswa kuelewa hapa ni kuhusu UFUFUO WA WAFU. Tuelewe vizuri kabisa kuwa kuna maisha baada ya kufa, japo hili si tatizo kubwa kwa watu wengi maana inapotokea mtu amekufa utasikia wanasema MUNGU AMWEKE MAHALI PEMA PEPONI. Japo ni maombi lakini hayo ni maombi SIFURI. Fuatana nami vizuri ili uelewe, wengine wanapeleka sadaka kwa viongozi wa dini kila mwaka kuwaombea ndugu zao waliokwisha kufa! Ndugu yangu unapoteza hela yako bure, hakuna kitu kama hicho.

Katika Mhubiri 12:7 Biblia inasema siku  ya mtu kuondoka duniani roho humrudia aliyeiumba, na mwili unarudi mavumbini. Nadhani hilo halina tatizo wengi wetu tunajua hilo.

Kwenye Kumb 34:1-7 tunaona Musa alipokufa mambo yake yaliishia hapo katika mwili.

Tukisoma pia katika 2Falme 2:7-11 Hapo tunamwona Eliya akipaa kwenda Mbinguni, kama Biblia inavyotueleza.

Kwenye Math 17:1-5, Hapo sasa tunaona baada ya miaka mingi ilipita tangu Musa afe na Eliya apae, Yesu akaja duniani, na tunaona hapo Eliya na Musa wanamtembelea (Yesu). Unaona jambo la ajabu kidogo: Musa alikufa, Eliya alinyakuliwa, kumbe walikutana, na wote wakafunga safari kuja kumtembelea Yesu katika mlima aliogeukia Sura. Hii inatupa matumaini, kwamba, kumbe mtu akifa huwa yuko mahali!

Math 27:51-54. Hapo ni wakati Bwana wetu Yesu alipokata roho msalabani, jambo kubwa lilitokea, makaburi yalifunguka, miili ya wengi waliokuwa wamekufa kitambo ikainuka na kuwatokea wengi. Hii pia inatuonyesha, na kuthibitisha kile Bwana wetu Yesu alichosema kuwa MIMI NDIO HUO UFUFUO.

Yoh 11:38-44. Hapo utaona uthibitisho kabisa kuwa siku moja katika kuishi kwake katika mwili, mtu mmoja aliyejulikana kama Lazaro aliugua.Dada zake wakatuma mtu akamwite Yesu. Alipokwenda kumwita, Yesu hakufanya haraka kuja, mpaka zikapita siku nne, mwisho Lazaro akafa, akazikwa, na wakawa wamekaa katika matanga, mwisho Yesu alikuja, akamkuta amekuwa kaburini kwa siku nne tayari!  Maandiko yanaonyesha jinsi Yesu alikuja, akamfufua Lazaro, akaendelea kuishi tena.

Maandiko niliyoweka hapo juu yanatuhakikishia kabisa kuwa kuna maisha baada ya kufa. Na watu wengi sana kama si wote wanaamini hivyo! Ila sasa mahali panapochenga watu ni namna gani wajiandae kabla hawajafa. Hilo ndilo tatizo. Wengi, kama nilivyosema, hawajiandai kwa kuwa wanafikiri kuwa wataombewa. Sasa nakuomba ufuatane nami kwa makini nikuonyeshe kitu.

Kabla mtu hajafa anatakiwa achague. Yeye mwenyewe aamue, na hakuna njia nyingine ambayo mtu atapita ili aweze kumuona Mungu. Maandiko yanasema kuwa baada ya kufa ni HUKUMU siyo baada ya kufa ni KUOMBEWA. Ebu thibitisha hili katika Waebrania 9:27 “Kwa kuwa watu wanawekewa kufa mara moja na baada ya kufa hukumu”- Unaona mstari huo unavyosema? Wengi hawajauona, ndio maana  wanangoja kuwa baada ya kufa WATAOMBEWA.  Ndio maana wengi pia huombea wafu, wengine humwambia Mungu: “MUWEKE PEMA PEPONI”. Ndugu yangu mtu mwenyewe ndiye anachagua kwenda pema peponi au kwenda kubaya motoni. Unaamua kwa njia gani.?

Rumi 10: 9-10. “Kwa sababu ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako kuwa Mungu alimfufua katika wafu utaokoka. Kwa maana kwa kwa moyo mtu huamini hata kupata haki, na kwa kinywa hukiri hata kupata wokovu”  (unaona vile wokovu wako ili uwe na maana ni pale unapokiri kwa kinywa, na kupata haki ni pale utakapoamini kwa moyo wako).

Nimesema baada ya kufa huwa hakuna nafasi tena ya KUTUBU  wala KUOMBEWA. Ebu tuangalie Yesu alivyofundisha hilo katika Luka 16:19-31:

“Akasema palikuwa na mtu mmoja tajiri, aliyevaa nguo za rangi ya  zambarau, na kitani safi, na kula siku zote kwa anasa, na maskini mmoja jina lake Lazaro, huwekwa mlangoni pake, ana vidonda vingi, naye alikuwa akitamani kushibishwa kwa makombo yaliyoanguka mezani pa yule tajiri. Hata mbwa wakaja wakamramba vidonda vyake. Ikawa yule masikini alikufa, akachukuliwa na malaika mpaka kifuani mwa Ibrahimu. Yule tajiri naye akafa, akazikwa. Basi kule kuzimu aliyainua macho yake alipokuwa katika mateso, akamwona Ibrahim kwa mbali, na Lazaro kifuani mwake. Akalia akasema; ee baba Ibrahim nihurumie! umtume Lazaro achovywe ncha ya kidole chake majini aburudishe ulimi wangu, Kwa sababu ninateswa katika moto huu. Ibrahim akajibu  akasema kumbuka ya kwamba wewe uliyapokea mambo mema yako katika maisha yako, na Lazaro vivyo alipata mabaya, na sasa yeye yupo hapa anafarijiwa, na wewe unaumizwa. Na zaidi ya hayo kati yetu sisi na ninyi kumewekwa shimo kubwa, ili wale watakao kutoka huku kwenda kwenu wasiweze, wala watu wa kwenu wasivuke kuja kwetu. Akasema ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso. Ibrahimu akasema wanao  Musa na Manabii wawasikilize wao. Akasema; la! baba Ibrahim, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu watatubu. Akamwambia, Wasipowasikiliza Musa na Manabii, hawatashawishika hata mtu akifufuka katika wafu”

Ndugu yangu, hebu tazama jinsi Bwana Yesu alivyoeleza suala hilo wazi wazi. Kama kungekuwa na kuombewa, basi huyu tajiri angeombewa, lakini hakuna, na unaona ndipo alikumbuka hata ndugu zake, akatamani awaambie wao wasije wakaenda aliko, lakini unaona hakukuwa na uwezekano wowote. Ukitaka kuwasaidia ndugu zako ni wakati wakiwa hai, baada ya kufa hakuna namna utakavyoweza kuwasaidia tena!

5. Hukumu ya Milele. Uf 20:11-15 “Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake, ambaye Nchi na Mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana, nikawaona wafu wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi, na vitabu vikafunguliwa, na kitabu kingine kikafunguliwa ambacho ni cha uzima, na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawa sawa na matendo yao. Bahari ikawatoa wafu waliokuwemo ndani yake, na mauti na kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake, wakahukumiwa kila mtu kwa kadri ya matendo yake. Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto.Hii ndiyo mauti ya pili, yaani hilo ziwa la moto. Na iwapo mtu yeyote hakuonekana ameandikwa katika cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto”.

Ndugu zangu habari ndiyo hiyo, kuwa, kuna HUKUMU ya MILELE. Ni vizuri tufahamu hivyo, maana pia kuna mafundisho yasiyo ya kweli kuwa kuna mahali ambapo watu watawekwa wateswe kidogo, kisha wapelekwe mahali pazuri baada ya hayo mateso kidogo. HAPANA! (kwa herufi kubwa). Tunafundishwa kabisa na Biblia kuwa kuna ufufuo wa watu wote, ili kila mtu apokee zawadi, au ujira wa kazi yake aliyoifanya duniani akiwa katika mwili. Biblia inaeleza wazi kabisa. Hebu tuthibitishe tena na hili katika Daniel 12:2: “Tena wengi wa hao walalao katika mavumbi ya nchi wataamka, Wengine wapate uzima wa milele, wengine aibu na kudharauliwa milele.”

Ndugu yangu, Biblia haikuficha kitu. Sisi tunapaswa kufuata kile inachosema. Tunapaswa kuiamini. Mungu aliishaweka utaratibu wake. Sisi tunatakiwa kukubali na kuufuata ndipo tutakuwa salama. Unaona hata kuingiza watu Jehanam aliweka mpangilio, sio holela, wapo watakaotangulia, na watakaomalizia, ona jinsi ilivyopangiliwa, tuendelee kujifunza kutoka kwenye Biblia kwenye Uf unuo19:20, “Yule mnyama akakamatwa, na yule Nabii wa uongo pamoja naye, yeye aliyezifanya hizo ishara mbele zake, ambazo kwa hizo aliwadanganya watu wale walioipokea ile chapa ya huyo mnyama, nao walioisujudia sanamu yake, hao wawili wakatupwa wangali hai katika lile ziwa la moto liwakalo kwa kiberiti”. Hao ndio watakaofungua Jehanam…

Ufunuo 20:10 “Na yule ibilisi mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na nabii wa uongo, nao watateswa mchana na usiku, hata milele na milele”. Huyo ndiye atafuatia kuingia Jehanam…

Ufunuo 20:1- “Mauti na kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto,hii ndiyo mauti ya pili, yaani hilo ziwa la moto”. Hao nao watafuata kuingia Jehanam…

Ufunuo 20:15- “Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto.”. Jehanam haikuumbiwa mwanadamu, Mungu alimpenda mtu mno, ndio maana unaona atamwingiza mwishoni kabisa! Atakuwa ni mwanadamu aliyeamua kumkataa Yesu, ndiye atakutana na moto huo. Anayesubiri akifa aombewe. Hebu nikushauri hivi: Amua kuchagua Yesu awe mwokozi wako kabla hujaondoka  katika mwili wako!

Ndugu yangu tumeiangalia misingi ya Mkristo tunayotakiwa kuiimarisha katika maisha yetu ya kiroho ikiwa tunataka kuyaona maisha yetu ya baadae, baada ya kutoka mwilini huu. Kwa kuwa bado ungali hai, fanya uamuzi leo. Njia pekee ni YESU. Hakuna  njia nyingine ya kufika kwa Mungu  muumba Mbingu na Nchi!

Mungu atusaidie tufanye uamuzi sahihi, tusije tukajuta mwishoni. Kumbuka ile mithali ya kiswahili inayosema- MAJUTO NI MJUKUU!

Mbarikiwe na Bwana kwa kufuatana nami kuanzia sehemu ya Kwanza ya somo hili. Na ninamuomba Mungu wa mbinguni azidi kuwajalia kuyatafakari yote tuliyopitia katika somo hili ili kila mtu aweze kuyafanyia kazi.

Ni mimi Ndugu yenu Mch. Samweli Imori.

 

Mstari Unaoniliza Kuliko Yote Katika Biblia – XVIII

 

Somo letu linaendelea. Katika mstari ule wa Luka 13:22 Biblia inaeleza kuhusu mtu mmoja aliyemuuliza Bwana Yesu kuhusu wingi wa watu wanaookolewa. Bwana Yesu akijibu swali hilo alisema kuwa JITAHIDINI KUINGIA KATIKA MLANGO ULIO MWEMBAMBA, KWA MAANA NAKWAMBIA KUWA WENGI WATATAKA KUINGIA LAKINI WASIWEZE. Pamoja na sababu nyingi ambazo nimekwisha kuzieleza katika masomo yaliyotangulia, leo katika Sehemu hii ya Kumi na Nane tunaendelea na sababu nyingine.

23. WATAKOSA MSINGI.

1Kor 3:10-11. “Kwa kadri ya Neema ya Mungu niliyopewa na Mungu, mimi kama mkuu wa wajenzi mwenye hekima, naliuweka msingi, na mtu mwingine anajenga juu yake, lakini kila mtu aangalie anavyojenga juu yake. Maana msingi mwingine hakuna mtu awezaye kuuweka, isipokuwa ni ule uliokwisha kuwekwa, yaani YESU  KRISTO.”

Wapendwa, leo tutauangalia Msingi. Kila nyumba unayoiona ina msingi, na misingi imetofautiana, msingi wa nyumba ya kawaida ni tofauti na msingi wa ghorofa.  Msingi wa ghorofa Moja ni tofauti na msingi wa ghorofa Kumi. Jinsi  ghorofa linavyokwenda juu  ndivyo msingi unatakiwa kwenda chini, na ndivyo inatakiwa pia wajenzi kuchanganya material kwa kipimo kinachofaa, vinginevyo ghorofa hilo litaishia kuanguka.

Hapo juu tumesoma kuwa hakuna msingi mwingine nje ya Kristo. Maana yake ni hivi ILE SABABU ILIYOKUFANYA USEME UMEOKOKA NI MHIMU SANA SANA.

Wengine waliokoka kwa sababu walikuwa wagonjwa. Walipoambiwa sasa unatakiwa kuokoka, kwa kuwa anaumwa akasema sawa, si kwamba moyo wake ulimpenda Mungu kwa kweli. Wengine walikutwa gerezani, walipoambiwa habari ya kuokoka, na wakaambiwa, ukiokoka Mungu atakutoa jela, na kwa kuwa walikuwa wamebanwa iliwalazimu wakubali na kweli Mungu aliwafanyia hivyo. Wengine walisikia wahubiri wakisema wewe unayeteseka na umaskinu njoo kwa Yesu, atakupa kile na kile, na kwa kuwa walikuwa na hali mbaya wakalazimika kufanya hivyo, na si kwamba mioyo yao ilikuwa kweli imeamua kumfuata Bwana Yesu.

Utakumbuka siku moja Yesu aliwaambia watu waliokuwa wanamfuata kuwa, MSIKITENDEE KAZI CHAKULA  KINACHOHARIKA, AKASEMA MNANIFUATA KWA SABABU  MLIKULA MIKATE MKASHIBA. Mpendwa hebu jiulize: KWA NINI UNAMFUATA YESU?

Tuendelee na somo letu katika kuuangalia MSINGI.

Katika Ebr 6:1-6 kuna maneno ambayo nimeyapanga kama ifuatavyo:

“Kwa sababu hiyo tukiacha, kuyanena mafundisho ya kwanza,  ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu,

1. TUSIWEKE MSINGI TENA WA KUZITUBIA KAZI ZISIZO NA UHAI.

2. NA WA KUWA NA IMANI KWA MUNGU.

3. NA WA MAFUNDISHO YA MABATIZO.

4. NA KUWEKEA MIKONO.

5. NA KUFUFULIWA WAFU.

6. NA HUKUMU YA MILELE.

Ndugu zangu watoto wa Mungu, Maneno hayo hapo juu  ndiyo misingi ambayo kila aliyeokoka alitakiwa kufundishwa. Hiyo ndiyo itakufanya uendelee mbele. Hata kama wewe utakuwa ni ghorofa, hautaweza kuporomoka kamwe!

Sasa tutaendelea kuyapitia moja baada ya jingine ili uweze kuelewa vizuri. Ni ombi langu kuwa Mungu wetu aliyetuokoa atatupatia Neema ya kuweza kuelewa vizuri kwa uongozi wa Roho mtakatifu.

1.Kutubia kazi ambazo hazina uhai. Ni kitendo cha mtu  kutubu dhambi zake kwa mtu. Wengine wanaita Kuungama. Vyovyote utakavyoiita lakini tunapaswa kuungama dhambi zetu kwa YESU, na pia ni kuungama na kuziacha, kutozirudia tena.

Mith 28:13 “Afichaye dhambi zake, hatafanikiwa, bali aziungamaye na kuziacha atapata rehema”. Mpendwa Biblia inajieleza. Tunatakiwa tuziungama na kuziacha tofauti na mafudisho mafu kuwa mtu uende kanisani kila jumapili uungame dhambi kwa mtu. Jumapili hii utaungama kwake, na jumapili ijayo, na ile ijayo, mpaka mwezi, mpaka mwaka, unaanza tena mwaka mwingine! Hapana. Nenda kwa Yesu, ungama na kuziacha, utapata rehema.

Katika Yoh 9:31 tunaona kuwa Mungu hasikii wenye dhambi. Kama utaishi na dhambi, elewa kuwa Mungu hakusikii kabisa wakati unaomba. Atakusikia pale tu ukiziungama na kuziacha, tangu hapo atakuwa anakusikia.

Mith 8:13 “Kumcha Bwana ni kuchukia uovu.” Unajua wapendwa, kila mtu anasema “kweli namcha Mungu” au “nampenda Mungu”. Lakini sikia, jipime hapo katika mstari huo unasema kuwa KUMCHA MUNGU NI KUCHUKIA UOVU.

Hebu tuendelee kuona jinsi ya kuungama au kutubu: Ni kutokurudia yale ambayo mtu ameamua kuyaombea msamaha kwa Mungu. Yaani ni kumaanisha kile unachokisema.

Katika Yoh 5:10-14 kuna kisa cha mtu aliyekuwa amelala miaka 38, na wengine walikuwa wanaponywa maji yanapotibuliwa, ila yeye alikuwa haponywi. Siku moja Bwana wa huruma alimkuta amelala, akamuuliza kama anataka kuwa mzima nay eye akasema HANA MTU WA KUMTIA KWENYE BIRIKA.  Nafikiri hakuwa ameelewa swali. Kama wengi wetu tusivyoelewa wakati Bwana ansema na sisi. Utakumbuka Adamu aliulizwa kwa nini UMEKULA TUNDA? AKASEMA NI YULE MWANAMKE ULIYENIPA NDIYE AMENIPA TUNDA. Kumbe kama angeulizwa kuwa “ni nani amekupa tunda ukala?” ndipo angejibu hivyo. Pamoja na kutokujibu swali sawa sawa lakini Bwana akamwambia SIMAMA  JITWIKE GODORO LAKO UENDE. Naye akasimama akajitwika godoro akaenda. Mafarisayo walipomsumbua kuwa mbona amejitwika godoro wakati ilikuwa ni sabato yeye aliwajibu kuwa yule aliyemfanya awe mzima ndiye aliyemwambia ajitwike godoro!

Kama vile wengi wetu tukiishaokoka, watu huwa wanajitokeza kuulizia wokovu wetu, kuwa kwa nini hili, kwa nini umeacha dini yetu, kwa nini hili na lile. Ebu jibu liwe ni kwamba: “YEYE aliyenifanya mzima ndiye ameniambia nijitwike godoro

Yoh 5:14 “Baada ya hayo Yesu akamkuta ndani ya hekalu, akamwambia, angalia umekuwa mzima, usitende dhambi tena, lisije likakupata jambo lililo baya zaidi”

Nimesema kutubu au kuungama ni kuacha, ni kugeuka upande mwingine, ni kuipa dhambi mgongo na kutokuirudia tena. Unaona Yesu alivyomwambia mtu huyu aliyekuwa amelala miaka 38, kuwa akirudia litampata baya zaidi ya hilo la kulala miaka 38. Je, ni lipi hilo baya zaidi?

Biblia inasema pepo akimtoka mtu hurudi tena, akikuta aliyemfukuza hayumo, huendea wengine SABA  walio wabaya zaidi ya yule, na hali ya mtu huyo huwa mbaya zaidi. Hayo yapo katika  Math 12:43

Katika Yoh 8:1-11 tunaona mwanamke mmoja aliletwa kwa Yesu, alikuwa amekamatwa kwenye zinaa, na wanawake wa namna ile walikuwa wanapigwa kwa mawe. Siku hiyo aliletwa kwa Yesu, na Yesu alimhurumia, akawaambia wale washtaki wake kuwa yeyote asiye na dhambi awe wa kwanza kumtupia jiwe, na wengine wafuate. Yule mwanamke alijua kuwa amekwisha, pengine alikuwa ameisha wahi kuona wengine wakipigwa kwa mawe, akawa anasubiri mawe. Biblia inasema Yesu akainama akawa anaandika chini, hatuelewi alikuwa anaandika nini, lakini wengine husema alikuwa anaandika dhambi ya kila mtu aliyekuwa pale, na kila mmoja alipoona vile, alikimbia. Mama yule alibaki peke yake na Bwana Yesu, na katika Yohana  8:10-11 “ Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia mwanamke, wako wapi washitaki wako?

2. Kuwa na Imani kwa Mungu. Ni kukubaliana na kile ambacho Neno  la Mungu linasema, hata kama kwa macho ya kibinadamu linaonekana kuwa haliwezekani kabisa. Ndiyo maana mtume Paulo akaandika kuwa: HATUENENDI KWA KUONA, BALI TUNAENENDA KWA IMANI. Hapo ndipo wanapopatikana au walipopatikana mashujaa wa Imani. Walikubaliana na Neno la Mungu bila kujali gharama. Wengine walikubaliana mpaka wakafa bila kubadilisha msimamo wao.

Ufunuo 2:10 “Usiogope mambo yatakayokupata, tazama ibilisi atawatupa baadhi yenu gerezani, ili mjaribiwe, nanyi mtakuwa na dhiki siku kumi. Uwe mwaminifu hata kufa, nami nitakupa taji ya uzima.

Yuda 1:5 “Tena napenda kuwakumbusha, ijapokuwa mmekwisha kuyajua haya yote, ya kwamba Bwana akiisha kuwaokoa watu  katika Nchi ya Misri, aliwaangamiza baadaye wale wasoioamini”

Ndugu yangu, wakati mwingine shetani analaumiwa bure. Hapo juu unaona kuwa Bwana akiisha kukuokoa unapaswa kumwamini kuwa anaweza kabisa kukufikisha kule alikokuahidi. Haitakiwi kumtilia mashaka maana mashaka huletwa na uoga. Uoga ukiishaingia, hofu inaingia, mashaka naye anasogea, ndipo kutetemeka nako kunakuja kwenye mwili. Utakumbuka Mungu alimwambia Gidion, katika Waamuzi 7 hivi: “watu hawa walio pamoja nawe ni wengi mno hata nikawatie Wamidiani katika mikono yao, wasije Israel wakajivuna, juu yangu wakisema, mkono wangu mwenyewe, ndio ulioniokoa, basi sasa nenda  tangaza habari masikioni mwa watu hawa, na kusema  MTU AWAYE YOTE ANAYEOGOPA NA KUTETEMEKA, ARUDI AONDOKE KATIKA MLIMA  GILIADI. NDIPO WATU ISHIRINI NA MBILI ELFU WAKARUDI, KATIKA WATU HAO, WAKABAKI WATU ELFU KUMI.

Unaona! Mungu haendi na waoga, haendi na wanaotetemeka, hao ndio unasikia wanakufa na pressure, mishtuko. Ukiishaokoka hautakiwi kuwa hivyo. Elewa siku zote kuwa VITA SI VYAKO, ELEWA ALIYEMO NDANI YAKO NI MKUU KULIKO ALIYE KATIKA DUNIA, ELEWA  UNAYAWEZA MAMBO YOTE KATIKA YEYE AKUTIAYE NGUVU.

3. Mafundisho ya Mabatizo. Mpendwa, ninafundisha Misingi au Msingi wa Mkristo, ambao ukiishakuwa ndani yako hakuna kitakachokutikisa kamwe. Kumbuka Biblia inasema kuwa mwenye haki ni jasiri kama SIMBA. Ndiyo maana Bwana wetu Yesu anaitwa  SIMBA WA KABILA YA YUDA. Hata katika Biblia kuna Neno USIOGOPE  mara idadi ya siku za mwaka mzima. Kwa hiyo kila ukiamka asubuhi kuna neno “USIOGOPE” liko hapo kukusalimia.

Kwa nini Biblia inasema MABATIZO?     Haisemi UBATIZO, ni MABATIZO. Hii inaonyesha ni Mengi.

a). Ubatizo wa Maji. Katika Math 3:13 tunamwona Bwana wetu Yesu akienda Yordani kubatizwa. Yohana akambatiza akiwa mtu mzima tofauti na siku zetu unaona watu wanabatizwa wakiwa watoto wadogo, na wanatafuta mtu anakuwa baba yake wa ubatizo. Hiyo siyo Biblia.

Katika Mark 16:14 Biblia inasema AAMINIYE NA KUBATIZWA ATAOKOKA. Huyo anayebatizwa anatakiwa kuamini yeye mwenyewe kwa moyo wake, ndipo abatizwe. Kinyume cha hapo tunafundisha mambo yetu wenyewe, wala siyo ya Mungu.

Rumi 6:4 “Tulizikwa pamoja naye kwa njia ya UBATIZO”. Ubatizo ni ishara ya kuwa mtu amekufa, na anazikwa kwenye maji. Wapo wahubiri wengi wanasema haijalishi ni maji gani, yawe maji mengi au maji kidogo mradi umebatizwa. Mpendwa, ebu sikia maandiko haya hapa katika Math 24:4 “Yesu akajibu akawaambia ANGALIENI MTU ASIWADANGANYE”. Ni juu yangu, ni juu yako, ni juu ya kila mtu kuangalia asidanganywe. Atakayekubali kudanganywa basi atakapofika kwa Yesu, ataulizwa ilikuwaje ukafanya hivyo? Atasema nilidanganywa. Nakuambia ndugu yangu kuwa wala hakutakuwa na msamaha.

Kumbuka Mungu alimuuliza  ADAM “Kwa nini umekula tunda nililowakataza kwamba msilile?” Jibu: Mwanamke uliyenipa. ( Bado alipata adhabu}

HAWA naye akaulizwa: “Kwa nini umekula tunda?” Jibu: Nyoka alinidanganya nikala.  Pamoja na majibu hayo mazuri lakini bado hao wazazi wetu wa kwanza waliadhibiwa tu. Yule aliyepewa na mwanamke, na yule aliyedanganywa, wote waliadhibiwa!.

Hapo nilikuwa nazungumzia ubatizo wa maji mengi, maana kama Biblia inasema ni ishara ya mazishi, basi tuelewe kuwa mtu akifa huzikwa mwili mzima wala sio kichwa peke yake!

Nadhani utaniuliza swali kuwa, Sasa hao wanaobatiza watoto wadogo, wameyapata wapi hayo mafundisho? JIBU: Mark 7:6-7 “Akawaambia Isaya alitabiri vema, juu yenu enyi wanafiki, kama ilivyoandikwa, watu hawa huniheshimu kwa midomo, ila mioyo yao iko mbali nami, nao waniabudu bure, wakifundisha mafundisho yaliyo maagizo ya wanadamu”. Nakushauri kuwa kila unachofundishwa ebu kikague kama kweli kiko kwenye NENO la Mungu, yaani BIBLIA.

b). Ubatizo wa Roho Mtakatifu. Mdo 1:6-7 “Basi walipokutanika, wakamuuliza, wakisema; Je, Bwana wakati huu ndipo unapowarudishia Israel ufalme? Akawaambia siyo kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoweka katika mamlaka yake mwenyewe. Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilkia juu yenu Roho mtakatifu, nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalem, na katika Uyahudi wote na Samaria na hata mwisho wa nchi”

Roho ajapo ndani ya mtu ndiye humpa nguvu za kushinda maovu. Ndiye anakupa nguvu za kuwa shahidi.

Rumi 8:26. Hatujui kuomba ila Roho mwenyewe hutuombea kwa kuugua kusikoweza kutamkwa. Roho wa Mungu alikuwa ndani ya Yesu, ndiye huyo huyo akiwa ndani yako utaishi kama alivyoishi Yesu. Atakuombea kama alivyomwombea Yesu.

Ebr 5:7 “Yeye siku hizo za mwili wake, alimtolea yule awezaye kumwokoa na kumtoa katika, maombi na dua pamoja na kulia sana na machozi, akasikilizwa kwa jinsi alivyokuwa mcha Mungu”. Mpendwa, kama Yesu ndivyo aliishi duniani, kwa kilio kikuu, naye alisaidiwa na Roho Mtakatifu, basi mimi na wewe kama tunataka tushinde tunamhitaji Roho mtakatifu, ndiye atakaye tusaidia.

Gal 4:6 “Na kwa kuwa ninyi mmekuwa wana, Mungu alimtuma Roho wa Mwanae  mioyoni mwetu, aliaye ABA yaani Baba”. Ndugu yangu pengine umeokoka, au hujaokoka, Ubatizo wa Roho mtakatifu ni muhimu sana katika maisha ya Mkristo, na huyo ndiye ataendelea kukufundisha Neno la Mungu na kukuweka kwenye kweli yote.

c). Ubatizo wa Mateso. Luka 12:49-53. “Nimekuja kutupa moto duniani, na ukiwa umeishawashwa, ni nini nitakalo zaidi, lakini nina ubatizo unipasao kubatizwa, nami nina dhiki kama nini hata utimizwe. Je, mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia la sivyo bali mafarakano. Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja, watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu wa kwa wawili, wawili kwa watatu. Watafarakana baba na mwanawe, mwana na baba yake, mama na binti yake na binti na mamaye, mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu”

Hayo yote yanaeleza jinsi safari ya Mbinguni inavyomkabili mtu peke yake bila kutegemeana. Kwa hiyo unatakiwa uiangalie Biblia inachokufundisha, kishike, kikumbatie. Wengine wanasema baba kanizuia kuokoka, mama kanizuia kuokoka, kaka, au baba mkwe. Hapana! Kila mtu atasimama mbele za Bwana atoe habari zake mwenyewe.

Bwana akasema anao ubatizo mwingine ambao ni shida kama nini kuutimiz!. Ndugu zangu, Yesu alikuja akatuachia kielelezo hapa duniani. Yaliyompata ndio yatatupata. Kama watu walimpenda, basi watatupenda tu na sisi, kama walimchukia ebu tujue kuwa yaliyompata ndiyo yatatupata. Ndio maana alisema mtu akitaka kumfuata AUBEBE MSALABA WAKE AMFUATE. Kumbuka MSALABA maana yake ni MATESO.

Ni kweli kwamba hatuwezi kusulubiwa kama alivyosulubiwa, ila tunasulubiwa kwa namna moja au nyingine.

Mdo 14:21-22. “Hata walipokwisha kuihubiri Injili katika mji ule, na kupata wanafunzi wengi, wakarejea mpaka Listra, na Ikonio, na Antiokia (yafuatayo nimeyapanga mwenyewe kuwa):

    i. WAKIFANYA IMARA ROHO ZA WANAFUNZI.

    ii. WAKIWAONYA WAKAE KATIKA ILE IMANI.

   iii.WAKIWATAARIFU KUWA TUMEPASWA KUINGIA KATIKA UFALME WA MUNGU KWA NJIA YA DHIKI NYINGI.

Ndugu zangu wapendwa, kusudi la Injili ya Kristo tunayoihubiri  linatakiwa  kuwa katika sehemu hizo 3.

Kufanya roho za wanafunzi kuwa imara. Kwa nini zifanywe Imara? Kwa kuwa baada ya kuokoka huwa tunakutana na mambo mazito kiasi kwamba kama mioyo yetu haiko imara kwa Neno la Mungu, hatuwezi kufika popote. Tutaishia kusema tu nimeokoka, lakini mwisho wa siku, unakuta moyo huo ambao haukufanywa imara umebomoka. Ndio maana kwenye milango yetu tunaweka makomeo, na tukiisha funga twaweza kulala. Na mioyo yetu inatakiwa kufanywa Imara. Ndiyo maana imeandikwa katika Mith 4:23 kuwa “Linda moyo wako kuliko yote uyalindayo, maana huko ndiko zitokazo chemi chemi za uzima”. Na moyo unalindwa kwa NENO la Mungu. Ndiyo maana imeandikwa kuwa NENO LA KRISTO LIKAE KWA WINGI NDANI YETU.

Kazi ya 3: Kuwataarifu kuwa kuingia mbinguni ni kwa njia ya dhiki nyingi. Ndugu yangu, Biblia vile ilivyoandikwa ndivyo ilivyo. Hatupaswi kuigeuza, wala kuichakachua, au kuigoshi, imeeleza wazi wazi kuwa tutaingia kwa njia ya DHIKI NYINGI. Pata muda soma vizuri Neno katika kitabu cha MASHUJAA WA IMANI, cha Waebrania sura ile ya 11.

1Pt 2:18-23. “Enyi watumishi, watiini bwana zenu, kwa hofu nyingi, sio wao walio wema na wapole tu, bali nao walio wakali, maana huu ndio wema hasa, mtu akivumilia huzuni kwa kumkumbuka Mungu, pale ateswapo isivyo haki, kwa maana ni sifa gani kustahimili, mtendapo dhambi na kupigwa makofi. Lakini kustahimili mtendapo MEMA NA KUPATA MATESO, huu ndio wema hasa mbele za Mungu, maana ndiyo mlioitiwa, maana Kristo naye aliteswa kwa ajili yenu, akawaachia kielelezo mfuate nyayo zake. Yeye hakutenda dhambi, wala hila haikuonekana kinywani mwake, yeye alipotukanwa hakurudisha matukano, alipoteswa, hakuogofya, bali alijikabidhi kwake ahukumuye kwa haki”.

Ndugu yangu, ebu soma hayo maandiko hapo juu. Mimi na wewe tujipime kwake huyo ambaye tunaambiwa tufuate nyayo zake. Je, tunazikanyaga nyayo zake kweli? Au zetu zimepanuka? Au zimepwaya?

2Timotheo 3:10-12. “Bali wewe umeyafuata mafundisho yangu, na mwenendo wangu, makusudi yangu, na Imani na uvumilivu, na upendo na saburi, tena na adha zangu na mateso, mambo yaliyonipata katika Antiokia, katika Ikonia, na katika Listra, kila namna ya adha niliyoistahimili, naye Bwana aliniokoa katika hayo yote. Naam na wote wapendao kuishi maisha ya utauwa wataudhiwa.”

Mistari hiyo inatuonyesha jinsi watumishi wa kweli walivyoishi, ambao Biblia inasema wazi wazi  kuwa TUMEJENGWA KATIKA MSINGI WA MITUME NA MANABII. Kwa kusema hivyo ni kwamba njia waliyoipitia ndiyo tutaipitia, ambayo ndiyo ile  Bwana wetu Yesu aliipitia. Ndio maana walikuwa wakipita na kuwajulisha kuwa wakae wakijua kuwa TUTAINGIA KWA NJIA YA DHIKI NYINGI.

Ndugu zangu leo nitaishia hapa katika sehemu hii ya Kumi na Nane. Misingi mingine iliyobakia, ambayo ni Kuwekea Mikono, Kufufuliwa Wafu na Hukumu ya Milele nitaielezea katika Sehemu ifuatayo ya Kumi na Tisa.

Ndugu mpendwa, ninakushauri kuwa baada ya kusoma Misingi hiyo niliyoielezea jikite katika kuitafakari na kuitendea kazi ili roho yako ipate kuwa imara katika safari hii, kwa maana ya kwamba dhiki zitakapokuja wala usishangae, na uwe na uwezo wa kupita na upate kuitwa MSHINDI!

Ubarikiwe na Bwana.

Ndugu yenu Mchungaji Samuel  Imori.