Moses Kulola Amepumzika

moses

Askofu Mkuu wa Evangelistic Assemblies God Tanzania (EAGT) Moses Kulola amefariki dunia leo tarehe 29/08/2013 katika hospital ya AMI (African Medical Investments) iliyopo Slipway jijini Dar es Salaam.

Askofu ana watoto wengi wa kiroho nchini Tanzania, Kanisa  linahuzinishwa na habari hizi, Bwana awape faraja kwa kipindi hiki,  “Kuishi ni Kristo na kufa ni faida”

Mazishi yatafanyika Mwanza siku ya Jumatano Septemba 4 kwenye kanisa la EAGT Bugando.

Jina la Bwana libarikiwe.

….UPDATE KUTOKA IKULU

THE UNITED REPUBLIC OF TANZANIA
DIRECTORATE OF PRESIDENTIAL COMMUNICATIONS
Telephone: 255-22-2114512, 2116898
              press@ikulu.go.tz

Fax: 255-22-2113425

PRESIDENT’S OFFICE,
      THE STATE HOUSE,
              P.O. BOX 9120,  
DAR ES SALAAM.
Tanzania.
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ameshtushwa na kuhuzunishwa na taarifa za kifo cha Kiongozi wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) Askofu Mkuu Moses Kulola ambaye ameaga dunia , Alhamisi, Agosti 29, 2013 katika Hospitali ya AMI iliyoko Masaki mjini Dar Es Salaam akiwa na umri wa miaka 84.

Rais kikwete ameelezea mshtuko na huzuni yake katika Salamu za Rambirambi alizomtumia Katibu Mkuu wa Kanisa hilo Bwana Brown Mwakipesile kufuatia kifo cha Askofu Mkuu Kulola.

“Nimeshtushwa, nimesikitishwa na kuhuzunishwa sana na taarifa za kifo cha Mtumishi wa Mungu wa muda mrefu na Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT), Marehemu Moses Kulola kutokana na maradhi yaliyomfanya wakati fulani apelekwe hadi India kupatiwa matibabu” amesema Rais Kikwete.

Rais Kikwete amesema alimfahamu Marehemu Askofu Moses Kulola kwa miaka mingi wakati wa enzi za uhai wake, kama Mtumishi Hodari wa Kiroho aliyejitoa vilivyo katika kuwahudumia Waumini wa Kanisa lake ambapo mahubiri yake yametoa mchango mkubwa katika kuimarisha imani za Waumini wake na kusaidia kwa kiasi kikubwa katika kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu.

Aidha Rais Kikwete amesema kifo cha Askofu Mkuu, Moses Kulola kimeacha pengo kubwa siyo tu kwa Waumini wa Kanisa lake hapa nchini, bali pia miongoni mwa wapenda amani kote nchini na kwingineko duniani kwa vile enzi za uhai wake, Marehemu aliweza kufikisha ujumbe muhimu wa kiimani kupitia mahubiri yake kwa watu wa mataifa mbalimbali ndani na nje ya  Bara la Afrika.

“Kwa niaba yangu mwenyewe na Serikali ninayoingoza, ninakutumia wewe Katibu Mkuu wa Kanisa la Evangelical Assembies of God Tanzania, Bwana Brown Mwakipesile na Waumini wote wa Kanisa hilo Salamu za Rambirambi  kutoka dhati ya moyo wangu kwa kumpoteza Kiongozi muhimu wa Kiroho.  Ninawajulisha kuwa niko nanyi katika wakati huu mgumu kwa sababu msiba wenu ni msiba wetu pia. Sala na mioyo yetu iko nanyi wakati wa maombolezo ya kifo cha Kiongozi huyo shupavu wa dini. Nawaomba wote muwe wavumilivu na wenye subira kwani yote ni Mapenzi yake Mola”, amesema Rais Kikwete.

“Vilevile kupitia kwako, naomba unifikishie Salamu zangu za Rambirambi na pole nyingi kwa familia, ndugu na jamaa wa Marehemu, Askofu Mkuu, Moses Kulola kwa kumpoteza Baba, Kiongozi Shupavu na Mhimili wa familia.  Natambua fika kwamba hiki ni kipindi kigumu sana kwao cha maombolezo.  Natambua machungu yenu wakati huu na naungana nanyi katika kumwomba Mwenyezi Mungu, Mwingi wa Rehema aiweke peponi roho ya Marehemu Moses Kulowa. Amina.”

Mazishi ya Marehemu, Askofu Mkuu wa Kanisa la Evangelistic Assemblies of God Tanzania (EAGT) yatafanyika mjini Mwanza Jumatano ijayo tarehe 4 Septemba, 2013.  Heshima za mwisho kwa mwili wa Kiongozi huyo zitatolewa siku ya Jumamosi tarehe 31 Agosti, 2013 katika Kanisa laEAGT karibu na Hospitali ya Temeke kuanzia saa 2.00 asubuhi hadi saa 6.00 mchana.

Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
29 Agosti, 2013

Balaa, Laana na mikosi ya kifamilia.

Na Mchungaji Josephat Gwajima

Mara nyingi unapoenda hospitali, daktari huwa anauliza kama kuna mtu katika ukoo wako, ana historia ya tatizo hilo na jibu lako humsaidia kujua tatizo lako kwa undani. Vivyo hivyo laana, mikosi na balaa vinaweza kufuata familia yako kama zilivyo baraka pia.

Ndio maana watoto wengi wa viongozi serikali huishia kuwa viongozi, na watoto wengi wa maskini hujikuta wanaishia kuwa katika umaskini zaidi, ni ukweli ulio dhahiri kuwa kilichotendwa na baba huwa kinashuka hadi kwa watoto wake. Ukisoma katika Mithali 13: 22 “Mtu mwema huwaachia wana wa wanawe urithi; Na mali ya mkosaji huwa akiba kwa mwenye haki.” Pia, Zaburi 37:25 “Nalikuwa kijana nami sasa ni mzee, Lakini sijamwona mwenye haki ameachwa Wala mzao wake akiomba chakula.”

Adamu na Hawa walipotenda dhambi, hukumu kwa mwanamke ilikuwa hivi, Mwanzo 3:15, Mungu aliweka uadui kati ya uzao wa mwanamke na uzao wa nyoka. Kwanini unafikiri Mungu aliweka uadui hata kwa watu ambao hawakuhusika? Jibu ni kuwa yaliyotendwa na wazazi au mababu wa ukoo yana matokeo sana katika maisha ya mtu ya leo. 2Timotheo 1:3-5 “…5 nikiikumbuka imani uliyo nayo isiyo na unafiki, ambayo ilikaa kwanza katika bibi yako Loisi, na katika mama yako Eunike, nami nasadiki wewe nawe unayo.” Kumbe kuna uwezekano wa tabia ya mtu kuunganishwa na familia au ukoo wake. Kama imani yaweza kusafiri kiukoo, vivyo hivyo na tabia ya kutokuamini au uovu mwingine waweza kusafiri kutoka kwa mtu kizazi kimoja hadi kingine.

Ndio maana inawezekana, mtu akajikuta anafanya tabia fulani, na ingawa haipendi lakini anaendelea kuifanya kumbe ni kwasababu ya ukoo wake. 1Petro 1:18-19 Waweza kuumkuta mtu mwongo, mwizi, mzinzi, mchoyo, mbisho kumbe ni kwasababu ya tabia za kurithi ambazo zinatokana na laana za familia. Kuna uwezekano mtu akajikuta hana ndoa ya kudumu, kumbe ni kutokana na laana iliyo katika ukoo.

Ni muhimu kumjua adui unayepambana naye, watu wengi sana wanajikuta wanapambana na adui wasiyemjua huku wakidhani wako sahihi, na mwisho hujikuta wana bidii yao haizai matunda, kumbe ni matokeo ya kupambana na adui usiyemjua. Huwezi kushindana na shetani bilankujua mbinu zake “watu wangu wanaangamia kwa kukosa maarifa.”

Jambo lingine la Muhimu, maamuzi yoyote unayoyafanya leo yana matokeo katika maisha yako na ya uzao wako. Ndio maana wana wa Israeli walipokuwa wanaingia katika nchi ya ahadi Yoshua aliwaambia, “chagueni hivi leo mtakaye mtumikia” uchaguzi unaoufanya leo una matokeo mazuri au mabaya katika maisha yako.

Biblia inasema kila andiko lenye pumzi ya Bwana lafaa kwa mafundisho, kwasababu hiyo tunaweza kujifunza kitu kutoka katika maisha ya baba wa Imani, Ibrahimu. Mwanzo (11:29-30), ibrahimu alikuwa hazai maana Sara alikuwa tasa, tunaona pia mwanaye Isaka naye akawa na tatizo hilohilo la kukosa mtoto kwa mkewe Rebeka (mwanzo 25:21); na jambo hilo halikuishia hapo kwani na Yakobo alipatwa na tatizo hilohilo.

Pia, kwa namna hiyihiyo ukifanya yaliyo mema mbele za Mungu, baraka zako hufuatana na uzao wako. Tunaona jambo hilo kuwa, baraka za Ibarahimu ziliweza kufuatana na uzao wake (Mwanzo 30:1-6; 13:15; 17:7-10) ahadi za Ibrahimu hazikuishia kwake tu bali zilipitiliza hadi kwa uzao wake. Kumbe baraka zaweza kusafiri kutoka kwa mababu hadi wabibi, vivyohivyo laana zaweza kusafiri kutoka kwa kizazi kimoja hadi kizazi kingine. Ndio maana hata Yoabu alipomuua Abneri, ambaye alikuwa awali amesamehewa na Mfalme Daudi, ile laana ilifika hadi kwa uzao wake.

Utajifunza pia kwa habari ya Yesu, walipotaka kumuua, wayahudi walitamka wazi kuwa “25 Watu wote wakajibu wakasema, Damu yake na iwe juu yetu, na juu ya watoto wetu.” Mathayo 27:24-26 wayahudi walijua ukweli huu kuwa laana zaweza pita kutoka uzao mboja wa uovu hadi mwingine, kwasababu hiyo inawezekana unaishi katika mateso leo kwasababu ya mambo yaliyopita huko nyuma.

Mungu hapendi kuwatesa wanadamu wala kuwahuzunisha (Maombolezo 3:33). Lazima usimame kinyume na kila laana katika familia yako na katika maisha yako, jitenge na kila laana za kutoka kwa familia au ukoo wako. Balaa, laana na mikosi ya familia yako na ivunjike katika jina la Yesu Kristo.

Na Mchungaji Josephat Gwajima

Paula White azua gumzo!!

Paula-White-Trumpet-Awards

Mchungaji maarufu Paula White hivi karibuni amezua maswali mengi kuhusu mavazi yake jinsi yanavyobadilika tofauti na alivyoanza huduma .

Mtandao wa Praise Radio wameandika “Mavazi ya Pastor Paula White yanaleta gumzo jinsi gani mwanamke wa Kikristo anapaswa kuvaa…”

Vyombo mbali mbali vya kikristo vimekuwa vikiandika kwamba kwa sasa Mchungaji Paula White amezidisha kuvaa mavazi yanayoonesha mwili wake.

Mwinjilisti Robert Kayanja

Robert Kayanja kiongozi wa kanisa la Miracle Centre Cathedral, Kampala, mji mkuu wa Uganda. Ni mmoja kati ya watu wenye nguvu sana nchini humo. Alimpokea Bwana Yesu akiwa na miaka 22. Alianza kanisa na watu wachache. Leo amekuwa mhubiri wa kimataifa pia ana vipindi vya kila wiki vyenye jina Miracle Life Television programmes vinavyorushwa Lighthouse na Daystar Televishen Networks ana chuo cha Biblia, Kituo cha kulelea watoto yatima pamoja na kituo cha TV.

Kanisa la Miracle Centre limeanzisha zaidi ya makanisa 1,000 nchini Uganda. Mungu amekuwa akimtumia  Mwinjilisti na Mchungaji Robert Kanyanja katika ishara na miujiza.

Mheshimiwa GeorDavie kuimba nyimbo za Injili!

Mhubiri wa kimataifa Nabii GeorDavie maarufu kwa jina la “Ngurumo ya Upako” ametambulisha nyimbo zake ziko hewani. Nabii huyu ambaye makazi yake ni Arusha Mungu amekuwa akimtumia katika Ishara na miujiza, hivi karibuni amefungua tawi la huduma yake nchini Marekani na amekuwa akienda nchi mbali mbali kwa ajili ya kuhudumia watu wenye matatizo.

Pia Geordavie Ministries wana studio ya injili N Y U FM 99.2 Kanda ya Kaskazini Arusha, ambapo wanarekodi waimbaji, TV na Vipindi vya Redio na kurusha hewani. Studio imefunguliwa mwanzoni mwaka huu.

Kwa kusikiliza nyimbo za Nabii Geordave Bonyeza hapa http://www.reverbnation.com/play_now/12946165

Askofu Gamanywa amshukuru Mungu, miaka 23 ya ndoa!

Askofu Gamanywa na mkewe Alhappiness wakitoa shukrani

HABARI KUTOKA GOSPEL KITAA

Rais wa shirika la kidini la Wapo Mission International Bishop Sylvester Gamanywa,wiki iliyopita alimshukuru Mungu pamoja na familia yake kwa kutimiza miaka 23 ya ndoa pamoja na mkewe katika kanisa la Pentekoste Tanzania Lindi street(city centre), kanisa ambalo ndilo lilimpatia vibali vya utumishi shambani mwa BWANA mpaka leo hii.

Akiwa na watoto wake wanne Excellent,Excel,Samael, David pamoja na mkewe mpenzi Alhappiness, Bishop Gamanywa alipata nafasi ya kuzungumza pamoja na familia yake na kubariki waumini waliofika kanisani hapo,wakimshukuru Mungu kwa uzima na afya pamoja na yote anayowatendea toka walipofunga ndoa mnamo tarehe nne mwezi wa tatu mwaka 1989.

Shirika la Wapo analoliongoza ndani yake kuna vituo vikubwa viwili vya ushauri wa kibiblia na maombezi(Biblical Counselling and intercession centres) BCIC Mbezi beach pamoja na Mbagala maji matitu ambapo watu mbalimbali wamekuwa wakibarikiwa na kufunguliwa kutoka matatizo mbalimbali yanayowaandama vituo hivyo ni maarufu kwa jina la Hakuna lisilowezekana kutokana na yale Mungu amekuwa akiyatenda katika maisha ya watu wake.

Kutoka kushoto, Askofu Gamanywa,mkewe Alhappiness watoto wao David,Samael,Excellent pamoja na Excel.

Pamoja na vituo hivyo pia shirika hilo linamiliki kituo cha redio cha kikristo cha Wapo radio FM 98.0 kilichopo maeneo ya kurasini jijini Dar es salaam,kituo ambacho kimekuwa baraka kwa wengi kutokana na vipindi vya kijamii na kiroho vinavyoendeshwa chini ya uangalizi wake Bishop Gamanywa.

Baadhi ya waumini waliokuwepo ibadani.
Askofu Gamanywa na familia yake wakiwa katika pozi na Rais wa jamhuri ya Muungano wa Tanzania Jakaya Kikwete
Askofu Gamanywa akiwa na familia yake.