Maneno yetu yaweje?

maneno

Leo hii napenda tuangalie Neno linasemaje kwa habari za kauli zetu kama wana wa Mungu tuliookolewa kwa Neema yake. Roho Mtakatifu yupo atusaidie na kutuwezesha kuishi kwa ushindi katika eneo hili pia: 

Maneno yenu yawe na neema siku zote, yakikolea munyu, mpate kujua jinsi iwapasavyo kumjibu kila mtu. – Wakolosai 4:6 SUV

Neno lo lote lililo ovu lisitoke vinywani mwenu, bali lililo jema la kumfaa mwenye kuhitaji, ili liwape neema wanaosikia. – Waefeso 4:29 SUV 

Neno la Mungu liko wazi kabisa, kama maneno yetu yana uovu wa aina yoyote ile iwe kebehi, dharau, masengenyo, chuki, visasi, lawama, majivuno, kiburi, shutuma na mambo kama hayo, basi tujue tumetoka nje kabisa ya Maandiko; tunatembea mwilini wala hatuenendi kwa Roho. Tusikubali kutembea mwilini hata kama tunadhani tuna haki ya kufanya hivyo, kwani kutembea mwilini ni kumpa ibilisi nafasi maishani mwetu. Tukipanda katika mwili tutavuna uharibifu bali tukipanda katika Roho tutavuna uzima wa milele (Wagalatia 6:8

Tudhamirie kuenenda kwa Roho na kamwe hatutazitimiza tamaa za mwili.

Tukumbuke pia kuwa maneno yetu yana nguvu ya kuumba au kuua, kujenga au kubomoa, kubariki au kulaani, kupanda au kung’oa. Mauti na uzima viko ndani ya uweza wa ndimi zetu nasi tutegemee kuvuna matunda ya kauli zetu. (Mithali 18:21).  

Ni vizuri tutambue ya kuwa Mungu ametupa dhamana kubwa kupitia kauli zetu, na 

Yeye atatuwezesha kuitumia kumletea utukufu tunapokubali kulitii Neno lake.

Bwana Yesu aliweka wazi chanzo cha mawazo, kauli na matendo yetu, kwani alisema hivi:

Mtu mwema katika hazina njema ya moyo wake hutoa yaliyo mema, na mtu mwovu katika hazina mbovu ya moyo wake hutoa yaliyo maovu; kwa kuwa mtu, kinywa chake hunena yale yaujazayo moyo wake. – Luka 6:45 SUV

Hivyo basi, kwa kuwa kiujazacho moyo wa mtu ndicho kimtokacho, ni muhimu sana kulijaza Neno la Mungu mioyoni mwetu. Na pia ni muhimu kuwa makini na yale tunayoruhusu mioyoni mwetu. Mtume Paulo kwa uvuvio wa Roho Mtakatifu aliongezea kusema, “Neno la Kristo na likae kwa wingi ndani yenu katika hekima yote…” – Wakolosai 3:16

Kadiri tunavyolipokea Neno la Mungu na kulitii, ndivyo tunavyofanywa upya nia zetu. Na tunapofanywa upya nia zetu basi hata mawazo yetu, maneno yetu na matendo yetu yanabadilika kuendana na Maandiko yasemavyo. Huko ndiko kuenenda kwa Roho.   

Kama maneno yetu hayawafai wahitaji na kama hayawapi neema wanaoyasikia basi tumepoteza nafasi ya Mungu kutukuzwa kupitia kauli zetu na pia tutakuwa tumepoteza nafasi ya kuwa wawakilishi wazuri wa Baba yetu wa Mbinguni anayewapenda watu wote na anayetaka wote waufikilie wokovu kupitia kwa Bwana Yesu. 

Mzidi kubarikiwa wapendwa,

–Patrick

2 thoughts on “Maneno yetu yaweje?

  1. Baba Mungu ktk jina la Yesu , ninaomba ukatuwekee mlinzi vinywani petu, mngojezi milangoni pa midomo yetu, Zaburi 141:3, hili tuweze kuongea na kusema yale yanayopendeza mbele zako na mbele za watu wote , hili jina lako litukuzwe na kuinuliwa baba , ktk jina la Yesu ninaomba na kushukru. Asante sana mteule wa Mungu Patrick kwa somo lako, ni maombi yangu kwa Mungu baba azidi kukubariki hili na wewe uzidi kutubariki na sisi. ninawapenda nyote wana SG ,mzidi kubarikiwa na Bwana.

  2. Ubarikiwe Mtumishi, na tuzidi kuomba ili nguvu ya Roho Mtakatifu iweke msukumo wa mabadiliko katika roho na nafsi zetu ili tuweze kuwa mashuhuda katika maisha yetu ya kila siku.

Andika maoni yako