Yesu ni BWANA!!

abel

Bwana wa Majeshi ya Mbinguni ndiye Bwana wetu leo, Bwana wa Majeshi ya Israeli ndiye Bwana wetu leo, ni yeye yule jana leo na hata milele “Yehovah Sabaoth”! Kamanda na Komandoo…Amiri Jeshi mkuu na Bwana wa Vita …anasimama kwa ajili yetu, upande wetu, katikati yetu Shujaa aokoae kishujaa…Tunasonga mbele! tunakaza buti, Tunapasua mawimbi, tunamtazama aliyeianzisha kazi njema mioyoni mwetu yuko pamoja nasi hadi tumalize kazi.. tunatiwa nguvu mpya, kama Tai tunapaa, ujana wetu unarejeshwa, tu majasiri kama Simba. Pamoja kwa umoja katika Roho mtakatifu tuna kazi Kubwa mbele, kuhakikisha wanyonge wanainuliwa, dhaifu wanapata nguvu, maskini wanafanikiwa, walio mbali wanafikiwa, wenye dhambi wanatubu, wagonjwa wanapona, mapepo yanatoka, hofu ya Mungu inatawala, na Bwana wetu – Nyota ya alfajiri, Simba wa kabila la Yuda, Mfalme wa wafalme, Bwana wa mabwana, Alfa na Omega ANATUKUZWA kuanzia mioyoni, makazini, kwenye biashara, makanisani, mashambani, angani na ardhini …Ulimwengu ujue nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana, na kwamba hakuna jina lingine juu ya JINA LA YESU. Kila goti lijiandae kwenda chini, kila ulimi ujiandae kukiri ya kuwa YESU NI BWANA! utukufu heshima na adhama vina MUNGU wetu BABA YETU! katika JINA LA YESU.

–Pastor Abel Orgenes

Mungu ni Mwaminifu!

pstabel

Wakati Mwingine unapatwa na mambo ya kuumiza sana moyo wako, inawezekana uliamini sana mtu fulani na akafanya tofauti na tarajio lako au akakutendea jambo ambalo limekuumiza sana…. Inawezekana tukio fulani limetokea la huzuni na kusikitisha na limeacha majeraha moyoni kiasi kwamba unaona maisha hayana maana tena…. Kuna wakati ungependa hata kumuomba Mungu akuchukue uondoke duniani….. Hata wakati wa kuomba unakosa cha kusema…hali hii huitwa pia ni kukosa MATUMAINI… Neno hili limekuja kwa nguvu kwangu kukwambia kwamba MUNGU NI MWAMINIFU, “He is too faithful to fail”… wakati huu ni wakati wa kuangalia Uaminifu wa Mungu – naye ni mwaminifu kukupa TUMAINI kipindi cha maumivu…naye Atabadilisha hali mbaya kuwa Njema kwa utukufu wake… Ataondoa maumivu yako na kukupa furaha, Amani na kujaza moyo wako kwa Upendo wake ambao haulinganishwi na chochote….Kwamba atafanya kwa njia gani na lini sijui, ila kwamba atafanya NAJUA kwa HAKIKA – maana MUNGU NI MWAMINIFU.

Waraka wa Roho Mtakatifu!

abel-o

Roho Mtakatifu anasema:

Nimekuwepo kabla ulimwengu kuumbwa, najua wakati uliopita, naelewa wakati uliopo najua na kushughulika na wakati ujao.

Nina alama ya hua, moto, fimbo, mafuta, maji, upepo na wingu lakini ni nafsi yenye hisia, mimi ni Mungu Roho.

Najua yaliyo katika moyo wa Mungu maana mimi ni sehemu ya ndani ya Mungu, mimi ni ndani ya Mungu, Mungu ndani ya Yesu na mimi ndani ya Yesu na naweza kuwa ndani ya mtu yeyote aaminiye na kunipokea.

Nimekuwa pamoja na wote waliomtumikia Mungu, niliwawezesha na walifanikiwa waliposikiliza ushauri wangu, niliwezesha kuzaliwa kwa Yesu na nikiwa ndani yake Aliweza kutimiza mapenzi ya Mungu yote, hata alipokufa alifufuka kwa nguvu na uweza wangu.

Mimi ni msaidizi na mwalimu wa kweli, hushauri mtu kusikia, kuamini na kupokea Neno.Huwezesha mtu kuzaliwa mara ya pili na akinipa nafasi hujaa ndani yake na kumwongoza katika njia za haki,na kumfanya akue, akomae na kuwa imara kiroho. Mimi ni nguvu itendayo kazi ndani ya mtu na naweza kufanya mambo ya ajabu mno kuliko uyaombayo au uyawazayo.

Kwa kazi yangu utafanyika imara katika utu wako wa ndani. Ukitaka kweli kuwa mtoto wa Mungu lazima ukubali kuongozwa nami, mimi ni ndani yako na huhisi maumivu yako wakati wa mateso na hukuombea kwa kuugua kusikowezwa kutamkwa.Mimi ni mpole na mnyenyekevu, ukinipa nafasi na usiponizima wewe na kila mtu utakayekutana naye ataona matokeo ya kuongozwa na mimi ambayo ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu, upole na kuwa na kiasi. Hakuna Sheria inayoweza kupinga mambo hayo.

Nitakuwezesha kuishi kwa mimi na kuenenda kwa mimi.

Ingawa mimi ni msaada wako mkuu lakini mara nyingi nakosa nafasi ya kukuongoza na kukushauri , ninatoa vipawa na karama ambazo mara nyingi hupingwa na kupigwa vita…

Ulimwengu unakusababishia dhiki, huzuni, fadhaa, majonzi na taabu za kila namna lakini mimi ni mfariji wako mkuu, faraja yangu kwako ni kuu kuliko faraja zingine zote.

Hata hivyo nitashinda, napenda kukufanya wewe kuwa mshindi, najua hila za adui na adui hawezi kusimama mbele yangu, ukiwa na mimi wewe ni tishio kwa adui na utashinda na zaidi ya kushinda…

Nipe nafasi nikuongoze kutimiza kusudi la Mungu maishani mwako, nikuongoze katika mapenzi ya Mungu baba yako, kwa msaada wangu utatenda makuu ili jina la Yesu lililotukuka sana litukuzwe maishani mwako.

Wako Roho Mtakatifu

Written by Pastor Abel Orgenes. 2010

Dondoo kitabu cha Yohana

abel

Miongoni mwa Injili zote nne, Injili ya Yohana ni ya aina ya pekee.Ingawa kwa ujumla inaonyesha maisha ya Yesu na huduma Yake, iko tofauti sana katika mpangilio na mfumo ukilinganisha na zile nyingine tatu.Injili hii haina mifano, ina miujiza miwili tu iliyoandikwa katika zile Injili nyigine zinazofanana (Mathayo, Marko na Luka) na mingine mitano ambayo ni Yohana peke yake anayeieleza.

Mtume Yohana aliandika Injili hii miaka mingi baada ya kufa na kufufuka kwa Yesu. Kusudi la kuiandika ilikuwa kwamba wale wanaoisoma wamwamini Yesu Kristo na kwa njia hiyo wapate uzima wa milele (Yohana 20:31). Yohana anaanza na utangulizi wa pekee ambao haumo katika Injili nyingine. Anaeleza juu ya kuwapo kwa Yesu pamoja na Baba kabla ya kitu cho chote kuumbwa. Kwa njia hii anaonyesha wazi kwamba Yesu hakuwa tu mwanadamu wa pekee bali ana asili ya Mungu. Katika Injili hii tunapata habari za baadhi ya miujiza ya Yesu na mafundisho Yake ambayo hayakutajwa katika Injili nyingine. Sehemu kubwa (Yohana 14-17 ) inaeleza mafundisho ambayo Yesu aliwapa wanafunzi wake kabla ya kifo chake. Sehemu maalumu inaeleza jinsi Yesu alivyojidhihirisha kwa wanafunzi wake baada ya kufa na kufufuka kwake.

Wazo Kuu:
Injili ya Yohana inatilia mkazo zaidi Uungu wa Kristo. Pia inatueleza kwa undani zaidi ishara ambazo Injili nyingine zinaziita miujiza, ili msomaji aweze kuamini kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu na kwamba kwa kuamini apate uzima wa milele.(20;30-31).Zile ishara ambazo mwandishi anazielezea zinatoa uthibitisho wa uweza wa Yesu Kristo wa kiungu na maana hasa ya maisha Yake pale ambapo mwanadamu hana uwezo.Neno “amini” linaonekana mara tisini na nane.Yesu anatambulishwa kama NENO katika Injili hii, pia anaitwa Nuru, Kweli, Upendo, Mchungaji Mwema, Mlango, Ufufuo na Uzima, Mkate wa Mbinguni na majina mengine.

Ule ukweli kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu umerudiwa mara kwa mara. Wakati huo huo ubinadamu wa Yesu unaonyeshwa katika hali Zake za kuchoka, kuhuzunika, kulia, nk

Mwandishi
Yohana ndiye mwandishi wa Injili hii,kwani huyu ndiye yule mwanafunzi mpendwa (13:23) aliyekuwa na Yesu kila mahali na ambaye ndiye aliyeegama kifuani mwa Yesu wakati wa chakula cha mwisho na wanafunzi Wake.Matukio ya Yohana kuwa na upendo na uhusiano wa karibu sana na Yesu umetajwa mara nyingi.Huyu ndiye Yohana mwana wa Zebedayo.Yohana alikuwa Mgalilaya mvuvi (Mk.1:19-20.) Yesu alipomwita. Yohana na Yakobo nduguye waliungana na Andrea na Petro katika uanafunzi wa Yesu. Mama yake Yohana alikuwa Salome dada yake Maria mamaye Yesu (ona Mat.27:56; Mk.15:40; Yh.29:25)

Tarehe:
Karibu na mwisho wa karne ya kwanza kama 90 B.K.

Mahali
Nyumbani kwa Yohana kulikuwa Efeso na ambako ndiko alikozikwa. Kwa hiyo kuna uwezekano mkubwa kwamba Injli hii iliandikiwa Efeso.

Mgawanyo
• Mwanzo unaonyesha kuwa Yesu ni Mungu (1:1-14)
• Huduma ya Yesu kabla ya kwenda Galilaya (1:15-4:54)
• Huduma ya Yesu huko Galilaya na upinzani uliomkabili huko Yerusalemu (5:1-10:42)
• Kufufuliwa kwa Lazaro (11:1-57)
• Kukamilishwa kwa huduma ya Bwana Yesu (12:1-13:38)
• Mafundisho ya mwisho ya Bwana Yesu (14:1-17:26)
• Kufa kwa Yesu na kufufuka kwake (18:1-20:10)
• Kuonekana kwa Yesu baada ya kufufuka (20:11-21:25)

Adui kukuletea uongo unaoangamiza ila unaonekana kama unahitajika

Mr+mrs

Shetani ni Mwongo. Usimwamini, Kamwe usiamini neno toka kwa Shetani. Maneno ya Yesu mwenyewe juu ya Shetani na uongo wake alisema “Ninyi ni watoto wa baba yenu Ibilisi, nanyi mnataka kutimiza matakwa ya baba yenu. Yeye alikuwa mwuaji tangu mwanzo, wala hakushikana na kweli maana hamna kweli ndani yake. Asemapo uongo husema yaliyo yake mwenyewe kwa maana yeye ni mwongo na baba wa huo uongo.”Yohana 8:44 (Biblica version)

Kumbe adui naye ana familia yake ya wasema uongo, familia ya wauaji, na wenye tamaa mbaya! Adui hawezi kuzungumza ukweli bila lengo la kudanganya, kupotosha na kuharibu. Anajua Neno la Mungu lakini analitumia visivyo kukusababishia kuchanganyikiwa na kutokutiii. Ni mjanja sana kiasi kwamba twamhitaji Bwana wetu kutulinda dhidi yake. Ana mbinu nyingi na njia nyingi za kuwakilisha ujumbe wake…
Ni muhimu sana kuwa na maarifa, kujaa neno na kuijua kweli na kumsikiliza Roho mtakatifu Hii itakusaidia usiamini maneno yake anayoweza sema… mfano: Haitaleta tofauti yeyote, fanya tu…Kidogo haitaumiza….Fanya mara hii tu basi….nk
Hii ni baadhi ya misemo anayoitumia sana kushawishi maishani mwa watu kupitia mawazo yako….Sasa hebu fikiri kidogo je wewe mwenyewe huwa unadanganya? Umewahi kusema kwa simu kuwa uko mahali Fulani wakati uko sehemu nyingine? Kwa nini?
Wangapi wamewahi kusema uongo? Ulianza kusema uongo ukiwa na umri gani? Unaposema uongo unakuwa unataka kupata vitu kwa njia isiyo halali? Unasema uongo unapotafuta mwenzi wa maisha, kazi, masomo, biashara na nini tena? Uko tayari kuibia wengine kupata kitakachokufurahisha wewe kwa uongo?
Je unachakachua?
Kama unafanya hivi iko damu ya adui, iko mbegu ya adui maishani mwako.iko roho ya adui inafanya kazi kwako Nimetaja damu sababu kuna wana wa ibilisi. Nimetaja mbegu kwa maana ya DNA ya adui. Matokeo ya madhara yake ni makubwa….Na unapodhani kwamba utadanganya na kukwepa bila kushikwa ndivyo unavyodanganyika zaidi… Isaya 15-18 Ninyi mnajisifu, “Tumefanya agano na mauti, tumefanya mapatano na kuzimu. Wakati pigo lifurikalo litakapopita, haliwezi kutugusa sisi, kwa kuwa tumefanya uongo kuwa kimbilio
letu na miungu ya uongo kuwa mahali petu pa kujificha.’’ 16Kwa hiyo hivi ndivyo BWANA Mwenyezi asemavyo:
Tazama, ninaweka jiwe katika Sayuni, jiwe lililojaribiwa, jiwe la pembe la thamani kwa ajili ya msingi thabiti, yeye atumainiye kamwe hatatiwa hofu. 17Nitaifanya haki kuwa kamba ya kupimia na uadilifu kuwa timazi, mvua ya mawe itafagia kimbilio lenu, huo uongo, nayo maji yatafurikia mahali penu pa kujificha. 18Agano lenu na kifo litabatilishwa, patano lenu na kuzimu halitasimama. Wakati pigo lifurikalo litakapowakumba litawaangusha chini.(version ya biblica)

Jitahidi sana kuelewa umuhimu wa kweli na uadilifu…
Usijifunze uongo jifunze kweli, usitegeemee uongo tegemea kweli, panda uadilifu, jifunze uadilifu na uwe mwadilifu. Uwe kama Mungu wetu ambaye hawezi kusema uongo Waebrania 6: 18 Mungu alifanya hivyo, ili kwa vitu viwili visivyobadilika, yaani ahadi Yake na kiapo Chake, ambavyo kwa hivyo Mungu hawezi kusema uongo, sisi ambao tumemkimbilia, tuwe na moyo mkuu kulishika lile tumaini lililowekwa mbele yetu. (Biblica version)

Ukimaliza kusoma hii waweza kumwomba msamaha Mungu kwa kusema na kutenda uongo, na kuomba msamaha kwa wale unaolazimika kuwaomba msamaha kwa kuwadnganya kadri utakavyoweza.
Kumbuka kama ambavyo hupendi kudanganywa usidanganye wengine…

Wako Abel na Rebecca Orgenes – “B” family ministry!

Nukuu na Dondoo za kitabu cha Samweli katika agano la kale

1SAMWELI

Utangulizi:
Katika andiko la Kiebrania, kitabu cha 1Samweli na 2Samweli vilikuwa kitabu kimoja kilichotambuliwa kwa jina hilo. Huku kugawanyika na kuwa vitabu kuwa viwili kulifanyika katika tafsiri ya Septuagint, yaani,Agano la Kale la Kiyunani, ambalo liliviita Kitabu cha Kwanza na cha Pili cha Wafalme. Kitabu cha 1Samweli kinaandika habari za maisha ya Samweli, Sauli na sehemu kubwa ya maisha ya Daudi. 1Samweli kinaanza kuelezea kuzaliwa kwa Samweli na mafundisho yake hekaluni. Kinaelezea jinsi alivyoiongoza Israeli akiwa kama nabii, kuhani na mwamuzi.

Wakati wana wa Israeli walipodai kuwa na mfalme, Samweli, kwa uongozi wa Mungu, alimtia Sauli mafuta kuwa mfalme wa kwanza wa Waisraeli. Lakini Sauli aliacha kumtii Mungu, naye Mungu akamkataa asiendelee kuwa mfalme. Kisha Mungu akamongoza Samweli akamtia Daudi mafuta kwa siri kuwa mfalme badala ya Sauli. Mapambano kati ya Sauli na Daudi ndiyo yaliyomo katika sehemu iliyobaki ya kitabu hiki. Ingawa tunajifunza mengi kuhusu watu hawa wawili, pamoja na kutokumtii Mungu kwa Sauli, pia kuna mkazo mkubwa kuhusu wema wao kwa Mungu.

Wazo Kuu:
Hiki kilikuwa ni kipindi cha mabadiliko katika historia ya Israeli, wakati taifa hili lilipoondokana na mfumo wa kuwa na waamuzi kama viongozi wao na kuwa na mfalme kama mataifa ya jirani yalivyokuwa. Samweli, akiwa nabii, kuhani na mwamuzi, alichangia kikubwa katika kipindi hiki.

Mwandishi:
Ingawa 1 na 2Samweli mapokeo yanasema mwandishi ni Samweli, ni vigumu sana yeye kuwa ndiye aliyeandika wakati kifo chake kimeandikwa katika 1Samweli 25. Ye yote aliyeandika vitabu hivi anaweza kuwa alitumia kitabu cha Yashari, ambacho kimetajwa katika 2Samweli 18 kama chanzo cha habari hizi. Uandishi wa Samweli, nabii Nathani na Gadi, “Daudi mwana wa Yese alitawala juu ya Israeli miaka arobaini: Alitawala huko Hebroni miaka saba na miaka thelatini na mitatu akatawala huko Yerusalemu” (1Mambo ya Nyakati 29:29.). Hawa ndio ambao wameeleza matendo yote ya Mfalme Daudi tangu mwanzo hadi mwisho.

Wahusika Wakuu:
Eli, Elikana, Hana, Samweli, Sauli, Yonathani, Daudi.

Mahali:
Kitabu kinaanzia wakati walipokuwa wanaongozwa na waamuzi na kuelezea Israeli kuondoka katika utawala wa Mungu na kuingia katika utawala wa wanadamu kwa kuwa na mfalme.

Tarehe:
1204 – 1035 K.K.

Mgawanyo:
• Eli kuhani na mwamuzi (1:1-4:22)
• Samweli kiongozi wa Israeli (5:1-8:22)
• Sauli mfalme wa kwanza wa Israeli (9:1-15:35)
• Kifo cha Sauli (31:1-13).