Bwana Yesu asifiwe!
Haja ya moyo wangu kwa Wakristo wenzangu hapa Strictly Gospel ni kuomba ushauri pamoja na kuhitaji muungane nami katika kuliombea suala hili.
Mimi ni kijana nimeokoka na ni mzaliwa wa kwanza kwenye familia yetu na mzaliwa wa kwanza kiroho kwa sababu Mungu alianza kuniokoa mimi ijapokuwa nina ndugu zangu wameokoka lakini bado hawajapokea neema yakuweza kusimama na Kristo.
Lililonileta ni suala hili kwamba nipo kwenye vita na sijajua nifanye nini kwenye jambo hili lililonipata mwaka huu.
Nyumbani kwetu tuna mdogo wetu wa kike ambaye ni mtoto wa mwisho. Tatizo lililojitokeza nilianza kuota ndoto juu ya mama yangu mzazi. Nilikuwa naota nawaona watu wanamuita majina mabaya sana. Nikiota hivyo mimi nakuwa nabishana nao ndotoni, nikiwakemea kuhusu maneno yao, lakini wao walikuwa wananishangaa sana.
Hapo mwanzo sikuwa naelewa nini kinaendelea. Lakini wakati nakaribia kurudi likizo nyumbani, kwani nilikuwa nipo muhula wa kwanza mwaka wa tatu namalizia masomo yangu ya shahada ya kwanza katika moja ya vyuo vikuu Tanzania, nilikuwa nasikia kuna wimbo wa injili wenye maudhui ya kumsihi Mungu anipe nguvu nisikate tamaa. Hapo sikuelewa kwa nini wimbo huu ulikuwa unakuja hasa asubuhi tu pale ninapoamka, unakuja kichwani.
Ndipo niliporudi nyumbani nikakuta habari mbaya sana ambazo sikuzitarajia maishani. Nilianza sikia kwa watu baki ya kuwa mama yangu anamkuwadia (anamtafutia wanaume) mdogo wangu ambaye alikuwa ana umri wa miaka 17 kwa wakati huo. Yeye ni wa kike na wa mwisho kwa wanaume. Sababu ya mama kumkuwadia ni eti ili apate pesa ya kulipa madeni!
Kwa kweli kama mtoto mkubwa niliposikia habari zile nikaamua kuongea na mdogo wangu, mimi kama kama kaka, na kutumia mbinu za kisaikolojia kumhoji. Baada ya kumhoji dipo akaniambia habari zote ambazo zilinifanya nikaunganisha ndoto ile niliyoiota siku za nyuma na ule wimbo uliokuwa unanielekeza nimuombe Mungu anipe nguvu nisikatee tamaa. Pamoja na hayo nilisikia na mengine mengi sana kiasi kwamba yalinihuzunisha na yaliniumiza na kunifanya niingiwe na uchovu wa kiroho ambao umenigharimu sana roho yangu.
Mdogo wangu huyo sasa kawa mjeuri sana. Ameshatoroka nyumbani kama mara nne; tunamtafuta; tunamrudisha.
Huku napo baba yangu maisha yake ndiyo siwezi elezea maana hayampi Mungu utukufu. Kwa kifupi ni kwamba roho za uzinzi na uasherati zimeivamia nyumba yetu. Wazazi wangu sasa wametengana na baba yangu anataka kuoa mwanamke, tuseme msichana, ambaye kwa kukadiria nimempita umri au tumelingana. Vita vimepamba moto kama asingekuwa Mungu, chuoni ningefeli kwasababu kuna wakati nilikuwa nashindwa kabisa hata kusoma!
Sasa nalileta kwenu, ndugu zangu katika Kristo, mnishauri hapa nifanya nini. Sambamba na ushauri huo ninaomba mniombee ili Mungu aiponye familia yangu.
By C.P